KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 4, 2014

KIBA: SINA BIFU NA DIAMOND



MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba amesema hana ugomvu wala bifu yoyote na msanii mwenzake nyota wa fani hiyo, Naseeb Abdul 'Diamond'.

Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC mwishoni mwa wiki, Kiba alisema amekuwa akishangazwa na taarifa hizo, ambazo zimekuwa zikiripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini.

"Mimi sina bifu au tatizo lolote na Diamond. Sielewi taarifa hizo zinatoka wapi,"alisema Kiba, ambaye ni msanii pekee nchini aliyewahi kurekodi nyimbo zake na baadhi ya wasanii maarufu duniani.

Kiba alisema uhusiano wake na Diamond ni mzuri kwa sababu wote ni wasanii na kila mmoja ana malengo yake katika fani ya muziki.

“ Namuheshimu sana, anaiwakilisha vyema nchi yetu, sielewi kwa nini watu wamekuwa wakizusha na kukuza vitu vya uongo. Nilidhani wangekuwa wamechoka, lakini bado tu wanazusha mambo kila kukicha,"alisema.

Hata hivyo, alikiri kuwa yeye si mpenzi wa nyimbo za Diamond na kusisitiza kuwa, haoni iwapo ana mpinzani katika fani hiyo hapa nchini.

Hivi karibuni, Kiba aliibuka na nyimbo mbili mpya, Mwana na Kimasomaso, ambazo zimeshaanza kushika chati katika vituo mbalimbali vya redio nchini na kuhusudiwa na mashabiki.

Kiba amerekodi nyimbo hizo baada ya kuwa kimya kwa zaidi ya miaka miwili, ukimya ambao ulikuwa ukitafsiriwa vibaya na mashabiki wake.

"Ni kweli kwamba nilikuwa kimya kwa muda mrefu, lakini si kwa sababu ambazo zimekuwa zikielezwa na watu mbalimbali. Ukimya wangu ulilenga kusoma mchezo unakwendaje na nitoke vipi,"alisema msanii huyo.

Kiba pia alikanusha madai kuwa, ukimya wake ulitokana na hali mbaya ya kifedha aliyokuwa nayo kutokana na nyimbo zake kutopokewa vyema na mashabiki kama alivyotarajiwa.

Kwa mujibu wa Kiba, video za nyimbo zake mpya zinatarajiwa kukamilika hivi karibuni kabla ya kuanza kuonyeshwa kwenye vituo mbalimbali vya televisheni.

Kiba alisema katika muziki, ni vizuri msanii kusoma mchezo mara kwa mara ili kujua utoke vipi badala ya kurudia kitu kile kile. Alisema ni muhimu kwa msanii kuwa mbunifu ili aweze kwenda na wakati.

Kabla ya kurekodi nyimbo hizo mbili mpya, Kiba aliwahi kutamba kupitia vibao vyake mbalimbali kama vile Cinderella, Mapenzi yanarun dunia, Single boy na Dushelele. Kibao cha Dushelele kiliweka rekodi ya kuuza nakala nyingi nchini na katika nchi jirani.

Sifa kubwa ya Kiba ni kutunga mashairi yenye mvuto na ujumbe mzuri kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kutumia nahau na semi mbalimbali. Kwa mfano, katika wimbo wake mpya wa Kimasomaso, ametumia msemo maarufu unaosema 'Mwenda tezi na omo, marejeo ngamani.'

Kiba pia ni mwimbaji mwenye sauti nzuri na yenye mvuto, ikiwa ni pamoja na kuwa hodari wa kuwaburudisha mashabiki anapokuwa stejini. Ameshafanya ziara za kimuziki katika nchi nyingi duniani.

Mwaka 2011 alikwenda Marekani kurekodi wimbo na wanamuziki nyota wa Afrika. Alishiriki kurekodi wimbo huo uliotungwa na mwanamuziki nyota duniani, Robert Kelly akiwa na kina 2Face (Nigeria), Navio (Uganda), Amani (Kenya), Fally Ipupa (DRC), JK (Zambia),
4x4 (Ghana).

No comments:

Post a Comment