KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, August 18, 2014

FIFA KUBORESHA MAKAO MAKUU YA TFF




Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (FIFA) limeahidi kuboresha makao makuu ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) yaliyoko kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Ilala ili yawe katika kiwango cha kisasa ikiwa ni
pamoja na kuwa na vitendea kazi na miundombinu ikiwa ni pamoja na upanuzi
wa ofisi.

Hatua hiyo itaiwezesha TFF kuwa na mazingira bora ya
kufanya shughuli zake kwa ufanisi.

Vilevile kupitia programu zake mbalimbali ikiwemo ile ya Goal, FIFA imeahidi
kushirikiana na TFF katika kuendeleza mradi wa kiuchumi kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume.

Mwanzoni mwa mwaka huu, TFF ilihamishia makao yake makuu katikati ya
jiji ili kupisha maendeleo ya kuiwezesha Karume kuwa kituo cha kisasa kwa
michezo na vitega uchumi.

Akiongea mwishoni mwa ziara ya kikazi nchini, Meneja Miradi wa FIFA
anayeshughulikia Programu za Afrika, Zelkifli Ngoufonja amesema
FIFA inaunga mkono wazo la kuboresha makao makuu ya Karume na itasaidia
kwa awamu uboreshaji huo.

Katika kuhakikisha usimamizi na utekelezaji
barabara wa mradi huo, ujumbe huo wa FIFA ulikubaliana na Kamati ya
Utendaji ya TFF kuboresha ofisi za Karume ili jengo la utawala lianze
kutumika huku mradi ukitekelezwa kwa awamu.

Pamoja na kuongelea mradi huo muhimu kimichezo na kibiashara, ujumbe huo
uliokuwa nchini kwa juma moja kufuatia mwaliko wa TFF ulikuwa na nafasi ya
kujadiliana na TFF kuhusu maboresho katika masuala mbalimbali yakiwemo ya
Utawala, Fedha, Masoko, Ufundi, Mashindano na timu za taifa.

Akiongea kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya TFF, Rais wa TFF Jamal Malinzi
aliushukuru ujumbe huo wa FIFA kwa msaada mkubwa katika historia ya
mahusiano kati ya FIFA na TFF.

Ujio huo unafuatia maombi ya TFF kuwa sehemu ya mradi wa Performance wa
FIFA. Mradi wa Performance unaoshirikisha nchi
mashirikisho 163 kati ya wanachama 209 wa FIFA, unalenga kuongeza ufanisi
katika uendeshaji na uongozi wa nchi wanachama wa FIFA.

No comments:

Post a Comment