UONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra (Sikinde), umemteua mwanamuziki mkongwe na mpiga drums nguli nchini, Habibu Abbas 'Jeff' kuwa mkurugenzi wa bendi.
Uteuzi huo umelenga kuuimarisha uongozi wa bendi, hasa katika masuala ya udhibiti wa mapato na matumizi ya fedha na nidhamu kwa wanamuziki.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa bendi hiyo, Hassan Bitchuka, alisema jana kuwa, uteuzi huo ulifanywa wakati bendi hiyo ilipokuwa ziarani nchini Kenya, mwezi uliopita.
"Katika bendi yetu kumekuwa na matatizo makubwa ya utovu wa nidhamu kwa wanamuziki, hivyo tumemteua Jeff kuwa mkurugenzi kwa lengo la kudhibiti vitendo hivyo," alisema mwanamuziki huyo mkongwe.
"Baadhi yetu sisi ni wapole na huwa tuna huruma sana linapokuja suala la kumchukulia hatua mwanamuziki anayeonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu mara kwa mara. Lakini sasa tunaamini Jeff ataimudu kazi hiyo kwa sababu hana woga,"aliongeza.
Kwa mujibu wa Bitchuka, hiyo ndio itakayokuwa kazi na majukumu ya Jeff na kwamba shughuli za viongozi wengine zitaendelea kama kawaida.
Mbali na Jeff, viongozi wengine wa Mlimani Park kwa sasa ni Abdalla Hemba, ambaye ni kiongozi mkuu na Mjusi Shemboza, ambaye ni katibu wa bendi. Bitchuka ni kiongozi mwandamizi.
Akizungumzia uteuzi huo, Jeff alisema ameupokea kwa mikono miwili na atashirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha kuwa, bendi hiyo inapata mafanikio makubwa zaidi.
"Ni kweli nimeteuliwa kuwa mkurugenzi wa bendi, nitakayeshughulikia nidhamu na kusimamia mapato na matumizi na mikataba yote itakayoingiwa na bendi,"alisema Jeff.
Hii ni mara ya pili kwa Jeff kuteuliwa kwenye uongozi wa bendi hiyo. Katika uongozi uliopita, Jeff alikuwa kiongozi mkuu huku Hamisi Milambo akiwa katibu wa bendi na Ramadhani Mapesa akiwa mtunza hazina.
No comments:
Post a Comment