UPANDE wa
Jamhuri katika kesi ya kukutwa bangi na misokoto,
inayomkabili msanii Wema Sepetu na wenzake, umeieleza mahakama kuwa upelelezi
wa kesi hiyo uko hatua za mwisho kukamilika.
Kutokana na
hilo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ameutaka
upande huo kujitahidi kukamilisha upelelezi huo mapema.
Wakili wa
Serikali, Constatine Kakula, alidai jana mbele ya Hakimu Simba, kuwa upelelezi
haujakamilika, hivyo aliomba kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi
hiyo.
Baada ya
kueleza hilo, Hakimu Simba aliutaka upande huo kujitahidi kukamilisha upelelezi
mapema.
Wakili Kakula
aliieleza mahakama kuwa, upelelezi huo uko hatua za mwisho kukamilika.
Kabla ya
kuingia katika chumba cha mahakama, Wema aliyekuwa amevalia gauni refu,
alielekezwa na askari kutafuta ushungi wa kufunika kifua chake, ambacho sehemu
kubwa kilikuwa wazi.
Kutokana na
hilo, mmoja wa wanawake waliokuwa wameongozana na Wema, alilazimika kutoa
mtandio wake mweusi na kumpatia msanii huyo ambaye alijifunika sehemu iliyokuwa
inaonekana.
Mbali na Wema, washitakiwa wengine
katika kesi hiyo ni Angelina Msigwa na
Matrida Abas.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na
shitaka la kukutwa na msokoto mmoja wa bangi na vipande viwili vidogo vya bangi,
vyenye uzito wa gramu 1.08.
Washitakiwa hao wanadaiwa walikutwa
na bangi na msokoto huo, Februari 4, mwaka huu, nyumbani kwao Kunduchi Ununio,
wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Wema na wenzake wako nje kwa
dhamana.
No comments:
Post a Comment