KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 27, 2016

YANGA YAPIGWA THALATHA NA MEDEAMA YA GHANA


JAHAZI la Yanga limeendelea kuzama katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Medeama ya Ghana.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Essipong Sports mjini Sekondi-Takoradi, Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa imeshafungwa idadi hiyo ya mabao.

Hiyo ni mechi ya nne mfululizo kwa Yanga kushindwa kutoka uwanjani na kishindo katika hatua ya makundi ya michuano hiyo, ikiwa imefungwa mechi tatu na kutoka sare moja.

Mabingwa hao wa soka nchini walianza michuano hiyo kwa kufungwa bao 1-0 na Mo Bejaia nchini Algeria, kabla ya kufungwa bao 1-0 na TP Mazembe na kutoka sare ya 1-1 na Medeama mjini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Medeama ilijipatia mabao yake kupitia kwa Daniel Amoah dakika ya saba, aliyemalizia kona ya Enock Atta Agyei.

Bao la pili lilifungwa na Abbas Mohammed, dakika ya 23 kabla ya kuongeza la tatu dakika ya 37.

Yanga ilijipatia bao lake la pekee dakika ya 25 lililofungwa kwa njia ya penalti na Simon Msuva baada ya Obrey Chirwa kuangushwa kwenye eneo lahatari.

Kipa Deo Munishi 'Dida' aliiokoa Yanga isiadhirike zaidi baada ya kuokoa penalti dakika ya 10 iliyopigwa na Malik Akowuah.

No comments:

Post a Comment