KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 1, 2013

MATAWI SIMBA KUANZA KUTOA MAONI YA MAREKEBISHO YA KATIBA LEO


MARA baada ya kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau kuhusu mapendekezo ya Katiba ya Simba, uongozi wa klabu unapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa wote walioshiriki kwenye hatua hiyo.

Mara baada ya kumalizika kwa hatua hiyo ya kwanza, matawi ya Simba sasa yanakaribishwa kuanza kutoa maoni yao kuanzia kesho (Jumanne), Oktoba Mosi mwaka 2013.
Matawi yatajadili na kutoa maoni yao kabla ya kuwasilisha kwa sekretarieti ya klabu iliyopo katika Ofisi za Makao Makuu Mtaa wa Msimbazi Dar es Salaam.

Sekretarieti ya Simba itapokea maoni haya hadi Oktoba 11 mwaka huu.
Sekretarieti ya klabu itayakusanya na kuyachambua maoni yote yaliyotolewa na baada ya uchambuzi huo, yatapelekwa kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ambao nao watafanya mapitio yao.
Uchambuzi na mapitio yatakayofanywa kwa baraka za Kamati ya Utendaji ndiyo ambayo yatapelekwa kwenye kikao cha Matawi kilichopangwa kufanyika Novemba 11 mwaka huu.
Wiki moja baadaye, yaani Novemba 19 mwaka huu, Kamati ya Utendaji kwa ridhaa iliyopewa na Katiba ya Simba SC, itapitisha vipengele vya kuombewa mabadiliko ya Katiba.
Vipengele hivyo ndivyo ambavyo vitawasilishwa Novemba 24 mwaka huu kwenye Mkutano Maalumu wa Mabadiliko ya Katiba uliotangazwa kufanyika na klabu katika Mkutano Mkuu wa wanachama uliopita.
Uongozi unawaomba wanachama kupitia matawi yao kushiriki kikamilifu katika mchakato huu adhimu kwa klabu. Ni matarajio ya klabu kwamba mchakato huu hautatumika kuwagawa bali kuwafanya wawe kitu kimoja kwa faida ya Simba.
Mungu Ibariki Simba SC. Nguvu Moja.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

No comments:

Post a Comment