KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 3, 2010

NMB yaipatia Stars mil.26/-

BENKI ya NMB imeipatia timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars fedha taslim sh. milioni 15 na vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 11.
Fedha na vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana kwenye hafla iliyofanyika kwenye ofisi za shirikisho hilo zilizopo uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam.
Akikabidhi fedha hizo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Biashara wa NMB, Imani Kajura alisema zimelenga kulipia gharama za kambi na posho kwa wachezaji.
Vifaa vilivyotolewa kwa timu hiyo ni viatu jozi 40, seti mbili za jezi, nguo za kawaida za kuvaa baada ya mazoezi jozi 30 na jozi 10 za makocha na viongozi wengine wa kikosi hicho.
Akipokea vifaa hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela aliushukuru uongozi wa NMB kwa jitihada zake za kuisaidia Taifa Stars kila inapokabiliwa na mechi muhimu.
Taifa Stars inajiandaa kurudiana na Rwanda katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya kuwania ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani. Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Jumapili mjini Kigali.
Katika mechi ya awali iliyochezwa mwezi uliopita mjini Dar es Salaam, Taifa Stars ilitoka sare ya bao 1-1 na Rwanda. Ili ifuzu kucheza fainali hizo, Taifa Stars italazimika kuishinda Rwanda ama kupata sare ya mabao 2-2.
Mbali na mechi hiyo, Taifa Stars pia inatarajiwa kumenyana na Brazil katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, inayotarajiwa kuchezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment