'
Friday, September 29, 2017
TASWA YALAANI TUKIO LA CHIRWA KUMPIGA MWANDISHI WA HABARI
CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na wahariri wa habari za michezo nchini, tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kushambuliwa kwa mwanahabari John Dande, zinazodaiwa kufanywa na straika wa Yanga, Obrey Chirwa, juzi Jumanne Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
TASWA na wahariri wa habari za michezo, tunaalani tukio hilo la kushambuliwa kwa Dande ambaye ni mpigapicha wa Kampuni ya New Habari 2006 Limited, kwani kitendo hicho si cha kiungwana bali ni udhalilishaji wa taaluma ya habari na hujuma kwa tasnia na mambo kama haya yanadhoofisha nguzo muhimu ya kujenga jamii yenye uelewa wa mambo yanayoendelea nchini na kudhoofisha mfumo wa kidemokrasia, ambao tunajitahidi kuuimarisha nchini.
Kukaa kimya, hata tukiliwazwa na kuombwa samahani kwa jambo hili, hakutatoa tafsiri nyingine kwa wana taaluma ya habari na jamii kwa ujumla isipokuwa kuliona jambo hili kama ni la kawaida.
Kama tukio hilo lingefanyika eneo la starehe au mitaani na mwandishi hakuwa kazini, tungelichukulia suala hilo kama faragha inayowahusu watu wawili, aliyepiga na aliyepigwa, lakini kutokana na kumtokea mwandishi akiwa kazini tena uwanjani, ndio tumelazimika kutekeleza wajibu wetu wa kuitetea taaluma na haki ya mwandishi wa habari kufanya kazi bila kusumbuliwa au vitisho.
Kifungu cha 7 cha sheria za huduma za habari Na 12 ya mwaka 2016 kinaaainisha uhuru wa habari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Hivyo ni vyema wadau wetu wakatambua kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro.
Tunatoa tamko hili la kulaani kitendo hicho kwa sababu sio cha kawaida hapa nchini kama ilivyo baadhi ya nchi nyingine ambazo waandishi wanapigwa na hata kuuliwa. Lakini tunachelea kulifumbia macho tukio hili kwa sababu kufanya hivyo ni kusema tunaridhika kupigwa na wachezaji na baadaye viongozi na hata mashabiki.
TASWA na wahariri wa habari za michezo na waandishi wa habari kwa ujumla hawana na hawatakuwa na muhali na mchezaji, kiongozi au shabiki yeyote wa michezo anayefanya kitendo kama hiki, kwani huo ni uhuni na sio mwanzo mzuri na tunataka mwendo kama huu ukome mara moja na yeyote mwenye malalamiko kwa mwandishi wa habari binafsi, au chombo chake afuate taratibu za kistaarabu zilizopo.
Hata hivyo kwa kuwa mhusika ameripoti tukio hilo kwenye vyombo vya usalama, tunawaomba waandishi wa habari wawe watulivu na waziachie mamlaka husika zitekeleze majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi.
Tunaomba ushirikiano mzuri kati ya waandishi, wachezaji na viongozi wa michezo ili tucheze na tufurahie michezo kwa amani na kila mmoja aheshimu kazi ya mwenzake. Michezo iwe furaha kwa wote. Tucheze bila kupigana.
UANACHAMA AIPS
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS), chenye makao yake makuu Lausanne, Uswisi, kimeanza kupokea maombi ya kadi kwa wanachama mwaka 2018/2019 kwa waandishi wa habari za michezo kutoka nchi mbalimbali duniani.
Maombi hayo yanafanyika kwa njia ya mtandao kwa wanachama wapya na wale wa zamani kupitia mtandao wao wa www.aipsmedia.com, ambapo ukiingia katika hiyo tovuti, utakuta maelekezo ya namna ya kupata kadi mpya, haichukui dakika tano kujaza na ukishaituma itakupa maelekezo zaidi ya hatua ya kufuata.
Tunawahimiza wanachama wetu kuchukua pia uanachama wa AIPS, kwani una faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kupata kadi ya uanachama ambayo inatoa fursa mbalimbali ikiwemo mafunzo ya muda mrefu na semina za michezo mbalimbali.
UCHAGUZI MKUU
Mapema mwezi huu tulitoa tamko la kuwepo Uchaguzi Mkuu wa chama chetu na kuwataka wanachama ambao wapo kwenye leja kuanzia Julai mwaka 2007 hadi Julai mwaka huu walipie ada zao za mwaka mmoja, ili kuhuisha uanachama wao na mwisho wa kufanya hivyo ni Septemba 30.
Lakini kutokana na muitikio mdogo sana katika ulipaji wa ada, Kamati ya Utendaji ya TASWA imeongeza muda hadi Oktoba 10 mwaka huu wanachama wote wahakikishe wanalipia ada hizo ili wahesabike wapo hai.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment