'
Thursday, July 21, 2011
Isha Mashauzi afungashiwa virago Jahazi
UONGOZI wa kundi la muziki wa taarab la Jahazi umetangaza rasmi kumtimua mmoja wa waimbaji wake nyota, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kundi hilo zimeeleza kuwa, Isha ametimuliwa kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo utovu wa nidhamu uliokithiri.
Uamuzi wa Jahazi kumtimua Isha umekuja miezi michache baada ya mwimbaji huyo pamoja na Leila Rashid kusimamishwa kwa tuhuma za kujiona bora kuliko wenzao.
Ilidaiwa wakati huo kuwa, Isha na Leila walikuwa na kawaida ya kuleta ‘mapozi’ wakati wa maonyesho ya kundi hilo na pia kufika mazoezini katika siku wanazopenda wenyewe.
Hata katika uzinduzi wa albamu ya saba ya kundi hilo, uliofanyika Mei mwaka huu kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam, waimbaji hao wawili hawakuonekana jukwaani.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Jahazi kilieleza juzi kuwa, uamuzi wa kumfukuza Isha umefikiwa na uongozi kutokana na kushindwa kuonekana kwenye maonyesho ya kundi hilo kwa muda mrefu.
Kufuatia kushindwa kuonekana jukwaani kwa mwimbaji huyo, uongozi wa kundi hilo uliamua nyimbo zake ziimbwe na waimbaji wengine chipukizi, ambao wamekuwa kivutio kikubwa.
Kuna habari kuwa, tayari Isha ameshaamua kuanzisha kundi lake, akishirikiana na mama yake mzazi, Rukia Ramadhani.
Isha alijizolea umaarufu mkubwa kupitia kundi la Jahazi, linaloongozwa na Mzee Yussuf. Mwimbaji huyo mwenye makeke, aliwahi kurekodi albamu yake binafsi mwaka jana, iliyozidi kumpatia umaarufu, inayojulikana kwa jina la ‘Mama nipe radhi.’
“Ni kweli tumeamua kumtimua Isha Mashauzi kwenye kundi letu kwa sababu tumeshindwa kuvumilia vitendo vyake,” kilisema chanzo cha habari.
“Amekuwa haonekani kwenye maonyesho ya kundi letu, tukimuuliza, majibu yake yanakuwa ya jeuri, kwa ujumla amekuwa akionyesha vitendo vya utovu wa nidhamu,”kiliongeza.
Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa kundi hilo, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa kuepuka malumbano kati yake na mwimbaji huyo, hawapo tayari kumpokea tena Isha kwenye kundi hilo.
"Kwa hatua aliyofikia, hatuwezi kumpokea tena Isha Ramadhani kwenye kundi hili. Tunashukuru Jahazi tuna waimbaji wazuri zaidi yake, aende tu, lakini ipo siku atalikumbuka kundi hili," alisema kiongozi huyo.
Hivi karibuni, Isha alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa, bado yeye ni mwimbaji wa Jahazi na hawezi kuhama kwa madai kuwa, ana mapenzi makubwa na kundi hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, kwa kipindi kirefu sasa, Isha amekuwa akifanya maonyesho kwa kujitegemea katika kumbi mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, kundi la Jahazi lipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uzinduzi wa albamu yake ya nane, inayotarajiwa kuzinduliwa baada ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Kiongozi wa kundi hilo, Mzee Yussuf alisema juzi kuwa, maandalizi kwa ajili ya uzinduzi wa albamu hiyo yamekamilika na itakuwa na nyimbo nne.
“Ninawahakikishia mashabiki wetu kwamba, albamu hii itakuwa bora kuliko zote zilizotangulia, hivyo wakae mkao wa kula kuisubiri,”alisema mtunzi na mwimbaji huyo mwenye kipaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Ukweli ni kwamba Bi. Isha Ramadhani amebobea katika ulingo huo wa Taarab! Bila kumpaka tope, ni laima Mzee akubali nafasi yake ya kuandaa vipaji kisha kuviachilia...haijalishi ilikuwaje,ni bora pande zote ziendelee kunawiri!Kwangu mimi moja wapo ya sababi zilizonifanya kuipenda Jahazi ni hao wawili Princess Mashauzi na Malkia Leila.Bado tutadumu na Mamaa Mashaui!
ReplyDelete