'
Tuesday, December 16, 2014
TFF YATUMA RAMBIRAMBI KIFO CHA KOCHA MSHINDO MADEGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Kocha Mshindo Madega kilichotokea leo (Desemba 16 mwaka huu) mjini Bukoba.
Mbali ya kuwahi kuwa mchezaji katika timu ya RTC Kagera, Kocha Madega aliwahi kufundisha timu za Kagera Stars, Mwadui na kombaini ya Copa Coca-Cola ya Mkoa wa Kagera.
Mchango wake katika mchezo wa mpira wa miguu tangu akiwa kocha na baadaye kocha utakumbukwa daima.
Tunatoa salama za rambirambi kwa familia ya marehemu, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA), Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Kagera na klabu ya Bukoba Veterans na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.
TFF itawakilishwa kwenye msiba huo na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA).
MICHUANO YA COPA COCA-COLA YAENDELEA KUTIMUA VUMBI
Michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya Taifa inaendelea leo jioni (Desemba 16 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani.
Uwanja wa Nyumbu uliopo mkoani Pwani utazikutanisha timu za Mjini Magharibi na Dodoma katika mechi ya kundi B, wakati kundi C kutakuwa na mechi kati ya Arusha na Mwanza itakayochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers uliopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Wakati kesho (Desemba 17 mwaka huu) ikiwa ni mapumziko, michuano hiyo itaingia hatua ya robo fainali keshokutwa (Desemba 18 mwaka huu) kwenye viwanja hivyo hivyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment