'
Wednesday, November 12, 2014
TAIFA STARS YATUA SALAMA J'BURG
Kikosi cha wachezaji 23 wa Taifa Stars tayari kimewasili Johannesburg, Afrika Kusini tayari kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Swaziland.
Mechi hiyo itafanyika Jumapili (Novemba 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Somhlolo jijini Swaziland. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwepo Johannesburg hadi Ijumaa itakapoondoka kwenda Mbabane.
Wachezaji wote walioitwa na Kocha Mart Nooij wapo kwenye msafara huo isipokuwa kiungo mshambuliaji Mrisho Ngasa ambaye amebaki Dar es Salaam kutokana na matatizo ya kifamilia.
Taifa Stars inatarajia kurejea nyumbani Jumatatu (Novemba 17 mwaka huu) saa 12.45 jioni kwa ndege ya South Africa Airways.
Wakati huo huo, kikosi cha maboresho cha Taifa Stars kitacheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya Rwanda kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 23. Mechi hiyo itachezwa Desemba 9 mwaka huu nchini Tanzania.
Kikosi cha maboresho cha Taifa Stars kinachoundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 23 kitakuwa kinakutana mara moja kila mwezi hadi Mei mwakani kwa ajili ya mazoezi na kucheza mechi moja ya kirafiki.
Kocha Mart Nooij atatangaza kikosi kwa ajili ya mechi hiyo na programu nzima mara atakaporejea kutoka Swaziland.
Tuesday, November 11, 2014
MAMIA WAMZIKA AMIGOLAS, JK AMLILIA, WASANII WAANGUA VILIO MAKABURINI
RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Rais Kikwete ametuma salamu hizo kuomboleza kifo cha mwanamuziki mwasisi wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Hamisi Kayumbu 'Amigolas'.
Amigolas alifariki usiku wa kuamkia Jumapili saa 5:30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.
“Nimehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha mwanamuziki Hamisi Kayumbu kilichotokea tarehe 9 Novemba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo”, alisema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ikulu jana, ilisema Rais Kikwete anatambua mchango mkubwa wa marehemu Amigolas, katika kuhamasisha maendeleo ya nchi yetu.
Taarifa hiyo ilisema Kayumbu alitoa mchango wake kupitia sanaa ya muziki kuwafikishia wananchi ujumbe muhimu wa masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Alisema Kayumbu alikuwa mfano unaofaa kuigwa na wasanii wengine nchini. Amigolas alikuwa kiongozi wa bendi mpya ya Ruvu Stars baada ya kuhama Twanga Pepeta.
“Kutokana na msiba huu, naomba upokee salamu zangu za rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa wanamuziki mahiri hapa nchini, pia ziwafikie wanamuziki wengine kote nchini kwa kumpoteza mwenzao”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Rais Kikwete amemwomba Dk. Fenella, kumfikishia salamu zake za pole kwa familia ya marehemu Kayumbu kwa kupotelewa na kiongozi na mhimili madhubuti.
Wakati huohuo, wasanii mbalimbali jana walishindwa kujizuia kuangusha vilio, baada ya mwili wa mwanamuziki mahiri marehemu Hamisi Kayumbu 'Amigolas' kuwasili nyumbani kwake Mburahati, Dar es Salaam.
Amigolas alifariki usiku wa kuamkia Jumapili saa 5:30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.
Mkurugenzi wa bendi ya Extra Bongo na mwimbaji hodari nchini, Ali Choki, alishindwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu kifo cha Amigolas.
Choki na Amigolas, walifanya kazi kwa karibu na pia waanzilishi wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' mwaka 1997.
Hata hivyo, baadhi ya wasanii walitoa maoni yao kuhusu kifo cha Amigolas aliyekuwa na sauti nzito jukwaani.
Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu, alisema Amigolas alikuwa mtu muhimu katik tasnia ya muziki na ametoa mchango mkubwa kwa wasanii chipukizi.
Naye Saidi Mabera 'Dokta' wa Msondo Ngoma alisema alimfahamu, Amigolas, tangu mwaka 1986 alipokuwa mwimbaji wa bendi ya Bicco Stars.
"Nilimfahamu marehemu Amigolas tangu mwaka 1986 akiwa Bicco Stars, naomba wanamuziki tumuenzi kwa kudumisha muziki wa asili," alisema Mabera.
Ramadhani Athumani 'Dogo Rama' wa Twanga Pepeta alisema, Amigolas, alikuwa kiungo muhimu na mmoja wa wasanii walimsaidia kukuza kipaji chake cha kuimba.
Naye Stara Thomas, alisema alianza kufahamiana na Amigolas akiwa bado kinda katika muziki, hivyo ametoa rai kwa wadau kumuombea.
"Tunamshukuru Mungu kwa sababu kifo hakikwepeki, jambo la msingi ni kumuombea ingawa alikuwa bado anahitajika,"alisema msanii wa maigizo nchini Steven Mengele 'Steve Nyerere'.
Kwa upande wake Hassani Mussa 'Super Nyamwela' wa Extra Bongo, alisema hakutarajia kama nguli huyo angefariki kwa ugonjwa wa moyo na amemtaja Amigolas alikuwa mhimili wa Twanga Pepeta.
Marehemu Amigolas alizikwa jana alasiri katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam na umati wa watu wakiwemo wasanii na watu mbalimbali maarufu.
Sunday, November 9, 2014
AMIGOLAS WA TWANGA PEPETA AFARIKI DUNIA
MWIMBAJI nyota wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta Internationa, Hamisi Kayumbu 'Amigolas', amefariki dunia.
Amigolas, alifariki dunia juzi saa 5.30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Mwanamuziki huyo alikuwa kiongozi mpya wa bendi ya Ruvu Stars baada ya kutamba kwa muda mrefu na Twanga Pepeta, ambapo pia aliwahi kuwa kiongozi.
Amigolas atakumbukwa kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika bendi ya Twanga Pepeta, ambapo alikuwa mmoja wa waimbaji wake mahiri, akishirikiana na Ally Choki, Luiza Mbutu, Khalid Chokoraa, Ramadhani Masanja 'Banza Stone'.
Akizungumzia kifo cha mwanamuziki huyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment, Asha Baraka, alisema marehemu Amigolas alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa miaka minne iliyopita.
Asha alisema tasnia ya muziki imempoteza mtu muhimu, ambaye alisaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa wasanii wanaong'ara katika bendi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Asha, Amigolas alijiunga na Twanga Pepeta mwaka 1998, wakati huo ikiwa inafanya maonyesho ya wazi kwenye baa kabla ya kuanza kupata umaarufu na kuteka soko la muziki nchini.
Marehemu Amigolas ameacha mke na watoto wanne na anatarajiwa kuzikwa leo kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
SIMBA YAFUTA MWIKO WA SARE, YAICHAPA RUVU SHOOTING 1-0
BAO lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, jana liliiwezesha Simba kupata ushindi wake wa kwanza katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.
Okwi alifunga bao hilo dakika ya 78 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Rashid Abdalla wa Ruvu Shooting, kutokana na shuti kali la Elias Maguri.
Ushindi huo uliwapa ahueni kubwa mashabiki wa Simba baada ya kuishuhudia timu yao ikitoka sare mechi sita mfululizo na hivyo kuhatarisha kibarua cha Kocha wao, Patrick Phiri kutoka Zambia.
Sare hizo pia zilisababisha uongozi wa Simba kuwasimamisha wachezaji wake nyota watatu, Amri Kiemba, Haruna Chanongo na Shaaban Kisiga kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa inazo pointi tisa baada ya kucheza mechi saba na imechupa hadi nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa nyumba ya Yanga kwa tofauti ya pointi tatu.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilipata nafasi kadhaa nzuri za kufunga mabao, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo.
Kuingia kwa Elias Maguli katika kipindi cha pili, aliyechukua nafasi ya Saidi Ndemla, kuliiongezea uhai safu ya ushambuliaji ya Simba, ambayo ilifanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Ruvu Shooting.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Mtibwa Sugar ilitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Manungu ulioko Turiani mjini Morogoro.
Awali, mechi hiyo ilichezwa juzi kwenye uwanja huo, lakini ililazimika kuahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha uwanjani. Hadi mechi ilipovunjika, Mtibwa ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Saturday, November 8, 2014
YANGA, AZAM ZASHINDA LIGI KUU, MBEYA CITY HOI
MABAO mawili yaliyofungwa na mshambuliaji Simon Msuva jana yaliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Msuva, ambaye aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima,alifunga mabao hayo dakika ya 73 na 88.
Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi saba, ikiwa inakabana koo na Azam, inayoshika nafasi ya pili.
Azam ilitoka uwanjani kifua mbele baada ya kuichapa Coastal Union mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Mabao ya Azam yalifungwa na beki Shomari Kapombe na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche. Bao la Coastal Union lilifungwa na Rama Salim.
Timu ya soka ya Mbeya City jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 ba Stand United katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Kipigo hicho ni cha tano kwa Mbeya City tangu ligi hiyo ilipoanza msimu huu, ambapo katika mechi saba ilizocheza, imeshinda moja na kutoka sare moja.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Prisons ya Mbeya ilichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa maafande wa Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Pambano kati ya Mtibwa na Kagera Sugar lililochezwa kwenye uwanja wa Manungu mjini Turiani, lilivunjika kipindi cha pili kutokana na mvua kubwa kuanza kunyesha.
Hadi pambano hilo lilipovunjika, Mtibwa ilikuwa mbele kwa bao 1-0. Pambano hilo sasa litachezwa leo.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo, Simba itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Ruvu Shooting.
Thursday, November 6, 2014
AZIM DEWJI AWATULIZA WANA SIMBA
MWANAMICHEZO maarufu nchini, Azim Dewji amewataka wanachama na wapenzi wa timu ya soka ya Simba kuamini timu yao bado ni bora, isipokuwa ipo katika kipindi cha mpito kuelekea katika mafanikio yatakayowashangaza wengi.
Kutokana na imani yake hiyo, ameshauri ni vyema wakatoa ushirikiano wa kila aina kwa viongozi, wachezaji na benchi lote la ufundi, vivyo hivyo akiwataka viongozi kushikamana na wachezaji na benchi la ufundi,badala ya kuanza kunyoosheana vidole.
Aliyasema hayo jana alipokuwa anazungumzia mwenendo wa klabu hiyoaliyowahi kuifadhili na kuipa mafanikio makubwa katika miaka ya 1990, lakini msimu huu ukionekana kuyumba, kwani tangu kuanza kwa ligi, imetoka sare katika mecho zake zote sita, hali inayowasonesha `wanazi’ wa klabu hiyo.
Alisema Simba inapitia mapito kama ya Manchester United ya England, ambayo tangu kuondoka kwa kocha wake wa zaidi ya robo karne, Sir Alex Ferguson iliyumba na hata kutemeshwa ubingwa kwa aibu, lakini sasa imeanza kurejesha makali.
“Sasa ukiangalia hata Simba si timu mbaya ndiyo maana ingawa haijashinda, haijapoteza mchezo pia. Haya yanatokana na mabadiliko mengi kwa wakati mmoja, kuanzia safu ya uongozi, benchi la ufundi na
hata wachezaji…hawa watu wanahitaji kupewa muda. Nakuhakikishia Simba hii itakuwa tishio
“Lakini wakati nikiwasihi wanachama na wapenzi kuwaunga mkono viongozi, wachezaji na kocha, naamini viongozi nao watumie busara ya kufanya kila linalowezekana kuwafanya wachezaji na makocha kujiamini na kujiona wana deni, lakini si kutishiana kila kukicha.
“Hii si sahihi na kwa mazingira ya vitisho, siku zote watabaki kuwa watu wa wasiwasi na kushindwa kuisaidia timu…tuwape nafasi, hakika mapinduzi ya kisoka yataonekana kwa sababu nimeona timu ina wachezaji wengi wenye vipaji,” alisisitiza Dewji.
Katika msimu huu wa ligi, Simba ilianza ligi kwa kutoka sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga kabla ya kupata sare mbili za matokeo ya 1-1 mbele ya Polisi Moro na Wakuja katika ligi hiyo, Stand United ya Shinyanga. Haikufungana na Yanga iliyokuwa inaaminika ni mara zaidi tangu ilipomnasa kocha Mbrazil Marcio Maximo katikati ya mwaka huu, ikatoka pia sare ya 1-1 na Prisons ya Mbeya na pia na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Wednesday, November 5, 2014
MPANDA UTD, UJENZI RUKWA KUANZA SDL
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu ambapo Mpanda United itakuwa mwenyeji wa Ujenzi Rukwa.
Mechi hiyo ya kundi A itachezwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga. Siku hiyo hiyo katika kundi hilo kutakuwa na mechi kati ya Mvuvumwa FC na CDA (Lake Tanganyika, Kigoma), na Milambo dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Kundi B mechi za ufunguzi ni kati ya Pamba na JKT Rwamkoma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba huku Bulyanhulu FC ikiwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga.
Abajalo FC ya Dar es Salaam itaikaribisha Kariakoo FC ya Lindi kwenye mechi ya kundi C itakayochezwa Uwanja wa Karume. Nazo Kiluvya United na Transit Camp zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
Kundi D mechi tatu za ufunguzi ni kati ya Town Small Boys na Volcano FC (Uwanja wa Majimaji, Songea), Njombe Mji na Mkamba Rangers (Uwanja wa Sabasaba, Njombe), na Wenda FC dhidi ya Magereza Iringa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
NOOIJ ATANGAZA KIKOSI CHA STARS KITAKACHOCHEZA NA SWAZILAND
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij ametangaza kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Swaziland itakayochezwa Novemba 16 mwaka huu jijini Mbabane.
Akizungumza Dar es Salaam, leo (Novemba 5 mwaka huu), Nooij alisema kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 10 mwaka huu saa 6 mchana kwenye hoteli ya Accomondia, na siku hiyo hiyo jioni kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.
Novemba 11 mwaka huu, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka kwenda Afrika Kusini ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya kuondoka Novemba 13 mwaka huu kwenda Swaziland.
Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho ni makipa Aishi Manula (Azam) na Deogratias Munishi (Yanga). Mabeki ni Abubakar Mtiro (Kagera Sugar), Aggrey Morris (Azam), Emmanuel Simwanda (African Lyon), Hassan Isihaka (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Osacr Joshua (Yanga), Said Moradi (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shomari Kapombe (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Haruna Chanongo (Simba), Himid Mao (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Said Ndemla (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Washambuliaji ni Juma Luizio (ZESCO, Zambia), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo).
Tuesday, November 4, 2014
KOCHA NOOIJ KUTAJA KIKOSI CHA STARS
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij keshokutwa (Novemba 5 mwaka huu) atatangaza kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) itakayochezwa ugenini Novemba 16 mwaka huu.
Nooij atatangaza kikosi hicho mbele ya waandishi wa habari katika mkutano utakaofanyika saa 4.30 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizoko ghorofa ya tatu, Jengo la PPF Tower jijini Dar es Salaam.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Swaziland, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Somhlolo jijini Mbabane.
MWAKIBINGI AONDOKA BODI YA LIGI KUU
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Silas Mwakibinga amemaliza mkataba wake tangu Oktoba 31 mwaka huu.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na TPLB wanamshukuru Mwakibinga kwa mchango wake kwa kipindi ambacho ameitumikia Bodi, na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya huko aendako.
TPLB hivi sasa iko katika mchakato wa kupata Ofisa Mtendaji Mkuu mpya kwa ajili ya kuziba nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Mwakibinga baada ya muda wa mkataba wake kumalizika.
Monday, November 3, 2014
ONYESHO LA MIAKA 50 YA MSONDO NGOMA LAFANA DAR
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimkabidhi cheti cha heshima kwa kiongozi wa bendi ya Msondo Ngoma, Said Mabela.
Mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa Msondo Ngoma, Kepteni mstaafu, John Simon (katikati) akielezea historia ya bendi hiyo wakati wa onyesho hilo.
JK AIBARIKI SUNDERLAND KUJENGA KITUO CHA MICHEZO KIDONGO CHEKUNDU MNAZI MMOJA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Profesa Jakaya Mrisho Kikwete akiwahutubia wageni waalikwa, wafanyakazi mbalimbali wa Kampuni ya Symbion pamoja na wananchi wakati wa hafla ya kutoa Kibali chake kwa Chuo cha Michezo cha Sunderland kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Umma uliopewa jina la Rais Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park. Tukio hilo limefanyika leo 1 Novemba, 2014 eneo la Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Biashara wa Chama cha Michezo cha Sunderland, Bi. Gary Hutchinson akimkabidhi zawadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Profesa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa hafla ya kutoa Kibali chake kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Umma uliopewa jina la Rais Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park. Tukio hilo limefanyika leo 1 Novemba, 2014 eneo la Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam
Sunday, November 2, 2014
DK. SHEIN AAHIDI KUINUA MICHEZO ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inaiendeleza sekta ya michezo sambamba na kuimarisha miundombinu yake ili Zanzibar iweze kurejesha hadhi yake katika sekta hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo, leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye sherehe za ushindi wa michezo mbali mbali ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM, zilizofanyika huko katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar ambazo pia,zimehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi mbali mbali wa serikali wanamichezo na wananchi.
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alisema kuwa katika kufanya hivyo, Serikali inapitia upya Sera ya Michezo ili iweze kufikia malengo ya Serikali katika kuinua sekta ya michezo hapa nchini.
Alisema kuwa wakati mchakato wa kuipitia upya Sera ya Michezo ukiendelea aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea na juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja mbali mbali vya michezo Unguja na Pemba.
Dk. Shein alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanja vitatu vya Kimataifa hapa Zanzibar vinaimarishwa ambapo hivi sasa tayari uwanja wa Amaan uliopo mjini Unguja uko tayari na kiwanja cha Gombani Pemba tayari kimeshajegwa ambacho ndani ya mwaka huu wa fedha uwanja huo utawekwa tatan katika eneo la kukimbilia.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeshafikia makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ya ujenzi wa uwanja wa Mao-te-tung ili nao uweze kutumika sambamba na viwanja vya Amaan na Gombani huku akieleza azma ya kuviimarisha viwanja vyengine mbali mbali vya Unguja na Pemba kwa lengo la kuendeleza michezo pamoja na kutoa fursa nzuri kwa wananchi waweze kuendeleza michezo kwa ufanisi zaidi hapa Zanzibar
Dk. Shein alipendekeza kuongezwa kwa mashindano ya mpira wa miguu ili kuleta ushindani katika vilabu vya mpira vya hapa Zanzibar pamoja na kuvishirikisha vilabu vyengine kadhaa.
Alisema kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuzijengea uwezo timu za Zanzibar ili ziweze kushiriki mashinadano ya ndani na nje ya nchi na kupata mafanikio na kusisitiza kuwa wakati umefika Zanzibar kuwa mshindani katika mashindano na kuchukua vikombe katika mashindano mbali mbali.
Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina vipaji vya kutosha na wanamichezo wa kufanya vizuri wapo, kinachotakiwa ni maandalizi bora na kuondoa migogoro katika uongozi wa vilabu na vyama vya michezo hapa Zanzibar.
Kwa kusisitiza hilo, Dk. Shein alitoa mfano wa mgogoro wa Chama Cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika uongozi uliopita ambapo ulisababisha wanamichezo wa timu ya Taifa ya Zanzibar walioshiriki katika mashindano ya 'Challange Cup' mwaka juzi kushindwa kuwakabidhi zawadi aliyowaandalia kutokana na migogoro kadhaa ndani ya chama hicho.
Alieleza kuwa iwapo mashirikiano mazuri yatakuwepo sekta ya michezo itapata mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa malengo yake ya kukuza sekta ya michezo nchini yanafanikiwa.
Dk. Shein alisema kuwa michezo ni afya, ukakamavu, inajenga udugu na kuleta ushirikiano na kwa hivi sasa, michezo ni ajira kwa hivyo ni vyema wananchi wote wakashiriki katika michezo japo ya vilabu vya mazoezi ili kuimarisha afya zao.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuridhishwa sana na mafanikio ya timu ya mpira wa miguu ya KMKM kwa kuwa mabingwa kwa misimu miwili mfululizo 2013-2014 na 2014-2015 pamoja na ushindi wa timu ya riadha pamoja na kupata ngao za hisani. "Naungana na nyinyi na wale wote wanaokupongezeni kwa mafanikio hayo", alisema Dk. Shein.
"Napenda kuwapongeza wanamichezo wa KMKM kwa kuchagua mbio hizi ambazo kwa kweli zinatukumbusha na sisi wengine enzi zetu katika michezo ya riadha hasa ya 'cross-country na field tract' tulishiriki vyema pamoja na mchezo huu wa kuvuta kamba ambapo mimi mwenyewe nilikuwa kocha", alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa Uongozi wa Awamu ya Kwanza ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ulichukua jitihada za makusudi kujenga Uwanja wa Amaan uliofunguliwa mwaka 1970 na ule wa Gombani uliofunguliwa mnamo mwaka 1992 wakati wa uongozi wa Awamu ya Tano ambapo ujenzi wake ulianza katika uongozi wa Awamu ya Nne chini ya Marehemu Sheikh Idrisa Abdul Wakil.
Dk. Shein vile vile, alisisitiza haja ya kila timu hapa Zanzibar kuwa na Klabu yake na jengo lake na kuunga mkono azma ya klabu ya KMKM kutaka kujenga jengo maalum la ghorofa litakalokuwa na eneo la kufanyia mazoezi (GYM), ukumbi wa mikutano na maduka ya vifaa vya michezo.
Mapema Dk. Shein aliyapokea mashindano ya mbio za kilomita kumi katika viwanja hivyo vya Maisara yalioanzia huko Kibweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, na kuwashirikisha wakimbiaji zaidi ya 200 ambapo mkimbiaji Philip Jacob Mambo kutoka Kikosi cha Mafunzo aliibuka mshindi wa kwanza na Mohamed Ramadhan kutoka KMKM ambae aliibuka mshindi wa Pili.
Kwa upande wa wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Albina Edward kutoka KMKM na mshindi wa pili alikuwa Nuru Nasib kutoka Kambi ya Mtoni. Mashindano hayo pia, yalijumuisha Makundi maalum ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mkimbiaji Ali Abdalla na mshindi wa pili alikuwa Amina Daudi Simba.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omar Kheir alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kushirikiana pamoja na wanamichezo hao wa Kikosi cha KMKM katika sherehe zao hizo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa KMKM Komodoo Hassan Mussa alisema kuwa mbio za kilomita 10 ambazo zilishirikisha wanamichezo zaidi ya 200 zimefanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu lakini zitafanyika kila mwaka katika siku itakayoteuliwa kuwa ya KMKM.
Katika risala yao nao wanamichezo wa KMKM walieleza mikakati inayochukiliwa katika kuendeleza michezo katika kikosi chao sambamba na kupongeza jinsi Serikali inavyowaunga mkono katika kufikia malengo waliyojiwekea
Sherehe hizo ziliambatana na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya sanaa vikiwemo Diamond Morden Taarab, Kidumbaki kilichoongozwa na Msani Makame Faki maarufu sauti ya zege, ngoma ya Kibati kutoka kikundi cha sanaa cha JKU, JKU Morden Taarab ambacho kiliimba wimbo maalum kwa ajili ya sherehe hiyo.
Pia, mchezo wa kuvuta kamba ulifanyika katika sherehe hizo ambao uliwashirikisha maafisa wa KMKM wanaofanya kazi pamoja na Wastaafu ambapo Wastaafu walipata ushindi na kukabidhiwa zawadi na Rais zikiwemo fedha taslim zilizotolewa na wapenda michezo.
YANGA, AZAM ZAPATA VIPIGO LIGI KUU, SARE YAZIDI KUIANDAMA SIMBA
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Azam jana walikwaa tena kisiki baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ndanda FC katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwande mjini Mtwara.
Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa Azam baada ya wiki iliyopita kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi mjini Dar es Salaam.
Bao pekee na la ushindi la Ndanda lilifungwa na Jacob Massawe dakika ya 15 na kuifanya ipate ushindi wake wa pili tangu ligi hiyo ilipoanza.
Washindi wa pili wa mwaka jana, Yanga nao walionja joto ya jiwe baada ya kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Bao pekee na la ushindi la Kagera Sugar lilifungwa na Paul Ngwai dakika ya 54 alipounganisha kwa kichwa krosi kutoka pembeni ya uwanja.
Katika mchezo huo, beki Nadir Haroub wa Yanga alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kichwa mchezaji mmoja wa Kagera Sugar.
Timu kongwe ya Simba nayo iliendelea kusuasua katika ligi hiyo baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa beki wake, Joseph Owino baada ya kuunganishwa wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Emmanuel Okwi.
Mussa Hassan Mgosi aliisawazishia Mtibwa dakika ya 56 na kufuta ndoto za Simba za kutoka uwanjani na ushindi wa kwanza katika ligi hiyo.
Katika mechi hiyo, kipa Manyika Peter wa Simba alionyesha ushujaa wa aina yake baada ya kupangua penalti ya David Luhende baada ya beki Hassan Isihaka kumwangusha Ame Ali wa Mtibwa ndani ya eneo la hatari.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union iliichapa Ruvu Shooting bao 1-0, Polisi Moro iliilambisha JKT Ruvu mabao 2-1.
TFF YAJIBU SHUTUMA ZA NDUMBARO
Oktoba 31 mwaka huu kupitia vyombo vya habari Wakili Damas Ndumbaro alitoa shutuma mbalimbali dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Tunapenda kuuleza umma wa Watanzania yafuatayo;
1.Hukumu dhidi ya Wakili Ndumbaro ilitolewa na chombo halali kwa mujibu wa Katiba ya TFF. Hivyo, TFF inatoa tahadhari kwa wanafamilia wa mpira wa miguu kutomhusisha Wakili Ndumbaro katika masuala ya mpira wa miguu katika kipindi hiki anachotumikia adhabu.
2.Hadi sasa TFF haijapokea rufani yoyote kutoka kwa Wakili Ndumbaro. Hii ni kwa kuwa kupitia barua yake kwa TFF aliagiza asikabidhiwe nyaraka yoyote kutoka TFF hadi Oktoba 30 mwaka huu, hivyo hukumu ya Kamati ya Nidhamu dhidi yake alikabidhiwa Oktoba 30 mwaka huu. Alichokifanya Wakili Ndumbaro ni kuleta TFF barua ya kusudio la kukata rufani.
3.Tuhuma za ubadhirifu wa TFF zilizotolewa na Wakili Ndumbaro si za kweli. TFF inatafakari hatua za kisheria na kikanuni za kuchukua dhidi ya tuhuma hizi.
4.Mkataba wa TFF na TBL:
TFF inapenda kuwahakikishia wadau wa mpira wa miguu kuwa hakuna ubadhirifu wa aina yoyote katika matumizi ya fedha za mkataba wa TFF/TBL. TFF ingependa itoe kwa umma ufafanuzi wa vipengele vya mkataba huo na jinsi unavyoendeshwa lakini masharti ya mkataba huo (confidentiality clause) yanatuzuia kufanya hivyo.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikutana na klabu za Ligi Kuu na kuzielekeza zikae na kujadili kanuni za Ligi, kisha zipendekeze maboresho ili yajadiliwe katika kikao kijacho cha Kamati ya Utendaji.
TFF inapenda kuchukue fursa hii kusisitiza umuhimu wa kufuata mifumo tuliyojiwekea katika kutatua matatizo/kero zetu mbalimbali, utulivu ni muhimu katika kuendeleza mpira wa miguu.
MAKOCHA 35 KUSHIRIKI KOZI YA LESENI C YA CAF
Makocha 35 wameteuliwa kushiriki kozi ya ukocha ya Leseni C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika mjini Morogoro kuanzia Novemba 5 hadi 19 mwaka huu.
Kozi hiyo itaendeshwa na Mkufunzi wa CAF, Sunday Kayuni na itafanyikia Mchikichini College ambapo washiriki wote wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao vya ukocha vya ngazi ya Kati (Intermediate) pamoja na vyeti vya kitaaluma vya elimu ya sekondari (academic).
Washiriki wa kozi hiyo ni Abdulmaliki Nemes (Airport FC), Ahmed Haule (Kilimanjaro Talented Youth Sports Centre), Ally Jangalu (Moro Kids), Amri Saidi (Mwadui FC), Athuman Kambi (Morogoro), Charles Mwakambaya (Burkina Faso FC), Damian Mussa (Alliance One) na Daudi Sichinga (Kasulu United).
Denis Maneva (Shule ya Msingi Logo), Edgar Juvenary (JUT- Mlale), Hamisi Mangolosho (Shule ya Msingi Mtimbwilimbwili), Henry Ngondo (Chalinze Academy), Issa Hamisi (Polisi Kilimanjaro), Jumanne Chale (Dar es Salaam), Kizito Mbano (Masasi Alliance), Martin Saanya (Magereza Morogoro) na Masoud Gumbwa (Sokoine University Academy).
Mbwana Makata (Oljoro JKT), Mrage Kabange (Kagera Sugar), Muhibu Muhibu (Stand United FC), Nsubuga Solomon (Kishoto FC), Nyamtimba Muga (Kizuka Secondary), Oscar Mirambo (Makongo), Rashid Abdallah (Tech Fort Academy), Renatus Shija (Rhino Rangers), Safari Nyerere (Elimu Sports Academy) na Said Lyakuka (Kizuka Stars).
Simeon Mwesa (Mtibwa Sugar U20), Simon Shija (Tabora), Suleiman Mtungwe (Ruvu Shooting), Swalehe Allawi Abdul (Alliance Academy), Yasin Bashiri (Kick Off Sports Academy) na Zuberi Katwila (Mtibwa Sugar).
Wakati huo huo, kutakuwa na kozi ya wiki mbili ya ukocha ya ngazi ya Kati (Intermediate) itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 29 mwaka huu.
Makocha wote wanaotaka kushiriki kozi hiyo wanatakiwa kutuma maombi katika Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA).
Thursday, October 30, 2014
29 WAITWAKIKOSI CHA MABORESHO TAIFA STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatarajia kuendelea na awamu ya pili ya maboresho ya timu ya Taifa (Taifa Stars) inayojumuisha vijana wenye umri chini ya miaka miaka 23.
Katika awamu hii, Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij ameteua majina ya wachezaji 29 ambao watakuwa wakiingia kambini mara moja kwa mwezi siku ya Jumapili baada ya kuwakilisha timu zao kwenye mechi za ligi.
Kikosi hicho cha maboresho kitakuwa kikifanya programu maalumu za mazoezi mpaka siku ya Jumatano na kucheza mechi za kirafiki na timu za ndani au nje ya nchi.
Lengo hasa la programu hiyo ni kuwajengea uwezo vijana wenye vipaji ambao walipatikana katika awamu ya kwanza ya mpango wa maboresho mwanzoni mwa mwaka huu Tukuyu mkoani Mbeya, lakini wamekuwa hawatumiki. Pia kuwandaa vijana ili kujenga timu ya ushindani na imara ya Taifa ya muda mrefu.
TFF ina imani kubwa kuwa programu hii itakuwa na manufaa kwa soka ya Tanzania. Timu hiyo itaingia kambini kwa mara ya kwanza Desemba 9 mwaka huu katika hoteli itakayotangazwa baadaye.
Wachezaji walioteuliwa ni Aishi manula (Azam), Benedict Tinoco (Kagera Sugar), Aboubakar Ally (Coastal Union), Miraji Adam (Simba), Andrew Vicent (Mtibwa Sugar), Gadiel Mbaga (Azam), Emmanuel Semwanda (African Lyon) na Joram Mgeveke (Simba).
Edward Charles (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Kassim Simbaulanga (African Lyon), Pato Ngonyani (Yanga), Adam Salamba (Kahama), Hassan Banda (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Hashim Magoma (Stand United), Makarani Ally (Mtibwa Sugar), Said Juma (Yanga) na Said Hamis (Simba).
Aboubakary Ally Mohamed (Zanzibar), Hassan Dilunga (Yanga), Hussein Malombe (Geita Gold), Muzamir Ally (Mtibwa Sugar), Shiza Ramadhan (Mtibwa Sugar), Omari Nyenje (Ndanda SC), Kelvin Friday (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Alfred Masumbakenda (Kahama) na Simon Msuva (Yanga).
LIGI DARAJA LA PILI KUANZA NOVEMBA 22
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 zitakazocheza katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyoketi jijini Dar es Salaam jana (Oktoba 29 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange ilipitia maandalizi maandalizi ya ligi hiyo ikiwemo mwongozo wake (roadmap).
Kwa mujibu wa mwongozo huo, usajili wa wachezaji utamalizika Oktoba 31 mwaka huu. Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Novemba 1 hadi 7 mwaka huu wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajia kukutana Novemba 11 mwaka huu kwa ajili ya kupitisha usajili.
Pia Kamati ya Mashindano imepitisha viwanja vya timu zote, isipokuwa uwanja wa timu ya Mpanda United ya Katavi na ule wa Town Small Boys ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Uwanja wa Town Small Boys haukupitishwa kwa vile hauna uzio wa kudumu ( wa chuma) wa kutenganisha wachezaji na washabiki, na pia ufikaji wa timu Tunduru ni mgumu kutokana na ubovu wa barabara ikizingatiwa kuwa ligi hiyo itachezwa hadi kipindi cha Masika.
Kwa upande wa uwanja wa Mpanda United, umekataliwa kwa vile hauna vigezo vya msingi vinavyotakiwa ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo, kutokuwa na nyasi na uzio wa kudumu kutenganisha wachezaji na washabiki.
Kutokana na uamuzi huo, Mpanda United sasa itatumia Uwanja wa Mandela uliopo Sumbawanga wakati Town Small Boys itachezea mechi zake kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
TFF YAWAOMBA WADAU WABUNI JEZI MPYA ZA TAIFA STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linakaribisha wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani na ugenini. Ubunifu ni lazima uzingatie rangi za bendera ya Taifa.
Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata sh. 1,000,000 (milioni moja), na mshindi wa jezi ya ugenini atapata pia sh. 1,000,000 (milioni moja).
Ubunifu utumwe kwenye anwani ya barua pepe: info@tff.or.tz au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden Avenue. Mwisho wa kupokea designs ni Novemba 15, 2014.
Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi kwa simu namba; 0713 210242 au 0714 634838.
MBEYA CITY YAINGIA MKATABA WA KIBIASHARA NA BENKI YA POSTA
MKATABA WA KIBIASHARA
Leo tarehe 30.Oct.2014, Mbeya City Fc inasaini mkataba wa makubaliano ya kibiashara na Benki ya Posta Tanzania (TPB).
Huu ni mkataba wa kibiashara (siyo udhamini) kwa maana kuwa kupitia kadi za ATM ambazo mashabikiwa Mbeya City Fc watapewa baada ya kufungua ‘akaunti’ wataweza kuichangia timu kupitia huduma za kibenki watakazokuwa wakizifanya kwa kutumia akaunti zao.
Mkataba huu pia utaifanya club kufahamu idadi ya mashabiki iliyonao nchini kote.
DISMAS TEN
AFISA HABARI NA MAWASILIANO
MBEYA CITY COUNCIL FC.
Subscribe to:
Posts (Atom)

















