KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, December 28, 2014

YANGA, AZAM HAKUNA MBABE



TIMU za soka za Yanga na Azam jana zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutokana na matokeo hayo, timu hizo mbili sasa zimefikisha pointi 14 kila moja, lakini Yanga inashika nafasi ya pili kutokana na kuwa na idadi ya mabao mengi ya kufunga.

Mtibwa Sugar, ambayo juzi ilitoka sare ya bao 1-1 na Stand United kwenye uwanja wa Manungu ulioko Turiani mjini Morogoro, bado inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 16.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tano lililofungwa na Didier Kavumbagu kwa shuti kali baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya.

Yanga ilisawazisha dakika mbili baadaye kwa bao lililofungwa na Amis Tambwe kwa shuti kali lililomshinda kipa Mwadini Ally wa Azam. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Mshambuliaji machachari na mwenye kasi, Simon Msuva aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 52 baada ya kufumua shuti kali la umbali wa mita 30 lililotinga moja kwa moja wavuni.

Azam ilisawazisha dakika ya 65 kwa bao lililofungwa na John Boko baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi iliyopigwa na Himidi Mao.

No comments:

Post a Comment