KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 3, 2011

Yanga hoi kwa Mtibwa

KASI ya Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara jana ilipunguzwa baada ya kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Bao pekee na la ushindi la Mtibwa lilifungwa na Hussein Javu, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Yusuf Mgwao. Alifunga bao hilo dakika ya 70 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Juma Abdul.
Kipigo hicho kilionekana kuwakera mashabiki wa Yanga, ambao mara baada ya mchezo, walimzonga Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga na kumtaka awatimue wachezaji wanaoshiriki kuihujumu timu.
Pamoja na kupata kipigo hicho, Yanga bado inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi nne kati yake na Simba, ambayo leo itacheza na African Lyon kwenye uwanja huo.
Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi kwa kufanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la Mtibwa, lakini mashuti ya washambuliaji wake, Jerry Tegete na David Mwape yaliokolewa na kipa Shabani Kado.
Mtibwa ilijibu mashambulizi hayo kwa wachezaji wake, Omary Matuta kuingia na mpira ndani ya eneo la hatari la Yanga, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Dakika tano baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Mtibwa nusura ipate bao wakati Ally Mohamed, alipounasa mpira ndani ya eneo la hatari la Yanga, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Nelson Kimathi.
Dakika ya 54 beki Fred Mbuna wa Yanga alipanda mbele na kumimina krosi iliyomkuta Nurdin Bakari, aliyejitwisha mpira kwa kichwa, lakini ulipaa sentimita chache juu ya lango.
Matuta alipoteza nafasi nyingine nzuri ya kuifungia bao Yanga dakika ya 55 baada ya kupewa pasi na Yusufu Mgwao, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.
Wachezaji wa Yanga, hasa safu ya kiungo walionekana kuchoka katika kipindi cha pili na kutoa mwanya kwa Mtibwa kutawala. Kocha Fred Felix Minziro alisema kipigo hicho kilitokana na bahati mbaya.

No comments:

Post a Comment