KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 26, 2017

KAPUMZIKE KWA AMANI MUSSA SORAGA



ILIKUWA saa tano usiku wa kuamkia jana, wakati nilipopokea ujumbe wa maandishi kupitia simu yangu ya mkononi kutoka kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Habari Leo, kituo cha Zanzibar, Khatib Suleiman, ukinijulisha msiba wa mwanahabari mwenzetu mkongwe Mussa Soraga.

Kwa mujibu wa Khatib, Soraga alifariki dunia juzi (Jumamosi), saa 12 jioni, akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) cha Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, ambako alilazwa akiwa chini ya uangalizi maalumu baada ya kupata ajali ya pikipiki.

Ajali hiyo ilitokea siku hiyo hiyo saa tano asubuhi, wakati Soraga akiwa anaendesha pikipiki yake aina ya Vespa, akitokea nyumbani kwake kwenda mjini, alipogongwa na mwendesha pikipiki mwingine maeneo ya barabara ya Dole na kuumia vibaya kichwani.

Wote wawili walikimbizwa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kupatiwa matibabu, lakini Soraga alipoteza maisha ilipofika saa nne usiku akiwa ICU. Mwenzake bado anaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo.

Marehemu Soraga, ambaye asili yake ni mkoa wa Morogoro, alizikwa jana, saa nne asubuhi, kwenye makaburi ya Dole.

Nilipokea taarifa hizo za kifo cha Soraga kwa uchungu mkubwa. Nilipatwa na uchungu kwa sababu tangu nilipofahamiana naye miaka ya mwishoni mwa 1980, alikuwa kama ndugu na kaka yangu.

Wakati huo Soraga alikuwa mwandishi wa habari za michezo wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, kituo chake cha kazi kikiwa Zanzibar, nami nikiwa mwandishi wa kujitegemea wa magazeti hayo. Mbali na uandishi, Soraga pia alikuwa mwajiriwa wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM).

Nilianza kuwa karibu na Soraga baada ya kuajiriwa na Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, mwanzoni mwa miaka ya 1990. Kila nilipopangiwa safari za kikazi kwenda Zanzibar, Soraga ndiye alikuwa mwenyeji wangu.

Alizoea kuja kunipokea bandarini, kunitafutia hoteli na pia kuhakikisha ananifikisha katika maeneo yote niliyotakiwa kufika kwa ajili ya kupata habari. Alikuwa zaidi ya mfanyakazi mwenzangu.

Ndio sababu haikuwa ajabu kwa Khatib, aliponitumia ujumbe ule juu ya kifo cha Soraga, kuandika: 'Zahor, rafiki yako Sogara amefariki kwa ajali'. Alikuwa na kila sababu ya kuandika hivyo kwa sababu waandishi wengi wa habari wa Zanzibar, hasa wakongwe, walikuwa wakiufahamu ukaribu niliokuwa naye.

Wakati nilipokuwa nikienda Zanzibar kwa ajili ya kuandika makala za michezo na burudani, Soraga ndiye aliyenifikisha kwa wanasoka wengi nyota wa zamani visiwani humo kama vile marehemu Mcha Khamis, marehemu Ali Issa, Ibrahim Kapenta na wengineo. Pia alinitembeza kwa waimbaji wengi wakongwe wa taarab visiwani humo na kunikutanisha na viongozi wa kikundi cha taarab cha Culture. Ama kwa hakika nilijifunza na kupata vitu vingi kutoka kwake.

Mbali na hayo, Soraga alikuwa mwandishi wa aina ya pekee visiwani Zanzibar. Haikuwa ikipita siku bila habari zake zinazohusu michezo na burudani kuwemo kwenye magazeti ya Uhuru na Mzalendo. Aliitendea haki tasnia hii kwa kufanya kile ambacho wanahabari wengi wa kizazi cha sasa wanashindwa kukifanya.

Kutokana na ukereketwa wake katika mchezo wa soka, Soraga aliwahi kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa timu ya KMKM na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi Kuu ya Zanzibar, mwanzoni mwa 2000. Pia alisafiri na timu hiyo katika nchi mbalimbali za Afrika kwa ajili ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Kama hiyo haikutosha, uongozi wake thabiti ulimwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), akiiwakilisha wilaya ya Magharibi B, wadhifa ambao aliendelea kuutumikia hadi mauti yalipomfika.

Ninayo mengi ya kumuelezea Soraga, lakini kwa sababu ya mshtuko na uchungu nilioupata kutokana na kifo chake, inaniwia vigumu kuyaeleza. Hakika sisi sote ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.

Nakumbuka siku mbili kabla ya Soraga kufikwa na mauti, niliposti kwenye mtandao wa facebook, makala zangu kadhaa za wachezaji wa zamani na wanamuziki nyota wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), waliowahi kutembelea Tanzania, ambazo niliandika miaka mingi ya nyuma.
Soraga alikuwa mmoja wa marafiki zangu wa FB waliochangia kwenye post hizo.

"Bosi wangu, hiki ndicho ninachokupendea. Unatukumbusha vitu vingi vya zamani," aliandika Soraga kwenye moja ya posti hizo.

Katika moja ya maandishi yangu kwenye posti hizo, nilimkumbusha Soraga vijiwe vya chakula, alivyokuwa akinipeleka kupata ugali, chakula ambacho ni adimu na ghali sana visiwani Zanzibar. Akaishia kucheka.

Pia, nikampa neno la shukurani, nikimueleza kuwa kamwe siwezi kumsahau katika maisha yangu kutokana na msaada mkubwa aliokuwa akinipatia kila nilipokwenda Zanzibar kikazi.

Katika majibu yake aliandika hivi: "Hata nami nakushukuru sana bosi wangu. Kwa ujumla tulisaidiana sana kikazi, kiasi kwamba tuliyafanya magazeti ya Uhuru na Mzalendo kupata chati huku Zanzibar kwa habari za michezo."

Pia aliandika: "Rafiki zetu uliowaulizia Mcha Khamis na Ali Issa walishatangulia mbele ya haki. Hawakupishana sana. Nasi sote ndio njia yetu." Kumbe ndio alikuwa akiniaga.

Marehemu Soraga alikuwa akipenda kuniita bosi kwa sababu miaka kadhaa ya nyuma nilikuwa Mhariri wa Michezo katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo, hivyo kila alipoandika habari au makala zinazohusu michezo na burudani, ilikuwa lazima zipitie kwangu. Hata nami nilipenda kumwita bosi kwa sababu ya uzoefu na ukongwe wake katika tasnia hii na pia ukweli kwamba, alinizidi kiumri.

Buriani Soraga. Umetangulia kwenda kule ambako kila mmoja wetu lazima atafika. Maana ishi vyovyote utakavyoishi, fanya chochote utakachokifanya, lakini hakuna atakayeweza kukiepuka kifo. Kila mmoja wetu atakumbana nacho kwa wakati na siku aliyopangiwa na Mungu. Ni siri kubwa ya Allah.

Japokuwa mauti huuwa mwili wa binadamu ukabaki kuwa vumbi kaburini, lakini yale yote aliyoyafanya hapa duniani, yatabaki kuwa kumbukumbu katika maisha ya wengine.

Pumzika kwa amani Bradha Soraga.

No comments:

Post a Comment