KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 24, 2013

KITABU CHA FERGIE CHAZUA BALAA


LONDON, England
KOCHA Mkuu wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amesema Carlos Tevez na Anderson, waliikosesha timu hiyo ubingwa wa Ulaya 2009 katika mchezo wa fainali dhidi ya Barcelona.

Kauli hiyo ya Ferguson ni mwendelezo wa mashambulizi yake kwa wachezaji wa Man United, kupitia katika kitabu chake alichokizindua juzi.

Katika mechi hiyo, Manchester United ilichapwa mabao 2-0 na Barcelona
na Ferguson, ameweka bayana kuwa, chanzo cha kipigo ni Anderson kushindwa kucheza vyema nafasi ya kiungo.

Alisema Anderson alipiga pasi tatu katika dakika 45 za mwanzo, lakini Tevez alikuwa mchoyo na alicheza mechi hiyo kwa ubinafsi.

"Michael Carrick alipwaya, lakini tatizo kubwa lilikuwa kwa Anderson," alisema kocha huyo, ambaye kwa sasa amestaafu.

Katika kitabu hicho, Fergie pia alielezea sababu ya kumpiga bei nahodha wa zamani wa England, David Beckham. Alisema mchezaji huyo alianza kuwa na majivuno na
kujiona mtu mzito kuliko kocha.

Fergie alisema, alianza kukorofishana na Beckham baada ya kumshutumu kwa kucheza vibaya katika michuano ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal mwaka 2003, ambapo Man United ilifungwa.

"Dakika moja, ambayo mchezaji wa Manchester United atafikiria ni mkubwa kuliko kocha, alipaswa kuondoka," ameandika Fergie katika kitabu hicho. "David alijiona mkubwa kuliki Alex Ferguson."

Fergie amesema pia kuwa, hakufurahishwa na maisha ya kifahari aliyokuwa akiishi Beckham, baada ya kufunga ndoa na Victoria Adams, mmoja wa wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi la Spice Girls.

Katika kipindi cha miaka 26, alichokuwa akiifundisha Man United, Fergie aliiwezesha kutwaa mataji 38 na kuwaongoza wachezaji wengi nyota kama vile Beckham, Eric Cantona, Cristiano Ronaldo, Peter Schmeichel, Bryan Robson, Roy Keane, Jaap Stam na Ruud Van Nistelrooy.

Fergie pia ameelezea alivyoamua kumweka benchi Wayne Rooney na kuiacha hatma yake kwa kocha mpya, David Moyes, alivyokataa kuwa kocha mkuu wa England mara mbili na jinsi alivyogombana na Rafael Benitez.

Kocha huyo wa zamani wa Man United, pia amempamba mshambuliaji Cristiano Ronaldo, akimwelezea kuwa ni mchezaji aliyejaliwa kipaji cha aina yake cha kucheza soka.

No comments:

Post a Comment