'
Sunday, March 19, 2017
YANGA YATUPWA NJE LIGI YA MABINGWA WA AFRIKA
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga jana walitupwa nje ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Zanaco ya Zambia.
Katika mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Lusaka, Yanga ilikuwa ikihitaji ushindi au sare ya mabao zaidi ya mawili ili iweze kusonga mbele.
Kwa matokeo hayo, Yanga imetolewa kwa faida ya bao la ugenini, ambalo Zanaco ililipata wiki iliyopita, timu hizo zilipotoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kutokana na kutolewa katika michuano hiyo, Yanga sasa imeangukia kwenye kapu la michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo sasa itavaana na timu nyingine iliyotolewa katika michuano hiyo ili kupata timu 16 zitakazofuzu kucheza hatua ya 16 bora.
Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam watashuka dimbani leo kurudiana na Moroka Swallows ya Swaziland mjini Mbabane.
Katika mechi ya awali, Azam ilishinda bao 1-0 hivyo inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment