'
Sunday, January 18, 2015
MICHUANO YA KOMBE LA TAIFA WANAWAKE YAINGIA RAUNDI YA PILI
Michuano ya Kombe la Taifa kwa Wanawake inaingia raundi ya pili kesho (Januari 17 mwaka
huu) kwa mechi za kwanza za raundi hiyo zitakazochezwa katika miji ya Bukoba, Arusha,
Mlandizi, Dar es Salaam na Katavi.
Jijini Dar es Salaam kutakuwa na mechi mbili ambapo mkoa wa kisoka wa Ilala utacheza na
Mtwara kwenye Uwanja wa Karume, wakati Uwanja wa Chuo cha Bandari uliopo Tandika
utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Temeke na Dodoma.
Mechi nyingine za michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin zitakuwa kati ya Kagera
na Mwanza itakayochezwa mjini Bukoba, Arusha na Tanga (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri
Abeid), Pwani na Kinondoni (Uwanja Mabatini, Mlandizi), na Katavi na Mbeya zitakazoonesha kazi
kwenye Uwanja wa Azimio.
Nazo Ruvuma na Iringa zitacheza Januari 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji. Mechi
hiyo itachezwa tarehe hiyo ili kusubiri matokeo ya mechi ya marudiano kati ya Shinyanga na
Simiyu.
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ilikutana jana (Januari 15 mwaka huu) kupitia ripoti ya mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza
kati ya Shinyanga na Simiyu ambayo ilivunjwa na mwamuzi katika daika ya 70.
Baada ya kupitia ripoti, Kamati imebaini kuwa licha ya vurugu alizofanyiwa mwamuzi, bado
mechi hiyo ingeweza kuendelea kwa kuchezeshwa na mwamuzi wa akiba kwa vile usalama
ulikuwepo baada ya yeye kupigwa.
Pia Kamati imeagiza Katiba wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo
aliyeripotiwa kumpiga mwamuzi suala lake lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa
hatua zaidi, wakati Kocha wa Simiyu, Emmanuel Babu ambaye naye alishiriki kumpiga mwamuzi
amesimamishwa wakati akisubiri kuchukua hatua zaidi.
Kamishna wa mechi hiyo Idd Mbwana, na mwamuzi Joseph Pombe wamefungiwa kwa miaka
miwili.
Mechi kati ya Shinyanga na Simiyu itamaliziwa dakika kumi zilizobaki kesho (Januari 17 mwaka
huu) mjini Shinyanga. Kila chama cha mkoa kitabeba gharama zake katika uendeshaji wa mechi
hiyo ambayo mwenyeji ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).
Timu itakayosonga mbele baada ya mechi hiyo itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili
ugenini Januari 19 mwaka huu dhidi ya Kigoma. Mechi za marudiano za raundi ya pili
zitachezwa kati ya Januari 21 na 22 mwaka huu.
Hatua ya robo fainali hadi fainali ambayo mechi zake zitachezewa jijini Dar es Salaam itaanza
Januari 26 mwaka huu. Fainali itachezwa Februari Mosi mwaka huu.
Vilevile Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imemfungia kwa miaka miwili Kaimu
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kwa
kushindwa kuingiza timu yake uwanjani kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza dhidi
ya Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Thursday, January 15, 2015
NOOIJ KUTAJA KIKOSI CHA TAIFA STARS MABORESHO
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij anatarajia kutaja kikosi cha Maboresho kitakachoingia kambini Januari 18 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda itakayofanyika Januari 22 mwaka huu jijini Mwanza.
Nooij atataja kikosi hicho kwenye mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Januari 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume.
RAUNDI YA PILI TAIFA CUP WANAWAKE JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya pili ya mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) zinachezwa wikiendi hii (Januari 17 mwaka huu) kwenye miji minane tofauti nchini.
Timu tisa zilizofuzu kutoka raundi ya kwanza baada ya mechi za nyumbani na ugenini akiwemo mshindwa bora (best loser) zitaungana na Ilala, Kinondoni na Temeke kucheza raundi ya pili. Mechi za marudiano za raundi hiyo zitachezwa Januari 21 mwaka huu.
Hatua ya robo fainali itakayochezwa Januari 26 na 27 mwaka huu pamoja na nusu fainali na fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Proin Promotions itafanyikia jijini Dar es Salaam.
RAMBIRAMBI MSIBA WA STEPHEN NSOLO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) uliotokea jana (Januari 13 mwaka huu) jijini Mwanza.
Msiba huo ni pigo kwa wadau wa mpira wa mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Nsolo alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi. Aliongoza SHIREFA akiwa Katibu kuanzia mwaka 1975 hadi 1994.
Kabla ya hapo alikuwa Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga kwa kipindi cha miaka kumi. Pia aliwahi kuwa mwamuzi wa daraja la kwanza na kamishna wa mpira wa miguu kwa muda mrefu.
TFF inatoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, SHIREFA na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa msiba huo.
Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo (Januari 14 mwaka huu) katika makaburi ya Shinyanga Mjini. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
POLISI MARA YAZUIWA KUCHEZA UWANJA WA KARUME
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeizuia timu ya Polisi Mara kutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma kwa mechi zake za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuanzia leo mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Uamuzi huo umechukuliwa kutokana na matukio ya vurugu na uvunjifu wa amani ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mechi za FDL zinazochezwa kwenye uwanja huo, ikiwemo ile ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Mwadui ya Shinyanga ambapo waamuzi walipigwa.
Kamati zinazohusika zitakutakana hivi karibuni kupitia matukio yote ya utovu wa nidhamu kwenye FDL, na hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika ikiwemo na viwanja ambavyo vimekuwa na sifa ya vurugu.
Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vina wajibu wa kutoa ulinzi wa kutosha viwanjani wakati wa mechi.
TANZANIA KUIKABILI KENYA BEACH SOCCER AFRICA
Timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa ufukweni (beach soccer) imepangiwa kucheza na Kenya katika raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa ajili ya fainali za Afrika za michuano hiyo zitakazofanyika Aprili mwaka huu nchini Shelisheli.
Mwenyekiti wa Kamati ya Beach Soccer, Ahmed Idd Mgoyi amesema jijini Dar es Salaam, leo kuwa Tanzania itaanzia ugenini ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Februari 13 na 15 mwaka huu nchini Kenya.
Mechi ya marudiano itafanyikaa nchini kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu. Iwapo timu ya Tanzania itasonga mbele, katika raundi ya pili itacheza na Misri ikianzia nyumbani kati ya Machi 13 na 15 mwaka huu.
Mgoyi alisema maandalizi ya Tanzania kushiriki kwenye mashindano hayo yameanza ambapo timu ya Tanzania Bara itacheza na Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kupata kikosi kimoja kitakachoingia kwenye michuano hiyo ya Afrika.
Alisema benchi za ufundi la timu ya Tanzania litaongozwa na John Mwansasu wakati Msaidizi wake ni Ali Shariff 'Adolf' kutoka Zanzibar, na Meneja wa timu hiyo ni George Lucas. Wote hao walishiriki kwenye kozi ya ukocha wa beach soccer iliyoendeshwa mwaka jana nchini na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kocha Mwansasu atatangaza timu ya Tanzania Bara, Januari 19 mwaka huu, na mazoezi ya pamoja na timu ya Zanzibar yatafanyika Januari 24 na 25 mwaka huu.
Wachezaji wa timu ya Tanzania Bara watatokana na michuano ya beach soccer iliyofanyika mwaka jana ikishirikisha timu za vyuo vya elimu ya juu vya Mkoa wa Dar es Salaam.
SIMBA BINGWA KOMBE LA MAPINDUZI
TIMU kongwe ya soka ya Simba jana ilitwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa Mtibwa Sugar kwa penalti 5-4 katika mechi ya fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.
Kipa Ivo Mapunda, aliyeingia dakika za mwisho ndiye aliyeibuka shujaa wa Simba baada ya kupangua penalti ya mwisho ya Mtibwa iliyopigwa na Vicent Barnabas.
Pambano hilo lilikuwa kali na gumu kutokana na kila timu kupania kushinda ili kuibuka na ubingwa.
Katika michuano hiyo, mshambuliaji Simon Msuva aliibuka kuwa mfungaji bora baada ya kupachika wavuni mabao manne na kumpiku mshambuliaji chipukizi wa Simba, Ibrahim Hijabu, aliyefunga mabao matatu.
Kipa Saidi Mohamed wa Mtibwa Sugar aliibuka kuwa kipa bora wa michuano hiyo wakati beki Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar aliibuka kuwa mwanasoka bora.
Tuesday, January 13, 2015
RONALDO ASHINDA TENA TUZO YA MWANASOKA BORA WA DUNIA 2014
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano Ronaldo,
amechaguliwa kuwa mwanasoka bora wa dunia kwa mwaka 2014.
Hii ni mara ya tatu kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Manchester United ya
England kushinda tuzo hiyo.
Mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, Ronaldo alishangilia kwa staili ya aina
yake kabla ya kwenda kwenye kipaza sauti na kutoa hotuba ya shukurani.
" Naweza kumuona mama yangu, familia yangu. Napenda kuwashukuru wote walionipigia kura, kocha wangu, wachezaji wenzangu na rais wa klabu yangu,"alisema.
Ronaldo alishinda tuzo hiyo baada ya kupata asilimia 37.66 ya kura zilizopigwa na kumbwaga
Lionel Messi, aliyepata asilimia 15.76 na Manuel Neuer aliyepata asilimia 15.72.
Mshambuliaji huyo alikabidhiwa tuzo yake na mwanasoka nyota wa zamani wa Arsenal na
Ufaransa, Thierry Henry.
MTEMVU AIAHIDI VYOMBO VIPYA VYA MUZIKI SIKINDE
MBUNGE wa Jimbo la Temeke (CCM), Abbas Mtemvu (kushoto), akizungumza na wanamuziki wa bendi ya Mlimani Park Orchestra 'Sikinde' wakati wa hafla ya kuwapongeza wenyeviti wapya wa serikali za mitaa, iliyofanyika juzi kwenye ukumbi wa Kata ya 15, Temeke, Dar es Salaam. Wengine pichani ni wanamuziki wa bendi hiyo, Hassan Bitchuka, Mbaraka Othman na Ramadhani Mapesa. (Picha na Emmanuel Ndege).
Na Emmanuel Ndege
MBUNGE wa Jimbo la Temeke (CCM), Abbas Mtemvu, ameahidi kuinunulia vyombo vipya vya muziki bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra 'Sikinde'.
Mtemvu alitoa ahadi hiyo juzi wakati wa sherehe za kuwapongeza wenyeviti wapya wa serikali za mitaa kutoka CCM waliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.
Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye ukumbi wa Kata ya 15, Temeke, Dar es Salaam, bendi za Sikinde, Msondo Ngoma na kikundi cha taarab cha Mashauzi Classic vilitoa burudani.
Mtemvu alisema ameamua kuinunulia vyombo vipya bendi hiyo, kutokana na maombi aliyoyapata kutoka kwa wanamuziki wake.
Mbunge huyo aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Uchumi na Maendeleo la mkoa wa Dar es Salaam (DDC), lililokuwa likiimiliki bendi hiyo, ambapo pia aliwahi kuinunulia vyombo vya muziki.
"Viongozi wa Sikinde waliwahi kuniomba niwanunulie vyombo vipya na nilikuwa tayari kufanya hivyo, lakini ufuatiliaji wao haukuwa mzuri. Kwa vile mmewasilisha tena ombi hilo leo (juzi), naahidi kufanya hivyo hivi karibuni,"alisema Mtemvu huku akishangiliwa na wanamuziki wa bendi hiyo.
Kwa mujibu wa Mtemvu, atatekeleza ahadi hiyo wiki ijayo na aliwataka wanamuziki wa bendi hiyo kujituma zaidi ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, alimshukuru Mtemvu kwa kulikubali ombi lao na kuahidi kuvitumia vyombo hivyo kuongeza ufanisi zaidi ili waweze kufika matawi ya juu zaidi.
Wakati huo huo, bendi ya Mlimani Park, imeamua kuwarejesha kundini wanamuziki wake wa zamani, mpiga solo Gasper Kanuti na mwimbaji Eddo Sanga.
Hemba alisema juzi kuwa, Kanuti alitambulishwa rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Eddo atatambulishwa Jumapili ijayo.
Monday, January 12, 2015
SIMBA, MTIBWA SUGAR KUWANIA KOMBE LA MAPINDUZI KESHO
TIMU za soka za Simba na Mtibwa Sugar, zinatarajiwa kushuka dimbani kesho kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, kumenyana katika mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, linatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa vile kila timu itapania kushinda ili kuibuka na ubingwa.
Simba ilifuzu kucheza fainali baada ya kuichapa Polisi Zanzibar bao 1-0 wakati Mtibwa Sugar iliitoa JKU kwa njia ya penalti tano tano baada ya kumaliza dakika 90 zikiwa sare.
Akizungumzia pambano hilo, Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, alisema hana wasiwasi wa timu yake kutwaa ubingwa.
Kocha huyo kutoka Serbia alisema, timu yake ipo imara na hawana hofu na wapinzani wao kwa vile wana uhakika mkubwa wa kutwaa ubingwa.
Goran alisema vijana wake wote wapo katika hali nzuri na wana ari kubwa ya kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya kihistoria.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime,alisema dakika 90 za mchezo ndizo zitakazoamua bingwa wa michuano hiyo.
Mecky alisema kikosi chake kipo mara na kinatambua nini la kufanya katika mechi hiyo na kusisitiza kuwa, hana hofu na wapinzani wao.
Sunday, January 11, 2015
STARS MABORESHO KUKIPIGA NA RWANDA JAN 22 MWANZA
Kikosi cha Taifa Stars Maboresho kitacheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya Rwanda itakayofanyika Januari 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mechi hiyo ni sehemu ya programu ya Kocha Mart Nooij kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya mechi za mchujo michuano ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN). Mechi za mchujo za michuano hiyo ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Rwanda zinaanza Mei mwaka huu.
Kocha Nooij anatarajia wakati wowote kutangaza kikosi cha timu hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ambacho kitakusanyika Januari 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam, na siku moja baadaye kwenda jijini Mwanza.
TAIFA CUP WANAWAKE KUPIGWA JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya kwanza za mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) zinachezwa kesho (Januari 10 mwaka huu) kwenye miji 11 tofauti nchini.
Katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin, Geita itakuwa mwenyeji wa Kagera (Uwanja wa Geita), Tabora itacheza na Kigoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Simiyu na Shinyanga (Uwanja wa Simiyu), Arusha na Manyara (Sheikh Kaluta Amri Abeid), na Kilimanjaro na Tanga (Uwanja wa Ushirika).
Mechi nyingine ni Lindi itaikaribisha Mtwara kwenye Uwanja wa Ilulu, Ruvuma na Njombe (Uwanja wa Majimaji), Mbeya na Iringa (Uwanja wa Sokoine), Katavi na Rukwa (Uwanja wa Katavi), Dodoma na Singida (Uwanja wa Jamhuri) na Pwani itakuwa mwenyeji wa Morogoro katika Uwanja wa Mabatini.
Timu hizo zitarudiana Januari 13 mwaka huu, ambapo baada ya matokeo ya nyumbani na ugenini timu iliyoshinda ndiyo itakayoingia hatua inayofuata ambayo pia itashirikisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
Hatua hiyo, mechi zake za kwanza zitachezwa Januari 17 mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika Januari 21 mwaka huu.
Baada ya hapo, hatua itakayofuata ni robo fainali, nusu fainali na fainali ambayo ndiyo itakayotoa bingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.
KILUVYA UTD, NJOMBE ZAKIMBIZA LIGI YA SDL
Kiluvya United ya Pwani na Njombe Mji ya mkoani Njombe ndizo timu pekee zilizomaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa kushinda mechi zote katika makundi yao, hivyo kujipatia pointi 15 kila moja.
Njombe Mji imeongoza kundi D lenye timu za Mkamba Rangers ya Morogoro iliyofikisha pointi nane, Wenda ya Mbeya pointi sita, Volcano FC ya Morogoro pointi sita, Town Small Boys ya Ruvuma pointi tano na Magereza ya Iringa yenye pointi moja.
Katika kundi C, Kiluvya United inafuatiwa na Mshikamano ya Dar es Salaam yenye pointi kumi, Abajalo pia ya Dar es Salaam pointi saba, Cosmopolitan na Transit Camp za Dar es Salaam ambazo kila moja imemaliza mzunguko huo ikiwa na pointi tano. Kariakoo ya Lindi haina pointi.
Mji Mkuu (CDA) ya Dodoma na Singida United ya Singida ndizo zinazochuana katika kundi A kila moja ikiwa na pointi nane. Mvuvuma FC ya Kigoma yenye pointi tano ndiyo inayofuatia, wakati Milambo ya Tabora ina pointi nne huku Ujenzi Rukwa ikikamata mkia kwa pointi moja.
Pia mchuano mkali uko katika kundi B ambapo JKT Rwamkoma ya Mara na Mbao FC ya Mwanza ziko kileleni kila moja ikiwa na pointi tisa. AFC ya Arusha inafuatia kwa pointi sita, Bulyanhulu FC ya Shinyanga ina pointi nne wakati Pamba FC ya Mwanza iko mkiani kwa pointi moja.
Mzunguko wa pili wa ligi hiyo itakayotoa timu nne zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao (2015/2016) utaanza kutimua vumbi Januari 24 mwaka huu.
Tuesday, January 6, 2015
TFF YAWAKABIDHI BEJI ZA FIFA WAAMUZI 18 WA TANZANIA



Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),Jamal Malinzi akimkabidhi Beji ya FIFA,Mwamuzi Jonesia Rukyaa katika hafla iliyofanyika jana kwenye Uwanja vya Karume Mchikichini,Jijini Dar es salaam.
Monday, January 5, 2015
FLOYD MAYWEATHER AFANYA KUFURU, AONYESHA MALI ZAKE, IKIWEMO NDEGE BINAFSI NA MAGARI LUKUKI
BONDIA Floyd Mayweather wa Marekani amefanya kufuru baada ya kupiga picha akiwa mbele ya ndege yake binafsi na magari manane ya thamani kubwa anayoyamiliki.
Mayweather, anayetajwa kumiliki utajiri wenye thamani ya pauni milioni 66.1, imeelezwa kuwa thamani ya magari yote manane anayoyamiliki ni pauni milioni tanio.
Mbabe huyo wa masumbwi huenda akaingiza mamilioni ya fedha iwapo atakubali kupambana na Manny Pacquiao.

MESSI AIPELEKA SIMBA ROBO FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI
TIMU ya soka ya Simba jana ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapaJKU bao 1-0 katika mchezo wa kundi C uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Bao pekee na la ushindi la Simba lilipachikwa wavuni na mshambuliaji machachari, Ramadhani Singano 'Messi' dakika ya 12.
Messi alifunga bao hilo kwa shuti kali la mguu wa kushoto baada ya kupokea pasi maridhawa kutoka kwa Saidi Ndemla.
Kwa matokeo hayo, Simba imetwaa uongozi wa kundi hilo ikiwa na pointi sita, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye pointi tano.
Pambano hilo lilikuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote mbili kuonyesha soka ya kiwango cha juu, hasa katika kipindi cha pili.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa jana, Mtibwa na Mafunzo ziligawana pointi moja moja baada ya kutoka suluhu.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea leo wakati KCCA ya Uganda itakapomenyana na KMKM, Azam na Mtende wakati Yanga itavaana na Shaba. Mechi hizo zitaanza kuchezwa saa tisa alasiri.
AZAM YAICHAPA KMKM 1-0
Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam FC wamepata ushindi wa kwanza katika Kombe la Mapinduzi, baada ya kuwalaza mabingwa wa Ligi Kuu visiwani hapa, KMKM 1-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar usiku huu.
Sifa zimuendee beki Shomary Kapombe aliyesababisha bao hilo pekee dakika ya 18, na kuifanya Azam FC sasa ifikishe pointi nne baada ya awali kutoa sare ya 2-2 na mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda.
Bao hilo lililfungwa na Khamis Ali ‘Chichi’, Nahodha wa KMKM aliyejifunga kwa kichwa akijaribu kuokoa shuti la Shomary Kapombe alilopiga kutoka umbali wa mita 25.
Mchezo ulikuwa mkali na timu hizo zilishambuliana kwa zamu muda wote, huku KMKM wakipoteza nafasi nyingi za kufunga kipindi cha pili.
KCCA sasa inaongoza Kundi B kwa pointi zake nne, sawa na Azam FC, lakini yenyewe ina wastani mzuri wa mabao baada ya jioni ya leo kuifunga Mtende mabao 3-0.
Mechi nyingine zilizochezwa leo, Taifa ya Jang’ombe imeilaza 1-0 Shaba Uwanja wa Mao dze Tung, wakati Yanga SC imeifunga Polisi mabao 4-0, mechi zote za Kundi A.
Michuano hiyo, itaendelea kesho kwa mechi za mwisho za Kundi C, Mtibwa Sugar wakimenyana na Mafunzo Saa 10:00 jioni na baadaye Simba SC na JKU Saa 2:15 usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Azam FC; Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, David Mwantika, Aggrey Morris, Mudathir Yahya, Erasto Nyoni, Salum Abubakar, John Bocco, Amri Kiemba na Brian Majwega.
KMKM; Mudathir Khamis, Abdulkadir Nemihi, Mwinyi Hajji Mngwali, Ibrahim Khamis Khatib, Khamis Ali Khamis, Iddi Mbegu Mrisho, Nassor Ali Omar, Tizo Chombo, Fakhi Mwalimu, Halid Hebi na Maulid Ibrahim Kapenta.
Thursday, January 1, 2015
KOCHA MPYA SIMBA ATUA DAR, WACHEZAJI WANANE WAGOMA KWENDA ZANZIBAR
KOCHA Mkuu mpya wa timu ya soka ya Simba, Goran Kopinovic, ametia saini mkataba wa kuinoa Simba kwa miaka miwili.
Goran, raia wa Serbia, alimwaga wino jana baada ya kufanya mazungumzo marefu na viongozi wa Simba.
Kocha huyo aliwasili nchini jana asubuhi na kufikia kwenye hoteli ya Double Tree iliyoko Masaki mjini Dar es Salaam.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, kocha huyo anatarajiwa kwenda Zanzibar leo kujiunga na timu hiyo, inayoshiriki kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Simba imepangwa kufungua dimba la michuano hiyo leo usiku kwa kumenyana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini jana, Goran alisema amekuja nchini kufanyakazi na anaamini atapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo.
Goran anachukua nafasi ya kocha wa zamani wa Simba, Patrick Phiri, ambaye alitupiwa virago mwanzoni mwa wiki hii kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wakati huo huo, kikosi cha Simba kimeondoka mjini Dar es Salaam leo kwenda Zanzibar bila ya wachezaji wake wanane nyota.
Wachezaji hao, wakiwemo Waganda watano, wamegoma kujiunga na timu hiyo kutokana na kutolipwa fedha zao za usajili.
Wachezaji wa Uganda waliomo kwenye mgomo huo ni Emmanuel Okwi, Joseph Owino, Dan Ssenkuruma, Simon Ssenkuruma na Juuko Murshid.
Kwa upande wa wachezaji wazalendo, ni kipa Ivo Mapunda, aliyekwenda Mbeya kwenye msiba wa mama yake, Shabani Kisiga na Jonas Mkude.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Selemani Matola, amesema hana taarifa za kutoweka kwa wachezaji hao. Amesema mchezaji pekee, aliyepata taarifa zake ni Mapunda.
Matola amekiri kuwa, anakwenda Zanzibar akiwa na wachezaji wachache, lakini aliahidi kuiongoza vyema timu hiyo kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Tuesday, December 30, 2014
SIMBA, MTIBWA KUFUNGUA DIMBA KOMBE LA MAPINDUZI KESHO
Na Salum Vuai, Zanzibar
SIMBA SC na Mtibwa Sugar, keshokutwa wanatarajiwa kukata utepe wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 uwanja wa Amaan, kuanzia saa 2:15 ukiwa mchezo wa kundi C.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa la marudiano kufuatia timu hizo kufungana bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo Khamis Abdallah Said, alisema mchezo huo utatanguliwa na mwengine wa kundi hilo kati ya maafande wa Mafunzo na JKU utakaoanza saa 9:00 mchana.
Mechi za kundi A zitaanza kwa pambano kati ya Shaba na Polisi mnamo saa 11:00 jioni.
Khamis, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), alisema mashindano hayo sasa yatashirikisha timu za Tanzania na Uganda pekee baada ya timu ya Ulinzi ya Kenya na Al Ahly ya Misri kushindwa kuthibitisha ushiriki wao.
Alifahamisha kuwa nafasi moja itajazwa na Sports Club Villa ya Uganda, na nyengine itatajwa baadae lakini itakuwa kutoka Zanzibar.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa, Januari 2, mwakani mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC, watatiana mikonini KCC ambao ndio wanaotetea taji hilo, zikiwa kundi B.
Mapema wakati wa alasiri, kutakuwa na mchezo mwengine wa kundi hilo, baina ya Mtende Rangers na mabingwa wa soka Zanzibar, KMKM.
Yanga SC ambao kwa miaka miwili iliyopita hawakushiriki mashindano hayo kwa sababu mbalimbali, wataanza resi za kuwania taji hilo Januari 3, dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda katika mchezo wa kundi A.
Wakati wa saa 10:00 alasiri, kutakuwa na mechi ya kundi C kati ya wajenga uchumi wa Zanzibar JKU na wazalishaji sukari wa Morogoro, Mtibwa Sugar.
Kwa jumla, timu zinazoshiriki mashindano hayo zimepangwa katika makundi matatu, ambapo kundi A linajumuisha timu za SC Villa, Yanga SC, Polisi na Shaba.
Mabingwa wa kombe hilo KCC, Azam FC, KMKM na Mtende Rangers ziko kundi B, huku kundi C likiundwa na wekundu wa Msimbazi Simba SC, Mtibwa Sugar, JKU na Mafunzo.
Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya robo fainali, na timu mbili zitapatikana kutokana na washindwa waliofanya vizuri (Best Loosers).
Fainali ya ngarambe hizo imepangwa kupigwa Januari 13, 2015.
WAAMUZI 18 WAPATA BEJI ZA FIFA
Waamuzi 18 wa Tanzania wamepata beji za uamuzi za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa mwaka 2015.
Idadi hiyo ambayo ni rekodi kwa Tanzania inahusisha waamuzi saba wa kike. Waamuzi wa kati wa kike waliopata beji hizo ni pamoja na Jonesia Rukyaa Kabakama aliyechezesha mechi ya Nani Mtani Jembe kati ya Simba na Yanga. Wengine ni Florentina Zablon Chief na Sophia Ismail Mtongori.
Waamuzi wasaidizi wa kike waliopata beji hizo ni Dalila Jafari Mtwana, Grace Wamala, Hellen Joseph Mduma na Kudura Omary Maurice.
Kwa waamuzi wa kati wa kiume ni Israel Mujuni Nkongo, Martin Eliphas Sanya, Mfaume Ali Nassoro na Waziri Sheha Waziri. Waamuzi wasaidizi ni Alli Kinduli, Ferdinand Chacha, Frank John Komba, John Longino Kanyenye, Josephat Deu Bulali, Samuel Hudsin Mpenzu na Soud Iddi Lila.
AZAM, SIMBA, YANGA, MTIBWA KUCHEZA KOMBE LA MAPINDUZI
Timu za Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga zitashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayofanyika kisiwani Zanzibar kuanzia Januari 1 hadi 13 mwakani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa ruhusa kwa timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake imeondolewa mahakamani.
Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za raundi ya tisa na kumi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitachezwa katikati ya wiki baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo.
Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba. Mechi za wikiendi ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa ruhusa kwa timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake imeondolewa mahakamani.
Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za raundi ya tisa na kumi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitachezwa katikati ya wiki baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo.
Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba. Mechi za wikiendi ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
Monday, December 29, 2014
PHIRI AFUNGASHIWA VIRAGO SIMBA
KLABU ya Simba imeamua kumfungashia virago Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri kutoka Zambia.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza jana kuwa, kocha huyo alitarajiwa kukabidhiwa rasmi barua ya kuvunja mkataba wake jana.
Kwa mujibu wa habari hizo, Simba imeamua kuvunja mkataba na Simba kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Simba imemfungashia virago Phiri siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, kocha huyo aliingoza Simba kuichapa Yanga mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyochezwa kwenye uwanja huo.
Phiri alikaririwa jana kwenye mitandao ya kijamii akithibitisha kutaarifiwa kuhusu kuvunjwa kwa mkataba wake.
Kocha huyo amesema ni suala la kawaida kumtokea kocha, hivyo hana kinyongo na uongozi wa klabu hiyo.
"Wamenitaarifu kuhusiana na kuachishwa kazi, hili si jambo jipya, ingawa niliona tungeweza kubadilisha mambo.
"Najua Simba wanataka kufanya vizuri, hivyo siwezi kumlaumu mtu na utaona mwendo wa timu yetu ulivyokuwa," alisema Phiri.
Phiri amesema anatarajia kurejea kwao baada ya kulipwa madai yake na uongozi wa Simba. Hakutaja kiasi anachoidai klabu hiyo kama mishahara na fidia ya kuvunjwa kwa mkataba.
YANGA MDOMONI MWA MBEYA CITY J'MOSI, SIMBA YAIFUATA MGAMBO SHOOTING
WAKATI raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ilikamilika Desemba 29 mwaka huu kwa mechi tatu, ligi hiyo itaingia raundi ya tisa Januari 3 mwakani kwa mechi tano.
Coastal Union itacheza na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Sokoine.
Ligi hiyo ambayo itachezwa mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.
Nayo mechi kati ya Mtibwa Sugar na Stand United ambayo jana ilivunjwa na mvua dakika ya 6 imemaliziwa leo ambapo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.
Wakati huo huo, mechi ya ligi iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex imemalizika kwa wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu. Bao hilo lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Hamisi Kasanga.
MBAO FC YAKAMATA USUKANI SDL
Timu ya Mbao FC ya Mwanza imekamata uongozi wa Kundi B la michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha JKT Rwamkoma ya Mara mabao 2-1.
Kwa matokeo hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa kwa kushinda mechi zote tatu dhidi ya Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma.
Mbao FC inafuatiwa na JKT Rwamkoma yenye pointi sita, Arusha FC pointi sita wakati Bulyanhulu na Pamba zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila moja. Kundi hilo litakamilisha mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi kati ya JKT Rwamkoma na Arusha FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.
Katika kundi A, Mji Mkuu (CDA) na Singida United ndizo zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba kila moja. Timu hizo zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa FC yenye pointi moja wakati Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina pointi.
Hata hivyo, Mvuvumwa FC na Milambo ziko nyuma kwa mechi moja. Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu kati ya timu hizo itachezwa kesho (Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Kiluvya United imeendelea kuchachafya kundi C baada ya kushinda mechi zote ne ilizocheza, hivyo kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano yenye pointi saba huku Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.
Nafasi ya nne inashikwa na Transit Camp yenye pointi nne, Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano wakati Kariakoo ambayo haina pointi ni ya mwisho. Hata hivyo, Cosmopolitan na Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.
Mechi zinazofuata za kundi hilo ni Januari 3 mwakani kati ya Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano (Ilulu), Transit Camp na Abajalo (Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya (Karume).
Kundi D, vinara bado ni Njombe Mji yenye pointi 12 ikifuatiwa na Wenda yenye pointi sita wakati Volcano FC iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano. Mkamba Rangers ina pointi nne, Town Small Boys ina pointi moja wakati Magereza FC haina pointi.
Katika kundi hilo leo (Desemba 28 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Magereza itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Januari 3 mwakani kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na Magereza, na Wenda na Mkamba Rangers.
Subscribe to:
Posts (Atom)
























