KIKUNDI cha taarab cha Five Stars cha mjini Dar es Salaam, hivi sasa kinasukwa upya baada ya kuondokewa na wasanii wake 13 katika ajali ya gari, iliyotolewa miezi michache iliyopita mkoani Morogoro.
Kwa sasa, uongozi wa kundi hilo upo kwenye hatua za mwisho za kuliunda upya kundi hilo, ambalo uzinduzi wake umepangwa kufanyika kesho kwenye hoteli ya Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kulisuka upya kundi hilo, tayari wameshapatikana waimbaji na wapiga ala kutoka vikundi mblaimbali, ambao wapo kwenye mazoezi makali kwa ajili ya kujiandaa kwa uzinduzi huo.
Miongoni mwa waimbaji wapya, wanaotarajiwa kuling’arisha kundi hilo ni pamoja na Mariam Mohamed, mshindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS) mwaka jana.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Mariam alisema ameamua kuelekeza nguvu zake katika muziki huo kutokana na uwezo mkubwa alionao kiuimbaji.
Mariam anaamini kuwa, kwa sasa soko la muziki huo ni kubwa, ikilinganishwa na miziki mingine na kuongeza kuwa, iwapo atakuwa makini katika kazi yake, anaweza kufika mbali.
Mwanadada huyo mwenye mtoto mmoja, amejaaliwa kuwa na sauti yenye mvuto na inayoliwaza. Pia ni mahiri katika kutibwirika awapo stejini na sifa hizo ni miongoni mwa zilizomwezesha kuibuka mshindi wa shindano la BSS mwaka jana.
Mariam alisema tangu akiwa mdogo, alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki huo na kwamba hawezi kuuacha kwa sababu upo kwenye damu yake.
Alisema uamuzi wake wa kujiunga na shindano la BSS ulilenga kuonyesha kipaji chake kwa vile alikuwa na imani kubwa kwamba, uwezo wa kuimba na kuvutia hadhira anao.
“Kwa kweli hakuna mtu aliyenishawishi kuupenda muziki huu. Hiki ni kipaji nilichorithi kutoka kwa marehemu babu yangu, ambaye alikuwa mwimbaji mashuhuri,”alisema.
Mariam alisema alianza kujifunza uimbaji kwa kuiga nyimbo za wasanii mbalimbali maarufu wa muziki huo hapa nchini na kuendelea kuonyesha kipaji chake alipokuwa akisoma shule ya msingi ya Kigogo Luhanga, Dar es Salaam.
Mwanadada huyo mwenye mwili uliojaajaa na kujengeka vyema alisema, akiwa katika shule hiyo, alishiriki mashindano ya kuimba na mara zote alikuwa akiiongoza shule yake kushinda.
Alisema kutokana na kuvutiwa na kipaji chake, baadhi ya walimu wa shule hiyo walimshauri aendeleze kipaji chake cha uimbaji kwa vile alikuwa na uwezo mkubwa wa fani hiyo.
Kutokana na uwezo mdogo wa familia yake, Mariam hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari. Baada ya kumaliza shule ya msingi mwaka 2007, aliamua kujihusisha na kazi za kufuma vitambaa, ususi na kupamba maharusi.
Mbali ya kuwa na kipaji cha uimbaji, Mariam pia ni hodari katika ususi wa nywele za aina mbalimbali. Utaalamu wake huo umemwezesha kujipatia umaarufu mkubwa katika eneo analoishi.
“Kwa siku nilikuwa naweza kusuka hata vichwa kumi, wateja wangu walikuwa wakitoka sehemu mbalimbali, hadi nikafikia uamuzi wa kutaka kufungua saluni," alisema.
Alisema kazi hiyo alikuwa akiifanya nyumbani kwao na kwamba wateja wake walikuwa wakimfuata kutokana na kutokuwa na ofisi maalumu.
Kabla ya kushiriki katika shindano la BSS, Mariam alijiunga na kikundi cha taarab cha Kings chenye maskani yake Mburahati, Dar es Salaam, lakini hakubahatika kurekodi nacho wimbo wowote.
Mwanadada huyo mwenye macho ya mwito alisema, aliamua kuimba nyimbo za taarab wakati wa shindano la BSS kwa lengo la kuonyesha kipaji na uwezo wake katika fani hiyo.
Tangu alipojiunga na kundi la Five Stars, Mariam amesema amesharekodi nalo wimbo mmoja, unaojulikana kwa jina la ‘Ulaumiwe wewe nani’. Alisema wimbo huo utapigwa kwa mara ya kwanza wakati wa onyesho la uzinduzi litakalofanyika kesho.
Kwa mujibu wa Mariam, lengo lake kubwa ni kutumia uwezo wake wote kuhakikisha kuwa, kundi hilo lililoundwa upya, linapata mafanikio makubwa kimuziki.
Aliushukuru uongozi wa kundi hilo na wasanii wenzake kwa kumpa ushirikiano mkubwa, hali aliyosema imezidi kumwongezea ari ya kiuimbaji.
Mariam alisema anapenda kuishi maisha ya kawaida na kusisitiza kuwa, kamwe katika maisha yake, hafurahii kuitwa nyota. Chakula kikubwa anachokipenda ni ubwabwa na maharage.
Mariam ametoa mwito kwa serikali kuisimamia vyema sheria ya hatimiliki ili wasanii waweze kunufaika na vipaji vyao, badala ya ilivyo sasa, ambapo alisema wanaonufaika ni wajanja wachache.
Mwimbaji huyo, ambaye ni mwenyeji wa Kilwa Masoko mkoani Lindi, amewataka wasanii nchini kuwa na ushirikiano na kusaidiana ili iwe rahisi kwao katika kutekeleza majukumu yao.
Mariam alizaliwa mwaka 1990 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam. Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne. Hajaolewa, lakini anaye mchumba na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment