KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 20, 2013

RAGE OUT SIMBA, KIBADENI, JULIO NAO WATUPIWA VIRAGO



KAMATI ya Utendaji ya Simba imemsimamisha mwenyekiti wa klabu hiyo Ismail Aden Rage kutokana na kukosa imani naye na kuwatupia virago Kocha Mkuu Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo 'Julio'.
Rage amekumbwa na rungu hilo kwa madai ya kukiuka makubaliano ya kamati ya utendaji na kutoa uamuzi wake binafsi, huku kocha Zdravock Logarusic raia wa Croatia akitangazwa ndiye mpya aliyemrithi Kibadeni na atasaidiwa na kocha wa vijana Suleiman Matola.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba Joseph Itang'are 'Kinesi', alisema uamuzi huo ulifikiwa juzi na kamati hiyo kwenye kikao ambacho kilihudhuriwa na wajumbe wote.
"Jana (juzi) kamati imekaa na kuamua kwa nia nzuri ya kuboresha utendaji na si kumkomoa mtu na moja ya maamuzi tuliyofikia, ni kumsimamisha mwenyekiti wetu (Rage) ambaye amekiuka makubaliano ya kamati na kufanya maamuzi yake binafsi," alisema Kinesi.
Alisema moja ya makubaliano aliyokiuka mwenyekiti huyo ni kusimamisha mkutano mkuu wa Simba wa marekebisho ya katiba uliopangwa kufanyika mwezi huu, kwa madai anasafiri.
Kaimu Makamu Mwenyekiti huyo alisema kosa lingine la Rage, kuyaagiza matawi yaendelee kutuma taarifa juu ya marekebisho hayo ya katiba.
Kinesi alisema licha ya kumsimamisha Rage kikao hicho pia, kiliazimia kufanya mkutano mkuu wa marekebisho ya katiba kama ulivyopangwa na sasa utafanyika Desemba mosi, mwaka huu katika ukumbi utakaotangazwa baadaye.
Alisema mkutano huo utakuwa na ajenda kuu mbili; kutokuwa na imani na Rage, na marekebisho ya katiba ya Simba.
Akifafanua kuhusu kifungu walichotumia kumsimamisha Rage, Kinesi alisema wametumia kifungu cha katiba ibara ya 30 (m) kinachoeleza kuwa, kamati ya utendaji inaweza kuchukua hatua zozote inazoona zinafaa kumwajibisha mwenyekiti.
Kutokana na uamuzi huo wa kumweka Rage kando, nafasi ya mwenyekiti kuanzia sasa inaikaimiwa na Kinesi na Kaimu Makamu Mwenyekiti ni Swed Nkwabi.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa Simba aliyesimamishwa hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa yupo nje ya nchi.
Hii ni mara ya pili Rage kusimamishwa katika klabu hiyo baada wanachama wapatao 700, kuitisha mkutano wa kumsimamisha uliofanyika katika ukumbi wa Star Light Hoteli mapema mwaka huu, lakini Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilipinga 'mapinduzi' hayo kwa maelezo kuwa ni batili.
Kuhusu benchi la ufundi la Simba, Kinesi alisema kamati hiyo iliona kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko na ndio maana imeazimia kumleta kocha huyo Logarusic aliyekuwa akiinoa timu ya Gor Mahia ya Kenya.
Alisema kocha huyo atawasili nchini Desemba mosi na tayari taratibu zote kuhusu mkataba wake ziko katika matayarisho.
Makamu mwenyekiti alisema mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha benchi la ufundi ambalo lilionekana kutofanya vyema katika mzunguko wa kwanza huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa wachezaji.
"Naamini baada ya kocha kuja mambo yatabadilika kwani tunachotaka kuona ni timu yetu ikifanya vizuri katika mzunguko wa lala salama na kuwania ubingwa," alisema Kinesi.
Simba imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza michezo 13.

No comments:

Post a Comment