KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, October 14, 2016

KIKOSI KIPYA CHA SERENGETI BOYS CHAANZA KUANDALIWA




Tanzania imeanza kuandaa kikosi kipya cha timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 - Serengeti Boys kitakachoshindana kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka hiyo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), limeiteua Tanzania kuandaa fainali hizo mwaka 2019 hivyo sasa TFF imeanza kuandaa vijana wake.

Kwa kuanzia tu, imeanza kuwamulika vijana 22 wanaosoma Shule za Alliance zilizoko Mwanza.

Mapema wiki hii, ilimuagiza Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu kwa Vijana, Kim Poulsen kupima uwezo wa vijana hao kwa kufanya nao mazoezi kwenye viwanja vya Alliance ambako amemaliza leo asubuhi na kusema: “Tuna timu bora ya taifa.”

“2019 si tu kwamba Tanzania itashiriki, bali kushindana. Lakini naipongeza TFF na Alliance kwa kuanza program ya kuandaa timu bora. Serengeti Boys ya sasa inayomaliza muda wake iliandaliwa kwa mwaka mkoja, lakini vijana hawa wenye umri wa miaka 12 na 13 ni hazina nyingine kubwa kwa taifa…

“Kwa jinsi nilivyowaona itoshe kusema tu tayari tuna timu. Nimesikia viongozi wa TFF wakisema kwamba jicho lao si kwa vijana hawa tu, bali pia kwa vijana wengine Tanzania nzima. Hili ni jambo zuri lenye manufaa mazuri,” amesema Poulsen alipozungumza na waandishi wa habari leo mara baada ya mazoezi ya asubuhi.

Nahodha wa timu hiyo ya vijana, alishukuru Alliance kwa malezi mazuri na TFF kwa kuendelea kuwajali hasa kwa sasa ambako nao wamesema ndoto zao ni kutaka kung’ara zaidi ya Serengeti ya sasa ambao walitolewa na Congo Brazzaville katika harakati za kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika, zitakazofanyika mwakani nchini Madagascar.

Vijana waliotolewa kwa sasa wanajipanga upya kwenda Korea Kusini kwa ajili ya kujiandaa na ratiba mpya ya CAF na FIFA kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 ambako timu ya taifa kwa hapa Tanzania inaitwa Ngorongoro Heroes. Ratiba za michuano ijayo ya kimataifa, itatolewa baadaye mwaka huu.

SIMBA YAZIDI KUCHANUA LIGI KUU, YANGA YAIUA MTIBWA, JAHAZI LA AZAM LAZIDI KUZAMA


SIMBA imezidi kujikita kileleni mwa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu baada ya kuibanjua Mbeya City mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Mabao yaliyoiwezesha Simba kutoka uwanjani na pointi zote tatu, yalipachikwa wavuni na washambuliaji Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya, kipindi cha kwanza.

Kutokana na ushindi huo, Simba sasa inazo poinri 20 baada ya kucheza mechi nane, ikifuatiwa na Stand United yenye pointi 17.

Ajib aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya ya sita kwa mpira wa adhabu uliotinga moja kwa moja wavuni, kufuatia Kichuya kuchezewa rfau ndani ya eneo la hatari.

Kichuya aliongeza bao la pili dakika ya 37 baada ya kuambaa na mpira pembeni ya uwanja na kufumua shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga walizinduka baada ya kuicharaza Mtibwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Walioiwezesha Yanga kuwatoa kimasomaso mashabiki wao ni Mzambia, Obrey Chirwa, likiwa bao lake la kwanza tangu ligi ilipoanza, Simon Msuva na Donald Ngoma. Bao la Mtibwa lilifungwa na Haruna Chanongo.

Vigogo wengine wa ligi hiyo, Azam waliendelea kuwakosesha raha mashabiki wao baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Bao pekee na la ushindi la Stand United, ambayo wiki iliyopita iliifunga Yanga idadi hiyo ya bao kwenye uwanja huo, lilifungwa na Adam Salamba dakika ya 52.

Monday, October 10, 2016

YANGA KUTUMIA UWANJA WA UHURU



Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inatarajiwa kuendelea keshokutwa Jumatano Oktoba 12, 2016 kwa michezo saba huku ule mchezo kati ya Young Africans ya Dar es Salaam dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro ukipangwa kufanyika Uwanja wa Uhuru jijini.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 6 kipendelea cha kwanza, Young Africans wametambulisha Uwanja wa Uhuru kama uwanja wa nyumbani kwa sasa baada ya kuleta maombi Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF) ambako baada ya kuyafanyia tathimini kwa mujibu kanuni hiyo ya sita, kipendelea cha sita, TFF imeiridhia klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani, kutumia uwanja wa Uhuru.

Hatua hiyo inafuatia na Serikali – mmiliki wa viwanja vya Uhuru na Uwanja Mkuu wa Taifa, kuzuia klabu hiyo pamoja na ya Simba kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa michezo yao ya nyumbani kutokana na vurugu.

Michezo mingine itakayopigwa Jumatano ni kati ya Mbeya City ya Mbeya na Simba ya Dar es Salaam, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya; Majimaji itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Stand United itaikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na katika mkoa huo huo Mwadui itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye dimba la Mwadui Complex huku timu pinzani za Mwanza ‘Mwanza Derby’ kati ya Mbao na Toto Africans itapigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo. Alhamisi Oktoba 13, 2016 Ruvu Shooting itacheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mabatini.

TASWA YAANDAA KONGAMANO MAALUMU LA MICHEZO OKTOBA 20




CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa kongamano maalumu Oktoba 20 mwaka huu kuzungumzia kuhusiana na mifumo ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe nchini za Simba na Yanga zipo mbioni kuingia.

Kama tunavyojua klabu za Simba na Yanga, hivi sasa zipo katika mchakato wa kubadilisha mfumo wao wa kiundeshaji, ambapo Simba inataka kuingia utaratibu wa hisa, wakati Yanga inataka kukodishwa.

TASWA inaamini yapo mambo ambayo pengine wanachama, mashabiki na hata wadau wa mpira wa miguu na wanamichezo kwa ujumla wanapaswa kufahamu kwa undani zaidi kuhusiana na mifumo hiyo miwili ili kuwe na uelewa mpana zaidi.

Ili kufanikisha mdahalo huo ambao ukumbi utakaofanyika utatangazwa hivi karibuni, TASWA imeunda Kamati ya watu sita kusimamia ambao ni Frank Sanga ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Juma Pinto (Mwenyekiti TASWA) na Asha Muhaji (Mhariri wa michezo gazeti la Rai).

Wengine ni Florian Kaijage (Mhariri Mipango Azam TV), Amir Mhando (Mhariri gazeti la Spotileo/Katibu Mkuu TASWA) na Shija Richard (Mhazini Mkuu TASWA).

Mapendekezo ya awali kuhusu washiriki wa kongamano hilo inatarajiwa lihusishe wataalamu kwenye sekta ya michezo, wahariri wa habari za michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ofisi ya Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Wengine ni wanasheria, wataalamu wa masuala ya hisa, viongozi wa klabu hizo na baadhi ya wadau muhimu wa soka nchini, wakiwemo viongozi wa soka wa zamani katika ngazi mbalimbali.

Hata hivyo kikao cha kamati hiyo kitakachofanyika kesho Jumanne kitaandaa utaratibu mzima wa kongamano hilo, ikiwemo kupanga waalikwa na namna ya uendeshaji utakavyokuwa na lengo pia liwe live (mubashara) katika televisheni ili wadau wengi zaidi wafuatilie.

Nawasilisha,

Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
10/10/2016

Sunday, October 9, 2016

BMT YAPINGA YANGA KUKODISHWA


BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limesema kwamba halitambui klabu ya Yanga SC kukodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu, kwa kuwa taratibu haazikufuatwa na Baraza la Wadhamini la klabu hiyo halitambuliki.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa BMT, Mohammed Kiganja amesema kwamba wao wanaendelea kutambua kama Yanga SC ni mali ya klabu na haijakodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu.
Kiganja amesema kwamba, taratibu hazikifuatwa katika mchakato mzima ulioifikisha Yanga SC kwenye kukodishwa, hivyo zoezi hilo ni batili.
“Hatupingi klabu zetu kufanya mabadiliko isipokuwa tunajaribu kuwakumbusha kufuata utaratibu wa kisheria na katiba zao. Kwa sababu unapobadilisha jina au kufanya marekebisho yoyote, ni lazima vikasajiliwe na kutambulika,”amesema.
Aidha, Kiganja amesema hata Baraza la Wadhamini wa Yanga lilipitisha uamuzi wa kuikodisha timu, haitambuliki kwa Msajili wa Vyama na Klabu na Michezo wa BMT, kwa Wajumbe wake wengi ni wa muda.
Amesema kati ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga lililoundwa Julai 5, mwaka 1973 ni wawili tu wanaotambulika na walio hai hadi sasa, ambao ni Dk. Jabir Idrisa Katundu na Juma Mwambelo, wakati wengine wamekwishafariki dunia.
“Mwembelo pamoja na kwamba bado yupo hai, lakini kwa muda sasa hahusishwi tena mambo yanayoendelea ya klabu hiyo,” amesema.
Kiganja amewataja Wajumbe wengine wa Baraza hilo la Muda, ambalo halikuwahi kusajiliwa wala kupitishwa kwenye Mkutano Mkuu ni Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mama Fatuma Karume, Francis Kifukwe, Amri Ramadhan, Juma Kambi na Abeid Mohammed.
Na akasema ili Yanga ikodishwe, inazotakiwa kwanza kifanyike kikao cha Kamati ya Utendaji itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kabla ya kwenda kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama, uwe wa dharura au kawaida na maamuzi yatakayofikiwa katika Mkutano yatapelekwa Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo litawasilisha suala hilo kwa Msajili.
“Sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) kinasema chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha katiba yake kitatakiwa idhini ya Msajili. Kifungu namba 11 (3) Msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha Katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT,” amesema Kiganja.
Katibu huyo wa BMT amesema kwamba mchakato huo wa Yanga kukodishwa ungekuwa halali tu kama taratibu hizo zingefuatwa na kupita kote.

BINSLUM TYRES YAIIGA JEKI KANDANDA DAY 2016


Kampuni ya uuzaji matairi nchini ya Bin Slum Tyres Ltd,imeendeleza utamaduni wake wa kulidhamini tamasha la ‘Kandanda Day’,ambalo litafanyika Oktoba 15,mwaka huu katika uwanja wa Jakaya M Kikwete  Park,Kidogo Chekundu.

Mratibu wa tamasha hilo,Fatma Dahir,amesema kwamba wanaishukuru kampuni hiyo inayoongoza kwa uuzaji matairi nchini kwa msaada wa fedha na vifaa kwa ajili ya tamasha hilo linalobebwa na kauli mbiu Dawati na Mpira.

“Kwanza kabisa tunapenda kuchukua fursa hii,kuishukuru sana kampuni ya Bin Slum,kwa kutuamini na kuwa pamoja zaidi ya miaka miwili katika kuhakikisha tamasha hili linaendelea kuboreka mwaka hadi mwaka,”alisema na kuongeza

“Kwa mwaka huu,kauli yetu mbiu ni Dawati na Mpira, ambayo lengo lake kuu ni kuhakikisha sisi kama wanamichezo tunaunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha shule zetu zina madawati ya kutosha,hivyo tunaamini kwa ushirikiano wa wanamichezo wanaounda kundi la Kandanda kwenye ukurasa wa facebook na wadau wengine,tunaweza kuchangia kitu kwa ajili ya elimu yetu.”

Fatma alisema,kwamba wanaamini udhamini wa fedha walioupata kutoka Bin Slum,utakua chachu ya ulifanikisha tamasha la mwaka huu,kuwa bora zaidi na kuweka historia kwa wanamichezo watakaoshiriki na shule itakayopata msaada wa madawati.

Kwa upande wa mwakilishi wa kampuni ya Binslum Tyres Ltd, Bwana Salim Said Al Jabry, alisema kwamba wameamua kuendeleza utamaduni wao wa kuchangia tamasha la kandanda pamoja na kuuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati nchini.

“Binslum Tyres tunafuraha kubwa ya kuendelea kuwa sehemu ya udhamini,ikumbukwe huu ni mwaka wa tatu  kwa kampuni yetu kudhamini  tamasha hili,ambalo kwetu ni faraja kuona wadau wanakutana pamoja na kushiriki pia kuisaidia jamii kupitia mchezo wa kandanda,”alisema Al Jabry na kuongeza:

“Kwa hiyo mwaka huu mbali na kutoa jezi kwa timu mbili mwenyeji ya Team Dizo Moja na Team Ismail,lakini pia tumetoa kiasi cha fedha kipatacho milioni moja kwa ajili ya kuchangia mchango wetu wa madawati na shughuri zingine za uendeshaji.”

Mwaka huu tamasha hilo linatarajia kushirikisha timu mbalimbali za makampuni ambazo zitacheza katika mfumo wa ligi,kab­­­la ya mshindi kupatikana katika mchezo wa fainali.

Mratibu wa Kandanda Day
Fatma Dahir

Saturday, October 8, 2016

MATAJIRI WA KIARABU KUONGOZA KAMATI YA MASHINDANO SIMBA




KLABU ya Simba SC ya Dar es Salaam imeunda Kamati mpya ya Mashindano, ambayo itakuwa chini ya Watanzania kadhaa wenye asili ya Kiarabu, akiwemo Mwenyekiti, Musley Al Ruwah.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Haji Sunday Manara amesema leo Dar es Salaam katika Mkutano na Waandishi wa habari kwamba Kamati hiyo imeundwa ili kuongeza nguvu katika vita ya ubingwa wa Ligi Kuu.
Na Manara, motto wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ‘Kompyuta’ amewataka watu wengine katika Kamati hiyo, ni Makamu Mwenyekiti, Alhaj Hassan Hassanoo na Wajumbe; Mohamed Nassor wenye asili ya Kiarabu pia, Cossmas Kapinga, Juma Pinto na Octavian Mushi.
Katika hatua nyingine, Manara amesema kwamba Simba imemuandikia barua Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye kumuomba awaombee msamaha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli waruhusiwe kuendendelea kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Manara alisema kwamba wameona umuhimu wa kuomba radhi kwa kitendo cha mashabiki wachache kuharibu raslimali ambazo zimejengwa kwa kodi za Watanzania wote.
“Rais ndiye msimamizi wa raslimali za nchi hii, hivyo tumemuandikia barua Waziri Nape kumuomba atuombee radhi kwa Rais Magufuli, kwa kitendo cha mashabiki wetu kung’oa vitu kwenye mchezo wa Oktoba 1 (2016) dhidi ya Yanga”, alisema Manara.
“Wakati tukiwa jukwaa kuu na kuona tukio lile likitendeka, tulitamani kuruka kwenda kuwazuia mashabiki wasing’oe viti, lakini hatukuweza, ilikuwa mbali, lakini tunaaahidi tukio kama lile halitatokea tena, kwani limeshusha thamani ya klabu yetu,”alisema.
Aidha, Manara ameiomba Serikali kupitia Menejimenti ya Uwanja wa Taifa kufunga kamera ili kunasa matukio kwa lengo la kuwabaini wahusika wa uharibifu. Akawaomba pia askari Polisi wanaopangiwa kusimamia usalama uwanjani kuhakikisha wanawatazama mashabiki badala ya kuangalia mchezo ili kujiweka tayari kupambana na wahalifu.

CAF WAJA KUKAGUA UWANJA WA CCM KIRUMBA



Wataalamu wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), wanatarajiwa kutua nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kukagua Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Huu ni utaratibu wa CAF ambako baada ya muda hutembelea nchi wanachama kuangalia maendeleo ya miundombinu ya mpira wa miguu kabla ya kupandisha hadhi ya viwanja kwa ajili ya michuano ya kimataifa inayosimamiwa na kuendeshwa na CECAFA, CAF na FIFA.

Ukaguzi huo unafanyika wakati Tanzania inasubiri majibu ya Uwanja wa Sokoine wa Mbeya ambao ulikwiisha kukaguliwa na mapendekezo ya uboreshwaji kutolewa ili uweze kupandishwa hadhi ya matumizi ya kuchezwa mechi kubwa kama vile fainali za Kombe la Shirikisho, Ngao ya Hisani, michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mechi kubwa za kimataifa za kirafiki na mashindano ya CECAFA, CAF na FIFA.

Viwanja ambavyo CAF na FIFA inavitambua nchini Tanzania hadi sasa ni Amani wa Unguja, Zanzibar; Kaitaba wa Kagera, Azam Complex na Uwanja Mkuu wa Taifa vya Dar es Salaam.

Endapo CCM Kirumba utapitishwa, kutakuwa na nafasi ya kuruhusu kuchezwa mechi kubwa kama vile fainali za Kombe la Shirikisho, Ngao ya Hisani pamoja na mechi kubwa za kimataifa za kirafiki na mashindano ya CECAFA, CAF na FIFA.

Kirumba inaingia kwenye orodha ya viwanja vya Gombani ulioko Pemba; Sokoine wa Mbeya, Kaitaba wa Kagera ambavyo vilikwisha kukaguliwa na sasa vinasubiri kupitishwa ili kutumika kimataifa. Ujio wa viwanja hivyo, utapanua wigo wa Tanzania kuandaa michuano mikubwa katika ngazi ya timu za taifa kimataifa.

TIMU 12 ZATHIBITISHA KUSHIRIKI LIGI YA WANAWAKE


Timu 12 zinatarajiwa kushiriki Ligi ya Taifa ya Wanawake inayotarajiwa kuanza Novemba mosi, mwaka huu kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Maendeleo ya Soka la Wanawake na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), zilizoridhia tarehe hiyo.

Tayari klabu zimeagizwa kuzingatia jina kuenenda na namba za jezi mgongoni ili kuepusha mkanganyiko wa wachezaji wakati wa ligi hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.

Timu 12 zinatarajiwa kushiriki ligi hiyo ambako kesho Oktoba 8, 2016 itakuwa ni siku ya kuchambua fomu za usajili wakati Oktoba 10, mwaka huu majina ya usajili yatatangazwa ambako pia klabu zitatumiwa kupitia anwani za barua pepe.

Oktoba 11 na 12, 2016 ni muda wa klabu kuleta mapingamizi yatakayosikilizwa Oktoba 15, mwaka huu. Majina ya pingamizi yatatangazwa kabla ya Oktoba 20, 2016 na maandalizi ya ligi yataendelea.

Wakati wote huo wa usajili, klabu hazina budi kutangaza aina ya rangi wanazotumia katika michezo ya nyumbani na ugenini na kutakiwa kusafiri na jozi zote mbili ili kuepuka mkanganyiko wa kufanana jezi.

Kutakuwa na jopo la makocha watakaofanya uteuzi wa wachezaji nyota watakaoitwa kwenye timu za taifa ambaye atagharamiwa na TFF.

Vyama vya mikoa visadie klabu katika bajeti zao kwa vile tathamini inaonyesha kuwa fedha zinazotoka hazitoshi. Vyama hivyo vya mikoa pia visaidie maandalizi ya michezo kama vile kuandaa uwanja nakadhalika ukioandoa waamuzi ambao watagharamiwa na TFF.

Hakutakuwa na zawadi ya fedha zaidi ya kombe la medali kwa timu shiriki, labda kama atatokea mdhamini mwingine. Hakutakuwa na zawadi kwa mchezaji bora, mfungaji bora, kipa bora, ingawa kutakuwa na jopo la kuwachagua. Mchezaji bora atachaguliwa kwenye hatua za mwisho wa mashindano, mfungaji bora atachaguliwa kuanzia hatua ya kwanza ya mashindano.

Thursday, October 6, 2016

SERIKALI SASA YARUHUSU WIMBO WA CHURA WA SNURA KUTUMIKA



Na Dotto Mwaibale

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeruhusu kupigwa kwa wimbo wa chura wa msanii Snura Mushi baada ya kuufunga kwa kuwa haukuwa na maudhui mazuri ya kitanzania.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Snura Mushi alisema wimbo wake na video umeruhusiwa kupigwa baada ya audio ya chura kufanyiwa marekebisho na kuifanya kuwa katika maudhui ya kitanzania.

Alisema ruhusa hiyo imetolewa kwa barua iliyoaandikiwa Septemba 26, 2016 yenye kumbukumbu HA.26/375/01’B’/137 ambayo gazeti hili lina nakala yake.

Kupitia mkutano huo msanii Snura Mushi kwa mara nyingine aliomba radhi kwa watanzania na Serikali kwa ujumla kwa usumbufu walioupata kwa video yake ya kwanza na kuwaomba waendelee kuiona video mpya iliyorekebishwa baada ya kuifuta ya kwanza.

(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com).

Wednesday, October 5, 2016

SAANYA ANUSURIKA KUFUNGIWA, KADI YA MKUDE YAFUTWA, SIMBA NA AZAM ZALIMWA FAINI



Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga faini ya sh. 5,000,000 (milioni tano) klabu ya Simba, kuiagiza ilipe gharama za uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki wake katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Oktoba Mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia Kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika jana (Oktoba 4, 2016), imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza mechi bila washabiki. Adhabu dhidi ya Simba imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu.

Vilevile kwa kuzingatia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu, Kamati imefuta adhabu ya kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi wa mechi hiyo kwa Jonas Mkude wa timu ya Simba baada ya kuthibitika bila mashaka kuwa nahodha huyo hakustahili kadi hiyo.

Mbali ya ripoti ya Kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo iliyoonyeshwa 'live', Kamati inaendelea na uchunguzi wa jambo lingine kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya, na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutangaza uamuzi wake.

Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuingia uwanjani baada ya mechi hiyo wakati yeye hakuwa miongoni mwa maofisa wa mechi waliotakiwa kuwepo katika eneo hilo.

Adhabu dhidi ya Manara ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(10). Eneo husika ni kwa ajili ya wachezaji, mabenchi ya ufundi, waamuzi, madaktari, huduma ya kwanza, wapiga picha na maofisa wengine wa mechi.

Klabu ya Azam imepigwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kwa kuvaa nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu kwenye mkono mmoja tu badala ya miwili ambapo ni kinyume na Kanuni ya 13(1), na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 13(6).

JKT Ruvu imepewa onyo na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya Msimamizi wa Kituo, na Ofisa wa Bodi ya Ligi kushambuliwa na mshabiki wa timu hiyo katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Mshabiki huyo amefungiwa miezi 12, na iwapo vitendo hicho vitaendelea Uwanja huo utafungiwa kwa mechi za Ligi Kuu.

Mwamuzi Ahmed Seif amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kumudu mechi kati ya African Lyon na Mbao FC ikiwemo kutoa adhabu ya penalti ambayo haikuwa sahihi. Pia Mwamuzi huyo alipata alama za chini ambazo hazimruhusu kuendelea kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

Pia Makamisha David Lugenge na Godbless Kimaro wamepewa onyo kwa kuwasilisha taarifa zenye upungufu katika mechi walizosimamia za raundi ya tano na saba.

Katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Mbeya Warriors imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kupitia mlango usio sahihi ikiwemo kuvunja kufuli kwenye mechi kati yao na Kimondo FC iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu Uwanja Vwawa mkoani Songwe. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Kwanza.

SERIKALI YAIFAGILIA SERENGETI BOYS, ITAELEKWA KAMBINI KOREA KUSINI



Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge na Vijana, Dk. Abdallah Possi amesema kwamba Serikali itaendelea kusapoti michezo kwa sababu ya umuhimu wake, lakini akataka kutafutwa mbinu za kuhakikisha wadhamini wanasapoti timu za taifa na klabu mbalimbali zinazoshiriki ligi zinazosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Dk. Possi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwapongeza vijana wa Timu ya Taifa ya Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, alisema kwamba fursa ipo ya kufanya vema katika michezo na ndiyo maana Serikali inasapoti michezo kwa sababu ya kuleta faraja, kuunganisha au kuleta umoja katika nchi yoyote kadhalika ni ajira.

Dk. Possi aliyesifu juhudi za TFF na timu hiyo, aliwapoza vijana hao akiwaeleza kuwa “Juhudi zilifanyika na mnaona kiwango kilichotumika kuandaa timu yenu. Matokeo mliyopata ndiyo mchezo. Kushindwa haina maana tumeishia hapa,” alisema Dk. Possi alipokuwa akiwapongeza vijana hao katika hafla hiyo iliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Ili kuepuka gharama kubwa za kuendesha timu hizo ambako Serengeti Boys imetumika karibu bilioni moja, Dk. Possi amesema kwamba kunahitajika kutengenezwa mfumo wa kupata wadhamini ili baadaye bidhaa za TFF zigombaniwe na hata kampuni zinazofanya biashara inayofanana zinaweza kuingia kudhamini katika ligi moja au klabu kwa sababu zitavuna maslahi.

Akiwageukia wachezaji, Dk. Possi alisema wachezaji hawana budi kuwa na nidhamu ya hali ya juu si katika kuonyesha kusabahi tu, bali kutunza mwili. “Mtafika mbali kama mkiwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja. Mna walimu, mna viongozi, ni vema mkawa mnawasikiliza wengine,” alisema Dk. Possi huku akitaja majina ya nyota waliofanikiwa kwa kuwa na nidhamu na wengine ambao walioanguka kwa kuwa na nidhamu mbovu.

Kabla ya kumkaribisha Dk. Possi, Rais wa TFF Jamal Malinzi alianza na kutoa taarifa ya matokeo huko Congo Brazzaville, akisema: “Ilikuwa siku mbaya sana kwangu. Watoto walikwenda kufia nchi. Lakini jahazi halijafika mwisho, kuvunjika kwa mpini, sio mwisho wa uhunzi. Userengeti Boys unakwisha na sasa unakuja Ungorongoro Heroes timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.”

Malinzi aliyetumia nafasi hiyo kumpa nafasi tena Kocha Mkuu wa vijana hao, Bakari Nyundo Shime alisema kikosi hicho kinapambana kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2019 na ili kujindaa timu hiyo inatarajiwa kwenda Korea Kusini kwenye mashindano maalumu itawasaidia kuongeza uwezo wenu, kutembea na kutafuta soko la kimataifa la soka.

Alisema kwamba mara baada ya timu hiyo kurejea, itakuwa inakusanhyika kila baada ya miezi mitatu ili kufanya mazoezi ya pamoja na kupata mchezo angalau mmoja wa kirafiki huku akitangaza kuwa vijana wa Mwanza, wanaosoma katika shule ya Alliance wanatarajiwa kuunda kikosi kipya cha timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

“Timu ile ya Mwanza ambayo kwa sasa ina vijana wa chini ya miaka 15, ndio watakaounda kikosi cha fainali za vijana ambazo zitafanyika hapa nchini mwaka 2018. Desemba watoto wale watacheza mechi ya kwanza ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, ambako watapigiwa wimbo wa taifa,” alisema Malinzi na kuongeza kuwa vijana walioibuliwa kutoka michuano ya Airtel Rising Stars nao watajumuishwa.

“Ligi ya wanawake inayokuja. Ndiyo nayo itazaa timu bora ya wanawake ambayoi itashiriki fainali za Kombe la Dunia hapo mwaka 2019. Ili tuweze kufanya yote haya, tunahitaji fedha na tayari tumeanzisha mfuko maalumu wa kuchangia timu hizi unaitwa TFF Fund ambao utakuwa na mtendaji wake na ofisi yake,” alisema na kuongeza, “Yote haya yanalenga Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2016.”

Timu hiyo iliyofanyiwa hafla, ilikuwa ikipambana kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini ikaondolewa na Congo Brazzaville kwa kufungwa bao 1-0 dakika za majeruhi hivyo kuondolewa kwa sheria za bao la ugenini. Mchezo wa kwanza Tanzania ilishinda 3-2 na katika mchezo wa marudiano, ilipoteza.

MALINZI: HATUWEZI KUITELEKEZA SERENGETI BOYS


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kwamba ataendelea kuwa karibu na vijana na Timu ya Tanzania ya vijana ‘Serengeti Boys’ licha ya kuondolewa na Congo kwenye harakati za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Madagascar, hapo Aprili, mwakani.

Mipango ya TFF kwa sasa inayoongozwa na Malinzi kwa sasa ni kuiiingiza timu hiyo kwenye program ya timu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 maarufu kwa jina la Ngorongoro Heroes baada ya kuguswa na kilio cha vijana hao ambao walishindwa kujizuia kumwaga machozi mbele ya Malinzi ambaye alifanya kazi kubwa kuwatuliza pamoja na viongozi wengine.

Serengeti Boys ilipoteza mchezo dhidi ya Congo Oktoba 2, 2016. Kwa kupoteza mchezo huo dakika ya pili kati ya nne ya nyongeza baada ya kumalizika kwa dakika 90, kumefanya vijana hao wa Tanzania kuenguliwa kwenye mashindano ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika – fainali zitakazofanyika Madagascar.

Dakika moja ndiyo iliyoipoteza Serengeti Boys kufuzu kwa fainali hizo kwa bao la dakika ya 92 la lililofungwa na Mountou Edoward.

“Niko nanyi, najua mna group la WhatsApp, naomba msifute namba yangu. Iwe humo na mambo yenu mengi naomba mniambie humo, na nitayashughulikia iwe binafsi au kiofisi. Nawahakikishia sitawaacha,” alisema Malinzi alipowafariji vijana hao ambao wanatarajiwa kuingia leo saa 3.00 usiku huu kwa ndege ya Shirika la Ndege ya Rwanda.

“Umri wenu bado sana wa kucheza soka. Program za TFF, CAF na FIFA ziko nyingi pia mnaweza kupata nafasi ya kucheza Olimpiki na kuna michuano mingi, sitawaacha,” alisema Malinzi na kusisitiza ana imani na timu hiyo ambayo kwa dakika 90 za mchezo dhidi ya Congo walipambana kwelikweli kutetea taifa lao pendwa Tanzania.

PAMBANO LA STARS, EHIOPIA LAFUTWA



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea barua kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ethiopia (EFF), ikielezea juu ya kufutwa kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliokuwa ufanyike Oktoba 8, 2016.

EFF imesema kwamba imelazimika kufuta mchezo huo ulikuwa kwenye kalenda ya FIFA kwa sababu za hali ya hewa si rafiki kwa sasa nchini Ethiopia.

Kwa barua hiyo, Kocha Mkuu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars), Charles Boniface Mkwasa atalazimika kuvunja kambi ya timu hiyo ambayo iliweka kwenye Hoteli ya Blue Pear iliyoko Ubungo, Dar es Salaam.

Mchezo huo uliratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao. EFF, ndio walioomba nafasi hiyo.

Ingekuwa ni faida kwa Tanzania kama ingeshinda mchezo huo kwa maana kina alama za nyongeza kama inatokea unaifunga timu mwenyeji.

Matokeo yake yangekuwa ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 132 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Ethiopia yenyewe inashika nafasi ya 126.

Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji. Timu nyingine bora kimataifa ni Ujerumani, Colombia na Brazil.

Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 34 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Algeria, Senegal, Tunisia na Ghana.

Monday, October 3, 2016

NDOTO YA SERENGETI BOYS KUFUZU KUCHEZA FAINALI ZA AFRIKA YAOTA MBAWA, YACHAPWA BAO 1-0 NA CONGO BRAZZAVILLE



NDOTO za timu ya soka ya Taifa ya vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys kufuzu kucheza fainali za Afrika mwakani, zimeota mbawa baada ya kuchapwa bao 1-0 na Congo Brazzavile.

Katika mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa jana mjini Librevvile, Serengeti Boys ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele.

Kutokana na kipigo hicho, Congo imefuzu kucheza fainali hizo kutokana na faida ya mabao ya ugenini, baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 3-3.

Katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Dar es Salaam, Serengeti Boys iliichapa Congo mabao 3-2.

WASANII NCHINI WAMETAKIWA KUTUMIA SANAA ZAO KUELIMISHA JAMII KUFANYA KAZI KWA BIDII.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bibi Leah Kihimbi akizungumza na wananchi pamoja na wasanii mbalimbali (hawapo pichani) wakati alipokua anafunga Tamasha la 35 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lilioandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Wilayani Bagamoyo Oktoba mosi.
Mtendaji Mkuu wa  Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbet Makoye akitoa hotuba kwa wananchi pamoja na wasanii mbalimbali (hawapo pichani) wakati  Tamasha la 35 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lilioandaliwa na Taasisi  hiyo  lilipofungwa rasmi Wilayani  Bagamoyo Oktoba mosi.
Vikundi mbalimbali vya burudani  kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) vikitoa burudani kwa  wananchi  pamoja na wasanii  mbalimbali (hawapo pichani) katika ufungaji wa Tamasha la 35  la Sanaa na Utamaduni  Bagamoyo  lilioandaliwa  na Taasisi  hiyo   Wilayani  Bagamoyo Oktoba mosi.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bibi Leah Kihimbi akiangalia bidhaa za urembo kutoka kwa mbunifu Mariam Kiiza kabla ya kufunga   Tamasha la 35 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo  lilioandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Wilayani Bagamoyo Oktoba mosi.
Baadhi ya wanachi walioshiriki ufungaji wa Tamasha la 35 la Sanaa na Utamaduni  Bagamoyo  lilioandaliwa  na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)  Wilayani Bagamoyo Oktoba mosi.
 

Na  Shamimu  Nyaki-WHUSM.

Katika kuhakikisha Watanzania wanafanya kazi kwa maendeleo yao na Taifa nchini Serikali imewataka wasanii mbalimbali kutumia Sanaa yao kuelimisha jamii umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii.

Wito huo umetolewa jana Wilayani  Bagamoyo  na Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na  Michezo  Prof. Elisante Ole Gabriel  katika hotuba yake ya kufunga Tamasha la 35 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lililoandaliwa na Taasisi ya Sanaana Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

Katibu Mkuu katika hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Mkurugenzi  Idara ya Maendeleo ya Sanaa ya Wizara hiyo Bibi. Leah Kihimbi amesema kuwa Wasanii wana nafasi kubwa ya kufikia Watanzania wengi kutokana  na kazi zao hivyo watumie nafasi  hiyo kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa Kufanya kazi.

“Wasanii  mkidhamiria jambo hufanyika  na uwezo wa kufanya hivyo mnao,ni vizuri mkatumia Sanaa yenu kuwaelimisha wanachi  manufaa ya kufanya kazi kwao wenyewe na Taifa kwa ujumla”.Alisema Prof.Ole Gabriel.

Kwa upande wake Mtendaji  Mkuu wa  Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbet  Makoye mbali na kuwashukuru  wasanii wote waliohudhuria  Tamasha hilo amewataka  pia waendelee kufanya Sanaa zenye ubora na zinazoitangaza Tanzania Ulimwenguni.

“Mmeshiriki vizuri katika Tamasha hili niwasihi muendelee kufanya Sanaa iliyo bora inayotangaza nchi yetu kote  Ulimwenguni ukizingatia tunazo Sanaa za aina mbalimbali ikiwemo ngoma,muziki,filamu na sanaa za ufundi”.Aliongeza Dkt.Makoye.

Aidha msanii  Ebeneza Lukas anaefanya muziki amesemaTamasha limempa ujuzi na weledi mkubwa katika Sanaa yake ukizingatia kuwa yeye ndio anaanza kufanya Sanaa.

Tamasha hilo lililofunguliwa Septemba 26 mwaka huu na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa naMichezo Mhe.Anastazia Wambura  limefungwa Oktoba mosi ambapo kazi mbalimbali za Sanaa zilifanyika ikiwa ni pamoja na  makongamano  na warsha mbalimbali.

SIMBA, YANGA ZAPIGWA MARUFUKU KUUTUMIA UWANJA WA TAIFA



Timu za soka za Simba na Yanga za Jijini Dar es Salaam zimezuiwa kutumia Uwanja wa Taifa kwa muda usiojulikana kutoka na mashabiki wao kusababisha uharibifu wa miumbombimu ya Uwanja  wa Taifa yakiwemo mageti ya kuingilia Uwanjani na kung’oa viti kwa upande wa mashabiki wa Simba.

Uamuzi huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam  na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akikagua na kutembelea maeneo yalioathirika na uharibifu uliofanywa na mashabiki wa Simba na Yanga katika mechi iliyochezwa Octoba Mosi 2016 katika Uwanja wa Taifa.

“Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki kuvunja mageti na kung’oa viti na sisi kama Serikali tumeamua kuzuia vilabu hivi vya Simba na Yanga kutotumia Uwanja wa Taifa mpaka tuitavyoamua vinginevyo hapo baadae” Alisistiza Mhe. Nnauye.

Mhe. Nape Nnauye ameongeza kuwa wameendaa mfumo wa kutumia kamera Uwanjani ili kubaini makosa yatakayokuwa yanafanyika ili kuzuia vitendo vya kihualifu na uharibifu katika Viwanja vya michezo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Alex Nkenyenge amesema kuwa wamesikitishwa sana na uharibifu ulitokea katika mechi ya Simba na Yanga na kusababisha uharibifu wa viti na mageti ya kuingilia Uwanjani.

Ameongeza kuwa kwa tathimini iliyofanyika mageti manne yameng’olewa na mashabiki kwa upande wa Simba na Yanga na pia kwa upande wa ndani jumla ya viti 1781 vimeng’olewa katika upande wa mashabiki wa Simba.

“Mara nyingi tumekubaliana kutunza Uwanja huu kwa ajili ya matumizi ya watanzania wote na kama wasimamizi tunasikitika kwa kitendo hiki kilichotokea na tujue kuwa ni kodi za wananchi ndio zilitumika kujenga Uwanja huu na pia ndizo zitazotumika kukarabati Uwanja tuwe na tabia ya kupenda na kutunza vya kwetu.

Klabu za Simba na Yanga zimekuwa na ushindani mkubwa katika soka la Tanzania na kumekuwa kukitokea mambo mbalimbali pale timu hizo zinapokutana ikiwemo uharibifu wa miundombinu katika Viwanja na vurugu kwa mashabiki pale mmoja wao anapofungwa.

AZAM YALAZIMISHWA SARE NA RUVU SHOOTING



AZAM FC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC ifikishe pointi 11 baada ya kucheza mechi saba, ikishinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Ruvu Shooting inafikisha pointi tisa baada ya kucheza mechi saba, ikishinda mbili, kufungwa mbili na sare tatu.
Fullyuzulu Maganga alianza kuifungia Ruvu dakika ya nane, kabla ya Jean Baptiste Mugiraneza kuisawazishia Azam FC dakika ya 46 akimalizia kona ya Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mcha akaifungia bao la pili Azam FC dakika ya 70, kabla ya mkongwe Shaaban Kisiga ‘Malone’ kuifunga timu yake ya zamani dakika ya 89 akiisawazishia Ruvu Shooting. 
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbeya City imeshinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya bao pekee la Ditram Nchimbi, wakati Mbao FC imelazimishwa sare ya 0-0 na JKT Ruvu Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wakati Maji Maji imefungwa nyumbani 2-0 na Stand United mjini Songea.

SIMBA YAOMBA RADHI


"Kwa masikitiko makubwa klabu ya Simba imesikitishwa sana na vitendo vilivyofanywa na baadhi ya washabiki wetu,cha kuvunja sehemu ya viti vya Uwanja wa Taifa, kitendo kilichotokea jana kwenye mchezo wetu wa Ligi kuu dhidi ya Timu ya Yanga.

Tungependa kuomba radhi kwa kadhia hii na klabu imekubali kulipia gharama za uharibifu huu.
Klabu itazungumza na wamiliki wa Uwanja huu kuona inalipaje gharama hizo.

Ni mategemeo yeti kuona jambo hili halitajikoze tena.

Lakini mbali na hayo klabu kesho Jumatatu itawasilisha malalamiko rasmi juu ya uchezeshaji mbovu wa waamuzi wa mchezo wa jana,hususan Mwamuzi wa kati Martin Sanya.

Sisi tunaamini vitendo viovu vilivyofanywa na washabiki wetu vilisababishwa na uamuzi wa hovyo kupita kiasi uliosababishwa na waamuzi hao.

Haieleweki ni kigezo gani mwamuzi huyo alitumia kulikubali goli la 'mpira wa pete'la mshambuliaji wa Yanga Amisi Tambwe na kulikataa goli halali la mshambuliaji wetu Ibrahim Ajibu.

Pia tumeshangazwa na kitendo cha kumpa kadi nyekundu nahodha wetu Jonas Mkude, ilhali kama nahodha alimfata kwenda kumlalamikia kitendo chake cha kukubali goli la 'hovyo 'la Tambwe.

Sote tumeona Sanya alijikwaa wakati anarudi nyuma na kuanguka,kisha kuanguka na kutoa kadi nyekundu kwa Mkude.

Kimsingi huyu mwamuzi ana historia ovu ya kuwabeba Yanga.

Hakuna asiyesahau msimu uliopita kwenye kombe la Shirikisho,Yanga walipocheza na Coastal Union kule Mkwakwani Tanga.Nini kilitokea!

Tunajua safari hii Tff na bodi ya Ligi zitatoa adhabu kali kwa waamuzi hawa ili iwe fundisho kwa maamuzi ya hovyo ya aina hii.

Pia klabu italalamika kitendo cha vyumba vyetu vya kubadilishia nguo(dressing room)kupuliziwa dawa zilizokuwa na nia ya kuwaathiri wachezaji wetu kabla ya mechi kuanza.

Tutaziomba mamlaka zifanye uchunguzi wa kina kubaini kitendo hiki kisicho cha kiungwana kinachosadikiwa kufanywa na wapinzani wetu.

Tunajua dhamira yao ni kuwafanya wachezaji wetu wachoke,lakini timu yetu ya Matabibu ilichukua hatua sahihi za kuwafanya wachezaji wetu waweze kumaliza dakika Tisini za mchezo kwa uwezo na weledi mkubwa.

Na mwisho klabu itoe malalamiko yake kwa Waziri wa mambo ya nchi,Mh Mwigulu Nchemba.

Waziri huyu bila shaka amesahau majukumu yake yake ya kazi na kugeuka kiongozi wa klabu ya Yanga.

Tunajua ni haki yake kuwa na mapenzi kwa klabu aliyoichagua.lakini vitendo vyake anavyovifanya vinaacha maswali mengi kuliko majibu, ukizingatia nafasi yake kama Waziri mwenye dhamana ya kuongoza Wizara nyeti.

Itakumbukwa majuzi waziri huyu alifanya ziara Mkoani Morogoro kuzungumza na vikosi anavyoviongoza.

Na inajulikana pia Refarii wa mchezo wa jana Martin Sanya ni mwajiriwa wa Jeshi la Magereza mkoani Morogoro. Sote tulishuhudia Jana Mwigulu alishangilia goli la hovyo la mwajiriwa wake Sanya.

Pia waziri huyu alitoa kauli tata kuwa angetamani siku moja klabu inayoshangilia wapinzani wa Yanga wakipigwa mabomu ya machozi na Askari wa jeshi la Polisi.

Kauli hii aliitoa wakati wa sherehe za kukabidhi zawadi kwa timu zilizoshinda msimu uliopita zilizoandaliwa na wadhamini wa ligi.kampuni ya Vodacom.

Tunajiuliza yale mabomu ya jana pale Uwanja wa Taifa ndio utekelezaji wa maagizo ya boss Mwigulu?

Lakini pia matumizi ya rasilimali za umma yakiwemo magari ya serikali ktk shughuli za mara kwa mara za klabu ya Yanga napo kunaacha maswali mengi mno.

Wanasimba wanauliza kila Waziri anayeshabikia Simba akiwepo Waziri Mkuu akifanya vitendo hivi kutakuwa na utawala gani serikalini?

Imani yetu viongozi wakuu wa nchi watamuonya mh Mwigulu,vingenevyo atatengeneza chuki baina ya washabiki wa Simba dhidi ya serikali yao.

Mwigulu atambue klabu ya Simba ina mamilioni ya washabiki kama ilivyo klabu yake anayoishabikia.
Hatutarajii kuona 'mahaba'yake yasio na staha yanachochea jambo ovu kwa wanasimba na serikali yao wanayoiamini na kuipenda sana,".

(Imetolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara)

SIMBA, YANGA HAKUNA MBABE





TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga, ambazo ni watani wa jadi, zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mashabiki wa Simba walifanya vurugu kubwa baada ya kung'oa viti na kuvirusha uwanjani.

Tukio hilo lilitokea dakika ya 23 baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Amis Tambwe, baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mbuyu Twite.

Mashabiki wa Simba walilalamikia bao hilo kwa madai kuwa Twite aliushika mpira kwa mkono wake wa kulia kabla ya kufumua shuti lililotinga wavuni.

Aidha, picha za televisheni za pambano hilo lililokuwa likionyeshwa moja kwa moja, pia zilithibitisha kuwa ni kweli Tambwe aliushika mpira huo kwa mkono kabla ya kufunga.

Baada ya mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro kupuliza kipenga kuashiria kwamba lilikuwa bao halali, ndipo mashabiki wa Simba walipoanza kung'oa viti na kuvirusha uwanjani.

Vurugu hizo zilidumu kwa dakika takriban tano, ambapo polisi wa kutuliza ghasia ilibidi watumie mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki hao.

Simba ilipata pigo baada ya kiungo na nahodha wake, Jonas Mkude, kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumsukuma na kumwangusha mwamuzi Saanya.

Katika kipindi cha pili, licha ya kubaki na wachezaji 10, Simba walionyesha soka ya kiwango cha juu na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 87 kwa bao lililofungwa na mshambuliaji machachari Shiza Kichuya.

Mshambuliaji huyo, ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Yanga, alifunga bao hilo kwa mpira mrefu wa kona uliotinga moja kwa moja wavuni.