KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 24, 2013

KAMATI YA RUFANI TFF YAAHIDI KUTENDA HAKI



KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewaahidi wadau wa mchezo huo kuwa, itafanyakazi zake kwa misingi ya haki.

Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe watano, Idd Mtiginjola amesema wapo kwa ajili ya kutenda haki kwa watu wote.

Mtiginjola alisema hayo juzi baada ya uzinduzi wa kamati hiyo, uliofanywa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kwa niaba ya rais wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga.

Mwenyekiti huyo alisema, kamati yao inaundwa na watu waadilifu, hivyo watafanya kazi kwa kuzingatia kanuni zilizopo na sheria nyingine za mpira wa miguu, ikiwemo Katiba husika.

“Niwakikishie kuwa, hatutafanya uamuzi kutokana na mawazo yetu, tufanya uamuzi kwa kuzingatia kanuni na sheria. Kamati hii ni chombo cha haki, hivyo itafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria. Sheria na haki ni vitu viwili tofauti. Sheria zipo kwa ajili ya kuitafuta haki,” alisema Mtiginjola, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, akiwa Wakili wa Kujitegemea.

Baada ya uzinduzi huo, Osiah aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi (instruments) mbalimbali, zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama wake, katiba ya TFF na katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mbali ya Mtiginjola, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti, Francis Kabwe, ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed Mpinga, ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.

Wajumbe wengine ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo, ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka Murtaza Mangungu, ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.

No comments:

Post a Comment