Na Furaha Omary
UPELELEZI wa kesi inayowakabili Rais wa
Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu' bado haujakamilika.
Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter
akishirikiana na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Leonard Swai, walidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hayo walidai mbele ya Hakimu Mkazi,
Godfrey Mwambapa, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa, ambapo waliomba
kuahirishwa hadi tarehe nyingine.
Hakimu Mwambapa aliahirisha shauri hilo
hadi Oktoba 11, mwaka huu, kwa kutajwa
na washitakiwa walirudishwa mahabusu.
Mara ya mwisho, upande wa jamhuri
uliieleza mahakama kuwa jalada la shauri hilo liko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka
nchini (DPP), hivyo wanasubiri lirejeshwe ili kujua kinachoendelea na
usikilizwaji wa shauri kama DPP atakuwa amejiridhisha na uchunguzi kuwa
umekamilika.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na
mashitaka matano, yakiwemo ya kutakatisha fedha, hivyo kuwafanya wakae mahabusu
kwa kuwa shitaka hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Mashitaka mengine yanayowakabili ni
kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za Marekani
300,000.
Washitakiwa hao wanadaiwa Machi Machi
15, mwaka jana, walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha
fedha ya Machi 5, mwaka jana, wakionyesha klabu ya Simba inalipa mkopo wa
USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati siyo kweli.
Pia, washitakiwa hao wanadaiwa
Machi 15, mwaka jana, katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe, Ilala, Aveva
akijua alitoa nyaraka za uongo, ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya
Machi 15,2016, wakati akijua ni kosa.
Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya
Machi 15 na Juni 29, mwaka jana, Dar es Salaam, kwa pamoja walikula
njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la
uhalifu.
Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,
mwaka jana, katika benki ya Barclays, Mikocheni, alijipatia USD 300,000, wakati
akijua zimetokana na kughushi.
Nyange anadaiwa kuwa Machi 15, mwaka
jana, katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni, alimsaidia Aveva kujipatia USD
300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.
No comments:
Post a Comment