KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 11, 2016

NAPE AFURAHISHWA NA RIPOTI YA TFF


Ripoti ya mwenendo wa mpira wa miguu Tanzania na mipango yake inayofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemfurahisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye hivyo moja kwa moja akaupongeza uongozi wa Rais Jamal Malinzi akisema unafanya kazi kubwa.

Kutokana na ripoti hiyo, Nape ambaye ni Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, aliridhia wadau wa mpira wa miguu kusapoti timu za taifa hususani Serengeti Boys – timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ambayo kwa sasa imepiga kambi Shelisheli kujiandaa kuivaa Congo-Brazzaville Jumapili ijayo.

Serengeti Boys inawania kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri katika fainali zitakazofanyika Antananarivo, Madagascar sawa na timu ya taifa ya soka la ufukweni ambayo inatarajiwa kusafiri kwenda Abidjan, Ivory Coast kucheza mchezo wa pili wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mchezo huo.

Timu nyingine ya taifa ni ile ya wanawake ya Tanzania Bara maaarufu kwa jina la ‘Kilimanjaro Queens’ ambayo kwa sasa iko Uganda kuwania taji la Chalenji ikishirikisha timu za taifa za Afrika Mashariki katika michuano ya inayotarajiwa kufanyika jijini Jinja kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, mwaka huu.

Nape amefurahishwa na mipango ya TFF baada ya kupeleka timu zote kushiriki michuano mbalimbali kwa vipindi mbalimbali na kwamba Serikali itasapoti lakini hapo baadaye baada ya kufuata taratibu mbalimbali baada ya Rais Malinzi kumfafanualia kuwa gharama za kuendesha mpira kwa mwaka zinafika shilingi bilioni 15, na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) huchangia asilimia tatu (3) tu ya bajeti nzima kwa mwaka.

“Kwa kuanzia msimu huu tu, FIFA imeongeza na sasa itafika asilimia 6 kwa mwaka,” alisema Malinzi jambo ambalo lilimshangaza Nape ambaye leo Septemba 10, 2016 alifanya ziara ya kutembelea TFF kujionea hali halisi na kushangazwa na taarifa za vyanzo mbalimbali zinazotuhumu shirikisho.



Nape alisema: “Serikali inasapoti maendeleo, lakini lazima yafuate taratibu, kanuni na sheria za soka.”

Katika eneo la kufuata taratibu, kanuni na sheria za soka hatua nyingine, Nape alitaka Malinzi na kamati zake kuwa wakali kwa kuwa huwa hawachui hatua mapema, inatokea wadau kutaka kuipanda kichwani TFF.

“Naagiza mchukue hatua mapema kukamua majipu kabla hajajaiva. Sasa ninyi mnasubiri kwa muda mrefu kabla ya kuchukua hatua, ndiyo maana wanawasumbua. Washughulikieni mapema, mkiwabana mapema watakaa kimya, kanuni mnazo, sheria mnazo, wabaneni,” alisema Nape.

Katika hatua nyingine, Nape alisema kwamba kuna mchakato unaendelea kwa sasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kwamba wanarejesha mamlaka ya kumiliki baadhi ya viwanja vya soka Makao Makuu ya chama badala mikoa ambako wamegundua kuwa kuna matatizo makubwa katika menejimenti.



NA HIZI NDIZO SALAMU ZA RAIS WA TFF, JAMAL EMIL MALINZI KWA MHESHIMIWA NAPE NNAUYE WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO UWANJA WA KARUME TAREHE 10 SEPTEMBA 2016



Mheshimiwa Waziri,



Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutukutanisha hapa leo.

Ni jambo la heshima na furaha kubwa sana  kwetu sisi wanafamilia ya mpira wa miguu Tanzania kwa kutembelewa na wewe Mheshimiwa Waziri na ujumbe wako. Mheshimiwa ahsante sana kwa tukio hili adhimu na karibu sana kwenye makazi ya mpira “home of football”.



Mheshimiwa Waziri tunashukuru kwamba umeweza kutembelea eneo letu na kujionea wapi huwa tunafanyia shughuli zetu mbali mbali za kuendeleza michezo.

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limesajiliwa chini ya sheria ya baraza ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1971  na madhumuni yake makuu  ni kuendeleza na kusimamia mpira wa miguu Tanzania. Katika kutekeleza azma hii shughuli zetu tumezigawanya katika maeneo makuu matano:



1. Utawala

Shughuli za kila siku za uendeshaji wa mpira wetu zinasimamiwa na Sekretariet ya TFF inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Mwesigwa Selestine. Chini yake ana vitengo vikuu vitano: Ufundi ambacho kinasimamia maendeleo ya mpira, Mashindano ambacho kinasimamia mashindano mbali mbali, Fedha na utawala, Sheria na vyama wanachama na cha tano ni cha biashara na masoko. Vitengo hivi kwa pamoja vinashirikiana kuhakikisha mpira unafundishwa, unachezwa na unasimamiwa vyema. Aidha zipo Kamati mbali mbali zinazotusaidia kutushauri kwenye mambo ya kitaalam na kutoa maamuzi vikiwa vyombo huru. Pia tunacho chombo chetu kinachoitwa Bodi ya Ligi kinachosimamia uendeshaji wa ligi zetu kuu tatu Ligi kuu ya daraja la kwanza na ya daraja la pili. Ligi kuu ya vilabu vya wanawake  inaendeshwa na kamati ya mpira wa wanawake.



2. Mashindano

Ili mpira uchezwe inabidi kuwepo na mashindano. Wakati wote TFF inafanya jitihada za kubuni mashindano mapya na kuhakikisha yaliyopo yanafanyika kwa mujibu wa kalenda. Kwa sasa TFF tunaendesha mashindano makuu ya kitaifa saba: Ligi kuu, Ligi daraja la kwanza, Ligi daraja la pili, Ligi ya mikoa, Kombe la Shirikisho, Ligi ya vijana na Ligi ya vilabu vya wanawake. Ukiondoa ligi daraja la pili na ligi ya mikoa mashindano yaliyobakia yote yanaonekana moja kwa moja kwenye (live) kwenye Televisheni. Shirikisho liko mbioni kuanzisha mashindano ya vilabu nane bora vya ligi kuu (Super 8). TFF pia huwa inasimamia mechi mbali mbali za kimataifa za mashindano na za kirafiki kwa timu za Taifa za rika mbali mbali za   wanawake na wanaume.



3. Masoko na Biashara

Kuendesha mpira ni gharama kubwa.  Wastani wa bajeti ya Shirikisho ni  shilingi bilioni kumi na tano kwa mwaka.Tunawashukuru FIFA ambao hadi mwaka jana walikuwa wanachangia asilimia 3% ya bajeti hii na kuanzia mwaka huu wanachangia asilimi 6% ya bajeti hii.  Jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika kuhakikisha shughuli za uendeshaji wa mpira hazikwamishwi na ukosefu wa fedha. Kitengo cha biashara na masoko kinafanya jitihada kubwa kuhakikisha kila shindano letu linakuwa na udhamini hata kama sio wa kukidhi mahitaji yote.



4. Miundombinu

Ni muhimu sana kuwa na miundo mbinu ya kutosha na yenye sifa ya kuchezewa mpira. Kwa kushirikiana na wamiliki mbali mbali wa viwanja vya mpira  TFF tumekuwa tukitoa ushauri wa namna ya kuendeleza na kutunza viwanja vyetu vya mpira ili vifae kuchezewa mpira wa kisasa. Aidha tunashukuru Halmashauri ya jiji la Tanga kwa kuiipatia TFF miliki ya eneo la ekari 18 jijini Tanga, kwa kushirikiana na FIFA eneo hilo litajengwa kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira cha TFF. Michoro yake  iko katika hatua za mwisho za maandalizi.



5. Maendeleo ya mpira wa miguu.

TFF tumejiwekea malengo mawili makuu: Kucheza fainali za dunia mpira wa miguu wa wanawake Paris mwaka 2019 na kucheza fainali za kombe la dunia wanaume mwaka 2026.

Kwa upande wa mpira wa wanawake katika kufikia azma hii mwaka huu tunaanzisha ligi kuu ya vilabu vya mpira wa wanawake (Tanzania Women Premier League). Kutokana na ligi hii vipaji vitaibuliwa kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu yetu ya Taifa Twiga stars. Kikosi hiki mwakani kitakuwa kikikusanywa mara kwa mara, kufanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki  za kimataifa ili kujiandaa na hatua za awali za kombe la dunia mwaka 2018.



Kwa upande wa maandalizi ya Taifa stars kuelekea mwaka 2026 tayari program yetu imeanza kwa kuwa na Serengeti Boys ambayo inapambana kucheza fainali za vijana za Afrika mwakani umri chini ya miaka 17. Kwa sasa kikosi hiki kiko kambini Seychelles kujiandaa na mechi dhidi ya Kongo tarehe 18 Septemba . Timu hii pia ndiyo itapambana kucheza fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 20 mwaka 2019. Aidha kwenye shule ya Alliance huko Mwanza tayari tuna kikosi cha awali cha timu ya  Taifa cha vijana umri chini ya miaka 15 ambacho kinaandaliwa kucheza fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tanzania tutakuwa wenyeji wa fainali hizi kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu.



Pia mwaka huu tunaanzisha ligi ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20. Kutokana na ligi hii mwakani itaundwa timu ya Taifa ya awali ya vijana  umri chini ya miaka 23 itakayopambana mwaka 2019 kutafuta fursa ya kucheza fainali za Olimpiki  Tokyo mwaka 2020. Kutokana na makundi haya makuu matatu kuanzia mwaka 2021 walimu wetu wa mpira wataweza kuanza kutengeneza kikosi imara cha Taifa stars kuelekea Fainali za Kombe la dunia 2026. Gharama kubwa zinahitajika kugharimia program hizi na tunaomba Serikali na wadau wengine mtushike mkono ili tufikie azma yetu ya kucheza World Cup 2026.



Mheshimiwa Waziri ninaomba nigusie uendeshaji wa ligi yetu kuu na utoaji wa leseni za vilabu.Kama nilivyosema hapo awali Ligi kuu inasimamiwa na bodi ya ligi kwa maelekezo ya kanuni za mashindano kama zinavyopitishwa na kamati ya Utendaji kila mwaka. Mheshimiwa Waziri kinacholiongoza Shirikisho katika uendeshaji wa ligi kuanzia usajili, upangaji wa ratiba,upangaji wa waamuzi na utoaji wa adhabu ni kwa mujibu wa kanuni tulizojiwekea na kauli mbiu ya #fairplay,haki mchezoni.

Ninaomba nieleze pia kuwa kufuatia maagizo ya FIFA sasa tupo hatua za awali za  kutoa leseni kwa vilabu zinazohalalisha vilabu kushiriki katika ligi. Mahitaji makuu ya leseni hizi ni klabu kuwa na menejimenti na kumbukumbu za mahesabu yake ya fedha ,kuwa na maeneo ya kufanyia mazoezi na kucheza mechi,kuwa na program za maendeleo ya mpira wa vijana na mwisho kueleza kinagaubaga nani anamiliki na kuendesha shughuli za kila siku za za klabu (ownership and control). Katika hili la umiliki ni marufuku klabu zaidi ya moja katika ligi moja kumilikiwa na mtu au mamlaka moja. Pia kanuni ya leseni za vilabu ina kipengele cha kipimo cha sifa cha nani anaruhusiwa kumiliki au kuendesha klabu ya mpira wa miguu , mipaka ya mamlaka yake na mahusiano na Shirikisho na mamlaka nyingine za juu zikiwemo Serikali,FIFA,CAF na CECAFA.

Mheshimiwa Waziri, ninaomba nimalizie kwa kukushukuru tena kwa kuchukua muda wako kuwa na sisi leo. Familia ya mpira wa miguu Tanzania inafarijika sana unapokuwa karibu na sisi na tunaahidi kuendelea kudumisha nidhamu katika utendaji wetu na kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali yetu, vyombo na mamlaka nyingine.

Ahsante na ubarikiwe sana.

AFRICAN LYON KUKIPIGA NA MBAO FC LEO



African Lyon ya Dar es Salaam kesho Septemba 12, 2016 itaikaribisha Mbao FC kwenye mchezo Mchezo huo Na. 28 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaofanyika Uwanja wa Uhuru jijini. 

Mara baada ya mechi hiyo, raundi ya tano itafanyika mwishoni mwa wiki ijayo kadiri ya ratiba.

TFF YAWALILIA WALIOKUFA NA KUJERUHIWA KWA TETEMEKO LA ARDHI



Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameshitushwa na taarifa za tukio la tetemeko kubwa ardhi lenye mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7 lililotokea jana Septemba 10, 2016 katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa kadhalika nchi za Burundi na Uganda.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa iliyopata athari kwa mujibu wa taarifa ni Mwanza, Mara na Kagera nchini na kuripotiwa kuua zaidi ya watu 10 na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa sambamba na kubomoa majengo mbalimbali.

Rais Malinzi mara moja anaungana na Serikali katika kusubiri tathmini na kisha kuangalia namna TFF itakavyoweza kusaidia kama sehemu ya wadau katika jamii. TFF inaamini kuwa baadhi ya waliopata maafa ni familia ya mpira wa miguu si ndani tu ya nchi, bali pia nje ya mipaka ya Tanzania.

Hivyo, Rais Malinzi ametutuma salamu za rambirambi kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki na anawaombea marehemu wapumzishwe mahali pema peponi. Amina. Na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Katika salamu hizo, pia Rais Malinzi amemtumia Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Burundi (BFF), Marlon Kuylen kwa sababu sehemu ya Bujumbura imeguswa na tetemeko hilo kadhalika ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Moses Magogo baada ya ripoti kuonesha kuwa tetemeko hilo limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda. Wataalamu wa elimu ya miamba – Jiolojia wanasema kwamba lilikuwa ni kubwa kwa mujibu wa vipimo.

Saturday, September 10, 2016

KOCHA SIANG’A ALIYEIFIKISHA SIMBA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2003 AFARIKI DUNIA


Na Mwandishi Wetu, NAIROBI
KOCHA aliyeiwezeha Simba SC kuitoa Zamalek ya Misri na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Mkenya James Aggrey Siang’a amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Sianga, ambaye nchini Tanzania alizifundisha pia Mtibwa Sugar na Moro United za Morogoro, amefariki dunia usiku wa Saa 6 jana katika hospitali ya Bungoma baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kiongozi wa Kefoca, Bob Oyugi amethibitisha habari za kifo cha Siang’a, ambaye enzi zake alidakia klabu za Gor Mahia, Luo Union na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.
James Siang’a (kulia) akipongezwa na mfadhili wa Simba, Mohamed Dewji mwaka 2003 
“Tumempoteza mtu wetu sana, Siang’a. Mchezaji wa zamani wa kimataifa amefariki ijumaa usiku kwa mujibu wa familia yake. Tunasubiri taarifa zaidi kutoka kwao ili kuendelea na hatua nyingine. Mwili wake upumzishwe kwa amani,” alisema Oyugi.
Siang’a aliidakia Kenya katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1972 na pia alikuwa kocha wa Harambee Stars mwaka 1999 na 2000, kabla ya kuhamia Tanzania kufundisha Simba, Mtibwa Sugar, Moro United na timu ya taifa ya Bara kwa muda mfupi mwaka 2002.
Amefundisha pia Express ya Uganda na Gor Mahia ya kwao baada ya kuondoka Tanzania.
Kwa Tanzania, mashabiki wa Simba SC watamkumbuka zaidi Sianga baada ya kuipa timu taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati visiwani Zanzibar mwaka 2002, kabla ya kuunda kikosi imara cha vijana wadogo kilichokuwa tishio katika soka ya Tanzania muongo wote huo.
Kikosi hicho kilikuwa kikiundwa na vijana kama Said Swedi, Ramazani Wasso, Boniface Pawasa, Victor Costa, Lubigisa Madata, Suleiman Matola, Primus Kasonzo, Christopher Alex, Shekhan Rashid, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Gabriel na Athumani Machuppa. 
Akiwa na vijana hao, Siang’a aliiwezesha Simba SC kuitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa wa Afrika katika hatua ya 16 Bora na kwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Sianga alizitoa BDF XI ya Botswana, Santos ya Afrika Kusini kabla ya Zamalek. Santos aliitoa kwa penalti 9-8 baada ya sare ya jumla 0-0 na Zamalek pia aliitoa kwa penaliti 3-2, baada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
Simba ikapangwa Kundi A pamoja na Ismailia ya Misri, Enyimba ya Nigeria na ASEC ya Ivory Coast na ikafanikiwa kushinda mchi mbili na kutoa sare moja.
Ilishinda 1-0 dhidi ya ASEC, 2-1 dhidi ya Enyimba na sare ya 0-0 na Ismailia katika mechi za nyumbani Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru), Dar es Salaam.
Katika mechi za ugenini, Simba SC ilifungwa 3-0 na Enyimba, 2-1 na Ismaili na 4-3 na ASEC.
Kituko kikubwa cha kukumbukwa cha Siang’a ni pale alipompiga kichwa aliyekuwa kocha wa SC Villa, Mserbia Milutin Sredejevic ‘Micho’ kwenye fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Simba SC ikilala 1-0 Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda.
Micho alikwenda kwenye benchi la Simba kumsalimia Siang’a aliyekuwa ana hasira za kipigo na kukosa Kombe na pia akilalamikia bao la Mkenya mwenzake, Vincent Tendwa aliyemalizia krosi ya kiungo Mtanzania, Shaaban Kisiga ‘Malone’ lilikuwa la kuotea – lakini akaambulia ‘ndoo’.
Kabla ya Micho kujibu, wawili hao wakatenganishwa na sherehe za ubingwa zikachukua nafasi yake Namboole.
Baada ya kuondoka Simba alifichua mpango wa kufuatwa na kiongozi mmoja wa klabu wakati huo kumshawishi wapokee hongo ya Zamalek timu ifungwe mwaka 2003.
Siang’a alidai alikataa na akaiongoza Simba kuitoa Zamalek, lakini kilichofuatwa ni kufukuzwa kwenye timu kwa chuki za kiongozi huyo mwenye asili ya Kiasia.
Mungu ampumzishe kwa amani gwiji huyo wa soka Kenya.
CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY

YANGA, AZAM ZAVUNA POINTI TATU LIGI KUU, LEO NI SIMBA NA MTIBWA


YANGA imeendelea kung'ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Majimaji mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Amis Tambwe aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Bao lingine lilifungwa na kiungo Deus Kaseke.

Kwa ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, ambapo imeshinda mbili, imetoka sare moja, kama ilivyo kwa timu kongwe ya Simba.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Azam ilitoka uwanjani na ushindi baada ya kuibugiza Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Ushindi huo uliiwezesha Azam kushinda mechi zote mbili ilizocheza Mbeya baada ya wiki iliyopita kuilaza Prisons bao 1-0 kwenye uwanja huo.

Kutokana na ushindi huo, Azam imeendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo, ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi nne wakati Mbeya City inazo pointi saba.

Mabao ya Azam yalifungwa na Khamis Mcha na Gonazo Thomas. Bao la Mbeya City lilifungwa na Rafael Daudi.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa juzi, Ruvu Shooting iliwalaza maafande wenzao wa JKT kwa bao 1-0, Mwadui ilitoka sare ya mabao 2-2 na majirani zao wa Stand United wakati Ndanda FC na Kagera Sugar zilitoka suluhu.

Friday, September 9, 2016

YANGA WENYEJI WA MAJIMAJI, AZAM KUKIPIGA NA MBEYA CITY KESHO


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho kwa michezo mitano ya Mzunguko wa Nne.

Miongoni mwa michezo hiyo, itakuwa ni ile ya upinzani wa jadi kati ya JKT Ruvu itakayokaribishwa na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Mwadui itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Mbali ya michezo hiyo, pia Young Africans itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, wakati Azam FC ambayo itakuwa mgeni tena kwenye Uwanja wa Sokoine ikicheza na Mbeya City na kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Ndanda itaikaribisha Kagera Sugar ya Kagera.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili Septemba 11, 2016 kwa Simba kuikaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, lakini uliokuwa uzikutanishe timu za African Lyon na Mbao hapo kesho umesogezwa mbele hadi Jumatatu Septemba 12, 2016. Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Uhuru baada ya African Lyon kubadili uwanja kutoka Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

KILIMANJARO QUEENS WAENDA UGANDA KUSHIRIKI KOMBE LA CHALENJI



Baada ya jana Septemba 8, 2016 kuilaza Burundi kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa, Timu ya Mpira wa Miguu ya Taifa ya wanawake wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’, inatarajiwa kuondoka leo kwenda Jinja, Uganda kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) maarufu kama Kombe la CECAFA itafanyika kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016.

Burundi pia inakwenda Uganda ambako imepangwa makundi tofauti katika michuano hiyo. Tanzania kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda,.

Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.

Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza na Uganda. Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.

Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.

Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa safari ya Uganda.

KOCHA MOHAMMED MSOMALI AZIKWA

Kocha na mchezaji mahiri wa zamani wa Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mohammed Msomali amezikwa leo Septemba 9, 2016 kwenye makaburi ya Kola yaliopo barabara ya zamani ya Dar es Salaam-Morogoro.

Mbali ya wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) waliohudhuria mazishi hayo kwa upande wa TFF iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi katika maziko hayo ya Msomali aliyefikwa na umauti akiwa na umri wa miaka 74.

Kocha Mohammed Msomali anaelezwa kuwa ‘gwiji’ la kandanda la Tanzania, alifariki dunia jana Septemba 08, 2016 saa saba mchana akiwa nyumbani kwake akisubiri kupata mlo wa mchana.

Katika nafasi ya kucheza, historia inaonesha kuwa Msomali nyota yake ilianza kuonekana kwenye timu mahiri ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam kabla ya kuchezea klabu nyingine za Young Africans pia ya Dar es Salaam, Mseto ya Morogoro, Timu ya Mkoa wa Morogoro ‘Moro Stars’ na Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kadhalika timu ya Bara ambayo ni maarufu kwa jina la Kilimanjaro Stars.

Wakati wa uhai wake, Msomali amepata kuzifundisha Mseto na Tumbaku za Morogoro ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Klabu Bingwa Tanzania) mwaka 1975. Pia alizinoa Young Africans, Timu ya Mkoa wa Morogoro ‘Moro Stars’ na kwa muda mrefu timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ sambamba na ile ya Bara ambayo ni maarufu kwa jina la Kilimanjaro Stars.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Mohammed Msomali mahala pema peponi.

KOZI YA MPIRA WA MIGUUNYAFUNGWA


Kozi ya makocha wa Mpira wa Miguu imefungwa leo Septemba 9, 2016 saa 5.00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Hosteli ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine ndiye aliyefunga kozi hiyo ambako pamoja na mambo mengine, alitoa shukrani za pekee kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) akisema: “Tunajivunia kwa upendeleo huu, bila shaka ni kwa sababu hata wanafunzi wanaofanya kozi hii, wanafanya vema.”

Mwesigwa amesema kuendelea kutolewa kwa kozi hiyo ni nafasi ya pekee kwa maendeleo ya soka hasa la wanawake hapa nchini.

Akijibu risala la wahitimu wa kozi hiyo ambayo ililenga kuonyesha changamoto ya vifaa vya kufundishia kama vile mipira, vifaa, koni, jezi na filimbi Katibu Mkuu Mwesigwa anasema pia TFF imebanwa na ushuru wa kukomboa vifaa mbalimbali vya maendeleo ya soka bandarini, lakini akaonyesha imani na Serikali ambayo itasaidia.

“Muundo wa kodi pia ni changamoto kwetu,” amesema Mwesigwa na kuondelea: “Kama vifaa kama hivyo mlivyovaa gharama yake ni kubwa, lakini kama ushuru utaondolewa basi tutaendeleza soka na pengine washiriki wanaweza kuwa wengi zaidi ya ninyi.”

Mwesigwa amesema kwamba huu ni mwanzo mzuri wa kuelekea kuwa na benchi la ufundi la wanawake litakalokuwa na makocha wanawake tupu au pengine kuwa na mchanganyiko hata kwenye timu ya wakubwa.

Awali, Mkufunzi wa kozi hiyo ya FIFA, Andrea Rodebaugh Huimon kutoka Mexico alisifu darasa lake la watu 30 ambalo lilipata vyeti vya FIFA akisema: “Lilikuwa zuri na litafika mbali kwa kuwa walikuwa wasikivu, wanaofuata wakati na kushiriki mazoezi vema. Ujumbe huu naupeleka FIFA.”

NAPE KUKUTANA NA VIONGOZI WA TFF KESHO


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye (MB) kesho Jumamosi Septemba 10, anatarajiwa kutembelea Ofisi za Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), zilizoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ulioko kwenye makutano ya barabara za Uhuru na Shaurimoyo, Ilala jijini Dar es Salaam.

 Akiwa TFF kuanzia saa 4.30 asubuhi, Waziri Nape atazungumza na Mwenyeji wake Rais wa Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji pamoja na Sekretarieti kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari ambao TFF imeawaalika katika ziara hiyo.

Katika ratiba hiyo, Nape ataonyeshwa maendeleo ya michezo hususani mashindano yanayodhaminiwa na Kampuni ya Airtel na kuratibiwa na TFF ambako kwa mikoa mbalimbali iliyofanya vema, kesho timu za wanawake na wanaume zitacheza hatua ya nusu fainali kabla ya fainali za Jumapili ambazo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Thursday, September 8, 2016

SIMBA, AZAM ZATAKATA LIGI KUU, AZAM YABANWA

BAO lililofungwa na mshambuliaji, Laudit Mavugo katika kipindi cha pili jana liliiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mavugo, mshambuliaji wa kimataifa kutoka Burundi, alifunga bao hilo dakika tatu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, baada ya kumalizia pasi maridhawa kutoka kwa Ibrahim Ajib.

Katika mechi hiyo ya kwanza ya ligi kuchezwa kwenye uwanja huo, baada ya kukarabatiwa na kukabidhiwa kwa serikali, Ruvu Shooting ilikuwa ya kwanza kupata bao.

Bao hilo lilifungwa na Abdulraman Mussa dakika ya saba, baada ya mabeki wa Simba kuzembea kuokoa mpira uliopigwa na Fully Maganga.

Simba ilisawazisha dakika ya 11 kwa bao lililofungwa na Ajib, akimalizia krosi kutoka kwa beki wa kushoto, Mohamed Hussein 'Tshabalala'. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo ya kusisimua, Simba ingeweza kutoka uwanjani na ushindi mkubwa wa mabao, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake, Ajib, Shiza Kichuya na  Mavugo ulikuwa kikwazo.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga walishindwa kutambe mbele ya Ndanda FC baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Wakati huo huo, Azam FC jana iling'ara ugenini baada ya kuichapa Prisons bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Bao pekee na la ushindi la Azam lilipachikwa wavuni na Kipre Balou katika kipindi cha pili.

Monday, September 5, 2016

STARS YAPIGWA 1-0 NA NIGERIA

HATIMAYE timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, imetupwa nje ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika, baada ya kuchapwa bao 1-0 na Nigeria.

Mechi hiyo ya kundi G, iliyochezwa jana kwenye uwanja wa Uyo, Akwa Ibom, ilikuwa ya kukamilisha ratiba kwa timu zote mbili, huku Nigeria ikiwa imeshika nafasi ya pili.

Bao pekee na la ushindi la Nigeria, lilifungwa na mshambuliaji wa Manchester City, Kelechi Iheanacho, dakika ya 78.

Kipa Aisha Manula aliibuka kuwa shujaa wa Taifa Stars kutokana na kuokoa mipira mingi ya hatari iliyoelekezwa kwenye lango lake.

Kutokana na kipigo hicho, Stars imemaliza mechi za kundi hilo ikiwa mkiani, kutokana na kuambulia pointi moja, huku Misri ikiwa imeshika usukani na kufuzu kucheza fainali hizo.

Friday, September 2, 2016

TAIFA STARS YAWASILI SALAMA NIGERIA



KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, kimewasili salama mjini Abuja kwa ajili ya mechi yake ya michuano ya Afrika dhidi ya Nigeria.

Kikosi hicho kilichoondoka juzi, kilitua mjini Abuja usiku wa manane na kupokewa na wenyeji wao, Chama cha Soka cha Nigeria.
 
Sentahafu wa Young Africans, Kelvin Yondani si miongoni mwa wachezaji 18 walioondoka  kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).

Taarifa ambazo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezipata ni kwamba Yondani ana matatizo ya kifamilia ambako hajayaweka sawa hadi timu hiyo inaondoka kwenda Nigeria na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa hajajaza nafasi hiyo.

 Mkwasa amekerwa na kitendo hicho, lakini TFF itasubiri ripoti ya kocha huyo mara baada ya kurejea kutoka Nigeria.

Timu hiyo imeondoka na wachezaji 18 huku ikitarajiwa kuungana na na Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta nchini Nigeria. Samatta - Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya Genk ya Ubelgiji anatokea jijini Brussels ambako makocha wake wamemwomba Mkwasa na Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba kumwangalia namna ya kumtumia kwa sababu ya uchovu wa mechi nzito zilizoipa matokeo mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya Uropa Ndogo.

Taifa Stars inakwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles utakaofanyika Septemba 3, 2016.

Licha ya mchezo huo kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kwa fainali hizo kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.

Wachezaji waliosafiri ni:
Makipa-
Said Kipao – JKT Ruvu
Aishi Manula – Azam FC

Mabeki
Vicent Andrew - Young Africans
Mwinyi Haji - Young Africans
Mohamed Hussein – Simba SC
Shomari Kapombe - Azam FC
David Mwantika - Azam FC

Viungo
Himid Mao - Azam FC
Shiza Kichuya – Simba SC
Ibrahim Jeba – Mtibwa Sugar
Jonas Mkude – Simba SC
Muzamiru Yassin – Simba SC
Juma Mahadhi - Young Africans
Farid Mussa Tenerif ya Hispania

Washambuliaji
Jamal Mnyate – Simba
Simon Msuva - Young Africans
Ibrahim Ajib – Simba SC
John Bocco - Azam FC
Mbwana Samatta –KRC Genk ya Ubelgiji

Viongozi waliosafiri na timu hiyo ni:
Ahmed Mgoyi - Mkuu wa msafara
Charles Boniface Mkwasa- Kocha Mkuu
Hemedi Morocco – Kocha Msaidizi
Hussein Swedi – Mtunza Vifaa
Richard Yomba – Daktari wa timu

TFF YAANDAA SEMINA KWA KLABU ZA WANAWAKE


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeandaa semina elekezi kwa klabu za Ligi Kuu za wanawake inayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.

Semina hiyo kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo, itafanyika Jumamosi Septemba 3, 2016 kwenye Ukumbi wa Hosteli za TFF zilizopo ofisi za Makao Makuu ya shirikisho hilo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, makutano ya barabara za Shaurimoyo na Uhuru jijini Dar es Salaam.

Ligi hiyo ya wanawake ni ya kwanza kufanyika nchini chini ya uongozi wa Rais Jamal Malinzi kwani kablaya hapo hapakuwa na ligi inayohusisha mikoa mbalimbali. 

Shukrani za pekee ziende kwa Kituo cha Televisheni cha Azam, kilichoamua kudhamini ligi hiyo pamoja na ile ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.

TFF imeandaa semina hiyo kwa ajili ya kuwapa maelekezo kuhusu kanuni za ligi, usajili wa timu na taratibu nyingine za ligi hiyo ikiwa ni pamoja na sheria za mpira wa miguu ambazo zimekuwa na marekebisho kwa msimu wa 2016/2017 kama zilivyotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
 
Timu shiriki katika ligi ni Viva Queens ya Mtwara, Fair Play FC ya Tanga, Panama FC ya Iringa, Mlandizi Queens ya Pwani, Marsh Academy ya Mwanza, Baobao Queens ya Dodoma, Majengo Queens ya Singida, Kigoma Sisters FC ya Kigoma, Kagera Queen pamoja na JKT Queens, Mburahati Queens na Evergreen Queens za Dar s Salaam.

NKOMA KUINOA KILIMANJARO QUEENS ITAKAYOCHEZA KOMBE LA CHALENJI


Shirikisho la Mpira Miguu Tanzania (TFF) limemteua Sebastian Nkoma kuwa Kocha Mkuu wa timu ya soka taifa ya wanawake wa Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Queens ambayo kwa mara ya kwanza inakwenda kushiriki mashindano ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016 jijini Jinja, Uganda.

Uteuzi huo wa Nkoma unakwenda sambamba na wasaidizi wake, ambao ni Hilda Masanche na Edna Lema wakati Meneja wa timu hiyo, Furaha Francis. Mtunza vifaa ni Esther Chabruma maarufu kwa jina la Lunyamila.

Kabla ya uteuzi huo, Nkoma alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Mpira wa Miguu ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambayo kwa sasa ipo kambi ndogo ya kwenye hosteli za TFF kujiandaa na kambi kubwa itakayofanyika Shelisheli kabla ya kuivaa Congo – Brazzaville kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo. Fainali hizo zitapigwa Aprili mwakani, nchini Madagascar.

Kilimanjaro Queens inatarajiwa kuanza mazoezi ya leo, Septemba mosi, 2016 ambako wachezaji watakuwa wanakwenda mazoezini Uwanja wa Karume, Ilala  na kurudi nyumbani hadi Jumapili ambako Jumatatu itasafiri kwenda Uganda kupitia Bukoba mkoani Kagera itakakoweka kambi tena ya siku nne. Septemba 8, mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi ambayo pia itakuwa njiani kwenda Uganda kwenye mashindano hayo yanayoratibiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Kwa mujibu wa CECAFA, michuano hiyo itafanyika jijini Jinja na Tanzania ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa nchi za Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda,.

Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.

Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza na Uganda. Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.

Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.

Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa safari ya Uganda.

MALINZI AMTUMIA SALAMU RAIS MPYA WA SOKA MISRI



Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za pongeza kwa Hani Abou-Reida kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais Mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Misri (EFA) katika uchaguzu mkuu uliofanyika juzi Jumanne Agosti 30, 2016 jijini Cairo.

Katika salamu zake, Rais Malinzi ameelezea kuwa kuchaguliwa kwa Hani Abou-Reida katika wadhifa huo ni kilelelezo cha familia ya mpira wa miguu ya Misri kuona umuhimu wake katika kutumikia shirikishi hilo sambamba na kuwa mwakilishi FIFA.

Rais Malinzi amesema ana imani na Abou-Reida kuwa ataweza kutumikia vema nafasi hiyo sambamba na kutumikia wadhifa wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Abou-Reida (63) ni mjumbe wa FIFA kutoka Kanda ya Afrika Kaskazini tangu mwaka 2009 na sasa ataongoza shirikisho la EFA kwa awamu ya kwanza kwa miaka minne ijayo akichukua nafasi ya Galam Allam aliyeongoza EFA tangu mwaka 2012.

Katika uchaguzi huo, wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa EFA waliochaguliwa ni pamoja na wale wenye majina maarufu kama vile Hazem Emam ambaye alikuwa nyota mahiri wa klabu ya Zamalek sambamba na kiungo mkabaji mahiri wa zamani wa klabu ya Al- Ahly. Nyota hao pia walipata kuchezea timu ya taifa maarufu kwa jina la Pharaohs.

Pia wamo Sahar El-Hawary, Hazem El-Hawary, Karam Kordi, Khaled Latif, Seif Zaher, Mohammed Aboud El-Wafa, Ahmed Megahed a Essam Abdel-Fatah.

FIFA YATOA WARAKA MPYA WA USAJILI WA WACHEZAJI



Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), limesambaza waraka mpya kwa wanachama wake, likiwamo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ukisema mameneja wote wa usajili wa wachezaji kwa mfumo wa Mtandao (TMS-Transfer Matching System Managers) hawana budi kujiunga na mawasiliano mapya ili kupata taarifa mbalimbali za usajili na uhamisho wa wachezaji.

FIFA limeleta mfumo huo unaoitwa GPX yaani Global Players Exchange ambao malengo yake ni kurahisisha kufanya usajili kwa mchezaji mmoja kwenda timu nyingine lakini kabla ya kufanya hivyo utasaidia kupata taarifa kamili za mchezaji huyo na shabaha kuu ni kurahisisha mawasiliano ya TMS Managers nchi nzima, klabu na mashirikisho mbalimbali duniani.

GPX ni kama mtandao wa kijamii unaoweza kulinganishwa na ‘WhatsApp’ unaofanya kuwa na mawasiliano ya karibu na FIFA imeagiza kuwa ni lazima mameneja wa TMS wa kila klabu na mashirikisho ya ya mpira wa miguu kujiunga na mtandao huo ambao si tu kwamba utafanya kazi katika nchi husika, bali pia unaunganisha ulimwengu wote.

Kwa mameneja wa usajili wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (SFDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) watakaokuwa tayari basi hawana budi kuwasiliana na Meneja Usajili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupata maelezo ya kina ya namna ya kujiunga na mtandao wa GPX.

Thursday, September 1, 2016

YONDANI AMCHEFUA MKWASA, SAMATTA KUUNGANA NA STARS IFIKAPO NIGERIA



KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Charles Boniface, ameelezea kuchukizwa kwake na kitendo cha beki Kevin Yondani wa Yanga kushindwa kuripoti kwenye kambi ya timu hiyo.

Yondani amegoma kuripoti kwenye kambi ya Taifa Stars,inayojiandaa kwa mchezo wake wa michuano ya Afrika dhidi ya Nigeria.

Akizungumza na waandishi  wa habari jana, Boniface alisema ameshangazwa na ukimya wa Yondani, ambaye hajatoa taarifa yoyote kuhusu kushindwa kwake kuripoti kambini.

Boniface alisema amejaribu kumpigia simu Yondani kwa siku mbili,lakini hakufanikiwa kumpata.

Taifa Stars iliondoka nchini jana usiku kwenda Nigeria, ambako itacheza na timu ya taifa ya nchi hiyo Jumamosi.

Mechi hiyo itakuwa ya kukamilisha ratiba kwa Taifa Stars kwa vile imeshatolewa.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta anatarajiwa kuungana na timu hiyo nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).

Hadi mchana wa leo Agosti  29, 2016 ni Kelvin Yondan pekee kutoka Young Africans ambaye hakuripoti kwenye kikosi hicho kilichopiga kambi yake kwenye Hoteli ya Urban Rose iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam. Kipa mpya wa timu hiyo, Said Kipao alijiunga na timu hiyo mara moja baada ya kuteuliwa na Kocha Mkuu, Charles Boniface Mkwasa.

Taifa Stars inatarajiwa kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles utakaofanyika Septemba 3, 2016. Licha ya mchezo huo kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.

TFF YATHIBITISHA KUSHIRIKI CHALENJI YA WANAWAKE




Shirikisho la Mpira Miguu Tanzania (TFF) limethibitisha kwa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kuwa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania itashiriki michuano ya kwanza ya Kombe la Chalenji kwa wanawake itakayofanyika kuanzia Septemba 11, 2016 hadi Septemba 20, 2016 kwa kushirikisha nchi saba wanachama wa shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa CECAFA, michuano hiyo itafanyika jijini Jinja na Tanzania ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa nchi za Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda.

Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.

Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza na Uganda. Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.

Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.

Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Tanzania inatarajiwa kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa safari ya Uganda.

MAAMUZI YA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI



Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji Jumapili ya Septemba 4, 2016 inatarajiwa kutoa hukumu ya shauri la mchezaji Hassan Ramadhan Kessy anayedaiwa na Klabu ya Simba kuvunja mkataba kwa kuanza kufanya mazoezi na klabu ya Young Africans sambamba na kusajili katika timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam kabla ya mkataba wake kufika mwisho Juni 15, 2016.

Simba imelalamika mbele ya kamati hiyo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa, mchezaji Hassan Kessy alivunja taratibu hizo akiwa ndani ya mkataba wa klabu hiyo yenye mashakani yake Barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati hiyo, shauri hilo lilisikilizwa na uamuzi wake utatolewa Jumapili ijayo. Hii ni baada ya kushindikana kusikilizwa kwa shauri jingine linalohusu Klabu Simba ikiilalamikia Klabu Young Africans, kuingia mkataba na mchezaji Hassan Ramadhani Kessy wakati bado ana mkataba na klabu Simba.

Shauri la Simba dhidi ya Young Africans lilishindika kusikilizwa kwa sababu Young Africans hawakutokea mbele ya kamati hiyo wakati wa kusikiliza shauri hilo, hivyo kamati itaiandikia barua Young Africans kukumbushwa kuhudhuria kwenye kesi hiyo Jumapili ijayo kabla ya kutolewa uamuzi. Kama hawakutokea tena, shauri hilo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.

Katika mashauri mengine,

Mathias Lule v Stand United

Malalamiko ya Kocha Mathias Lule. Lule anadai mshahara, usajili na bima ya matibabu kwa Stand United. Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

Ametre Richard v Simba

Madai ya malimbikizo ya mishahara kwa Ametre Richard dhidi ya Simba. Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamekubaliana kukutana Jumatano Agosti 31, 2016 na kuleta yatokanayo TFF.

Wachezaji watatu v Mbeya City

Kamati umeamua kuwa Mbeya City ya Mbeya iwalipe wachezaji wake wa zamani, Abdallah Juma, Temi Felix na Erick Mawala madai yote ya malimbikizo ya mshahara na fedha za usajili.

Kinondoni Sports Academy (KISA) v klabu 5 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara

 (i)           KISA inadai fidia za malezi kwa Azam baada ya kumsajili mchezaji Omary Maunda, ambako Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

(ii)         KISA inadai fidia za malezi kwa Kagera Sugar baada ya kumsajili mchezaji Hussein Abdallah, ambako Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

 (iii)       KISA inadai fidia za malezi kwa Mtibwa Sugar baada ya kumsajili mchezaji Daniel Jemedari, ambako Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

 (iv)        KISA inadai fidia za malezi kwa Majimaji ya Songea baada ya kumsajili mchezaji Joseph Njovu. Shauri hili sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdaiwa Majimaji kutotokea kwenye kesi. Majimaji wameagizwa kukuhudhuria shauri hilo vinginevyo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.

(v)          KISA inadai fidia za malezi kwa Toto African ya Mwanza baada ya kumsajili mchezaji Jafari M. Jafari, ambako Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

(vi)        KISA inadai fidia za malezi kwa JKT Ruvu ya Pwani baada ya kumsajili mchezaji Najimu Maguru, ambako Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

 SPUTANZA v Young Africans

Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA), kilileta malalamiko dhidi ya Young Africans kuhusu madai ya usajili wa Jerry Tegete, Omega Seme na Hamisi Thabiti. Shauri hili sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdaiwa Young Africans kutotokea kwenye kesi. Young Africans wameagizwa kukuhudhuria shauri hilo vinginevyo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.

Coastal Union v Simba SC

Coastal Union ilileta malalamiko dhidi ya Simba Sports Club kuhusu madai ya fidia ya wachezaji Ibrahim Shekwe, Hemed Hamisi na Abdi Banda. Imeamuriwa kuwa Simba iilipe mara moja Coastal Union fidia ya shilingi milioni tano.

Coastal Union v Kagera Sugar
Coastal Union ilileta malalamiko dhidi ya Kagera Sugar kuhusu madai ya fidia ya mchezaji Ibrahim Sheku. Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

Coastal Union v Mbeya City

Coastal Union ilileta malalamiko dhidi ya Mbeya City kuhusu madai ya fidia ya wachezaji Fikirini Bakari na Ayub Yahaya. Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

Coastal Union v Young Africans

Coastal Union ilileta malalamiko dhidi ya Young Africans kuhusu madai ya fidia ya mchezaji Juma Mahadhi. Shauri hili sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdaiwa Young Africans kutotokea kwenye kesi. Young Africans wameagizwa vinginevyo kukuhudhuria shauri hilo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.

Coastal Union v JKT Ruvu

Coastal Union ilileta malalamiko dhidi ya JKT Ruvu kuhusu madai ya fidia ya mchezaji Yusuf Chuma. Shauri hili sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdaiwa JKT Ruvu kutotokea kwenye kesi. JKT Ruvu wameagizwa kukuhudhuria shauri hilo vinginevyo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.

Bakari Shime v Mgambo JKT

Malalamiko ya Kocha Bakari Shime kudai ya mshahara dhidi ya Mgambo JKT. Kamati umeamua kuwa Mgambo JKT imlipe Shime na uongozi wa klabu hiyo umeahidi kumlipa Shime kiasi cha Sh 8,500,000 ndani ya wiki tatu kuanzia tarehe ya uamuzi huu.

Mchezaji Ally Rashid Ally v Simba

Malalamiko ya Mchezaji Ally Rashid Ally kudai kunyimwa stahiki zake na Klabu ya Simba. Shauri hili sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdai Ally Rashid Ally kutotokea kwenye kesi. Ally Rashid Ally ameagizwa kukuhudhuria shauri hilo, vinginevyo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.

Wachezaji Omary Seseme, Said Omary na Edward Christopher v Toto African

Malalamiko ya wachezaji Wachezaji Omary Seseme, Said Omary na Edward Christopher dhidi ya Toto African kudai mishahara na fedha za usajili. Kamati umeamua kuwa Toto African iwalipe wachezaji hao na uongozi wa klabu hiyo umeahidi kumlipa ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe ya uamuzi huu.

Wachezaji Rajab Isihaka na Said Mketo v Ndanda FC

Malalamiko ya wachezaji Rajab Isihaka na Said Mketo v Ndanda FC dhidi ya Ndanda kudai mishahara na fedha za usajili. Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

Simba SC v Mbaraka Mussa Yusufu

Simba ilileta malalamiko dhidi ya Mchezaji Mbaraka Mussa Yusufu kuhusu madai ya utoro kazini. Kamati imeridhia pande mbili kwenda kulimaliza suala hilo nje ya kamati kama ambavyo wameomba. Wamepewa wiki moja kufanya hivyo na na kuleta yatokanayo TFF.

Lipuli FC v Mbeya City

Lipuli ilileta malalamiko dhidi ya Mbeya City kumsajili mchezaji Mackyada Makolo bila kufuata utaratibu. Shauri hili sasa litasikilizwa Jumapili ijayo ya Septemba 4, 2016 baada ya kushindikana kusikilizwa kutokana na mdaiwa Mbeya City kutotokea kwenye kesi. Mbeya City wameagizwa kukuhudhuria shauri hilo vinginevyo litasikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi upande mmoja.

Lipuli v Ruvu JKT

Lipuli ilileta malalamiko dhidi ya JKT Ruvu kumsajili Mchezaji Kassim Kisengo bila kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kutolipa ada ya mkoa na wilaya. Pande zote mbili zilimalizana.