KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, December 23, 2014

JK AMPONGEZA DIAMOND KWA KUTWAA TUZO ZA AFRIKA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza mwanamuziki Nassib Abdul maarufu kwa jina la Diamond na Mshindi wa Shindano la Big Brother Africa, Idris Sultan kwa kuiletea sifa Tanzania kupitia sanaa.


Rais Kikwete ametoa Pongezi hizo alipokutana na Msanii Diamond Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumanne Desemba 23, 2014 , ambapo Msanii huyo amemwonyesha tuzo tano alizoshinda baada ya kupambanishwa na wasanii wengine wa Afrika.

Pamoja na pongezi hizo kwa Diamond na Idris kwa kile alichosema wameitoa nchi kimasomaso, Rais Kikwete amewasihi wasanii hao kujihadhari na athari za umaarufu na utajiri katika umri mdogo,zikiwemo kujitumbukiza katika matumizi ya dawa za kulevya na ulevi.

Kikwete amewaasa kuwa ni muhimu kwa wasanii hao kutumia mapato wanayoyapata katika kazi zao za usanii kwa kujijenga kifamilia ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba zao za kuishi na wanafamilia wanaowategemea pamoja kuwasaidia wasanii wenzao.

“Umaarufu katika sanaa yoyote ile ni wa kupita hivyo tumieni umaarufu mlio nao sasa kama fursa ya kujijenga kimaisha na sio kutumbukia katika kadhia za kidunia kama vile ulevi, ukorofi mbele ya jamii na mambo mengine yasiyofaa", aliwaasa Mhe. Rais.

Rais Kikwete pia alimpongeza Sultan kwa kuiletea Tanzania sifa na kumtakia mafanikio zaidi katika shughuli zake za baadaye. Rais Kikwete alisema kuwa Sultan hakuifedhehesha Tanzania kwa kutofanya mambo yaliyo kinyume na maadili ya Mwafrika alipokuwa katika jumba la Big Brother Africa.

Kwa upande wake,Diamond amemshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa ushirikiano anaoutoa kwa wasanii hapa nchini, hali ambayo amesema ndiyo iliyowawezesha kupata mafanikio kitaifa na kimataifa.

Diamond pia amemuahidi Rais Kikwete kutekeleza yote aliyomuasa kuhusu kujiheshimu na kutolewa umaarufu alionao, na kwamba ataendelea kufanya kazi zake za usanii wa Muziki kwa juhudi zake zote kuitangaza nchi.

Msanii huyo pia amemweleza Rais Kikwete kuwa hivi karibuni atapokea tuzo nyingine ya sita kutoka huko Nigeria.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
23 Desemba,2014

No comments:

Post a Comment