'
Sunday, February 26, 2017
SIMBA PUNGUFU YAIDUWAZA YANGA
LICHA ya kucheza ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, Simba jana ilionyesha maajabu baada ya kusawazisha na kuibwaga Yanga mabao 2-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10, baada ya beki wake wa kushoto, Javier Bokungu kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Obrey Chirwa wa Yanga.
Kabla ya Bokungu kutolewa, Yanga ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na kuifanya Simba iwe kwenye wakati mgumu wa kutafuta bao la kusawazisha huku mashabiki wake wakiwa wamenyong'onyea.
Iliwachukua Yanga dakika tano kuhesabu bao kwa njia ya penalti baada ya beki Novatus Lufunga wa Simba kumkwatua Chirwa ndani ya eneo la hatari. Bao hilo lilifungwa na Simon Msuva.
Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Joseph Omog wa Simba kipindi cha pili, yaliongeza uhai kwa timu hiyo licha ya kubaki ikiwa na wachezaji 10. Kocha huyo aliwaingiza Jonas Mkude, Saidi Ndemla na Shiza Kichuya.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo aliisawazishia Simba dakika ya 66 baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Kichuya.
Kichuya aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 80 kwa shuti kali la mbali lililompita kipa Deo Munishi wa Yanga na mpira kujaa wavuni.
Kutokana na ushindi huo, Simba inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 54, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 49, huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment