KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 1, 2017

SIMBA, YANGA ZAGOMA KUCHEZA NA MAMELODI SUNDOWN



KLABU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zimegoma kucheza mechi za kirafiki za kimataifa na mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Yanga imegoma kucheza na vinara hao wa soka barani Afrika kwa kile kilichodaiwa kuwa, Kocha wake, George Lwandamina, amekataa kwa kuhofia wachezaji wake kuumia.

Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Lwandamina aligomea mechi hiyo kwa madai kuwa mchezo huo ungeingilia programu zake za maandalizi ya mechi za ligi kuu.

“Hatutacheza na Mamelodi kwa sababu kocha ameukataa huo mchezo, amesema unaingilia programu zake, kama unavyojua kwa sasa tupo kwenye hatua ngumu ya Ligi Kuu na wakati huo huo tunaingia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika,” kilisema chanzo cha habari.

Kufuatia Yanga kugomea mchezo huo, waandaaji wa mechi hiyo mbali na kusikitishwa na uamuzi huo, wamefanikiwa kuishawishi Azam kuchukua nafasi ya mabingwa hao wa soka nchini.

Mamelodi ilikuwa icheze na Simba jana kabla ya kuivaa Yanga kesho. Kutokana na mabadiliko hayo, mabingwa hao wa Afrika Kusini sasa kesho watacheza na Azam.

Mamelodi imekuja nchini kwa mwaliko wa klabu ya African Lyon, inayomilikiwa na Rahim Kangezi, kwa ajili ya kushiriki kampeni ya kupiga vita ujangili.

Kwa upande wa Simba, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', amesema Kocha Joseph Omog aliwasilisha mapendekezo ya kugomea mechi hiyo.

Kaburu alimkariri Omog akisema kuwa, kwa sasa Simba haiwezi kucheza mechi hiyo kwa vile inashiriki kwenye ligi kuu na mechi zake zote zilizosalia ni muhimu.

Kiongozi huyo wa Simba alisema mchezo huo ulikuwa mzuri na muhimu kwao, lakini tatizo ni kwamba, umekuja katika wakati mbaya hivyo wanalazimika kuuacha.

No comments:

Post a Comment