KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, March 25, 2017

TAIFA STARS KUJIPIMA NGUVU KWA BOTSWANA LEO


Na Alex Matias,Dar es salaam
Nahodha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samatta amedai mabadiliko ya kikosi cha timu hiyo yaliyofanywa na Kocha Mkuu, Salum Mayanga hayawezi kuathiri nguvu na mipango yao ya kupambana katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Botswana utakaopigwa jioni ya Leo uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Alisema Kocha Mayanga aliamua kufanya mabadiliko hayo kutokana na kutambua udhaifu uliopo kwenye kikosi hicho, hivyo kuamua kuwaita wachezaji wengine wapya ambao wataleta chachu ya ushindi kwa timu hiyo iliyo katika nafasi ya mbaya ya msimamo wa viwango vya Shirikisho la Soka Duniani(FIFA) vilivyotolewa hivi karibuni.
Samatta alisema ni kweli timu ya Taifa inahitaji wachezaji wazoefu watakaoendeleza mbinu zitakazotolewa na Kocha Mkuu lakini wengi wa wachezaji wakongwe waliopo kwenye timu hiyo walishindwa kuonesha uwezo wao na hatimaye kuipeleka timu mahali pasipo stahili kuelekea.
“Nasikia jinsi watu wanavyolaumu uamuzi uliofanywa na Kocha Mayanga, lakini mi nataka niwaambie ukweli Watanzania kwamba hawa wachezaji ambao wanawasema ni wakongwe ni lazima na wao wakae pembeni wawapishe wachezaji wapya waoneshe uwezo na kitu kipya walichokuwa nacho ambacho kitakuja kuliinua taifa katika anga la kimichezo,” alisema Samatta.
Kwa upande wake Kocha Mayanga, alisema mchezo huo ni wa kwanza kwake utampatia nafasi ya kujua mapungufu na uhiamara wa kikosi chake kabla ya kuelekea kwenye michuano ya AFCON inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi Juni mwaka huu.
Alisema kutokana na mazoezi mazuri waliyoyafanya kwa siku nne mfululizo yatawasaidia kuibuka na ushindi mkubwa pamoja picha ya ubora wa kikosi hicho chenye malengo ya kupanda maradufu kwenye viwango vya FIFA.
Alidai anaamini wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho watatumia akili na nguvu zao zote ili kuhakikisha Botswana haichomoki na ushindi wa aina yoyote ile huku akiwataka watanzania kujenga imani na kikosi hicho chenye wachezaji vijana zaidi.
“Kwenye kikosi chetu hiki safari hii kuna wachezaji wengi ambao ni vijana, niliwaamini na ndio maana nikaamua kuwaita kwenye kikosi change, kwahiyo Watanzania tarajieni makubwa zaidi katika mchezo wetu huu wa kesho(leo) utakaopigwajijini Dar es Salaam,” alisema Mayanga.
Alisema ni vigumu kutoa ahadi katika mchezo wa mpira wa miguu kutokana na kwamba hawajui timu wanayokwenda kushindana nayo imejiandaa vipi dhidi ya mchezo huo ambao unaumuhimu mkubwa kwa pande zote  mbili.
Wakati huohuo, Kocha wa Timu ya Botswana, Peter Buttler alisema wanauchukulia mchezo wao wa kirafiki na Taifa Stars kuwa ni zaidi ya wa kirafiki kutokana na kuona umuhimu uliopo kwenye mchezo huo ambao unatambuliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na (FIFA).
“Tumekuja Tanzania kupambana na naomba niwashukuru kwa ukarimu wao wote waliotuonesha ila kiukweli ni lazima tuibuke na ushindi kwa gharama yoyote ile kwa sababu tunataka tupande zaidi kwenye msimamo wa viwango vya soka katika mataifa ya Afrika tofauti na hivi ilivyo sasa,” alisema Buttler.
Mbali na hilo, Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Alfred Lucas alitoa taarifa za kubadilishwa kwa kiwango cha chini cha gharama za kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo ambapo hapo awali ilikuwa ni Tsh. 5,000 na sasa kuwa ni Tsh.3,000.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA FULL SHANGWE

No comments:

Post a Comment