KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 10, 2013

MGOSI AANZA KIBARUA JKT RUVU

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars, Musa Hassan 'Mgosi' ameanza rasmi mazoezi na timu yake mpya ya JKT Ruvu.

Mgosi, ambaye alirejea nchini hivi karibuni akitokea China, alikokwenda kucheza soka ya kulipwa, alianza mazoezi hayo jana kwenye uwanja wa Mlalakuwa, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Charles Kilinda alisema jana kuwa, wanatarajia kuanza rasmi kumtumia Mgosi katika mechi za mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Kilinda alisema Mgosi alikwenda China kwa ajili ya michuano maalumu, iliyowashirikisha wachezaji kutoka nchi za Afrika, ambapo aliongoza kwa kufunga mabao.

Mgosi alisajiliwa na JKT Ruvu kabla ya kuanza kwa ligi, lakini alishindwa kuichezea katika mzunguko wa kwanza kutokana na kukosa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kwa mujibu wa Kilinda, ujio wa Mgosi utazidi kukiimarisha kikosi chake kutokana na uzoefu wake wa michuano mbalimbali na pia umahiri wa kupachika mabao.

"Tumeshapata uhamisho wake kutoka DRC na sasa Mgosi ataanza kuvaa jezi za JKT Ruvu katika mzunguko wa pili,"alisema kocha huyo, ambaye aliwahi kuichezea Yanga miaka ya 1980.

No comments:

Post a Comment