KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 28, 2011

Yanga kujipima ubavu kwa Coastal Union

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani Jumapili ijayo, kumenyana na Coastal Union katika mechi ya kirafiki itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, pambano hilo ni maalumu kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Sendeu alisema, katika mechi hiyo, Kocha Sam Timbe atawatumia wachezaji wake wapya kadhaa waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Mbali na kuwajaribu wachezaji hao wapya, Sendeu alisema kocha huyo pia atapima uwezo wa kikosi chake baada ya kufanya mazoezi kwa wiki mbili kwenye uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani, Dar es Salaam,
“Hii ni nafasi nzuri kwa Kocha Timbe kuona ni kwa kiasi gani wachezaji wake wameweza kushika mafunzo aliyowapa hadi sasa na pia timu inavyoweza kucheza kwa ushirikiano,”alisema.
Wachezaji wapya wa Yanga wanaotarajiwa kushuka dimbani Jumapili ni pamoja na Kenneth Asamoah, Haruna Niyonzima, Shabani Kado, Hamisi Kiiza, Oscar Joshua, Idrisa Rashid, Godfrey Taita.
Kwa upande wa Coastal Union, mechi hiyo itakuwa ya pili ya kirafiki kwenye uwanja huo baada ya wiki iliyopita kuibuka na ushindi dhidi ya Azam FC.
Kwa sasa, Coastal Union ipo mjini Mombasa, nchini Kenya, ambako imekwenda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo. Timu hiyo inanolewa na Kocha Hafidh Badru.

No comments:

Post a Comment