KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, October 19, 2014

SIMBA, YANGA HAKUNA MBABE


 MSHAMBULIAJI Elias Maguri wa Simba akitafuta mbinu za kumtoka beki Oscar Joshua wa Yanga
 AMRI Kiemba wa Simba akiwania mpira na Andrey Coutinho wa Yanga
 KIPA Manyika Peter wa Simba akidaka mpira mbele ya washambuliaji wa Yanga
MSHAMBULIAJI Denilson Jana (namba 9) akikokota mpira huku akichungwa na kiungo Jonas Mkude wa Simba
TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga jana zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sare hiyo ilikuwa ya nne mfululizo kwa Simba tangu ligi hiyo ilipoanza Septemba 29 mwaka huu na ya kwanza kwa Yanga, ambayo imeshinda mechi mbili, kupoteza moja na kutoka sare moja.

Katika mechi hiyo, kivutio kikubwa kilikuwa kipa chipukizi wa Simba, Manyika Peter, ambaye alilazimika kukaa langoni baada ya makipa Ivo Mapunda na Hussein Sharrifu kuwa wagonjwa.

Licha ya kuwa mechi yake ya kwanza katika ligi hiyo, timu ikizihusisha timu hizo kongwe, Manyika alionyesha umahiri mkubwa wa kulinda lango lake na kuwafanya mashabiki wa Simba wamshangilie kila alipodaka ama kuokoa mpira wa hatari.

Timu hizo zilicheza kwa kukamiana tangu mwanzo wa mchezo huku mabeki Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Kevin Yondan na Oscar Joshua wakimwekea ulinzi mkali mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba.

Nao mabeki Joseph Owino, Hassan Isihaka, Lucian Gallas na Idrisa Rashid, waliwawekea ulinzi mkali Genilson Santos 'Jaja' na Andrey Coutinho, ambao walishindwa kufurukuta.

Timu zote mbili zilipata nafasi kadhaa nzuri za kufunga mabao, lakini zilipotezwa na washambuliaji wake, Jaja wa Yanga, Okwi na Elias Maguri wa Simba kutokana na mashuti yao kushindwa kulenga lango.

Friday, October 17, 2014

SIMBA, YANGA NANI KUCHEKA KESHO?




TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zinashuka dimbani kesho kumenyana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hilo la watani wa jadi, linasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kwa vile ndilo litakalomaliza ubishi wa timu ipi bora kati ya hizo msimu huu.

Simba itashuka dimbani huku mwenendo wake katika ligi hiyo ukiwa wa kusuasua baada ya kutoka sare katika mechi zote tatu za mwanzo.

Katika mechi yake ya kwanza, Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 na Coastal Union, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Moro kabla ya kulazimishwa sare nyingine ya bao 1-1 na Stand United ya Shinyanga.

Nayo Yanga ilianza vibaya ligi hiyo baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, lakini ikazinduka katika mechi mbili zilizofuata baada ya kuichapa Prisons mabao 2-1 na kisha kuichapa JKT Ruvu mabao 2-1.

Katika mechi hiyo, Simba huenda ikawakosa makipa wake wawili, Ivo Mapunda na Hussein Sharifu 'Casillas' kutokana na kuwa majeruhi, hali inayomchanganya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri.

Iwapo makipa hao watashindwa kushuka dimbani, tegemeo pekee la Simba litakuwa kwa kipa wake chipukizi, Manyima Peter, ambaye ni mtoto wa kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika.

Ivo alivunjika kidole cha mkono wiki mbili zilizopita wakati Sharifu ameumia kifundo cha mguu na atakuwa nje ya uwanja kwa miezi sita.

Hata hivyo, Phiri alisema taarifa za madaktari waliomtibu Ivo zimeeleza kuwa, huenda kipa huyo akawa fiti kabla ya mechi ya kesho.

Katika kujiandaa na mechi hiyo, Simba ilikwenda kuweka kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini na pia kucheza mechi tatu za kirafiki, ambapo ilichapwa mabao 2-0 na Jomo Cosmos, ilifungwa mabao 4-2 na Bidvest Wits na kutoka suluhu na Orlando Pirates.

Kwa upande wa Yanga, wachezaji wake Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kevin Yondan, ambao walikuwa majeruhi, kwa sasa wapo fiti na wameanza mazoezi ya pamoja na wenzao.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo amesema wachezaji wake wote wapo fiti na wana ari kubwa ya kushinda mchezo huo ili kulinda heshima yao.

Pambano hilo litachezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo, ambaye Yanga iliandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikilalamika kwamba haina imani naye na kutaka abadilishwe.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Umande alisema jana kuwa, wameamua kuyatupilia mbali maombi hayo ya Yanga kwa sababu hayana mashiko.

"Yanga waliandika barua ya kumlalamikia Mkongo katika mechi zao, lakini sisi tunachoangalia ni jinsi gani mwamuzi anatafsiri vyema sheria 17 za soka na katika hilo, Nkongo analimudu vyema,"alisema.

Hata hivyo, Umande alisema wameamua kumbadilisha mshika kibendera Ferdinand Chacha wa Mwanza, ambaye nafasi yake sasa itachukuliwa na Samuel Mpenzu kutoka Arusha. Mshika kibendera mwingine katika mechi hiyo atakuwa John Kanyenye kutoka Mbeya.

Thursday, October 16, 2014

RATIBA LIGI DARAJA LA KWANZA YAREKEBISHWA


Mechi nne za Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zimefanyiwa marekebisho ili kutoa fursa ya matumizi ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

Timu za African Lyon na Kimondo FC ambazo awali zilikuwa zicheze Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, sasa zitacheza Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Nayo mechi ya Polisi Dar es Salaam na Majimaji ya Songea iliyokuwa ichezwe Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, sasa itachezwa Oktoba 27 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.

Mechi ya Friends Rangers na Ashanti United iliyokuwa ichezwe Mabatini mkoani Pwani, Oktoba 26 mwaka huu, sasa itachezwa Uwanja wa Karume, Oktoba 28 mwaka huu.

Pia mechi ya Lipuli FC na JKT Mlale iliyokuwa ichezwe Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, imesogezwa mbele kwa siku moja. Mechi hiyo sasa itachezwa Oktoba 26 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.

UCHAGUZI MDOGO BODI YA LIGI NOVEMBA 15



Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) utafanyika Novemba 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam ambapo moja ya ajenda ni uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi moja ya uongozi kwenye bodi hiyo.

Nafasi hiyo ya ujumbe kwenye Kamati ya Uendeshaji ya TPLB iliyokuwa ikishikiliwa na Kazimoto Muzo imebaki wazi baada ya klabu yake ya Pamba ya Mwanza kushuka daraja kutoka la Kwanza hadi la Pili.

Hivyo, wagombea wa nafasi hiyo ni kutoka kwenye klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Klabu hizo zina nafasi mbili kwenye Kamati ya Uendeshaji ya TPLB ambapo nyingine inashikiliwa na Omari Mwindadi wa klabu ya Mwadui ya Shinyanga.

SDL WAONGEZEWA MUDA WA USAJILI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza muda wa usajili wa wachezaji kwa timu za Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa siku saba ambapo sasa utamalizika Oktoba 21 mwaka huu.

Awali usajili huo unaofanyika kwa njia ya mtandao (online) ulikuwa umalizike jana (Oktoba 14 mwaka huu), lakini ni klabu chache ndizo zilizoweza kusajili ndani ya muda uliopangwa.

Klabu ambazo hazijakamilisha shughuli hiyo ya usajili, zinatakuwa kukamilisha ndani ya siku hizo saba kwani TFF haitaongeza tena muda wa usajili. Vilevile klabu za SDL zinakumbushwa kuwasilisha majina ya viwanja vya nyumbani ambavyo timu zao zitatumia kwenye ligi hiyo.

TFF ilifanya mafunzo ya usajili kwa maofisa usajili wa klabu hizo Oktoba 6 na 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Timu za SDL zimegawanywa katika makundi manne ya timu sita zitakazocheza ligi kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Kundi A lina timu za Mpanda United ya Katavi, Ujenzi (Rukwa), Mvuvumwa FC (Kigoma), Mji Mkuu FC (Dodoma), Milambo (Tabora) na Singida United (Singida).

Kundi B ni Mbao FC (Mwanza), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), JKT Rwamkoma (Mara), Pamba (Mwanza) na AFC (Arusha). Kundi C ni Navy, Mshikamano, Transit Camp na Abajalo za Dar es Salaam, Kiluvya United (Pwani) na Kariakoo (Lindi(.

Timu zinazounda kundi D ni Magereza (Iringa), Town Small Boys (Ruvuma), Njombe Mji (Njombe), Volcano FC (Morogoro), Wenda FC (Mbeya) na Mkamba Rangers (Morogoro).

Tuesday, October 14, 2014

YANGA YAIENDEA SIMBA KAMBINI KUNDUCHI



Kikosi cha Young Africans Sports Club

Kuelekea kwenye mpambano wa watani wa jadi YANGA Vs SIMBA siku ya jumamosi Oktoba 18, kikosi cha timu ya Young Africans kimeingia kambini leo mchana katika hoteli ya Landmark iliyopo eneo la Kunduchi kujiandaa na mchezo huo ambao umeteka hisia za wapenzi wa soka nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kocha mkuu Marcio Maximo ameingia kambini na kikosi cha wachezaji 28 kujiandaa na mchezo huo ambapo kikosi chake kitakua kikifanya mazoezi katika Uwanja wa Boko - Veterani kila siku kujweka fit kwa kuzisaka pointi tatu muhimu siku ya jumamosi.

Akiongelea kuhusu maandalizi ya mchezo huo, Maximo amesema anashukuru vijana wake wote wapo katika hali nzuri kiafya, kifikra na morali ni hali ya juu kuelekea kwenye Dar Derby siku hiyo jumamosi.

Natambua mechi za wapinzani wa jadi huwa hazitabiriki, ila sisi kama Yanga tunajiandaa kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo dhidi ya Simba SC siku ya jumamosi, makosa yaliyokuwa yakijitokeza katika michezo iliyopita tumeshayafanyia kazi" alisema Maximo.

Wachezaji saba waliokuwa kwenye kambi ya timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) wameungana na wachezaji wengine leo wakiwa fit kabisa na hakuna mchezaji majeruhi hali inayompelekea kuwa na kikosi kipana cha maandalizi.

Wachezaji waliongia kambini kujianda na mchezo huo wa jumamosi ni:

Walinda mlango: Juma Kaseja, Ally Mustafa "Barthez" na Deo Munish "Dida"

Walinzi: Juma Abdul, Salum Telela, Oscar Joshua, Amos Abel, Edward Charles, Rajab Zahir, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani, na Nadir Haroub "Cannavaro"

Viungo: Mbuyu Twite, Said Juma "Makapu", Omega Seme, Hamis Thabit, Nizar Khalfani, Issa Ngao na Haruna Niyonzima.

Washambuliaji: Geilson Santos "Jaja", Andrey Coutinho, Said Bahanuzi, Hamis Kizza, Saimon Msuva, Mrisho Ngasa, Hussein Javu na Jerson Tegete.

KUZIONA SIMBA NA YANGA SH. 7000



Kiingilio cha chini kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba itakayochezwa Jumamosi (Oktoba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 7,000.

Washabiki watakaolipa kiingilio hicho ni wale watakaokaa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo jumla yake ni 36,693 katika uwanja huo wenye viti 57,558. Viingilio vingine ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.

Tiketi zitakazotumika kwenye mechi hiyo ni za elektroniki, na zimeanza kuuzwa jana (Oktoba 13 mwaka huu). Tiketi zinapatikana kwa mtandao wa M-PESA, CRDB Simbanking na maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo zaidi ya mia moja sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo namba 27 itakayochezeshwa na mwamuzi Israel Mujuni Nkongo akisaidiwa na John Kanyenye na Ferdinand Chacha itaanza saa 10 kamili jioni. Kamishna wa mechi hiyo ni Salum Kikwamba kutoka mkoani Kilimanjaro.

Washabiki wanatakiwa kununua tiketi mapema, kwani hazitauzwa uwanjani siku ya mechi. Milango yote ukiwemo ule wa upande wa Mbagala (Uwanja wa Ndani) itafunguliwa kwa ajili ya washabiki, na itakuwa wazi kuanzia saa 4 asubuhi.

Magari maalumu tu yenye stika ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia uwanjani kwa kupitia Barabara ya Mandela. Pia washabiki hawaruhusiwi kuingia uwanjani wakiwa na silaha, vitu vya vyuma na mabegi makubwa. Barabara ya kuingilia upande wa Chang’ombe itafungwa kwa watumiaji wa magari.

Sunday, October 12, 2014

TAIFA STARS YAIUA BENIN 4-1



 BEKI Shomari Kapombe wa Taifa Stars akiondosha mpira kwenye lango lake wakati timu hiyo ilipomenyana na Benin kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi.
 MRISHO Ngasa wa Taifa Stars akimfunga tela beki wa Benin wakati wa pambano hilo
HIKI ndicho kikosi cha Taifa Stars kilichoiua Benin jana

TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana iliwapa raha Watanzania baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Benin.

Katika mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-1.

Ushindi huo ulikuwa wa kwanza mkubwa kwa Taifa Stars dhidi ya timu kutoka mataifa ya Afrika Magharibi. Mara ya mwisho Taifa Stars kupata ushindi wa aina hiyo ilikuwa mwaka juzi wakati Taifa Stars ilipoichapa Morocco mabao 3-1 katika michuano ya Afrika.

Iliwachukua Taifa Stars dakika 16 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na beki Nadir Haroub 'Cannavaro', akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Erasto Nyoni kutoka pembeni kidogo ya uwanja.

Kiungo Amri Kiemba aliwainua vitini mashabiki dakika ya 4 baada ya kuifungia Taifa Stars bao la pili baada ya kupokea krosi kutoka kwa Shomari Kapombe na kuwazidi mbio mabeki wawili wa Benin kabla ya kuubetua mpira ukampita kipa Farnoue Fabien.

Bao la tatu la Taifa Stars lilipatikana dakika ya 49 kupitia kwa Thomas Ulimwengu, akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Mrisho Ngasa kutoka pembeni ya uwanja.

Juma Luizio, aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ngasa, aliihakikishia Taifa Stars ushindi dakika ya 71 baada ya kuifungia bao la nne, akiunganisha krosi ya Ulimwengu.

Benin ilipata bao la kujifariji dakika chache kabla ya mpira kumalizika kupitia kwa Didier Sossa baada ya mabeki wa Taifa Stars kuzembea kumkaba.

SITTI MTEMVU NDIYE MISS TANZANIA 2014


Miss Tanzania 2014, Siti Abass Zuberi Mtemvu akipunga mkono mara baada ya kuvikwa taji hilo usiku wa kuamkia leo katika shindano lililoshirikisha warembo 30 na kufanyika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam. Siti Mtemvu ametwaa taji hilo lililokuwa likishikiliwa na Happyness Watimanywa.
Mrembo wa Redd's Miss Tanzania 2014,Sitti Abbas Mtemvu akiwa katika picha ya pamoja na Mshindi wa pili,Lillian Kamazima (kulia) na Mshindi wa Tatu,Jihhan Dimachk mara baada ya kutawazwa rasmi usiku huu kwenye ukumbi wa Mlimani City,jijini Dar es Salaam.Sitti Mtemvu alianza kwa kunyakua Redds Miss Chang'ombe na baadaye Redds Miss Temeke. Sitti ni binti wa Mbunge wa Temeke, Mhe. Abbas Mtemvu.
Redd's Miss Tanzania aliemaliza muda wake,Happiness Watimanywa akimvisha taji Redd's Miss Tanzania wa sasa, Sitti Mtemvu
Mbunge wa Temeke, Abbasi Mtemvu, mwenye kofia na familia yake wakifuatilia shindano hilo.

MPULIZA SAXAPHONE WA ZAMANI WA MSONDO NGOMA, ALLY RASHID AFARIKI DUNIA, AZIKWA


HAWA ni baadhi ya wanamuziki wakongwe waliohudhuria mazishi ya Ally Rashid

 Ally Rashid, wa tatu kulia akiwa na wanamuziki wenzake wakongwe
Jeneza lenye mwili wa marehemu Ally Rashid likipelekwa makaburini

Mwanamuziki wa zamani aliyekuwa mpiga saxaphone aliyejulikana pia kama Mzee Saboso, Ally Rashid amefariki dunia jana mchana.  Mzee Ally kwa mara ya mwisho alikuwa bendi ya Msondo Ngoma.

Umati mkubwa wa watu ulijitokeza kumzika Ally Rashid mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alifariki jana mchana. Mazishi yalifanyika katika makaburi ya Keko Machungwa, kaburi lake likiwa jirani kabisa na la mwanamuziki mwingine nguli Moshi William.

Mazishi ya Mzee Alyy yalifanyika muda wa saa nne asubuhi na pia kuhudhuriwa na wanamuziki wengi wa zamani na hata wa sasa, akiwemo Mchizi Mox, ambaye alikuwa kimwita marehemu baba yake mdogo

HISTORIA YA ALLY RASHID KHAMIS ‘SABOSO’

Ally Rashid ‘Saboso’, huyo ni mpulizaji nguli wa ‘Saxophone’ aliyewahi kuzitumikia bendi kadhaa za hapa nchini na kutokea kujizolea sifa kemkemu kutokana na umahiri wake wa kucheza na chombo hicho.

Hivi tunavyozungumza Saboso amepoteza uwezo wa kupuliza Saxophone kutokana na kuwa, anasumbuliwa na maradhi ya kupooza kwa muda mrefu sasa.Mwandishi wa makala hii alimtembelea Saboso nyumbani kwake Keko, jijini Dar es Salaam anapougulia na kuongea naye mengi kuhusiana na maisha yake, muziki pamoja na maradhi yanayomsumbua.

“Maradhi haya yamenianza miaka kadhaa nyuma, nikiwa na bendi yangu ya Msondo Ngoma, siku moja tulikuwa natumbuiza kwenye ukumbi mmoja kule Mbagala Rangi Tatu, ambao jina lake silikumbuki vema,” anasema Saboso.

“Wakiwa katikati ya shoo, ghafla aliibuka mwanamke mnene aliyevaa nguo nyekundu na kumuomba kucheze naye, lakini alimkatalia kutokana na desturi yake ya kutokupaparika na wanawake, hususan akiwa kazini. Yule mwanamke alimlazimisha sana kucheza naye na alivyoonekana kuwa kero, Mabera aliamrisha atolewe kinguvu, lakini kabla hilo halijafanyika, aliyeyuka na hapohapo Saboso akaanza kuishiwa nguvu. Saboso anasema kuwa, alianza kuhisi ulimi wake unakuwa mzito na kutokea kwa dalili nyingine za kupooza ambapo aliamua kukaa chini baada ya kushindwa kusimama.

“Dansi lilipomalizika Romario alinisindikiza nyumbani kwa vile njia yetu ni moja tukaachana mbele, lakini nilipomgongea mlango mke wangu na kunifungulia, alionekana kunishangaa sana,” anasema Saboso.

Saboso alipoingia ndani aliamua kumuuliza mke wake juu ya mshangao wake, akamwambia kuwa wakati ananifungulia mlango, alimuona mwanamke kasimama nyuma yake na baadaye akayeyuka na kupotea.

Baada ya matukio hayo, hali ya maradhi iliendelea kumsumbua Saboso na takriban miezi miwili baadae alipata nafuu na kurejea kazini baada ya familia yake kumuhangaikia mno.

“Lakini miezi sita hivi baada ya kupona, siku moja nikiwa kwenye baiskeli yangu maeneo ya Kamata, Kariakoo naelekea kazini, nikaanguka ghafla na kupoteza tena nguvu,” anasema Saboso. Alichomudu kukifanya pale ni kuita taksi ya karibu iliyompeleka ofisini kwao Ilala, ambapo wanamuziki wenzie walipomuona waliamua kumuwahisha Hospitali ya Amana.

Saboso anasema kuwa, akiwa Amana ndipo alikatikiwa kabisa na kauli akawa hajimudu kuzungumza. Familia yake ikaanza tena kumuhangaikia hadi leo bila dalili yoyote ya mafanikio.

Saboso anasikitika akisema, bendi yake ya Msondo Ngoma imemsusa na kumtelekeza kabisa, licha ya kuwa alipatwa na matatizo hayo wakati akiwa kazini.

Anasema, ana miaka minane sasa kitandani na katika miaka yote hiyo, hajapata msaada kutoka Msondo, zaidi ya kutembelewa mara chache huko nyuma na baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo ambao si viongozi.

“Nawakumbuka waliowahi kunitembelea, wengine ikiwa ni mara moja tu, ambao ni Romario, Hamis Mnyupe, Ibrahim Kandaya, Huluka Uvuruge na Ismail Mapanga ambaye kwa sasa ni marehemu,” anasema saboso.

Anasema kuwa, Meneja wao, Said Kibiriti alifika mara moja tu kumjulia hali na kukata mguu akiwa kasahau kwamba, naye alishiriki majadiliano ya kukopa vyombo Unguja, baada ya Jumuia ya Wafanyakazi kujitoa.

Historia ya Saboso kimuziki inaanzia mwaka 1952 alipokuwa mpiga ngoma wa bendi ya Zanzibar Jazz, baadae akahamia Afrika Jazz ya hukohuko Zanzibar alipoanza pia kuimba.

Mwaka 1959 alihamishia virago jijini Dar es Salaam alipojiunga na bendi ya Dar es Salaam Jazz iliyomkutanisha na wanamuziki Nassor Mtondoo, Grey na Uporoto, akabahatika kurekodi hapo kibao ‘Shukrani Natoa’.

“Mwaka 1960 nikatua Western Jazz, Wema Abdallah akanipokea na hapo nikakubalika zaidi kwa mashabiki kiasi cha kupachikwa jina hili, ‘Saboso’ kutokana hasa na kushiriki kuimba wimbo ‘Saboso’,” anasema.

Saboso anasema kuwa, akiwa Western Jazz, Saboso aliimba pia vibao kama ‘Jela ya Mapenzi’, ‘Ulokusudia Mwenzangu’ na ‘Veronica’ huku vilevile akishiriki kupuliza Saxophone ndogo aliyojifunza kidogokidogo wakati ule alipokuwa kisiwani Unguja.

Mwaka 1972 akachomoka Western Jazz na kujiunga na bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Kimbunga Stereo), alipokutana na magwiji wengi akiwamo Kapteni John Simon.

Akiwa hapa, ‘Baba Mwenye Nyumba’ ni kati ya vibao ambavyo Saboso alipuliza Saxophone kwa ufundi mkubwa, kabla ya mwaka 1977 kutimkia Orchestra Double O ya Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kii’ ambako hata hivyo hakuwahi kurekodi.

“Mwaka 1978 niliingia Orchestra Bima Lee iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Magnet Tingisha’ na kukutana na wababe wa muziki kama Joseph Mulenga, Shaaban Dede, Jerry Nashon, Othman Momba na Hamis Sama,” anasema Saboso.

Saboso ambaye ni kati ya waasisi wa bendi ya Shikamoo Jazz, aliorekodi na kusafiri nao sehemu mbalimbali duniani, anajivunia kupuliza Saxophone ya kiutu uzima kwenye vibao vingi vya Bima Lee vikiwamo‘Pesa’, ‘Visa vya Mesenja’ na ‘Baba Mwamvua’.

Balaa la Saboso halikukomea huko tu, bali hadi katika miaka ya hivi karibuni alipoingia Msondo Ngoma na kushiriki kikamilifu kwenye albamu mbili ambazo ni ‘Kaza Moyo’ na ‘Ajali’.

Unapomuuliza kuhusu kazi alizozifanya mwenyewe ambazo zinamvutia hata anapozisikiliza hivi sasa, Saboso anayejivunia umaarufu katika muziki, anakutajia vibao ‘Baba Mwamvua’ na ‘Pesa’ vya Bima Lee.

Nyumba anayoishi Saboso aliyewafundisha kupuliza Twahili Mussa na Mafumu Bilali ‘Bombenga’ kupuliza Saxophone, aliijenga mwaka 1961 alipoajiriwa kiwanda cha nguo kilichokuwa kinajulikana kama Tanganyika Textile Mills.

“Hapo nilikuwa mpishi wa rangi za mashuka na mwanamuziki pia, ambapo nilikopeshwa sh. 300, sh. 100 nilinunua kiwanja na kuanza kujenga taratibu, huku mabati nikikopeshwa na Bima,” anasema Saboso.

Alizaliwa miaka 75 nyuma, Ndagoni Pemba na elimu yake ya msingi aliichukulia jijini Tanga katika miaka ambayo haikumbuki kabisa hivi sasa. Mzee Ally Rashid amefariki leo 10 Oktoba 2014.
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI   HABARI NA MAKALA HII IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA WANAMUZIKI WETU YA JOHN KITIME.

Thursday, October 9, 2014

MUJUNI KUZIHUKUMU SIMBA NA YANGA OKTOBA 18




MWAMUZI Israel Mujuni Nkongo anatarajiwa kuchezesha pambano la watani wa jadi la ligi kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga.


Pambano hilo litachezwa Oktoba 18 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Silas Mwakibinga alisema waamuzi wa pembeni watakuwa ni Fednandi Chacha kutoka Mwanza na John Kanyenye kutoka Mbeya.

Alisema Mwamuzi wa mezani atakuwa ni Hashimu Abdalah na Kamishna wa mechi hiyo ni Salum Kikwamba.

Alisema maandalizi ya mechi hiyo yanaendelea vema huku timu zote zikiwa katika maandalizi kwa ajili ya mchezo huo.

Tayari Simba wamekwea pipa juzi kuelekea Afrika Kusini kujiandaa na mchezo huo huku Yanga ikiendelea kujifua katika viwanja vya Loyola Dar es Salaam.

Mwakibinga alisema mbali na mechi hiyo pia kwa upande wa timu nyingine mechi zitaendelea kama kawaida ambapo Mtibwa Sugar itacheza dhidi ya Polisi Morogoro katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Pia Ndanda FC itashuka dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara, Kagera Sugar dhidi ya Stand United utakaochezwa uwanja wa Kaitaba na Coastal Union dhidi ya Mgambo JKT katika uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Alisema pia siku hiyo kutakuwa na mechi kati ya Azam na Mbeya City utakaochezwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Tanzania Prison itaumana dhidi ya JKT Ruvu katika uwanja wa Azam Complex Chamazi Dar es Salaam.

Wednesday, October 8, 2014

MISS TANZANIA KUFANYIKA JUMAMOSI MLIMANI CITY DAR


Mkurugenzi wa Kampuni ya Rino International Agency ambao ni waratibu wakuu wa Mashindano ya Miss Tanzania,Hashim Lundenga (kulia) akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo,juu ya onyesho la Redd's Miss Tanzania 2014 linalotarajiwa kufanyika Oktoba 11,2014 katika Ukumbi wa Mlimani City,Jijini Dar.Katikati ni Meneja wa Kinywaji cha Redd's ambao ni Wadhamini Wakuu wa Mashindano hayo,Victoria Kimaro na kushoto ni Meneja Maria Stopes Tanzania,Anna Shanalingigwa. (Picha zote na Othman Michuzi,MMG).

Meneja wa Kinywaji cha Redd's ambao ni Wadhamini Wakuu wa Mashindano ya Miss Tanzania,Victoria Kimaro (kushoto) akizungumzia zawadi watakayotoa kwa Washindi watakaopatikana kwenye Shindano hilo la Redd's Miss Tanzania 2014,ambapo mwaka huu mshindi wa kwanza katika kinyang'anyiro hicho atajinyakulia kitita cha sh. Mil. 18 taslim huku washindi wengine wakiendelea kuondoka na zawadi mbali mbali.Katikati ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Rino International Agency ambao ni waratibu wakuu wa Mashindano ya Miss Tanzania,Hashim Lundenga na kulia ni Meneja wa Hoteli ya JB Belmont,Gillian Macheche pamoja na Afisa Habari wa Miss Tanzania,Hidan Ricco.

LUNDENGA AMBWAGA PRASHANT PATEL MAHAKAMANI


NA FURAHA OMARY


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemruhusu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Lino International Agency, ambayo ni waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, kuendelea na shindano hilo litakalofanyika Jumamosi, wiki hii, katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Hatua hiyo, inatokana na mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na mshirika wa Lundenga, Prashant Patel ya kutoa zuio la muda la mashindano hayo.

Uamuzi huo, ulitolewa juzi jioni na Hakimu Mkazi Frank Moshi, baada ya kusikiliza maombi hayo yaliyowasilishwa na Patel kupitia Wakili wake Benjamin Mwakagamba.

“Mahakama baada ya kusikiliza maombi ya kutoa zuio la shindano hilo, imeona hakuna sababu za msingi zilizowasilishwa na mleta maombi (Patel) za kuweza kusimamisha shindano hilo,” alisema.

Hakimu Moshi alisema Patel aliwasilisha maombi hayo akidai kwamba kuna haki inakuikwa katika mkataba baina yake na Lundenga na bado zinaendelea kukiukwa.

Madai mengine ya Patel ni kwamba Lundenga amekuwa akiwasiliana na wafadhili na wadhamini wa shindano hilo bila ya kumshirikisha, hivyo alikuwa anaomba shindano hilo lisimamishwe kusubiri uamuzi wa mahakama.

“Hakukuwa na mashiko katika sababu za kutaka kutoa zuio na mahakama imejiuliza kama litatolewa linaweza kuleta athari kwa watu waliojitokeza, wadhamini na wanaotarajia kunufaika nalo kwa namna moja au nyingine kisa hawakujua kama kuna mgogoro.”

“Hata kama shindano litaendelea, madai ya msingi ya Patel yapo pale pale na hayaathiri. Shindano liendelee kama lilivyopangwa kwa kuwa kesi ya msingi inahusu fedha,” alisema Hakimu Moshi.

Patel alifungua kesi ya msingi mahakamani hapo dhidi ya Lundenga, Septemba 29, mwaka huu na baadae kuwasilisha maombi ya zuio la muda la mashindano hayo.

Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Lundenga kwa kupitia wakili wake Audax Kahendaguza, aliwasilisha pingamizi la awali kupin ga kusimamishwa kwa shindano hilo. Mapema, jana mahakama hiyo ilisikiliza pingamizi la awali la Lundenga na kutolea uamuzi wa kulitupilia mbali.

Kutokana na kutupiliwa mbali kwa pingamizi hilo, mahakama hiyo ilisikiliza maombi ya Patel ya kutaka zuio la shindano hilo.

BENIN YATAJA NYOTA WAKE WATAKAOIVAA STARS




Kocha wa timu ya Taifa ya Benin, Olle Didier Nicolle ametaja kikosi cha wachezaji 18 kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumapili (Oktoba 12 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mfaransa huyo ameita wachezaji 13 wanaocheza nje ya nchi hiyo akiwemo kiungo Stephane Sessegnon wa West Bromwich Albion ya Uingereza kwa ajili ya mechi hiyo ya Kalenda ya FIFA itakayoanza saa 11 jioni.

Wachezaji wengine katika kikosi hicho ni Didier Sossa (AS Dragons FC de I’Oueme, Benin), Abdel Fadel Suanon (Etoile Sportive du Sahel, Tunisia), Jodel Dossou (FC Liefering, Austria), Sessi D’almeida (FC Girondis Bordeaux, Ufaransa), Mohamed Aoudo (JS Saoura, Algeria) na Saturnin Allagbe (US Krake, Benin).

Steve Mounie (HSC Montpellier, Ufaransa), Farnolle Fabien (Clermont Foot Auvergne 63, Ufaransa), Jordan Adeoti (SM Caen, Ufaransa), Michael Pote (Omonia Nikosia, Cyprus), David Djigla (FC Girondis Bordeaux, Ufaransa) na Seidou Baraze (Kawkab Marrakech, Morocco).

Jean Ogouchi, Centre Mberie Sportif Club, Benin), Nafiou Badarou (ASO Chlef, Algeria), Eric Tossavi (Avrankou Omnisport, Benin), Fortune Ore (US Krake, Benin) na Seibou Mama (US Krake, Benin).

Msafara wa timu hiyo utaanza kuingia nchini kesho (Oktoba 9 mwaka huu) kwa nyakati tofauti, na utakuwa umekamilika (Oktoba 10 mwaka huu). Timu hiyo itafikia hoteli ya JB Belmont.

TFF YATIMIZA MIAKA 50 YA UANACHAMA FIFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo (Oktoba 8 mwaka huu) linaadhimisha miaka 50 ya kujiunga na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Katika kuadhimisha siku hii TFF ilipanga kufanya tafrija fupi ya kuwaenzi wale wote waliotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania katika kipindi hicho cha miaka 50.

Hafla hii itafanyika katika siku nyingine itakayopangwa. Orodha kamili ya watunukiwa imeambatanishwa hapa (attached).

Tuesday, October 7, 2014

WANYARWANDA KUZICHEZESHA STARS NA BENIN, MKUDE, MGEVEKE NA KINDA WA AZAM WAONGEZWA KIKOSINI



Waamuzi kutoka Rwanda ndiyo watakaochezesha mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kati ya Taifa Stars na Benin itakayofanyika Jumapili (Oktoba 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Hakizimana Louis ndiye atakayeongoza waamuzi hao wa FIFA kwa kupuliza filimbi kwenye mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni. Atasaidiwa na Simba Honore na Niyitegeka Jean Bosco.

Mechi hiyo itatanguliwa na ile ya viongozi wa dini- Kiislamu vs Kikristo kudumumisha upendo, amani na ushirikiano itakayoanza saa 9 kamili alasiri. Tiketi za elektroniki zitakazotumika kwa mechi hiyo tayari zimeanza kuuzwa kwa kiingilio cha sh. 4,000 na sh. 10,000.

Wakati huo huo, Kocha Mart Nooij ameongeza wachezaji watatu kwenye kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ili kukiongezea nguvu kwa ajili ya mechi hiyo.

Wachezaji walioongezwa ni Jonas Mkude na Joram Mgeveke kutoka timu ya Simba, na Gadiel Michael wa Azam.
MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Oktoba 8 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF, Jengo la PPF Tower.

TANZANIA YAKOSA UENYEJI FAINALI ZA AFRIKA 2017


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefahamishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa Tanzania haitaweza kuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika- AFCON 2017 kwa kuwa haijawahi kuandaa fainali zozote za vijana Afrika. Fainali hizo ni zile za vijana wenye umri chini ya miaka 17 na 20.

Hivyo, TFF inaelekeza nguvu zote katika kuandaa Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka U17 mwaka 2019.

Tunapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanazania, Jakaya Kikwete kwa kututia moyo katika kuomba uenyeji wa AFCON 2017.
Pia tunamshukuru Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kwa juhudi binafsi alizozionyesha katika jitihada za Tanzania kuomba uenyeji wa AFCON 2017.
TFF inaamini kwa dhati kuwa uenyeji wa Afrika U17 2019 utaifungulia Tanzania milango ya kuandaa mashindano makubwa zaidi.

MASHIRIKISHO YA SANAA YAANDAA SEMINA KWA MAOFISA WA ULINZI NA USALAMA



Na Beatrice Lyimo, Maelezo

UMOJA wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania umeandaa semina itakayofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 22-23 Oktoba mwaka huu kwa Maofisa wa vyombo vya ulinzi na Usalama pamoja na vyombo vya usimamizi wa sheria nchini ikiwa ni mkakati wa taasisi hiyo katika kukabiliana na tatizo la wizi wa kazi za wasanii nchini.

Hatua hiyo inakuja kufuatia Umoja huo kutoridhishwa na hatua stahiki ikiwemo adhabu zinazochuliwa na vyombo vyenye mamlaka ya kulinda na kutetea haki za wasanii nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu (Oktoba 6, 2014), Katibu wa Umoja huo, Godfrey Ndimbo alisema taasisi hiyo imekusudia kuendesha semina ya siku mbili kwa Maofisa wa taasisi za Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Mahakimu kwa malengo ya kutambua na kuthamini kazi za wasanii nchini.

“Tumeamua kushirikisha Maofisa wa Polisi, Maofisa wa Uhamiaji, na Mahakimu kwa kuwa tumebaini kuwa adhabu ya mtu ambaye anapatikana na hatia ya wizi wa kazi za msanii ni ndogo, tukiweza kuwashirikisha polisi na watu wa uhamiaji wataweza kujua tatizo lilivyo na jinsi ya kulikabili” alisema.

Aidha Ndimbo alisema semina hiyo, ambayo ni sehemu ya maandalizi ya siku ya Msanii Tanzania, inatarajia kushirikisha wasanii mbalimbali nchini, ambapo mada mbalimbali zinatarajia kuwasilishwa ikiwemo elimu kuhusu mafao ya uzeeni, matibabu kupitia bima za afya, Haki Miliki na HakiShiriki.

Aidha Ndimbo alizitaka taasisi mbalimbali kujitokeza katika kusaidia semina hiyo, kwa kuwa mafunzo hayo yamelenga katika kuwasaidia na kuwaendeleza wasanii wa Tanzania, hivyo kuungana na wasanii wengine ulimwenguni katika kusheherekea siku ya Msanii Duniani inayoadhimishwa tarehe 25. Oktoba kila mwaka ulimwenguni.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo, Ndimbo alisema katika maadhimisho hayo kutokuwepo na tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya Humanitarian Award na Life Time Achievement ambazo zitatolewa kwa wasanii bora waliofanya kazi nzuri na kuthaminiwa na jamii.

“Tunaamini kwa tuzo hizi zitatoa changamoto kwa wasanii kujihusisha zaidi na jamii na kufanya kazi zao kwa ufanisi. Hii itawapa changamoto kufanya kazi bora na kusisitiza kauli mbiu ya mwaka huu isemayo Sanaa ni kazi” alisema.

Monday, October 6, 2014

MAKOCHA 32 KUHUDHURIA KOZI YA OLIMPIKI


Makocha 32 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watahudhuria kozi ya ukocha ya ngazi pevu (advance) iliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kupitia Olympic Solidarity kwa ushirikiano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 13 mwaka huu.

Kozi hiyo itakayomalizika Oktoba 25 mwaka huu, itaendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ulrich Marriot kutoka Shelisheli, na makocha wanatakiwa kuripoti hosteli za TFF zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Oktoba 12 mwaka huu jioni.

Makocha hao ni Ahmed Suleiman Simba (Alliance), Akida Saidi (Lindi), Ally Bushir Mahmoud (Zanzibar), Aloyce Akwilin (Pwani), Amin Rashid Mdowe (Zanzibar), Augustino Dakto Damian (Katavi), Athuman Bilal (Shinyanga), Bakari Shime (Tanga), Charles Mayaya (Shinyanga) na Choki Abeid (Geita).

Edna Lema (Morogoro), George Melchior (Kagera), Godfrey Kapufi (Katavi), Hamis Mabo (Kigoma), Hawa Bajangero (TWFA), Ibrahim Mulumba (Geita), Jemedari Said (TAFCA), Kenny Mwaisabula (TAFCA), Madenge S. Omari (Mara), Milambo Camil (Tabora) na Mohamed D (Ruvuma).

Mohamed Ismail Laiser (Manyara), Mohamed Muya (Dodoma), Ngawina Ngawina (Mtwara), Nicholas Kiondo (Ilala), Osuri Charles Kosuri (Simiyu), Rachel Palangyo (TWFA), Salvatory Edward (Temeke), Seif Bausi Nassor (Zanzibar), Yusuf Macho (Kigoma), Wilfred Mollel (Iringa) na Zacharia Mgambwa (Rukwa).

Makocha watakaofaulu kozi hiyo watapewa Leseni C za ukocha za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

MASHINDANO YA U 12 TAIFA KUFANYIKA MWANZA




Mashindano ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 12 yatafanyika Desemba mwaka huu jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa kutangaza mpango wa programu ya vijana inayolenga Fainali za Afrika za U17 mwaka 2019 ambapo Tanzania imeomba kuwa mwenyeji, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema mashindano hayo yatashirikisha kombaini za mikoa yote.

Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Desemba 6 hadi 12 Mmwaka huu, na timu zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza, Desemba 5 mwaka huu. Bajeti ya mashindano hayo ni sh. milioni 350.

Rais Malinzi aliwashukuru wakurugenzi wa shule za Alliance (James Bwire) na Lord Baden Powell (Kanali mstaafu Idd Kipingu) kwa kukubali shule zao kuwa za kwanza kuanzia programu hiyo ya vijana.

Pia aliishukuru kampuni ya Symbion ambayo imetoa sh. milioni 100 kwa ajili ya kuunga mkono mashindano hayo ya U12. Symbion ni moja ya wadau wanaoshirikiana na TFF katika mpango wa miaka mitano ya programu za vijana.

Mkurugenzi wa Symbion, Stewart John Hall aliwasilisha kwa waandishi wa habari programu hiyo ambayo imeambatanishwa (attached).

KIINGILIO CHA CHINI STARS VS BENIN BUKU NNE



Kiingilio cha mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Benin (Squirrels) itakayochezwa Jumapili Oktoba 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni sh. 4,000.

Mashabiki watakaolipa kiingilio hicho katika mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa ni kwa ajili ya viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu. Kwa washabiki watakaokaa jukwaa la VIP B kiingilio ni sh. 10,000. Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo ni za elektroniki.

Viti vya VIP A na C hakutakuwa na viingilio, na badala yake vitatumika kwa ajili ya wageni maalumu watakaolikwa kutoka katika madhehebu ya dini za Kikristo na Kiislamu.

Mechi kati ya Taifa Stars na Squirrels itaanza saa 11 kamili jioni, na itatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo, amani, udugu na ushirikiano kati ya timu za taasisi za dini ya Kiislamu na Kikristo itakayochezwa kuanzia saa 9 kamili alasiri.

Wakati huo huo, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini leo (Oktoba 6 mwaka huu) kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi dhidi ya Benin.

Timu hiyo chini ya Kocha Mart Nooij kesho (Oktoba 7 mwaka huu), Jumatano (Oktoba 8 mwaka huu) na Ijumaa (Oktoba 10 mwaka huu) saa 10 jioni itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Thomas Ulimwengu kutoka timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) na kiungo Mwinyi Kazimoto kutoka timu ya Al Markhiya ya Qatar tayari wametua nchini kujiunga na kikosi cha Taifa Stars.

Naye mshambuliaji Juma Liuzio kutoka timu ya Zesco ya Zambia anawasili nchini kesho (Oktoba 7 mwaka huu) mchana kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Ndola kupitia Nairobi.

Kwa mujibu wa Kocha Nooij, timu hiyo itakuwa na vipindi (sessions) 11 vya mazoezi kabla ya kucheza na Benin (Squirrels). Stars itafanya mazoezi asubuhi na jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa ambapo baadhi yatafanyika Uwanja wa Taifa, na mengine kwenye uwanja mwingine.

Wachezaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Mwinyi Kazimoto anayechezea timu ya Al Markhiya ya Qatar wanawasili nchini kesho (Oktoba 6 mwaka huu).

Naye mshambuliaji Juma Liuzio anayechezea timu ya Zesco ya Zambia atawasili nchini keshokutwa (Oktoba 7 mwaka huu) kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Ndola.

TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI, WACHEZAJI WA NJE WATUA



Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaingia kambini leo (Oktoba 6 mwaka huu) kujiwinda kwa mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Benin itakayochezwa Oktoba 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaingia kambini kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi cha wachezaji 26 walioitwa na Kocha Mart Nooij kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 11 jioni.

Kwa mujibu wa Kocha Nooij, timu hiyo itakuwa na vipindi (sessions) 11 vya mazoezi kabla ya kucheza na Benin (Squirrels). Stars itafanya mazoezi asubuhi na jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa ambapo baadhi yatafanyika Uwanja wa Taifa, na mengine kwenye uwanja mwingine.

Wachezaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Mwinyi Kazimoto anayechezea timu ya Al Markhiya ya Qatar wanawasili nchini kesho (Oktoba 6 mwaka huu).

Naye mshambuliaji Juma Liuzio anayechezea timu ya Zesco ya Zambia atawasili nchini keshokutwa (Oktoba 7 mwaka huu) kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Ndola.

MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Oktoba 6 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF, Jengo la PPF Tower.

MAFUNZO YA USAJILI LIGI DARAJA LA PILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaendesha mafunzo ya usajili kwa klabu za Ligi Daraja la Pili (SDL) yatakayofanyika kesho na keshokutwa (Oktoba 6 na 7 mwaka huu) kwenye hosteli ya TFF iliyopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia saa 3 asubuhi.

Mafunzo hayo yatahusu usajili wa mtandao ambao ndiyo klabu hizo zitautumia kwa ajili ya Ligi hiyo itakayoanza baadaye mwezi ujao katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.

Kesho mafunzo hayo yatakuwa kwa ajili ya maofisa wa usajili wa klabu za Abajalo, Arusha FC, Kiluvya United, Magereza Iringa, Milambo SC, Mji Mkuu (CDA), Mkamba Rangers, Mshikamano, Mvuvumwa FC, Navy, Njombe Mji, Singida United, Transit Camp, Volcano FC na Wenda FC.

Oktoba 7 mwaka huu mafunzo hayo yatahusisha maofisa usajili wa klabu za Bulyanhulu FC, Eleven Stars, JKT Rwamkoma, Kariakoo Lindi, Mbao FC, Mpanda United, Pamba, Town Small Boys na Ujenzi Rukwa.

MABADILIKO YA MECHI ZA FDL KUNDI B
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko kwa baadhi ya mechi za kundi B Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kupokea barua kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) ikieleza kuwa Uwanja wa CCM Kirumba utatumika kwa shughuli za kidini kuanzia Oktoba 16 hadi 19 mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, mechi namba 17 kati ya Toto Africans na Green Warriors iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo Oktoba 18 mwaka huu sasa itafanyika Oktoba 20 mwaka huu.

Mabadiliko hayo pia yameathiri mechi namba 19 kati ya Green Warriors na Oljoro JKT ambayo sasa itachezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Oktoba 23 mwaka huu badala ya Oktoba 21 mwaka huu.

Vilevile mechi namba 25 kati ya Burkina Faso na Oljoro JKT imesogezwa mbele kwa siku moja kutoka Oktoba 25 mwaka huu hadi Oktoba 26 mwaka huu. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.