KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 3, 2011

CHEZA SIKINDE UPATE KONYAGI


MWAKILISHI wa Mauzo wa Kampuni ya Konyagi, Sankey Mbuja (kulia) akimkabidhi zawadi ya kinywaji cha Konyagi mwanadada Tina Method (kushoto) baada ya kuibuka mshindi wa kujibu maswali yanayohusu bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra. Shindano hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. Wengine pichani ni wanamuziki wa bendi hiyo, Hassan Kunyata, Hamisi Milambo na Habibu Jeff.
BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’, imeanzisha utaratibu wa kuwazawadiwa mashabiki wake vinywaji katika maonyesho yake inayoyafanya kila siku za Jumamosi kwenye ukumbi wa DDC, Kariakoo, Dar es Salaam.
Kiongozi wa bendi hiyo, Habibu Abbas ‘Jeff’ alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, zawadi hizo zinatokana na udhamini walioupata kutoka Kampuni ya Konyagi.
Jeff, ambaye ni mmoja wa wanamuziki wakongwe wa Sikinde alisema, kampuni hiyo imeamua kuidhamini Sikinde kila Jumamosi kwa lengo la kutangaza kinywaji hicho.
Kwa mujibu wa Jeff, wakati wa maonyesho hayo, uongozi wa bendi huwazawadia mashabiki wanaojibu vizuri maswali kuhusiana na Sikinde na wanamuziki wake.
“Maswali yetu hulenga historia ya bendi, wanamuziki na majina ya nyimbo zetu mbalimbali za tangu mwaka 1978 na mashabiki wanaoyajibu vizuri tunawapa zawadi ya konyagi,”alisema.
Katika onyesho la mwishoni mwa wiki iliyopita, mwanadada Tina Method aliibuka mshindi wa kwanza wa zawadi ya Konyagi baada ya kumudu vyema kutaja majina ya wanamuziki wawili pekee waliopo kwenye bendi hiyo tangu ilipoanzishwa hadi sasa. Wanamuziki hao ni mpuliza tarumbeta Joseph Benard na mpiga drums, Jeff.
Naye Mwakilishi wa Mauzo wa Konyagi katika maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam, Sankey Mbuja alisema wamefurahishwa na promosheni inayofanywa na Sikinde kwa kinywaji hicho.
Alisema kutokana na ukongwe wa bendi hiyo katika masuala ya muziki wa dansi, maonyesho yake yamekuwa yakihudhuriwa na mashabiki wengi hivyo kupata nafasi ya kukitangaza vyema kinywaji hicho.

No comments:

Post a Comment