KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 28, 2011

Tunataka ubingwa wa Afrika-Timbe



KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, Sam Timbe ametamba kuwa, lengo lake msimu ujao ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa klabu za Afrika.
Timbe alitoa majigambo hayo jana wakati wa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika asubuhi kwenye uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani, Dar es Salaam.
Majigambo hayo ya Timbe yamekuja wiki kadhaa baada ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame baada ya kuichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali, iliyochezwa mapema mwezi huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema kwa sasa, hana haja ya kuhangaikia mataji ya Afrika Mashariki na Kati kwa vile ameyakinai, hivyo anataka kuweka rekodi mpya ya kutwaa ubingwa wa Afrika.
Timbe, ambaye ni raia kutoka Uganda alisema, tayari ameshatwaa Kombe la Kagame akiwa na klabu za Villa na Polisi za Uganda, Atraco ya Rwanda na sasa Yanga ya Tanzania Bara.
Alisema hakuna kocha anayeweza kufikia rekodi yake kwa sasa na kusisitiza kuwa, dhamira yake ni kuongeza mataji mengine zaidi akiwa Yanga.
“Nina uhakika wa kutwaa tena ubingwa wa Tanzania Bara msimu ujao nikiwa na Yanga na nashukuru kuona kwamba kikosi changu kimekamilika,”alisema kocha huyo.
Kocha huyo asiye na mbwembwe na makeke alisema, amepania kuhakikisha Yanga inafuzu kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa wa Afrika mwakani na ikiwezekana kutwaa ubingwa.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba, Yanga ilishawahi kucheza hatua hiyo mwanzoni mwa miaka ya 2000, hivyo lengo langu ni kwenda mbali zaidi, ikiwezekana kucheza nusu fainali na kutwaa ubingwa,”alisema.
Aliongeza kuwa, anafurahishwa na mazoezi ya timu yake yanayoendelea kwenye uwanja wa Jangwani kwa vile wachezaji wake wamekuwa wakiyafuata na kuyashika vyema maelekezo yake.
Kwa sasa, Yanga inajiandaa na mchezo wake wa kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya mahasimu wao Simba, utakaopigwa Agosti 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, mechi hiyo ilikuwa ipigwe Agosti 17 kwenye uwanja huo, lakini umezogezwa mbele ili kutoa nafasi kwa wachezaji wa timu hiyo, kuichezea timu ya Taifa, Taifa Stars katika mechi ya kirafiki dhidi ya Palestina.
Wakati huo huo, wachezaji wa Yanga jana asubuhi walionekana kuyafurahia mazoezi waliyokuwa wakipewa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe kwenye uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam.
Katika mazoezi hayo, wachezaji wa timu hiyo walikuwa wakibebana wawili wawili na kuruka viunzi kwa lengo la kujenga stamina kabla ya kucheza soka.

No comments:

Post a Comment