KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, March 15, 2015

YANGA KUDADADEKI! YAWABAMIZA WAZIMBABWE 5-1


YANGA SC imetanguliza mguu mmoja hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ili Yanga isisonge mbele, inabidi ifungwe mabao 4-0 na Platinum katika mchezo wa marudiano wiki ijayo mjini Bulawayo.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Djamaladen Aden Abdi, aliyesaidiwa na Hassan Eguech Yacin na Abdallah Mahamoud Iltireh wote wa Djibouti, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Mabao ya Yanga SC yalifungwa na viungo Salum Abdul Telela ‘Master’ dakika ya 32 na Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ dakika ya 43, wakati bao la Platinum lilifungwa na Walter Musoma dakika ya 45.

Kipindi cha pili, Yanga waliongeza makali na kufanikiwa kupata mabao matatu zaidi, ambayo yanawafanya waende Bulawayo kwenye mchezo wa marudiano, wakiwa wana kazi ndogo tu.

Mabao hayo yalifungwa na Amisi Tambwe dakika ya 47 na Mrisho Ngassa mawili dakika ya 55 na 90.
Mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Simon Msuva alimsetia krosi nzuri Ngassa kufunga bao la tano.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul/Hassan Dilunga, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Salum Telela, Simon Msuva/Kpah Sherman, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe na Said Juma ‘Kizota’.

Platinum FC; Petros Mhari, Raphael Muduviana, Kelvin Moyo, Gift Bello, Thabit Kamusuko, Wellington Kamudyariwa/Simon Shoko, Wisdom Mtasa/Aaron Katege, Brian Muzondiwa, Obrey Ufiwa/Emmanuel Mandiranga, Walter Musoma na Elvis Moyo.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

OKWI AINYONGA MTIBWA SUGAR


BAO la Emmanuel Anord Okwi dakika ya 90 ushei limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Simba SC sasa inafikisha pointi 29 baada ya mechi 18 na kuendelea kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa watetezi, Azam FC pointi 30 za mechi 16 sawa na vinara Yanga SC, wenye pointi 31.

Okwi alifunga bao hilo, wakati tayari baadhi ya wapenzi wa Simba SC wameanza kutoka uwanjani, wakiamni matokeo ni sare.  Mganda huyo, alifunga baada ya kupata pasi ya Abdi Banda na kumchambua vizuri kipa aliyefanya kazi nzuri leo, Said Mohamed Kasarama.

Mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, aliyesaidiwa na Yussuf Sekile wa Ruvuma na Abdallah Rashid wa Pwani, Simba SC ndiyo waliotawala na kutengeneza nafasi nyingi, lakini hawakuwa na bahati ya mapema.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi aliiongoza vyema safu ya ushambuliaji ya Mtibwa Sugar akisaidiana na Ame Ally, lakini wakaishia kuisumbua tu ngombe ya Simba, iliyoongozwa na beki chipukizi, Hassan Isihaka.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Said Ndemla, Abdi Banda, Elias Maguri, Emmanuel Okwi na Simon Sserunkuma/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk46.

Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Said Mkopi, Dacis Luhende, Salim Mbonde, Andrew Chikupe, Shaaban Nditi, Ally Sharrif, Henry Joseph, Ame Ally/Mohammed Mkopi dk66, Muzamil Selemba/Ally Yussuf dk86 na Mussa Hassan Mgosi/Vincent Barnabas dk75.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

MKUTANO MKUU TFF WAMALIZIKA SALAMA NA KWA AMANI


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) jana limefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka katika ukumbi wa Morogoro hoteli ya mjini Morogoro ambapo mgeni Rasmi alikua ni mkuu wa mkoa wa Morogoro Dr Rajabu Rutengwe.

Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Dr Rutengwe aliushukuru uongozi wa TFF nchini kwa kuweza kuandaa mkutano mkuu mzuri na wa kisasa ambao pia ulifanyikia katika mkoa wake wa Morogoro.

Akiongea na wajumbe wa mkutano mkuu Dr Rutengwe alisema, TFF ina changamoto ambazo inapaswa kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wa mpira wa miguu nchini kwa ujumla, changamoto hizo ni kukosekana kwa wataalamu wa vyakula, wataalamu wa tiba na wataalamu wa saikolojia.

Dr Rutengwe aliomba TFF kwa kushirikiana na serikali inapaswa kuandaa wataalamu wengi wa masuala hayo ili kuweza kuendana na mahitaji ya kuwaanda wanamichezo bora ambao watakua tayari kwa ushindani na sio ushiriki.

Aidha mkuu wa mkoa huyo aliipongeza Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuupa mkoa wa Morogoro uenyeji wa mkutano mkuu ambapo pia umefanyika na  malengo kufanikiwa kwa asilimia mia moja, na kusema kwa niaba ya serikali ya mkoa wapo tayari kupokea tena mwaliko wa uenyeji wa mikutano mbalimbali ya TFF.

Mkutano ulijadili Ajenda za kawaida ambazo ni Kufungua Mkutano ni Uhakiki wa Wajumbe,  Kuthibitisha Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita, Yatokanayo na Mkutano uliopita, Hotuba ya Rais, ripoti kutoka kwa Wanachama,  Kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji.

Zingine ni Kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013, Kuthibitisha ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu, Kupitisha bajeti ya 2015, Marekebisho ya Katiba,  Mengineyo na  Kufunga Mkutano.
Kwa mara ya kwanza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limepata bendera yake ambayo ilipitishwa na mkutano mkuu na asubuhi ya jumapili Machi 15 mwaka huu, imepandishwa kwa mara ya kwanza Morogoro hoteli.
Aidha wajumbe wa mkutano mkuu pia wamepitisha azimio la kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini (FDF), ambapo kutaundwa kamisheni maalum itakayoshugulikia suala hilo.
Lengo la kamisheni hiyo ni kuisaidia TFF kuandaa na kuratibu mipango ya maendeleo ya soka la watoto, vijana, wanawake nchini na kuviwezesha vyama vya soka vya mikoa (FA), vyama shiriki vya TFF kujiendesha katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya soka la vijana.
Pia mkutano mkuu huo ulitoa azimio la kuitaka serikali itoe msamaha wa kodi kwa vifaa vya michezo hasa vinavyotumika kufundishia watoto michezo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 125 na kati yao wajumbe watano ni wanawake.
Kikao kijacho cha mkutano mkuu kitafanyika kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu.


27 WAITWA TAIFA STARS ITAKAYOIVAA MALAWI


Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars ) Mart Nooj, ametangaza kikosi cha wachezaji 27 watakaoingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi utakaofanyika uwanja wa CCM Kirumba jijin Mwanza Machi 29, 2015.

Taifa Stars inayotarajia kucheza na The Flames mwishoni mwa mwezi huu, itaingia kambini machi 22 machi  katika hotel ya Tansoma kujiandaa na mchezo huo kabla ya kuelekea jijini Mwanza machi 24 kwa maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo.

Wachezaji walioitwa kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo ni; Magolikipa,  Deogratius Munish (Yanga), Aishi Manula na Mwadini Ali (Azam FC), walinzi ni Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris (Azam FC), Mwinyi Haji (KMKM), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Oscar Joshua (Yanga), Abdi Banda na Hassan Isihaka (Simba SC).

Viungo ni Frank Domayo, Salum Abubakar, Amri Kiemba, Mcha Khamis (Azam FC), Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United), washambuliaji Mwinyi Kazimoto (Al Markhiry - Qatar),

Saimon Msuva , Mrisho Ngasa (Yanga), Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta (Tp Mazembe - Congo DR), John Bocco (Azam FC), na Juma Luizio (Zesco United - Zambia)

Timu ya Taifa ya Malawi inatarajiwa kuwasili jijini Mwanza machi 27, 2015 ikiwa na kikosi kamili, wakiwemo wachezaji nane wanaocheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini, Msumbuji, Congo DR na Zimbambwe.

Malawi inashika nafasi ya 91 katika viwango vipya vya FIFA Duniani vilivyotolewa mwezi huu, huku Tanzania ikipanda kwa nafasi saba na kushika nafasi ya 100.

KOCHA SYLVESTER MARSH AAGWA




RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu wa nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za ramirambi kwa familia ya Marsh, kufuatia kifo cha kocha wa Taifa ya vijana Sylvester Marsh kilichotokea jana jijini Dar es salaam.

Katika salam zake kwa familia ya marehemu, Mh. Malinzi amesema familia ya mpira wa miguu
nchini TFF imeshtushwa na msiba huo na kusema Shirikisho na Taifa limempoteza mtu muhimu
katika mpira wa miguu nchini.

Mwili wa marehem Marsh utaagwa leo saa 6 kamili mchana, katika kanisa la Hospital ya Taifa
Muhimbili na kutasafirishwa kuelekea Igoma jijini Mwanza kwa mazishi majira ya saa 8 kamili
mchana kwa basi dogo (coaster) la TFF.

Marsh alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.

Taarifa zinasema Marsh alikuwa amekuja Muhimbili kuhudhuria kliniki yake ya kawaida juu ya
maradhi ya saratani ya koo yaliyokuwa yakimsumbua na ghafla hali yake ikabadilika juzi hadi kufariki
dunia.

Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj
Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa,
akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Wadenmark, Jan Poulsen na Kim
Poulsen.

Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kushinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oktoba
mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Star na Marsh akaondoka pamoja na Kim
Poulsen. Sasa Mholanzi, Mart Nooij ndiye kocha Stars, anasaidiwa na Salum Mayanga.

Tangu hapo Marsh amerudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.

Mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, alimsaidia kocha huyo hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana na kurejea Mwanza.

Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.

Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam.

Miongoni mwa mafanikio yake akiwa kocha, mwaka 2005 aliiwezesha Kagera Sugar kutwaa
Kombe la Tusker, ikiifunga Simba SC katika fainali mabao 2-1 Dar es Salaam.

Mwaka 2004, akiwa Msaidizi wa Kibadeni katika U17, maarufu Serengeti Boys, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Gambia, baada ya kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe.

Hata hivyo, timu hiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji waliogeuka nyota wa taifa kwa miaka 10 iliyopita kama Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Amir Maftah na wengine, ilienguliwa fainali za Gambia kwa kashfa ya kumtumia Nurdin Bakari aliyekuwa amezidi umri.

Mwaka 2009, Marsh akiwa Msaidizi wa Maximo Taifa Stars, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.

Inaelezwa kwa muda wote wa Marsh kufanya kazi na timu za taifa hakuwahi kuwa na Mkataba, bali alikuwa kama ‘deiwaka’ maana yake hakuweka mbele maslahi, bali uzalendo.

Bwana ametoa, bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Mbele yake, nyuma yetu. Mungu ampumzishe kwa amani mwalimu Sylvester Marsh. Amina.


Wednesday, March 11, 2015

MAANDALIZI MKUTANO MKUU WA TFF YANAENDELEA VIZURI, AJENDA ZATAJWA






Maandalizi ya mkutano mkuu wa mwaka wa TFF utakaofanyika mjini Morogoro kati ya Machi 14,15 mwaka huu katika Ukumbi wa Morogoro Hotel yanaendelea vizuri.

 Agenda za mkutano mkuu ni:

1.Kufungua Mkutano
2. Uhakiki wa Wajumbe
3. Kuthibitisha Ajenda.
4. Kuthibitisha Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita.
5. Yatokanayo na Mkutano uliopita.
6. Hotuba ya Rais.
7. Ripoti kutoka kwa Wanachama
8. Kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji.
9. Kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013.
10. Kuthibitisha ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu.
11. Kupitisha bajeti ya 2015
12. Marekebisho ya Katiba
13. Mengineyo
14. Kufunga Mkutano.

TANZANIA KUIVAA MISRI IJUMAA BEACH SOCCER


Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni (Beach Soccer) inatarajiwa kucheza na timu ya Taifa ya Misri siku ya ijumaa majira ya saa 10 kamili jioni, mchezo utakofanyika katika klabu ya Escape 1 Msasani jijini Dar es salaam.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kinaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo, ambapo kwa takribani wiki mbili kipo kambini Bamba Beach wakijifua kwa mchezo huo.

Tanzania ilifuzu hatua ya pili baada ya kuiondoa timu ya Taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 12 -9, na endapo itafanikiwa kuwaota Misri, itafuzu moja kwa moja kucheza Fainali za soka la Ufukweni zitakazofanyika Visiwa vya Shelisheli mwezi April  mwaka huu.

Waamuzi wa mchezo huo ni Eid Haitham Eid Hassan (Sudan), mwamuzi msaidzi wa kwanza  Abaker Mohamed Bilal (Sudan), mwamuzi msaidizi wa pili Abdalla Hassain Hassaballa, mtunza muda (time-keeper) Boubaker Bessem (Tunisia) wakati kamisaa wa mchezo huo ni Khiba Herbert Mohoanyane kutoka Lesotho.

Nayo timu ya Taifa ya Misri inatarajiwa kuwasili Dar es salaam kesho (jumatano) mchana, ambapo itafikia katika hoteli ya Double Tree by Hilton iliyopo Masaki, huku waamuzi wa mchezo huo wakitarajiwa pia kuwasili kesho na kufikia katika hotel ya Protea Oysterbay.

Aidha siku ya alhamis makocha wa timu zote wataongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume kuanzia majira ya saa 5 kamili asubuhi.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini Misri kati ya Machi 20,21 na 22 mwaka huu.

Kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu , Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), inaitakia kila la kheri na ushindi timu ya Taifa ya soka la ufukweni (Beach Soccer) katika huo dhidi ya Misri.
Wakati huo huo michezo miwili ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyokuwa iichezwe kesho (jumatano)  kati ya JKT Ruvu dhidi ya Young Africans katika uwanja wa Taifa, na Mgambo Shooting dhidi ya Azam FC uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga imeahirishwa  na sasa mechi hizo zitapangiwa tarehe nyingine.

SIMBA, YANGA ZAINGIZA MIL 436



Mechi no.117 iliyowakutanisha Simba na Yanga katika uwanja wa Taifa, imeingiza jumla ya sh. milioni 436,756,000 kutokana na idadi ya watazamaji 49,758 waliokata tiketi kushuhudia mchezo huo.

Watazamaji 309 walikata tiketi za VIP A, 1,310 VIP B, 1,533 VIP C, Rangi ya Machungwa (Orange) 9,913 huku viti vya rangi ya bluu na kijani wakiingia watazamaji 36,693.

Mgawanyo wa mapato ya mchezo huo ni VAT 18% sh.66,623.796, FDF timu mwenyeji sh. 17,415,300, FDF TFF sh.7,463,700, Gharama za tiketi sh.11,669,600.

Mgao wa Uwanja sh. 50,037,540.51, Gharama za mchezo sh.28,354,606.29, Bodi ya Ligi (TPLB) sh. 26,686,688.27, TFF sh.20,015,016.20, DRFA sh. 11,675,426.12, klabu ya Simba sh. 115,086,343 huku Yanga wakipata sh.81,727.83.

Wakati huo huo Ligi Kuu ya Vodacom itaendelea kesho siku ya jumanne katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wenyeji timu ya Polisi Morogoro watawakaribisha Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani.

Siku ya jumatano JKT Ruvu watawakaribisha Young Africans katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku jijini Tanga Mgambo Shooting wakiwa wenyeji wa timu ya Azam FC.

Aidha mechi ya Kombe la Shirikisho (CC) barani Afrika kati ya Young Africans dhidi ya timu ya FC Platinum ya Zimbabwe, itafanyika siku ya jumapili Machi 15, 2015 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Monday, March 9, 2015

OKWI APELEKA KILIO JANGWANI


BAO lililofungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi dakika ya 51, jana liliiwezesha Simba kuwatambia watani wao wa jadi Yanga, kwa kuwachapa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Okwi alifunga bao hilo kwa shuti la umbali wa mita zipatazo 25 baada ya kuwazidi mbio mabeki wawili wa Yanga na kumpima kipa Ally Mustafa Barthez, aliyekuwa ametoka langoni.

Ushindi huo umeiwezesha Simba kuendeleza ubabe kwa Yanga katika mechi walizokutana hivi karibuni. Walipokutana mwaka jana katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba iliichapa Yanga mabao 2-0.

Katika mechi hiyo, vijana wa Simba walionyesha soka ya kiwango cha juu hasa dakika za mwisho kutokana na kugongeana pasi nyingi bila wachezaji wa Yanga kugusa mpira.

Washambuliaji Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Amisi Tambwe na Danny Mrwanda walikuwa mwiba katika ngome ya Simba, lakini umaliziaji wao mbovu uliwakosesha mabao.

Yanga ilipata pigo kipindi cha pili baada ya kiungo wake Haruna Niyonzima kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano baada ya kubutua mpira huku mwamuzi akiwa amepuliza filimbi ya kuotea.

Saturday, March 7, 2015

TAIFA STARS KUIVAA MALAWI


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashuka dimbani jumapili Machi 29 mwaka huu, kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mchezo huo wa kirafiki ambao upo katika kalenda ya FIFA kwa timu za Taifa (Machi 23-31) na utatarajiwa kuanza majira ya saa 10 na nusu jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

NKONGO KUCHEZESHA ZESCO Vs AS KALOUM              
Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania mwenye beji ya FIFA, Israel Mjuni Nkongo amechaguliwa kuchezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) kati ya wenyeji Zesco FC ya Zambia dhidi ya AS Kaloum ya Guinea.

Katika mchezo huo wa kwanza wa mzunguko wa pili, Nkongo atasaidiwa na washika kibendera John Kanyenye na Josephat Bulali na mwamuzi wa akiba Waziri Sheha wote kutoka Tanzania, huku Kamisaa wa mchezo akiwa Mayixole Elvin Shishana kutoka nchini Afrika Kusini

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 13,14,15 Machi mwaka huu nchini Zambia.

KUZIONA SIMBA, YANGA KESHO SH.7,000


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa siku ya Jumapili kati ya Simba SC na Young African utakaofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 kamili za jioni.

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, akisaidiwa na Soud Lila (DSM) mshika  kibendera wa kwanza, Florentina Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa pili, Mwamuzi wa akiba Israel Mjuni (DSM), na kamisaa wa mchezo ni Ame Santimeya (DSM).

Viingilio vya mchezo huo,  VIP A sh. 40,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh. 20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya Bluu na Kijani ikiwa ni sh. 7,000.

Tiketi zitaanza kuuzwa keso (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi katika vituo vya,  Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo),  Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).

Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru, barabara ya Chang'ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.

TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.

Aidha katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).

Wednesday, March 4, 2015

SAFARI YA MWISHO YA MAREHEMU KOMBA

JENEZA lenye mwili wa marehemu John Komba likiteremshwa kaburini wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana kijijini kwake Lituhi, Mbinga mkoani Ruvuma
RAIS Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka mchanga kwenye kaburi na marehemu Komba
Mke wa marehemu Komba, Salome Komba (kushoto) akiweka shada la maua kwenye kaburi la mumewe
Watoto wa marehemu Komba wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu baba yao
Watoto wa marehemu Komba wakiweka mashada ya maua kwenye kaburi la maua
Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Komba
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Komba
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Mchemba na Katibu Mwenezi, Nape Nnauye wakiweka shada la maua kaburini
Msanii Khadija Kopa akiwa na majonzi baada ya kuweka shada la maua kwenye kaburi la Komba

Tuesday, March 3, 2015

BEACH SOCCER YAENDELEA KUJIFUA BAMBA BEACH

Timu ya Taifa ya Tanzania ya Sola la Ufukweni (Beach Soccer) iliyoingia kambini mwishoni mwa wiki Bamba Beach Kigamboni, inaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya timu ya Taifa Soka la Ufukweni ya Misri mwishoni wiki ijayo.

Maandalizi ya mchezo dhidi ya timu ya Misri yanaendelea vizuri Bamba Beach Kigamboni chini ya kocha mkuu John Mwansasu ambaye aliingia kambini mwishoni mwa wiki na wachezaji 14.

Mchezo wa kwanza unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya Machi 13 katika klabu ya Escape 1 Msasani jijini  Dar es salaam na marudio yake kufanyika baada ya wiki moja nchini Misri.

Tanzania ilifanikiwa kufuzu hatu ya pili baada ya kuitoa timu ya Taifa ya Kenya kwa jumla ya mabao 12- 9, mchezo wa awali Mombasa Tanzania ilishinda kwa mabao 5-3, na mchezo wa marudiano uliofanyika klabu ya Escape 1 kuibuka na ushindi wa mabao 7-6.

Fainali za Mataifa Afrika kwa Sola la Ufukweni (Beach Soccer) zinatarajiwa kufanyika mwezi April 2015 katika Visiwa vya Shelisheli.

TFF YATUMA SALAM ZA PONGEZI FMF


Rais wa Shrikisho la Mpira wa Miguu nchini –TFF Bw. Jamal Malinzi ametuma salama za pongezi kwa Rais Boubacar Diara wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Mali (FMF) kwa kutwaa Ubingwa wa Afrika kwa vijana U17.

Katika salam zake, Malinzi amesema mafanikio mazuri waliyoyapata  FMF yametokana na uongozi bora, kamati ya utendaji na mipango thabiti waliyoiweka katika soka la Vijana.

Kwa kutwaa Ubingwa wa vijana Afrika U17, Mali wamepata nafasi ya kuliwakilisha Bara la Afrika kwenye fainali za U17 za Dunia nchini Chile pamoja na nchi za Afrika Kusini,Guinea na Nigeria.

Mali wametwaa Ubingwa wa vijana Afrika U17 baada ya kuifunga timu ya taifa ya vijana ya Afrika Kusini (Amajimbo's) kwa mabao 2-0.

Kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu , Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), watanzania wanawapa pongezi  Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Mali (FMF) wa kutwaa Ubingwa huo.

Aidha Rais Malizi pia ametuma salam za pongezi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Afrika Kusini (SAFA) Bw. Dany Jordaan kwa timu ya Amajimbo's kushika nafasi ya pili.

Amajimbo's ndio timu pekee kusini mwa Bara la Afrika watakaowaklisha kwenye fainali za U17 za Dunia nchini Chile.
 

UJENZI RUKWA, VOLCANO FC ZASHUSHWA DARAJA

Timu za Ujenzi Rukwa na Volcano FC ya Morogoro zimeshushwa madaraja mawili hadi ligi za wilaya baada ya kushindwa kufika uwanjani kwenye mechi zao za Ligi Daraja la Pili (SDL).

Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za matukio mbalimbali ya ligi hiyo.

Ujenzi Rukwa ilishindwa kwenda Kigoma kuikabili Mvuvumwa FC ya huko wakati Volcano FC haikutokea kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo ilitakiwa kucheza na Wenda FC.

Uamuzi wa Kamati ya Mashindano umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 27 ya SDL ambapo mbali ya kushushwa madaraja mawili, lakini pia timu hizo zimepigwa faini ya sh. milioni moja kila moja. Vilevile matokeo yote ya mechi zao kwenye Ligi hiyo yamefutwa.

Nayo Singida United imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Ujenzi Rukwa kubainika kumchezesha mchezaji asiyestahili (non qualified) kwenye mechi iliofanyika Februari 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Mchezaji Emmanuel Elias Mseja wa Mbao FC amepigwa faini ya sh. 100,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya kukojoa uwanjani kwenye mechi dhidi ya AFC iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

 Pia viongozi wa Mbao FC, Abdallah Chuma (Daktari) na Meneja Yasin Abdul wamefungiwa miezi sita na faini ya sh. 100,000 kila mmoja kwa kumtukana na kumtishia maisha Kamishna wa mechi hiyo.

Nayo klabu ya AFC imepigwa faini ya sh. 300,000 kutokana na washabiki wake kuifanyia vurugu timu ya Bulyanhulu FC kwenye mechi yao iliyofanyika Februari 7 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Timu ya Magereza Iringa imepigwa faini ya jumla ya sh. 200,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting), na uwanjani kwenye mchezo wao na Njombe Mji uliochezwa Februari 21 mwaka huu.

Naye mchezaji wa timu Amasha Mlowasa amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 100,000 kwa kumtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi hiyo.

Monday, March 2, 2015

KIKWETE AONGOZA MAELFU YA WAOMBOLEZAJI KUUAGA MWILI WA KEPTENI KOMBA


RAIS Jakaya Kikwete na mkewe Salma Kikwete wakitoa heshima mbele ya jeneza lenye mwili wa mbunge wa Mbinga Magharibi, Kepteni John Komba kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana
RAIS Jakaya Kikwete akimfariji mke wa marehemu Kepteni John Komba, Salome Komba wakati wa kuuaga mwili wake
MAKAMU wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal akitoa heshima mbele ya mwili wa marehemu John Komba
RAIS mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi akitoa heshima mbele ya jeneza lenye mwili wa Kepteni Komba
RAIS mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa akitoa heshima mbele ya jeneza lenye mwili wa Kepteni Komba
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akitoa heshima zake mbele ya mwili wa Komba
JENEZA lenye mwili wa marehemu John Komba likiwa ndani ya ukumbi wa Karimjee kabla ya waombolezaji kuanza kutoa heshima
MBUNGE wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka akibubujikwa na machozi baada ya kuuaga mwili wa marehemu John Komba
RAIS mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa akiteta jambo na Spika wa Bunge, Anne Makinda wakati wa kuuaga mwili wa marehemu John Komba

Sunday, March 1, 2015

MWILI WA KEPTENI KOMBA KUSAFIRISHWA KESHO KWENDA SONGEA, ALITABIRI KIFO CHAKE, ALIAGIZA MWILI WAKE UPITISHWE MBAMBABAY



NA  DUSTAN  NDUNGURU  SONGEA

MWILI wa mbunge wa jimbo la Mbinga magharibi kapteni John Komba aliyefariki jana katika hospitali ya TMJ jijini Dar es salaam unatarajiwa kuwasili kesho mjini Songea,mkoani Ruvuma tayari kwa mazishi.

Akiongea na uhuru mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Oddo Mwisho alisema kuwa mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili uwanja wa ndege wa mjini hapa kesho majira ya mchana ambapo baadaye utapelekwa moja kwa moja ofisi za CCM mkoa kwa ajiri ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho.

Alisema baada ya wananchi wa manispaa ya Songea kupata fursa ya kuaga mwili utasafirishwa hadi katika kijiji cha Lituhi kilichopo wilayani Nyasa ambako alizaliwa na kwamba mazishi yanatarajiwa kufanyika februari 3 mwaka huu.

Mwisho alisema viongozi mbalimbali wa kitaifa wanatarajiwa kuanza kuwasili mkoani humo kwa ajiri ya kushiriki mazishi kuanzia leo na kwamba maandalizi yanaendelea kufanyika kwa ajili ya kufanikisha shughuli hiyo.

Alisema wilaya ya Nyasa imepata pigo kubwa baada ya kuondokewa na viongozi wake wawili katika kipindi cha siku mbili ambapo kabla ya kifo cha Komba asubuhi ya februari 27 mwaka huu aliyekuwa katibu wa CCM wa wilaya ya Nyasa Rhoda George alifariki dunia katika hospitali ya mkoa wa Iringa ambako alilazwa kutokana na kusumbuliwa na maradhi na kwamba februari 28 kapteni Komba ambaye pia ni mjumbe wa NEC kupitia wilaya hiyo alifariki dunia.

Alisema baada ya kupokea taarifa za kufariki kwa katibu huyo wa chama,Kapt.Komba alituma shilingi laki tano za rambirambi fedha ambazo alizituma kwa mwenyekiti huyo wa mkoa.

"Niliwasiliana naye jana asubuhi kabla sijaondoka Songea kwenda Iringa kwa ajili ya kushiriki mazishi ya katibu wetu wa wilaya ya Nyasa na akaniambia nakutumia shilingi laki tano kama rambirambi"alisema.

Mwisho alisema baada ya kuanza safari ya kuelekea Iringa  wote  njiani walikuwa wakiwasiliana kwa nyakati tofauti ambapo mara baada ya kufika mjini Iringa alipiga simu ikapokelewa na mtoto wake huku akimweleza baba yake amefariki.

Wakati huohuo mwenyekiti wa wazazi wa wilaya ya Nyasa Frank Ligola alisema Kapt.Komba wakati wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zilizofanyika desemba mwaka jana katika kila mkutano alisikika akisema maneno ambayo ni kama yalikuwa yakitabiri kifo chake ambapo alidai akifa maiti yake ipitishwe kwanza Mbamba bay kabla ya kwenda kuzikwa kijijini kwake Lituhi.

"Unajua wakati mwingine ni kama alikuwa akitabiri kifo chake wakati wa kampeni za uchaguzi alisema nikifa maiti yangu itapitishwa hapa Mbamba bay kwanza na kuzikwa itakuwa Lituhi"alisema Ligola.

Hata hivi novemba mwaka 2005 mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mbinga magharibi Kapt.Komba akiwa kijijini kwake Lituhi aliwaambia waandishi wa habari kuwa atakuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka kumi,ambapo tangu wakati huo mpaka mwaka huu alikuwa akitimiza mwaka ambao alijitabiria atahitimisha safari zake kama mbunge.

        

JK ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA FAMILIA YA KEPTENI KOMBA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kepteni John Damian Komba, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM na msanii hodari sana wa kizazi chake.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda na Katibu Mkuu wa CCM, MheshimiwaAbdulrahman Kinana, Mheshimiwa Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kepteni John Komba, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea mchana wa leo, Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam.”
“Kwa hakika, sina maneno ya kutosha kuelezea kwa fasaha hasara ambayo taifa letu na chama chetu kimepata kutokana na kifo cha Kepteni Komba. Taifa letu limepoteza hazina kubwa na mtu muhimu. Nimemjua Kepteni Komba kwa muda mrefu sana, nimefanya naye kazi. Alikuwa msanii ambaye kiwango chake cha usanii kilikuwa hakipimiki, alikuwa na sifa kubwa za uongozi, alikuwa mpenzi, mzalendo na mtu mwaminifu sana kwa taifa lake na katika jambo lolote aliloliamini.,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo na kuongeza:
“Akiwa mwalimu, lakini hasa akiwa Mlinzi wa Taifa katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kepteni Komba alithibitisha sifa zake kama mlinzi wa taifa kwa kipaji chake cha kutunga na kuimba nyingi za kuhamamisha wanajeshi wetu katika ulinzi wa nchi yao. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kisanii kutunga nyimbo za aina zote – ziwe za maombolezo, ziwe za kutoa hamasa, ziwe za makaribisho, ziwe za kampeni za kisiasa na kijamii ama ziwe za kampeni maalum.”
“ Mheshimiwa Komba alikuwa Mbunge hodari sana na wananchi wa Nyasa wamepoteza mtetezi wa uhakika. Mheshimiwa Komba alikuwa mcheshi, aliyependa sana utani na alikuwa na uongozi mkubwa wa kutambua na kulea vipaji vya sanaa na wasanii kama alivyothibitisha katika kuanzisha na kulea Kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT) na kabla ya hapo .”
“Kupitia kwenu Waheshimiwa, naomba mnifikishie salamu zangu za dhati kabisa kwa Wabunge wote ambao wameondokewa na mwenzao na wananchi wa Jimbo la Nyasa na Mkoa wote wa Ruvuma ambao wamepoteza mwakilishi na kiongozi wao. Ndani ya Chama chetu, naomba salamu zangu ziwafikie wanachama wetu wote kwa kupoteza mwanachama mwenzao, ziwafikie viongozi na hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo imepoteza mwakilishi mwenzao na wasanii wote wa Tanzania One Theatre (TOT) ambao Kiongozi wao ameondoka duniani,” amesema Rais na kumalizia:
Naungana na wanafamilia kuomboleza kifo cha rafiki yetu, ndugu yetu na kiongozi mwenzetu. Napenda wanafamilia wajue kuwa natambua uchungu wao katika kipindi hiki na tahayari yao ya  kuondokewa na mhimili wa familia. Niko nao katika maombolezo na katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Kepteni John Damian Komba. Amen.”

SIMBA YANGURUMA DAR, YAITANDIKA PRISONS 5-0






SIMBA jana ilizinduka na kutoa onyo kwa timu zinazoshiriki kwenye michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibugiza Prisons mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya kuibuka na ushindi huo mnono, Simba imebaki kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 16.

Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 31, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Kagera Sugar yenye  pointi 24.

Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na watazamaji wachache, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0. Mabao yote hayo yalifungwa na mshambuliaji chipukizi Ibrahim Hajibu.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi na Ramadhani Singano 'Messi'.

AZAM YATUPWA NJE KOMBE LA AFRIKA

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika, Azam jana waliyaaga mashindano hayo baada ya kuchapwa mabao 3-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Khartoum, Azam ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele.

Kutokana na kipigo hicho, Azaam imetolewa kwa jumla ya mabao 3-2 kufuatia kushinda mechi ya awali mjini Dar es Salaam kwa mabao 2-0.

Dalili za Azam kutolewa katika michuano hiyo zilianza kujionyesha mapema kutokana na waamuzi wa mchezo huo kutoka Zambia kuwapendelea wenyeji.


Katika kudhihirisha upendeleo wa dhahiri, wenyeji walizawadiwa penalti kipindi cha kwanza, lakini iliokolewa na kipa Aishi Manula.