MAKOCHA wanne wa soka kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya wamewasilisha maombi ya kutaka kuinoa Yanga.
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Llyod Nchunga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, makocha hao wanataka kurithi mikoba ya Kostadin Papic, aliyetangaza kujiuzulu wiki iliyopita.
Nchunga alisema miongoni mwa makocha waliowasilisha maombi hayo ni pamoja na Sam Timbe kutoka Uganda.
Alisema tayari wameshafanya mazungumzo ya awali na Timbe na kuongeza kuwa, yamefikia hatua nzuri na wanatarajia kumalizana naye hivi karibuni.
Mwenyekiti huyo alisema makocha wengine waliowasilisha maombi hayo wanatoka katika nchi za England, Jamhuri ya Czech na Slovenia, lakini hakutaja majina yao.
Lakini uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, makocha hao ni Roy Barreto kutoka England, Simeon Efremon kutoka Jamhuri ya Czech na Ivo Von kutoka Slovenia.
Barreto aliwahi kuwa kocha mkuu wa Zimbabwe na kwa sasa anaishi nchini Afrika Kusini. Kocha huyo ametuma wasifu wake kwa njia ya mtandao.
Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umemtangaza Mwesingwa Celestine kuwa kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo.
Celestine anachukua nafasi ya Lawrence Mwalusako, aliyetangaza kujiuzulu wadhifa huo wiki iliyopita.
No comments:
Post a Comment