KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 1, 2014

FAMILIA YA AMINA NGALUMA YAISHUKURU JAMBO SURVIVOR





FAMILIA ya aliyekuwa mwimbaji mahiri nchini marehemu Amina Ngaluma ‘Japanese’, imeishukuru bendi ya Jambo Survivor ya Thailand kwa ushirikiano mkubwa iliyoutoa mpaka kufanikisha kuletwa Dar es Salaam kwa mwili wa mwimbji huyo na hatimaye kuzikwa.

Pia imewashukuru wadau wa muziki na Watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa na kuwafariji wakati wote wa kipindi kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao aliyezikwa Mei 24 mwaka huu Kitunda, Machimbo Dar es Salaam.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na mume wa mwimbaji huyo, Rashid Sumuni ilisema hawana cha kuwalipa badala yake Mwenyezi Mungu ndiye atakayejua cha kuwalipa.

“Mimi binafsi na familia ya Mzee Ngaluma, tunaishukuru bendi ya Jambo Survivor ya Thailand chini ya kiongozi wake Hassan Shaw kwa juhudi zao walizofanya mpaka kuuleta mwili hapa nyumbani.

“Hatuna tatizo nao na tunawatakia kila la heri katika kazi zao, juhudi walizofanya wakati wanataka kuokoa uhai wa mke wangu alipougua ghafla tunazithamini sana, pia msaada wao kwetu kuuleta mwili Dar es Salaam ni kubwa na tunautambua,” alisema Sumuni.

Pia alisema masuala yote yanayohusiana na msiba huo wasemaji ni familia na kueleza kuwa hwatahusika na mtu mwingine yeyote atakayekuwa anatoa kauli ambazo hakutumwa na familia yao.

“Tunawashukuru mashabiki wa Amina, wdau wa muziki na Watanzania wote waliokuwa nasi bega kwa bega wakati wa msiba. Sote tumuombee mwenzetu dua njema,” alisema Sumuni.

Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki dunia Mei 15 mwaka huu kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor.

Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’, Double M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.

Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya na amepata kufanya kazi Omani na Dubai na kutunga vibao mbalimbali vilivyopendwa na mashabiki.

No comments:

Post a Comment