KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 26, 2012

SAINTFIET-ALIAJIRIWA KWA BASHASHA KAONDOKA KICHWA CHINI


JAPOKUWA huenda usiku wa Ijumaa iliyopita haukuwa mzuri kwa watu wengi, lakini kocha Tom Saintfiet kwake ulikuwa mbaya zaidi.
Kocha huyo hakutegemea kama mazungumzo yaliyochanganyika na malumbano kati yake na viongozi wa Yanga mbele ya wachezaji wakati alipofuatwa kwenye hoteli ya Protea Masaki, Dar es Salaam ili aeleze sababu za timu kuvurunda katika ligi kuu, kama yangefuta kibali chake cha kuishi Tanzania, nchi inayosifika kuwa kisiwa cha amani.
Hawezi kuendelea kuishi kwenye ardhi ya bongo kwa sababu hana kazi kwa sasa na yeye ni mgeni, hivyo akilipwa chake arudi Ubelgiji kuendelea na maisha ya Ulaya.
Kwake maisha ya Masaki ni 'bye bye' na aliyapa kisogo baada ya kumalizika kwa kikao cha kumjadili na kuambiwa kuwa kibarua chake kimeota nyasi kuanzia muda huo.
Saintfiet ni kati ya makocha walioweka rekodi ya kukaa kipindi kifupi katika klabu hiyo, baada ya kuondolewa kwenye kiti cha enzi akiwa amedumu siku zipatazo 80.
Kati ya siku hizo, tatu zilikuwa za kukamilisha mazungumzo ya kuinoa Yanga baada ya kuwasili nchini, ambapo alitia saini mkataba wa miaka miwili unaodaiwa ulikuwa na thamani ya sh milioni 600.
Lakini Saintfiet ameshindwa kufaidi mamilioni hayo baada ya kuanza kazi Julai 6, mwaka huu, na kufukuzwa Septemba 21! Hajadumu hata miezi mitatu, lakini ukweli ni kwamba huo ndio mwanzo na mwisho wake kupiga mzigo Yanga.
AMEKOSA NINI?
Kwa mujibu wa kocha huyo, ameshangazwa kuambiwa na kiongozi mmoja wa juu kuwa 'kazi basi', lakini dhahiri shairi amemwaga unga baada ya kushupalia sera zake na kukataa kupindishwa na kibosile huyo.
Inadaiwa Mtakatifu Tom hakuwa radhi kuwa kocha wa 'ndiyo mzee' na alijibu mapigo kila alipoona hajazungumzwa vizuri. Kumbe hakujua kama kauli zake zinamchefua mwajiri.
Kitendo bila ya kuchelewa, mwajiri alimwambia kuanzia Ijumaa usiku huo hana kazi na baada ya hapo kikao kikafungwa kwa kila mtu kupitia mlango wake kwenda kulala.
Mzizi wa kikao hicho ulitokana na matokeo mabaya kufuatia Yanga kulazimishwa suluhu na Tanzania Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Sokoine na mchezo uliofuata wiki iliyopita timu hiyo ilifungwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
Viongozi wa Yanga wanasema kosa la kocha huyo kuwaruhusu wachezaji kwenda kucheza muziki usiku mjini Mbeya baada ya kushindwa kuifunga Prisons, ambapo kitendo hicho wanasema sawa na utovu wa nidhamu.
Clement Sanga, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, anasema kuwa jambo la pili kocha huyo ni mkaidi na haambiliki, anataka anachosema kikubaliwe.
Kwa mfano, alikuwa hataki wachezaji wakae kambini, hasa baada ya kutoka Mbeya, ambapo aliamua timu irudi Dar es Salaam na kwenda Morogoro siku mbili baadaye wakati wangeweza kufika mji kasoro bahari na kubaki kambini kuwasubiri Mtibwa.
Ingawa hayo yanaochukuliwa kama makosa yaliyochangia kocha huyo kufukuzwa, ikiwemo kuzungumza 'kwa sana' na vyombo vya habari, kutoboa siri ya kudai mshahara, hana gari, nyumba ya kuishi na wachezaji kulazwa 'mzungu wa wanne', ukweli unabaki pale pale kuwa alitimuliwa kwa sababu ya kutoleana lugha kali na mwajiri wake.
"Tulikuwa tunajadiliana (na bodi ya klabu), waliniuliza maoni yangu kuhusu kinachoendelea, nilitoa mawazo yangu kwa uwazi kabisa, lakini watu wengine walikuwa na mawazo yao juu ya klabu inavyopaswa kuendeshwa, .... akasema kuanzia sasa huna kazi," alisema kocha huyo.
KUVUNJWA MKATABA/KIJEMBE
Hakuna anayejua vipengele vilivyomo katika mkataba wa miaka miwili aliosaini kocha huyo na Yanga, lakini hakuna njia ya kukwepa kumlipa fidia ya kiasi ambacho kitategemeana na vipengele vya mkataba vinasemaje.
Kisheria mlipa fidia ni Yanga kwani ndiye anayetambulika katika mikataba hata kama alishawishiwa na watu binafsi kuja kufanya kazi hiyo.
Kocha huyo juzi kupitia BBC alidai licha ya Yanga kumtupia virago, haijakabidhi barua ya kueleza uamuzi huo na kushangazwa kupoteza ulaji kutokana na mechi mbili.
"Baada ya mechi mbili huwezi kusema tumeanza vibaya, Mourinho (Jose) ana wachezaji bora Hispania, lakini hawezi kushinda kila mechi," anasema Saintfiet.
Amerusha kombora kuwa kufanya vibaya kwa Yanga kulichangiwa na kuongezwa wachezaji wapya ambao hakuwataka isipokuwa aliwatumia kutokana na maslahi ya watu binafsi ambao hakuwataja.
"Nilikuwa na orodha yangu, lakini wao walinunua wachezaji wasiohitajika."
Tangu alipofukuzwa Ijumaa iliyopita, anasema uongozi wa klabu hiyo haujawasiliana naye kujadiliana naye jinsi ya kumlipa fedha zake.
AMETOKA NIGERIA NA MKOSI
Nuksi kwa Saintfiet ilianza wakati alipokuwa Nigeria, ambako mkataba wake wa miaka minne wa Mkurugenzi wa Ufundi ulikatishwa na waziri wa michezo wa nchi hiyo.
Mkataba huo ulipigwa chini ndani ya miezi mitatu akiwa bado hajaanza kazi katika Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF).
Wiki kadhaa baada ya kuteuliwa, Mbelgiji huyo hakuripoti kazini kutokana na kuwepo mvutano juu ya uamuzi huo, ambao ulifutwa Agosti, mwaka huu, na waziri mpya wa michezo, Bolaji Abdullahi.
Uamuzi wa Abdullahi kumtimua kocha huyo ulipokewa kwa hisia tofauti na Wanaigeria kwa baadhi kushangazwa na wengine kumpongeza waziri huyo wa michezo.
Miongoni mwa waliomfagilia waziri huyo ni makocha wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Adegboye Onigbinde na Joe Erico.
Walisema wazo la kuajiri bosi wa kigeni wa ufundi halikuwa sahihi kwa kutambua kuna makocha wengi Nigeria wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.
“Waanzilishi wa wazo hili ni wabinafsi kwa sababu wanatambua makocha kadhaa wa Nigeria wanao uwezo wa kufanya kazi hiyo vizuri," anasema Onigbinde.
“Uzoefu gani ambao anao mkurugenzi wa kigeni, makocha wa Nigeria hawana?” alihoji.
“Ni usaliti mpaka wakati huu nchi yetu kuamini itaimarishwa na watu kutoka nje kuliko wazawa.
Erico alisema kama NFF inataka kuajiri mkurugenzi wa ufundi wa kigeni, haina budi kumwajiri mtu anayefahamu kwa kina mazingira ya soka na historia ya Nigeria.
Kocha wa zamani wa Super Eagles, Paul Hamilton, ametofautiana na Wanigeria hao juu ya kuamini kuna mzawa mwenye ubavu wa kuwa mkurugenzi wa ufundi.
'Filamu' ya Saintfiet iliishia hivyo Nigeria na hatimaye alikuja Yanga Julai mwaka huu kukamilisha mazungumzo ya ajira nyingine iliyovunjika ndani ya siku 77, wakati Nigeria kibarua chake kilidumu siku 90.
Kwaheri Mtakatifu Tom kwani ulipokewa na mashabiki 300 kwa ngoma na vifijo, lakini mnaondoka watatu; wewe, mchumba wako na dereva teksi kwenda uwanja wa ndege wa JNIA tayari kwa safari ya kurudi Ubelgiji.
Kama hana kosa, Yanga watamkumbuka na kama alikosea, hatakumbukwa na yeyote.
Kufukuzwa kocha huyo ni mwendelezo wa kimbunga kilichotua Yanga mapema Ijumaa mchana na kusambaratisha sekretarieti yote chini ya Katibu Mkuu, Mwesigwa Celestine, Masoud Saad-Mtawala, Luis Sendeu,Ofisa Habari na Hafidh Mohamed aliyechomolewa katika umeneja wa timu na kuhamishiwa katika mipango.
REKODI YA SAINTFIET YANGA
1. Yanga v JKT Ruvu (kirafiki) 2-0
2. Yanga v Atletico (Burundi, Kagame) 0-2
3. Yanga v Waw Salam (Sudan, Kagame) 7-1
4. Yanga v APR (Rwanda, Kagame) 2-0
5. Yanga v Mafunzo (Z’bar, Kagame) 1-1 (5-3 penati)
6. Yanga v APR (Rwanda, Kagame) 1-0
7. Yanga v Azam (Kagame) 2-0
8. Yanga v African Lyon (kirafiki) 4-0
9. Rayon v Yanga (kirafiki, Rwanda) 0-2
10. Polisi v Yanga (kirafiki, Rwanda) 1-2
11. Yanga v Coastal Union (kirafiki) 2-1
12. Yanga v Moro United (kirafiki) 4-0
13. Prisons v Yanga (Ligi Kuu) 0-0
14. Mtibwa v Yanga (Ligi Kuu) 0-3

No comments:

Post a Comment