'
Thursday, February 25, 2016
KAPUMZIKE KWA AMANI KASSIM MAPILI
Na Rashid Zahor
FANI ya muziki wa dansi nchini juzi ilipata pigo baada ya mwanamuziki mkongwe na nguli, Kassim Mapili, kufariki dunia akiwa usingizini.
Mapili, alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi, nyumbani kwake Tabata Matumbi, ikiwa ni siku chache baada ya kushiriki kwenye mazishi ya mtangazaji wa Redio Tumaini, Fred Mosha, aliyezikwa Jumatatu iliyopita kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kifo cha Mapili kilijulikana baada ya majirani kutomuona kwa siku mbili nzima na kutia shaka, ndipo walipoamua kuvunja mlango wa chumba chake na kumkuta akiwa amelala kitandani, akiwa amekata roho.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, mazishi ya mwanamuziki huyo mkongwe na mahiri katika kupiga gita la solo na kuimba, yanatarajiwa kufanyika leo kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Kifo cha marehemu Mapili kimewagusa watu wengi, si wanamuziki na mashabiki wa fani hiyo pekee, bali hata wananchi wa kawaida. Alikuwa mcheshi na anayependa kujichanganya na watu mbalimbali. Lakini kikubwa zaidi alikuwa smati kwa mavazi na msafi kupindukia.
Mara nyingi marehemu Mapili alipenda kuvaa suti na kofia. Na kama hakuvaa suti, basi alipenda kuvaa suruali, shati na tai bila kuacha kofia. Huo ndio ulikuwa utamaduni wake.
Nilianza kufahamiana na marehemu Mapili mwanzoni mwa miaka ya 1990, nikiwa mwandishi wa habari wa kujitegemea katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Kiongozi na pia Mwananchi na Majira wakati yalipoanzishwa.
Umaarufu na uhodari wake kimuziki ndio ulionifanya niandike makala hii iliyotoka kwenye gazeti la Kiongozi, toleo la pili la Julai, 1992.
ALIKOTOKEA
Marehemu Mapili aliwahi kuziongoza bendi nyingi za muziki wa dansi hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), kilipoanzishwa, wadhifa ambao aliendelea nao hadi mwaka 1993, licha ya kuwepo kwa migogoro mingi ya kiuongozi.
Akiwa kiongozi wa chombo hicho kilichoanzishwa mwaka 1982, kwa madhumuni ya kutetea maslahi ya wanamuziki wa Tanzania, Mapili alifanya mengi. Ndiye aliyebuni mtindo wa kuzikutanisha bendi zaidi ya mbili (Top Ten Show) na kufanya onyesho kwa wakati mmoja. Pia ndiye aliyetoa wazo la kuundwa ka kundi la Tanzania All Stars.
Marehemu Mapili pia ndiye aliyefanya juhudi za kukutana na wanamuziki wenzao wa Kenya mwaka 1988, kwa lengo la kuzungumzia hakimiliki za wanamuziki wa Afrika Mashariki na pia kubadilishana mawazo na ujuzi.
MUZIKI HAUKUMNUFAISHA KITU
Akizungumzia manufaa aliyoyapata kimuziki wakati huo, marehemu Mapili alikiri wazi kuwa muziki wa dansi haukumnufaisha chochote kwa kile alichodai kuwa, isingekuwa rahisi kwa mwanamuziki wa Tanzania kufaidika kutokana na kutokuwepo kwa sheria ya hakimiliki.
"Ingekuwepo sheria ya hakimiliki, bila shaka leo hii ningezungumza na wewe nikiwa kwenye jumba langu kubwa na pengine ningekuwa na magari lukuki ya kutembelea.
"Lakini maisha yetu wanamuziki wa Tanzania ni ya kusikitisha sana. Mwanamuziki anaweza kupiga muziki miaka hata 30, lakini asifaidike na chochote. Na hata anapokufa, wanawe hawana cha maana cha kurithi kutokana na jasho lake. Mfano mzuri ni wa marehemu Mbaraka Mwinshehe na Hemed Maneti,"alisema Mapili wakati huo akiwa nyumbani kwake Ilala, Dar es Salaam, huku akionekana kuwa na majonzi makubwa usoni.
Akielezea hali ya muziki ilivyokuwa wakati huo, marehemu Mapili alisema kiupigaji, muziki ulikuwa umepanda, lakini hakukuwa na maendeleo yaliyofikiwa katika hali za maisha ya wanamuziki kutokana na kutokuwepo kwa sheria ya hakimiliki.
Alisema kupanda kwa kiwango cha muziki wa dansi wakati huo, kulipaswa kwenda sambamba na kuinuka kwa hali za maisha ya wanamuziki. Alisema kilichopanda wakati huo kilikuwa ni kuibwa kwa nyimbo za wanamuziki na kuuzwa holela na maharamia wa muziki.
Mapili, ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wanamuziki wa Tanzania, alisema kigezo cha nyimbo nzuri ni kuuzwa na kununuliwa kwa wingi.
Aidha, alisema nyimbo zote za wanamuziki wa Tanzania zilipokuwa zinapigwa nchini Kenya, zilikuwa na haki ya kulipwa na kwamba CHAMUDATA kwa wakati huo, ilifikia makubaliano na wenzao wa Kenya kwamba fedha hizo zilikuwepo, lakini ufuatiliaji wa vyombo vinavyohusika kiserikali ulikuwa mbovu.
HALI YA MUZIKI
Akizungumzia tungo za wanamuziki wa Tanzania kimashairi, Mapili alisema hazikuwa zikivutia sana kama ilivyokuwa kwa wanamuziki wa miaka ya 60 hadi 80. Alilaumu mtindo wa bendi nyingi kutunga na kurekodi nyimbo nyingi kwa wakati mmoja, ambazo zilitungwa bila mpangilio wa kuvutia.
Kwa upande wa waimbaji na wapigaji wa ala za muziki wa enzi zake, marehemu Mapili alieleza kuvutiwa na watunzi na waimbaji mahiri wa zamani wa mkoani Morogoro, marehemu Salum Abdalla na marehemu Mbaraka Mwinshehe. Pia alieleza kuvutiwa na kiongozi wa bendi ya Shikamoo Jazz hadi sasa, Salum Zahor na bendi za Western Jazz, Tabora Jazz, Jamhuri Jazz na Atomic Jazz.
Alisema nyimbo zilizotungwa na kuimbwa na wanamuziki hao na bendi zao bado zinapendwa hadi sasa kutokana na ala kupangiliwa kwa ufundi wa hali ya juu na mashairi kuwa na mvuto wa aina yake.
Marehemu Mapili pia aliwalalamikia viongozi wa serikali waliokuwa wakisimamia maslahi ya wasanii kwa kutowapa kipaumbele, badala yake walikuwa wakipenda kuwatumia katika hafla mbalimbali za kitaifa na kuwalipa ujira kidogo.
Alisema matatizo ya wanamuziki yalikuwa yakieleweka wazi, lakini viongozi wa serikali walikuwa wakiyaafumbia macho. Vilevile alilaumu mtindo wa kuhamisha masuala yanayohusu utamaduni kutoka wizara moja hadi nyingine na hivyo kukwamisha juhudi zao za kutetea maslahi yao.
Mkongwe huyo wa muziki alisema maonyesho ya Top Ten yaliyokuwa yakiandaliwa na CHAMUDATA kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), yaliwavutia mashabiki wengi na kuleta ushindani uliosaidia kuinua kiwango cha muziki, lakini baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuingilia kati na kutaka wawe waandaaji, yalikufa kabisa.
Alisema tamaa ya viongozi wa BASATA ndiyo iliyosababisha hali hiyo, kwa kudhani kuwa kulikuwepo na manufaa fulani yaliyotokana na mashindano hayo.
ASHAURI MUZIKI WA ASILI UENZIWE
Ili kuinua kiwango cha muziki nchini wakati huo, marehemu Mapili alitoa mwito kwa wanamuziki wa Tanzania kupiga muziki wa kiasili na kuacha kupiga muziki wa kuiga kutoka nchi jirani, hasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
"Kuna umuhimu hivi sasa kubadili mwelekeo wetu kimuziki na kufuata nyayo za wenzetu wa Tatunane na Tanzanites. Tujaribu kuuondoa muziki wetu kwenye ala za asili na kuuweka kwenye ala za kisasa. Hivi ndivyo wafanyavyo hata wenzetu wa mataifa mbalimbali hapa Afrika,"alisema.
Alitoa mfano wa baadhi ya nyimbo nyingi za asili zilizopigwa na bendi za Tanzania kuwa zinavutia, hivyo aliwashauri wanamuziki kuendeleza juhudi hizo, ikiwezekana kujifunza zaidi namna ya kutumia ala mbalimbali za kisasa za muziki ili waweze kwenda na wakati.
Marehemu Mapili pia alizishauri bendi za Kitanzania kutoajiri idadi kubwa ya wanamuziki, hali inayoweza kusababisha mishahara na marupurupu yao kuwa hayaridhishi. Alishauri bendi kuwa na idadi ndogo ya wanamuziki ili ufanisi na maslahi ya wanamuziki yawe ya kuridhisha.
Aliwataja wanamuziki waliokuwa wakimvutia wakati huo kuwa ni Moshi William (sasa marehemu), Remmy Ongara (naye marehemu) na Hassan Bitchuka.
Alimsifu marehemu Moshi kuwa tungo zake zilikuwa zinagusa hisia, nyimbo za Remmy zilikuwa na hisia kali na mashairi ya matukio na kwamba sauti ya Bitchuka ina mvuto na iwezayo kumliwaza msikilizaji.
ALIVYOANZA MUZIKI
Marehemu Mapili alizaliwa mwaka 1942 mkoani Lindi. Alisoma katika shule ya msingi ya Lionja Mission kuanzia 1949 hadi 1956, ambapo alikatisha masomo na kupelekwa kusoma masomo ya Quraan.
Alianza kujishughulisha na muziki mwaka 1960, katika bendi ya White Jazz ya Lindi na mwaka uliofuata, alichukuliwa na marehemu Ahmad Omar kwenda Mtwara, alikojiunga na bendi ya Mtwara Jazz.
Mwaka 1963, alirejea tena Lindi na kujiunga na bendi ya Jamhuri, ambayo baadaye aliibadili jina na kuiita TANU Youth League. Baadhi ya wanamuziki aliokuwa nao katika bendi hiyo ni Athumani Manzi, Ali Bamtoto na Kaisi.
Mwaka 1965, alifuatwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa wakati huo ili kwenda kufungua bendi ya muziki, ambayo aliita Lucky Star Jazz. Aliiongoza bendi hiyo kwa miezi michache kabla ya kuamua kuhamia Dar es Salaam baada ya kufuatwa na marehemu Ahmed Kipande wa Kilwa Jazz.
Huko alikutana na wanamuziki wengine nyota wa wakati huo kama vile Saidi Vinyama, Hassan Shabani, Juma Town, Athumani Omar, Kisi Rajabu, Abdu Baker na Juma Mrisho.
Baadhi ya nyimbo maarufu alizotunga wakati huo ni Kutyangatyanga mpunguti, Doli, Nililazwa jela na Kukurukakara mwatati.
Alikaa Kilwa Jazz kwa miezi michache kabla ya uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kumuomba kuanzisha bendi, ambayo aliiongoza kwa miezi michache na kuamua kubisha hodi Polisi Jazz, baada ya kufuatwa na Mzee Lawi Sijaona. Huko akateuliwa kuwa mwalimu wa muziki.
Mwaka 1969, alifuatana na bendi ya kwanza ya wanawake hapa nchini, Womes Jazz, ambayo alikuwa akiifundisha muziki, kwenda Kenya kushiriki kwenye sherehe za siku ya Kenyatta.
Baadhi ya wanamuziki aliokwenda nao Kenya ni pamoja na Mama Raheli, Kijakazi Mbegu, Mwanjaa Ramadhani, Siwema Mponji, Mwamvita Mwagoha, Rukia Hassan, Mary Kilima na mmoja aliyemtaja kwa jina la Josephina.
Akiwa katika bendi ya Polisi Jazz, Mapili aliweza kutunga nyimbo kadhaa zilizompatia umaarufu mkubwa. Baadhi ya nyimbo hizo ni Pongezi viongozi Tanzania, Kashma Kaligi, Josephina, Afrika tutaikomboa, Teddy, Dunia ni watu, Ulimi wa pilipili na Hongera Zimbabwe.
Aliiacha bendi ya Polisi mwaka 1980, akiwa na cheo cha sajenti na kujiunga na Tanzania Stars, ambayo ilikuwa ikipiga zaidi nyimbo za kuiga. Baadaye aliishauri kubadili mwelekeo na kuanza kupiga nyimbo zao wenyewe. Ndipo alipoibuka na tungo kama vile Mawazo, Jamila, Chiriku, Sanura mtoto wa Ilala, Safari sio kifo na Tuzo gani nimpe mke wangu.
Aliamua kustaafu muziki mwaka 1987 na kujikita zaidi katika kuisimamia CHAMUDATA, akiwa bado mwenyekiti. Akiwa kiongozi wa chama hicho,alitunga wimbo wa kuomboleza kifo cha Rais wa kwanza wa Msumbiji, marehemu Samora Machel, aliyefariki dunia mwaka 1986, akishirikiana na marehemu Marijani Rajabu.
Vilevile alishiriki katika kuunda kundi la Tanzania All Stars, lililorekodi nyimbo nne, ambazo ni Kifo cha Samora, Miaka 10 ya CCM, Azimio la Arusha na Kuwajibika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment