KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, September 29, 2012

SIMBA YACHANJA MBUGA, YAIUA PRISONS



SIMBA leo imezidi kuchanja mbuga katika michuano ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Prisons mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo zilimaliza kipindi cha kwanza zikiwa sare ya bao 1-1.
Simba ililazimika kumaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 baada ya beki wake wa kushoto, Amir Maftah kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Khalid Fupi wa Prisons.
Prisons ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 10 lililofungwa na Elias Maguri kwa shuti lililombabatiza beki Juma Nyoso na kumpoteza maboya kipa Juma Kaseja.
Sunzu aliisawazishia Simba dakika ya 45 kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Mrisho Ngasa, ambaye tangu alipojiunga na klabu hiyo msimu huu, amekuwa tegemeo kubwa la timu hiyo.
Ngasa aliifungia Simba bao la pili dakika ya 55 kwa shuti dhaifu, ambalo kipa David Abdalla wa Prisons alilidaka, lakini mpira ulimpokonya na kutinga wavuni.
Kutokana na kuonyeshwa kadi nyekundu, Maftah hataichezea Simba katika mechi ijayo dhidi ya Yanga, itakayochezwa Jumatano ijayo. Nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Paul Ngelema.
Mbali na Maftah, mchezaji mwingine atakayeikosa mechi hiyo ni mshambuliaji, Emmanuel Okwi ambaye alionyeshwa kadi nyekundu wakati Simba ilipomenyana na JKT Ruvu. Okwi amefungiwa mechi tatu.
Simba imeendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi nne, ikifuatiwa na Azam yenye pointi tisa.

No comments:

Post a Comment