KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 17, 2011

Rose, Bahati wapigwa kumbo


WANAMUZIKI nyota wa Injili nchini, Rose Muhando, Bahati Bukuku na Flora Mbasha mwishoni mwa wiki iliyopita walishindwa kung’ara katika tuzo za muziki huo baada ya kupigwa kumbo na waimbaji chipukizi.
Licha ya majina ya waimbaji hao watatu kuwemo katika tuzo ya mwimbaji bora wa kike, walifunikwa na waimbaji chipukizi Martha Mwaipaja, Christina Shusho, Upendo Nkone na Upendo Kilahiro.
Mshindi wa tuzo hiyo alikuwa Christina, ambaye aliwafunika vibaya Rose na Bahati.
Boniface Mwaitege aliibuka mshindi wa tuzo ya mwimbaji bora wa kiume wakati tuzo ya kundi bora la mwaka ilinyakuliwa na Double E.
Tuzo ya wimbo bora ilinyakuliwa na mwimbaji mkongwe Upendo Nkone wakati tuzo ya video bora ya mwaka ilinyakuliwa na John Lisu kupitia wimbo wake wa Jehova yu hai.
Mwimbaji chipukizi Miriam Shilwa alitwaa tuzo ya balozi bora wa jamii baada ya kumshinda Flora.
Mratibu wa tuzo hizo kutoka Tanzania Gospel Music Award (TGMA), Harris Kapiga alisema washindi walipatikana kutokana na kupigiwa kura na mashabiki wa muziki huo.
Wanamuziki wengine wa kiume waliopigiwa kura ya kuwania tuzo ya mwimbaji bora wa kiume walikuwa Jackson Bent, Fanuel Sedekia, Ambwene Mwasongwe na John Lisu.
Waimbaji wengine waliokuwa wakiwania tuzo ya wimbo bora ni Christina Mbilinyi ‘Nasubiri baraka zangu’, Miriam Mauki ‘Double Double’, Upendo Kilahiro ‘Usifurahi mwenzako anapofanikiwa’ na Martha Mwaipaja ‘Usikate Tamaa’.
Tuzo ya wimbo bora kwa wanaume iliwaniwa na Thomas Bernard ‘Jehova ananipa kushinda’, Christopher Israel ‘Hosana’, Danford Sunday ‘Mwacheni Mungu’, Aaron Kyara ‘Juu Mbinguni’ na Charles Thobias ‘Akili zangu zimefika mwisho’.

Sunday, March 13, 2011

BONANZA LA WANAHABARI LILIVYOFANA DAR








Wadau kutoka vyombo mbalimbali vya habari, vikiwemo Uhuru Publications Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani na Radio Uhuru wakijiburudisha wakati wa bonanza la vyombo vya habari lililofanyika jana kwenye ufukwe wa klabu ya Cine iliyopo Msasani, Dar es Salaam. Bonanza hilo liliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) na kudhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).




Friday, March 11, 2011

MISS UTALII 2011 APATIKANA

HUYU ndiye Adelqueen Njozi, Miss Utalii 2011. Alishinda taji hilo mwishoni mwa wiki iliyopita katika shindano lililofanyika kwenye hoteli ya Kiromo iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani. Hapa alikuwa akizungumza na waandishi wa habari juzi kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dar es Salaam.

SURVIVALS SISTERS WAPEWA BAJAJ

RAIS Jakaya Kikwete juzi alitekeleza ahadi aliyotoa kwa wasanii wa kundi la muziki wa kizazi kipya la Survival Sisters baada ya kuwazawadia Bajaj kwa ajili ya kuwasaidia katika shughuli zao mbalimbali. Pichani, Kaimu Mnikulu Kassim Mtawa akikabidhi Bajaj hizo kwa wasanii hao, Irene Malekela (kushoto) na Ratifa Abdalla. (Picha ya Ikulu).


Thursday, March 10, 2011

Semsekwa: Nilitimuliwa Extra Bongo kimizengwe


MWIMBAJI na rapa machachari wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International, Greyson Semsekwa amedai kuwa, alitimuliwa katika bendi ya Extra Bongo Next Level kimizengwe na bila kujua tatizo lake.
Akihojiwa katika kipindi cha televisheni cha Nyumbani ni Nyumbani cha TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita, Semsekwa alisema kiongozi wa Extra Bongo, Ally Choki alifikia uamuzi wa kumtimua bila kumueleza kosa lake.
“Kusema kweli Choki hakuwahi kuniita kunieleza kosa langu, nilisoma habari hizo kupitia kwenye vyombo vya habari,”alisema mwanamuziki huyo.
Semsekwa alisema katika bendi ya Extra Bongo, maamuzi yote yanafanywa na mtu mmoja (Choki) na kwamba hakuna uongozi wa pamoja.
“Mfukuze mtu kwa sababu maalumu, sio unalipuka tu. Huku ni kuvunjiana heshima,”alisema rapa huyo, ambaye alijizolea sifa kwa rapu yake inayosema ‘kichaa kapewa rungu’.
“Kabla ya kufikia uamuzi wa kumfukuza mtu kazi, unatakiwa umwite na kumweleza kosa lake na ikiwezekana unamwandikia barua na kama kuna madai yake unamlipa,”alisema.
“Yeye (Choki) baada ya kutoa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, akawa ananikimbia, simu anazima, kwa nini? Kiongozi wa bendi unakuwa mwoga?”aliongeza.
Semsekwa ametoa shutuma hizo kwa Choki siku chache baada ya Extra Bongo kuwatimua wanamuziki wake kadhaa na kuajiri wengine wapya saba.
Wanamuziki wapya waliochukuliwa na Extra Bongo ni pamoja na Rogert Hegga ‘Caterpilar’, Saulo John ‘Ferguson’, George Kanuti, Oseah, Isaack Buriani ‘Super Danger’, Otilia Boniface ‘Kandoro’ na Hassan Mussa ‘Super Nyamwela’
Akiwatambulisha wanamuziki hao kwa waandishi wa habari, Choki alijigamba kuwa, amepania kuifanya bendi yake iwe tishio kimuziki nchini.
Semsekwa alisema hana kinyongo na TOT na kwamba yote yaliyotokea kwake yamekwisha kwa vile ameshajipanga upya katika bendi ya Twanga Pepeta.
Alisema ameamua kujiunga na Twanga Pepeta kwamba sababu ni bendi kongwe na yenye mafanikio makubwa na pia ndiyo iliyomtambulisha kimuziki.
“Niliwahi kuimbia Twanga Pepeta kabla ya kwenda Extra Bongo. Hiki ni chuo cha mafunzo. Hata hao wanaoidharau, walipata sifa na umaarufu walipokuwa Twanga Pepeta, “ alisema.
“Nashangaa, mtu amejifunzia maisha hapa, halafu anapotoka anapadharau na kupakashifu. Huko ni kupotoka,”alisema.
Semsekwa alisema aliamua kwenda Twanga Pepeta yeye mwenyewe baada ya kupata taarifa za kutimuliwa kwake Extra Bongo na kusisitiza kuwa, hajapoteza kitu.
“Nitaibuka na mambo mapya na mazito. Nataka kule nilikitoka wajue kwamba wamepoteza chombo chenye thamani kubwa,”alisema.
“Ukiondoa Msondo Ngoma na Sikinde, hakuna tena bendi nyingine bora hapa nchini kama Twanga Pepeta. Hizi zingine ni sawa na raba za kichina. Ukitaja bendi tano bora nchini, huwezi kuikosa Twanga Pepeta. Nami niliamua nije kwenye bendi bora,”alisema.

K-One akamilisha albamu yake mpya

MSANII chipukizi wa muziki za kizazi kipya nchini, Karim Othman amekamilisha kazi ya kurekodi albamu yake ya kwanza, inayojulikana kwa jina la ‘Sina hakika’.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Karim, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la K-One alisema, albamu hiyo itakuwa na vibao sita, alivyovirekodi kwenye studio za Baucha Records.
K-One alisema amerekodi baadhi ya vibao vyake kwa kuwashirikisha wasanii mbalimbali nyota wa muziki huo kama vile Tundaman, Chegge, Ali Kiba, Madee na Baker.
Alisema ameamua kurekodi na wasanii hao kwa lengo la kuzipa nyimbo zake ladha tofauti na pia kuongeza ushirikiano kati ya wasanii wakongwe na chipukizi hapa nchini.
“Unajua hii ni albamu yangu ya kwanza, hivyo nitakapotoka lazima nitoke kiaina sio kiubabaishaji, ndio maana niliomba kampani ya wakali hawa watano,”alisema.
Alivitaja vibao vitakavyokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Ngoja niseme’, ‘Dhahabu’, ‘Nielewe’, ‘Niwaambie’, ‘Weekend special’ na ‘Sina hakika’.
Kwa mujibu wa K-One, albamu hiyo inatarajiwa kuingia sokoni mwishoni mwa mwezi huu chini ya usimamizi wa Baucha Records.
Msanii huyo mwenye sura ya mvuto alisema pia, tayari ameshatengeneza video ya wimbo wa ‘Sina hakika’, ambao ndio utakaobeba albamu hiyo. Video hiyo imerekodiwa na kampuni ya Showbize.
“Nawaomba mashabiki wangu wakae tayari kunipokea kwa sababu ninakuja kwa mtindo wa aina yake. Nakuja kuwashika,”alisema msanii huyo mwenye maskani yake Kiwalani, Dar es Salaam.

BASATA kuboresha tuzo za muziki za Kili

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) linatarajia kuzipa taswira mpya tuzo za muziki za Tanzania, kuanzia zile zitakazofanyika mwaka 2012.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema mjini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii kuwa, tayari bodi ya baraza hilo imeshapitisha uamuzi wa kuboresha tuzo hizo.
Materego alisema hayo wakati wa Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye ukumbi za baraza hilo uliopo Ilala Sharrifu Shamba mjini Dar es Salaam.
Alisema lengo la uamuzi huo ni kuzifanya tuzo hizo ziwe na mvuto, ubora na kuwa maarufu katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki kutokana na jinsi zitakavyoandaliwa na kufanyika.
“Baraza kila mara limekuwa likifanyiakazi mapendekezo na michango ya wadau, hivyo kuanzia tuzo za muziki za mwaka 2012, kutakuwa na marekebisho makubwa yatakayoshirikisha wadau wengi na lengo kuu ni kuzipa taswira mpya na kuzifanya zizidi kuwa na ubora,” alisisitiza.
Materego alisema wamekuwa wakizifanyia maboresho tuzo hizo kila mwaka, lakini baadhi ya wadau wamekuwa wakizilalamikia kwa madai kuwa, hazijakidhi ubora na hadhi inayotakiwa.
Alitoa mwito kwa wadau kujikita kwenye kutoa changamoto za kujenga, lakini huku wakielewa kwamba, tuzo hizo hazina muda mrefu kiasi cha kuweza kumaliza changamoto zote zilizopo.
“BASATA iko wazi muda wote kupokea changamoto na michango ya wadau, ndiyo maana kwenye mpango mkakati wa Baraza wa mwaka 2011-2014, tumebeba kwa kiwango kikubwa ushauri uliopatikana kwenye jukwaa hili la sanaa,” alisema Materego.
Awali, msanii Witness anayepiga muziki wa miondoko ya hip hop aliwasilisha mada kuhusu uzoefu wake kwenye tuzo mbalimbali za muziki barani Afrika.
Katika mada yake hiyo, Witness alieleza kukerwa kwake na tabia ya vyombo vya habari na kumbi za burudani nchini kupiga nyimbo za nje kwa kiwango kikubwa pasipo kuzipa nafasi zile za nyumbani.
“Ukienda Afrika Kusini radio na kumbi zao za burudani hupiga kwa asilimia kubwa muziki wao na hiki ndicho kinaufanya muziki na wanamuziki wa nchi hiyo kuvuma na kutambulika dunia nzima. Hapa kwetu ni tofauti, utakumbana na miziki ya akina 50 Cent na Ja Rule, kuna haja ya hili kusimamiwa kikamilifu,” alisema.

Mwalala ampibu Timbe

Na Emmanuel Ndege
MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Yanga, Bernard Mwalala ametua nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Kocha Sam Timbe.
Mwalala alitua nchini wiki iliyopita kwa ajili ya kufanyiwa majaribio na Timbe ili aweze kuichezea tena Yanga msimu ujao.
Mshambuliaji huyo aliyeichezea Yanga kwa mafanikio makubwa, alikuwepo uwanjani wakati timu hiyo ilipomenyana na mahasimu wao Simba katika mechi ya ligi na kutoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Mwalala alisema amekuja nchini kwa ajili ya kukutana na Timbe ili kuangalia kama anaweza kumfanyia majaribio.
"Napenda kujiunga tena na Yanga. Nilikuwa Uganda kwa siku chake pale SC Villa, sasa nataka kurejea kuitumikia klabu hii, ambayo naipenda toka moyoni mwangu,"alisema mchezaji huyo ambaye ni raia wa Kenya.
Mmoja kati ya viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema mchezaji huyo ameshafanya mazungumzo na Timbe.
Mchezaji huyo pia amekuwa akifika kwenye mazoezi ya Yanga mara kwa mara yanayofanyika katika uwanja wa Uhuru huku akionyesha kuvutiwa na wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho.
Akizungumzia ujio wa mchezaji huyo, Timbe alisema anamfahamu vizuri Mwalala na ana imani ataweza kuisaidia timu hiyo katika msimu ujao wa ligi kuu.
Hata hivyo, Timbe alisema atalazimika kumfanyia majaribio mchezaji huyo kabla ya kuamua kumsajili au la.

Simba yaikodia ndege TP Mazembe



KIKOSI cha wachezaji 20 wa Simba kinatarajiwa kutua nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wiki jayo kwa ajili ya pambano lao dhidi ya TP Mazembe.
Simba na TP Mazembe zinatarajiwa kumenyana mwishoni mwa wiki ijayo, katika mechi ya awali ya raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, msafara huo utawajumuisha mashabiki 25 pamoja na wabunge na baadhi ya wafanyabiashara maarufu nchini.
Rage alisema mipango yote kwa ajili ya safari hiyo inaendelea vizuri na kuongeza kuwa, wana imani kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo.
Mwenyekiti huyo alisema kamati ya utendaji ya Simba inatarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kupanga mikakati zaidi ya kushinda pambano hilo.
Kwa mujibu wa Rage, uongozi umewaandalia wachezaji zawadi murua iwapo watashinda mechi hiyo. Hata hivyo, Rage hakuwa tayari kutaja zawadi hizo.
Habari zaidi zimeeleza kuwa, benchi la ufundi la Simba limeshapata kanda za video za mechi mbalimbali za TP Mazembe kwa ajili ya kusoma mbinu za wapinzani wao.
Simba itakwenda Congo baada ya mechi mbili za ligi kati yake na Ruvu Shooting na AFC ya Arusha. Ilitarajiwa kucheza na Ruvu Shooting jana mjini Morogoro kabla ya kuvaana na AFC keshokutwa mjini Arusha. Naye Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alijigamba jana kuwa, wamejiandaa vyema kuwashinda wapinzani wao na kusisitiza kuwa, ushindi ni lazima.

Mosha abwaga manyanga Yanga



HALI ndani ya klabu ya Yanga imeendelea kuchafuka baada ya Makamu Mwenyekiti, Davis Mosha kuandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo.
Taarifa za kuaminika zilizopatikana jana na kuthibitishwa na kiongozi mmoja wa juu wa Yanga zimeeleza kuwa, Mosha aliwasilisha barua hiyo juzi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mosha amefikia uamuzi huo kutokana na kuzuka tena kwa hali ya kutokuelewana kati yake na Mwenyekiti, Llyod Nchunga na mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji.
Mosha ametangaza uamuzi wake huo siku chache baada ya kurejea nchini kutoka Uingereza na kushirikiana na viongozi wenzake wa Yanga katika kuiandaa timu kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Simba.
Makamu Mwenyekiti huyo, ambaye imeelezwa kuwa ana nguvu kubwa ya kulinyima raha kundi la Friends of Simba, amekuwa haelewani na Nchunga licha ya kukutanishwa mara kadhaa kwa lengo la kumaliza tofauti zao.
Habari zaidi zimeeleza kuwa, Mosha aliandika barua hiyo baada ya kupata shinikizo kubwa kutoka kwa wajumbe wa kamati, kufuatia uamuzi wao wa kubariki kujitoa kwa Manji kuifadhili klabu hiyo.
Imeelezwa kuwa katika kikao cha kumjadili Manji, Mosha alionekana kuwa na msimamo mkali wa kutaka uongozi usimpigie magoti mfadhili huyo, ambao ulipingwa vikali na Nchunga.
Yanga imejikuta ikiingia kwenye mzozo mwingine mkubwa baada ya Manji kuandika barua ya kujiuzulu kwa kile alichodai, kuandamwa na kashfa za kuihujumu timu hiyo.
Uamuzi huo wa Manji umeugawa uongozi wa klabu hiyo katika makundi mawili, ambapo moja linaupinga na kumtaka arejee wakati lingine limebariki kuondoka kwake na kutaka asinyenyekewe.
“Mosha ameamua kuachia ngazi ili kulinda heshima yake na kumwacha Nchunga afanye anavyotaka,” kimesema chanzo cha habari.
Kuna habari kuwa, huenda wajumbe wengine zaidi wa kamati ya utendaji ya Yanga wakatangaza kujiuzulu, kufuatia kubainika kuwepo kwa mipango ya kuwatimua kwenye uongozi watu wanaompinga Manji.
Juhudi za kumtafuta Nchunga ili athibitishe taarifa hizo, hazikufanikiwa jana kwa vile kila alipopigiwa simu yake ya mkononi, haikuwa na majibu.

BINGWA KOMBE LA NSSF KUPATA Mil 3.5/-

MKURUGENZI wa Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Crescentius Magori (kushoto) akikabidhi vifaa vya michezo kwa Katibu wa klabu ya Uhuru, Rashid Zahor (kulia) katika hafla iliyofanyika jana makao makuu ya mfuko huo mjini Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Kombe la NSSF, Masoud Saanani. (Picha kwa hisani ya Francis Dande wa globu ya Jami).

BINGWA wa michuano ya soka ya Kombe la NSSF kwa mwaka 2011, atazawadiwa kitita cha sh. milioni 3.5 wakati mshindi wa netiboli atapata sh. milioni tatu.
Akitangaza zawadi hizo kwa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori alisema, mshindi wa pili katika soka atazawadiwa sh. milioni 2.5 na watatu sh. milioni 1.5.
Magori alisema mshindi wa pili wa netiboli atazawadiwa sh. milioni mbili wakati mshindi wa tatu atapata sh. milioni moja. Alizitaja zawadi zingine kuwa ni sh. milioni 2.5 kwa wafungaji wa michuano yote miwili.
Kwa mujibu wa Magori, wameamua kuiboresha zaidi michuano ya mwaka huu kwa kuongeza zawadi kwa washindi, ambapo jumla ya zawadi zote ni sh. milioni 14.
Mkurugenzi huyo alisema NSSF inaona fahari kuandaa michuano hiyo kwa vile imekuwa ikisaidia kutangaza shughuli zake na kuwataka washindi waheshimu kanuni walizojiwekea.
Alisema kamati ya mashindano imejitahidi kuzifanyiakazi dosari zote zilizojitokeza katika michuano iliyopita na kuongeza kuwa, katika siku zijazo, huenda ikazishirikisha timu zingine kutoka nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Masoud Saanani alisema, jumla ya timu 17 zinatarajiwa kuchuana katika mchezo wa soka na zingine 11 katika netiboli.
Masoud alivitaja vyombo vya habari vitakavyoshiriki katika michuano ya mwaka huu kuwa ni wenyeji NSSF, Mlimani Media, Changamoto, New Habari, IPP Limited, Global Publishers, Habari Zanzibar, Mwanahalisi na Radio Kheri.
Vingine ni Free Media, Uhuru Publications Ltd, Tumaini Media, Mwananchi, Jambo Leo, Sahara Communications, Business Times na TBC.
Mwenyekiti huyo alisema michuano ya mwaka huu itachezwa kwa mtindo wa ligi, ambapo timu za soka zimegawanywa katika makundi manne, moja likiwa na timu tano na matatu yakiwa na timu nne kila moja.
Alisema kundi A litakuwa na timu za Business Times, Changamoto, NSSF na Mlimani Media wakati kundi B litakuwa na timu za Habari Zanzibar, Global Publishers, New Habari na Radio Kheri.
Kundi C litakuwa na timu za Uhuru, Mwananchi, Mwanahalisi, Tumaini Media na Sahara Communications wakati kundi D litakuwa na timu za IPP, TBC, Jambo Leo na Freee Media.
Kwa upande wa netiboli, Masoud alisema kundi A litakuwa na timu za NSSF, Global Publishers na Tumaini Media, kundi B timu za Mwananchi, Uhuru, New Habari na Free Media wakati kundi C litakuwa na timu za Business Times, Habari Zanzibar, TBC na IPP.
Michuano ya mwaka huu imepangwa kuanza Machi 19 hadi Aprili 16 mwaka huu na itachezwa kwenye viwanja vya TCC na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu (DUCE) vilivyopo Chang’ombe, Dar es Salaam.
Katika mechi za ufunguji, mabingwa watetezi wa soka, Business watamenyana na wenyeji NSSF wakati katika netiboli, Global Publishers watamenyana na Tumaini Media.

Wednesday, March 9, 2011

Soka si uadui



WACHEZAJI Juma Kaseja (juu kushoto) wa Simba na Shadrack Nsajigwa wa Yanga wakipongezana mara baada ya pambano kati ya timu hizo kumalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.

PICHA nyingine chini inamuonyesha mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba na Isaack Boakye wa Yanga wakipozi katika picha ya pamoja

Marlaw, Besta kufunga ndoa keshokutwa


Wanamuziki wawili wa muziki wa bongo fleva hapa nchini, Marlaw na Besta Jumamosi hii wanatarajia kuwa mwili mmoja kwa kufunga pingu za maisha.
Mmiliki wa blogu hii anawatakia kila la heri katika maisha ya ndoa,mtangulizeni Mungu katika ndoa yenu na mpendane,mvumiliane na kuheshimiana. Pia mawasiliano yawe nguzo yenu katika kudumisha urafiki wenu na mapenzi yenu.

Friday, March 4, 2011

Simba, Yanga nani zaidi kesho?


Na Rashid Zahor
HAYAWI hayawi yamekuwa. Baada ya subira na majigambo ya muda mrefu, hatimaye miamba miwili ya soka nchini, Simba na Yanga leo inakutana katika mechi ya ligi kuu ya Vodacom, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hilo linalogusa hisia za mashabiki wengi wa soka nchini, linatarajiwa kuwa kali na gumu kwa vile kila timu imepania kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, iliyochezwa Oktoba 16 mwaka jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Yanga iliichapa Simba bao 1-0.

Je, Yanga itaendeleza ubabe wake kwa Simba ama vijana hao wa Msimbazi watalipiza kisasi kwa wenzao wa Jangwani?

Swali hilo na mengineyo kadhaa ndiyo yaliyotawala hisia za mashabiki wa klabu hizo mbili, ambao baadhi yao huangua kilio, kupatwa na huzuni au hata kushindwa kula kila timu yao inapofungwa.

Hadi sasa, Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 38 baada ya kucheza mechi 17, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 37 kutokana na michezo 16. Azam ni ya tatu kwa kuwa na pointi 36 katika mechi 18 ilizocheza.

Simba itaingia uwanjani ikitokea mafichoni Zanzibar, ilikokwenda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo wakati Yanga itatokea kambini Bagamoyo mkoani Pwani.

Mechi hiyo itakuwa mtihani wa kwanza kwa Kocha Sam Timbe wa Yanga, aliyeanza kuinoa timu hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita, lakini ni ya kawaida kwa Kocha Patrick Phiri wa Simba, ambaye ameshazoea mikikimikiki ya timu hizo mbili.

Timbe alikaririwa juzi akisema kuwa, amemkabidhi jukumu la kuiongoza timu hiyo, kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’, ambaye amerejea kwenye kiwango chake cha kawaida baada ya kusimamishwa kwa miezi kadhaa na kocha wa zamani, Kostadin Papic.

Kocha huyo kutoka Uganda alisema, timu yake itawakabili wapinzani wao, ikiwa haina hofu kwa kuwa wanatambua vyema umuhimu wa mechi hiyo na wamejiandaa kwa kila hali kuibuka na ushindi.

Hata hivyo, Timbe alisema timu yake itamkosa kiungo mchezeshaji, Ernest Boakye kutokana na kuwa majeruhi. Alisema mchezaji huyo anasumbuliwa na maumivu ya goti la kushoto.

Kwa upande wa Simba, itawakosa kiungo Hillary Echessa na beki John Owino kutokana na kuwa majerehu. Pia itamkosa kiungo Mohamed Banka, aliyetimuliwa kambini kwa makosa ya utovu wa nidhamu. Lakini itakuwa na faraja kubwa baada ya mshambuliaji wake nyota, Emmanuel Okwi kupona maumivu ya kifundo cha mguu na kurejea uwanjani.

Ushindani mkali katika mechi ya leo unatarajiwa kuwa kwa washambuliaji, Jerry Tegete, Davis Mwape wa Yanga, Mbwana Samatta na Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba, ambao kila mmoja amepania kufunga mabao.

Pambano hilo litachezeshwa na mwamuzi Oden Mbaga kutoka Dar es Salaam, ambaye anatambuliwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA). Atasaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga na Maxmillian Mkongolo wa Rukwa. Mwamuzi wa akiba atakuwa Army Sentimea wa Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 30,000 kwa jukwaa la VIP A, sh. 20,000 jukwaa la VIP B, sh. 10,000 jukwaa la VIP C, sh. 7,000 na sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa na bluu na sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya kijani mzunguko.

Timu zinatarajiwa kupangwa hivi:

Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi, Ibrahim Job, Nsa Job, Kigi Makasi, Davis Mwape, Jerry Tegete.

Simba: Ally Mustapha, Haruna Shamte, Amir Maftah, Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Jerry Santo, Rashid Gumbo, Mbwana Samatta, Patrick Ochan, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Nico Nyagawa.

Msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom hadi sasa ni kama ifuatavyo:

P W D L GF GA Pts
Yanga 17 11 5 1 23 4 38
Simba SC 16 12 1 3 31 14 37
Azam 18 11 3 4 33 12 36
Mtibwa Sugar 18 8 6 4 18 17 30
Kagera Sugar 18 8 5 5 18 15 29
JKT Ruvu 18 6 7 5 17 16 25
Toto African 18 5 5 8 16 21 20
African Lyon 18 4 7 7 14 23 19
Polisi Dodoma 18 4 5 9 8 16 17
Ruvu Shooting 17 3 6 8 12 19 15
Maji Maji 18 2 6 10 10 19 12
AFC 18 3 2 13 12 36 11

Samatta aipania Yanga


Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta wa Simba amesema amejigamba kuwa, lazima awafunge mabao mahasimu wao Yanga katika mechi kati yao keshokutwa.
Akizungumza na Burudani mjini hapa juzi, Samatta alisema amejipanga vyema kuhakikisha anaifunga Yanga kwa mara ya kwanza akiwa amevaa uzi wa Simba.
Samatta alisema anaridhishwa na mazoezi wanayopewa na Kocha wao Patrick Phiri kwa ajili ya mechi hiyo na kusisitiza kuwa, wamejipanga vyema kulipa kisasi cha kufungwa na Yanga katika mzunguko wa kwanza.
Mbali na kushinda mechi hiyo, Samatta alisema lengo la timu yake ni kutwaa tena ubingwa wa ligi hiyi ili wapate nafasi nyingine ya kushiriki michuano ya kimataifa.
"Nawawaomba mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi na timu yao kwani mazoezi tunayoyafanya ni mazuri na pia waweke matumaini makubwa ya kuondoka na ubingwa,”alisema.
Mshambuliaji huyo aliyepachikwa jina la Golden Boy Junior, alitamba pia kuwa, hawana wasiwasi na pambano lao la michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Simba inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho kwa ajili ya pambano lao dhidi ya Yanga litakalofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

PAMBANO LA WATANI WA JADI LANUKIA

WACHEZAJI Jerryson Tegete (kulia) na Athumani Iddi 'Chuji' (kushoto) wa Yanga wakiwa mazoezini mjini Bagamoyo jana kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano lao la ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba litakalochezwa keshokutwa mjini Dar es Salaam. (Na mpiga picha wetu)

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri akitoa maelekezo kwa wachezaji wake juzi wakati wa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika juzi kwenye uwanja wa Fuoni, Zanzibar. (Picha na Haroub Hussein).

WACHEZAJI wa Simba wakiwa mazoezini juzi chini ya Kocha Patrick Phiri (kulia) kwenye uwanja wa Fuoni mjini Zanzibar. Simba inajiandaa kwa pambano lake la ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Yanga, litakalochezwa keshokutwa mjini Dar es Salaam. (Picha na Haroub Hussein)





Acheni kunifuatafuata


MWIGIZAJI filamu nyota wa Nigeria, Stella Damasus amewataka watu waache kufuatilia maisha yake binafsi, badala yake wajikite zaidi katika kazi yake.
Stella alisema mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa kuwa, uhusiano wake na watu ni kazi anayoifanya na siyo kile kinachotokea chumbani kwake.
“Watu wanapaswa kujifunza kuacha kufuatilia maisha yangu. Chochote kinachohusu maisha yangu nje ya kazi, sipendi kukizungumzia,”alisema mwigizaji huyo ambaye pia anamiliki bendi ya muziki.
Stella pia aliwashushia lawama nzito waandishi wa habari wa Nigeria kwa madai kuwa, ni wachache sana wanaoandika habari za uchunguzi. Alisema wengi wamekuwa wakiandika habari za uzushi na uchochezi.
Mcheza filamu huyo alisema anapenda kuishi maisha ya kawaida na hataki kuona umaarufu wake ukiathiri maisha yake kwa namna yoyote.

Kelvin adai yeye si mtukutu

MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Kelvin Ikeduba amesema yeye si mtu mbaya kama watu wengi wanavyomfikiria.
Kelvin alisema mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa kuwa, kuna tofauti kubwa kati ya tabia yake halisi na zile anazoigiza kwenye filamu mbalimbali.
Mwigizaji huyo alisema, licha ya kucheza filamu nyingi akiwa kijana mtukutu, hiyo si tabia yake na haina maana kwamba ni kijana mbaya.
“Kelvin aliye nyuma ya kamera ni kijana wa kawaida tu. Lakini angeweza kuwa kijana mbaya iwapo anataka iwe hivyo,”alisema.
“Inawezekana ni kwa sababu ya mwonekano wangu, nimecheza filamu nyingi nikiwa kijana mtukutu, lakini hii haina maana kwamba mimi ni mtu mbaya,”alisisitiza.

Funke Akindele aporwa


KUNDI la majambazi mwishoni mwa wiki iliyopita lilivamia hoteli ya Imperial ya mjini Lagos na kupora vitu kadhaa na mamilioni ya fedha kutoka kwa wateja, akiwemo mcheza filamu machachari, Funke Akindele.
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema, Funke pamoja na watu wengine wa familia yake, walikuwemo kwenye hoteli hiyo wakati wa tukio hilo, lakini hakuna aliyejeruhiwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, kabla ya uvamizi huo, majambazi hao walipiga risasi hewani kutishia watu na baadaye walianza kuulizia mahali alipokuwepo mwigizaji huyo.
Funke alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini alikataa kulizungumzia kwa undani zaidi ya kumshukuru Mungu kwamba alikuwa salama.
Chanzo cha habari kilisema jumla ya fedha na vitu vilivyoibwa na majambazi hao vinakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Naira milioni mbili za Nigeria.

Ramsey Nouah awa mchungaji!


MSHINDI wa tuzo ya mwigizaji bora wa kiume wa filamu wa mwaka 2010, Ramsey Nouah amesema haoni tatizo kwake kuigiza nafasi ya mchungaji katika filamu ya ‘The Perfect Church’.
Akizungumza mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita, Ramsey alisema awali, hakupenda kuigiza nafasi hiyo, lakini baadaye alijipa moyo na kuona ni changamoto mpya kwake.
Ramsey, ambaye amecheza filamu hiyo kama Mchungaji Benson, alisema ameifurahia nafasi hiyo kwa vile imemtofautisha na filamu nyingi alizowahi kucheza, hasa zinazohusu masuala ya mapenzi.
Mtunzi wa filamu hiyo, Wale Adenuga alisema, ana hakika itapata mafanikio makubwa sokoni kwa vile wametumia utaalamu wa hali ya juu katika kuitengeneza.
Mbali na Ramsey, wasanii wengine walioshiriki kucheza filamu hiyo ni pamoja na Funke Akindele, Hakeem na Ngozi, ambao wameigiza kama bibi na bwana Ojo.