'
Thursday, October 20, 2016
YANGA YAIBUGIZA TOTO AFRICAN MABAO 2-0, AZAM YALAZIMISHWA SARE NA MTIBWA SUGAR
MABINGWA watetezi Yanga jana waliwapa ahueni mashabiki wao baada ya kuichapa Toto African mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inazo pointi 18 baada ya kucheza mechi tisa huku ikiwa inaendelea kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Simba na Stand United.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa na Simon Msuva, ndio walioiwezesha Yanga kutoka uwanjani na pointi zote tatu baada ya kuifungia mabao hayo mawili.
Chirwa alifunga bao la kwanza dakika ya 29 alipounganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Simon Msuva. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Bao la pili lilifungwa na Msuva dakika ya 56 baada ya Deus Kaseke kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Wakati huo huo, Jahazi la Azam jana liliendelea kudidimia baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar katika mechi ya ligi kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliochezwa usiku, Mtibwa ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya pili lililofungwa na Rashid Mandawa kabla ya Himid Mao kuisawazishia Azam dakika ya 11 kwa njia ya penalti.
Kwa matokeo hayo, Azam sasa inazo pointi 13 baada ya kucheza mechi 10 wakati Mtibwa imefikisha pointi 16 kutokana na kucheza mechi 11.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Ruvu Shooting ilitoka sare ya bao 1-1 na Mwadui, Ndanda ilitoka sare ya bao 1-1 na Mbeya City, Prisons iliichapa Stand United mabao 2-1 wakati Majimaji iliona mwezi kwa kuifunga African Lyobn mabao 2-0.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment