KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, October 2, 2017

YANGA YABANWA MBAVU NA MTIBWA SUGAR, SIMBA YAKWEA KILELENI MWA LIGI KUU



MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita walikwaa kisiki mbele ya Mtibwa Sugar baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu.

Kutokana na sare hiyo iliyopatikana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Mtibwa iliendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano huku Yanga ikiwa nafasi ya sita.

Hata hivyo, Mtibwa Sugar ilienguliwa kwenye uongozi na Simba jana, baada ya timu hiyo kongwe kuilaza Stand United mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Ushindi huo uliifanya Simba iongoze ligi hiyo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yake na Mtibwa na Azam, kufuatia kila moja kuwa na pointi 11.

Iliwachukua Simba dakika 17 kuhesabu bao la kwanza kupitia kwa winga wake, Shiza Kichuya, kwa shuti kali la umbali wa mita 20, baada ya kupewa pasi na Erasto Nyoni. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Bao la pili la Simba lilifungwa na Laudit Mavugo dakika ya 47 baada ya kuwatoka mabeki wa Stand United, akiwa amepokea pasi kutoka kwa Haruna Niyonzima.

Stand United ilipata bao la kujifariji dakika ya 52 kupitia kwa Mtasa Munashe kwa njia ya penalti.

Katika mechi nyingine iliyochezwa mwishoni mwa wiki, Azam iligawana pointi na Singida United baada ya kutoka nayo sare ya bao 1-1.

No comments:

Post a Comment