KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, December 9, 2011

KITWANA MANARA; Tumepiga hatua kimaendeleo, si kimashindano

KITWANA Manara (kushoto) akiwa na mwanasoka mwenzake mkongwe, Peter Tino



KAMA kuna mwanasoka aliyewahi kuweka rekodi ya pekee na ya aina yake hapa nchini, si mwingine zaidi ya mkongwe Kitwana Manara.Ndiye mchezaji pekee aliyeweza kucheza nafasi ya kipa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na nafasi ya mshambuliaji kwenye klabu yake ya Yanga.
Mkongwe huyo pia ndiye mchezaji pekee aliyeweka rekodi ya kucheza soka kwa miaka mingi kuliko mchezaji mwingine yeyote Tanzania. Alianza kucheza soka mwaka 1960 na kutundika daruga zake ukutani mwaka 1980.
Manara alianza kuvaa jezi za Taifa Stars mwaka 1961 akitokea klabu ya Cosmo ya Dar es Salaam. Alistaafu kuichezea timu hiyo mwaka 1975 akiwa klabu ya Yanga.
Alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga walioiwezesha timu hiyo kuwa ya kwanza nchini kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970.
Katika hatua zote hizo mbili, Yanga ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana, ambapo katika robo fainali ya mwaka 1969, iliondoshwa kwa njia ya kura ya shilingi baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika robo fainali ya pili mwaka 1970, Yanga ilikutana tena na Asante Kotoko, ambapo katika mechi ya awali, zilitoka sare ya bao 1-1 na katika mechi ya marudiano, hazikufungana.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane katika muda wa nyongeza, lakini kutokana na giza kutanda uwanjani, mechi ilivunjika dakika ya 19 na hivyo kuhamishiwa kwenye uwanja huru wa mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mechi hiyo ya tatu, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Asante Kotoko na kutolewa kwenye hatua hiyo. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa chini ya Victor Stanculescu kutoka Romania.
Manara pia alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza michezo ya All Africa Games mwaka 1973 na kutinga nusu fainali, ambapo ilitolewa na Algeria baada ya kuchapwa mabao 2-1.
“Kwa kweli kama ni rekodi ya mwanasoka aliyecheza soka kwa miaka mingi hapa nchini na kwa nafasi mbili tofauti, hakuna anayeweza kuifikia rekodi yangu,”alisema. “Mimi nilianza kuichezea timu ya taifa kuanzia kwenye michuano ya Gossage hadi ilipobadilishwa jina na kuitwa Chalenji.”
Akizungumza na Uhuru hivi karibuni kuhusu mafanikio ya soka katika miaka ya 50 ya Uhuru, Manara alisema Tanzania imepiga hatua kubwa na kupata mafanikio ya kuridhisha.
Akitoa mfano, Manara alisema japokuwa kiwango cha uchezaji soka miaka ya nyuma kilikuwa juu ikilinganishwa na hivi sasa, kuwepo kwa vifaa vingi vya michezo na viwanja vya kisasa vya kuchezea mchezo huo ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Alisema miaka ya nyuma, vifaa vya michezo vilikuwa vichache na viwanja vilivyotumika kuchezea mchezo huo vilikuwa vya kawaida.
“Hivi sasa, timu yetu ya taifa imepata udhamini mkubwa, wachezaji wanalipwa vizuri, klabu zinamiliki viwanja vyao vya kuchezea soka, haya yote kwangu mimi ni mafanikio makubwa,”alisema.
Manara pia alieleza kufurahishwa kwake kuona Taifa Stars ikipata maandalizi kama ilivyo kwa baadhi ya nchi za mataifa ya Ulaya huku ikipatiwa huduma zote muhimu.
Alisema miaka ya nyuma, ilikuwa vigumu kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo kila ilipocheza ama kuhamasika na kuvaa fulana zenye rangi ya bendera ya taifa.
Manara alisema pia kuwa, soka inayochezwa hivi sasa ni ya kasi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, lakini baadhi ya vitu vinavyofanywa na wanasoka maarufu duniani kama vile Lionel Messi wa Barcelona ya Hispania si vigeni kwa Tanzania.
Aliwataja baadhi ya wanasoka wa zamani waliokuwa na uwezo wa kucheza na mpira wanavyotaka, kupiga chenga na kupangua idadi kubwa ya mabeki kwa wakati mmoja kuwa ni pamoja na Mbwana Abushiri, Emily Kondo, Arthur Mambeta, Sunday Manara na Abdalla Kibadeni.
Alisema uwezo wa wanasoka hao haukuweza kutambulika kimataifa kutokana na kutokuwepo kwa vyombo vingi vya habari kwa ajili ya kuwatangaza. Alisema vyombo vilivyokuwepo wakati huo kama vile magazeti, vilikuwa vichache na teknolojia ya televisheni haikuwepo.
Manara alisema Tanzania ni nchi pekee kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki iliyoweza kutoa wanasoka wengi nyota, ikilinganishwa na nchi za Kenya na Uganda.
Akizungumzia uongozi wa soka nchini, Manara alisema viongozi wa zamani wa klabu hawakuwa na elimu kubwa, lakini waliweza kubuni vitu vingi na kuziletea mafanikio makubwa klabu zao.
Akitoa mfano, alisema viongozi wa Yanga waliweza kununua nyumba mtaa wa Mafia kwa sh. milioni 11 kutokana na mapato ya sh. milioni 20 katika mechi kati yao na Abaluya ya Kenya na siku hiyo wachezaji hawakulipwa hata nauli.
“Hivyo utaona kuwa, uongozi wa zamani ulikuwa wa kujitolea zaidi na viongozi walihakikisha kila mchezaji anatafutiwa kazi na walicheza kwa moyo kwa sababu walikuwa wanachama wa klabu wanazochezea hivyo ilikuwa vigumu kuzihujumu,”alisema.
Alisema viongozi wa sasa wa klabu wana elimu kubwa, lakini wanakosa ubunifu na mashabiki wa klabu kongwe za Simba na Yanga wamekosa imani kwa viongozi wao, hasa timu zao zinapofungwa katika mechi muhimu.
Mkongwe huyo alisema ubunifu wa viongozi wa zamani ulianza kutoweka miaka ya 1976, ambapo klabu za Simba na Yanga zilianza kutawaliwa na migogoro mingi, iliyosababisha zigawanyike.
Alisema migogoro hiyo ndiyo iliyosababisha klabu ya Yanga kugawanyika na kuzaliwa Pan African na ile ya Simba nayo kugawanyika na kuzaliwa Nyota Nyekundu.
Manara alisema migogoro ya mara kwa mara ndani ya klabu hizo, ilichangia kwa kiasi kikubwa kudumaza maendeleo ya soka na timu ya taifa kwa vile Simba na Yanga ndizo zinazotoa mchango mkubwa kwenye timu ya taifa.
“Asikudanganye mtu, mafanikio ya Taifa Stars yanapaswa kuanzia klabuni. Kukiwa na migogoro kwenye klabu hizo mbili, timu yetu ya taifa nayo itakuwa mbovu,”alisema.
Manara ameupongeza uongozi wa sasa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuleta mageuzi makubwa katika mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kurejesha nidhamu kwa viongozi na kuleta utendaji mzuri.
“Kwa kweli mabadiliko katika uongozi wa chama cha soka yameonekana. Zamani pale uwanja wa Karume kulikuwa na jengo dogo tu kwa ajili ya ofisi za chama, lakini hivi sasa kuna ghorofa na uwanja wa kisasa wa mazoezi. Haya ni mafanikio makubwa,”alisema.
“Serikali nayo imejitahidi sana kutuletea makocha wa kigeni kwa ajili ya timu ya taifa na wachezaji wamekuwa wakihamasika kuichezea. Haya nayo ni mafanikio makubwa,”aliongeza.
Manara alimmwagia sifa kemkem Rais wa TFF, Leodegar Tenga kuwa ni kiongoni pekee aliyeleta mageuzi makubwa katika uongozi wa soka nchini na pia kuleta heshima kwa chama hicho.
Alisema nidhamu ndani ya shirikisho hilo imekuwa kubwa na kamati zimeachwa zifanyekazi zake kwa uhuru mkubwa bila ya kuingiliwa.
“Kwa kweli hajatokea kiongozi aliyeleta amani na utulivu katika chama cha soka kama Tenga. Waswahili wanasema, mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Tenga anastahili pongezi,”alisema.
Hata hivyo, Manara alisema wapo viongozi wengine wa chama hicho waliofanya vizuri huko nyuma, lakini hakuna anayeweza kufikia rekodi ya Tenga.
Manara amelitaka shirikisho hilo kufanya jitihada zaidi liwe na uwanja wake wa kuchezea soka kwa ajili ya kuongeza mapato yake, tofauti na ilivyo sasa, ambapo linategemea zaidi mgawo wa mechi za ligi kuu na za kimataifa.
Ameiomba serikali ifikirie kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo ili vijana wengi zaidi waweze kumudu kuvinunua na hivyo kuongeza hamasa kwao ya kushiriki katika mchezo huo.
Manara pia ametoa mwito kwa viongozi wa klabu na vyama vya soka, wawe wabunifu wa vyanzo vya mapato na uendeshaji wa mchezo huo kisasa zaidi badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi.
"Umefika wakati sasa, lazima kuwe na mabadiliko. Kiongozi anapochaguliwa kuongoza klabu, awe mtendaji wa kazi anayeipenda klabu yake. Asiwe mtu wa kuweka mbele mapato,"alisema.
Amewataka wanasoka wa Tanzania waone thamani ya kucheza soka kwa sababu mpira ni ajira na mchezaji anaweza kulipwa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya usajili pekee.
“Kama mchezaji anaweza kulipwa milioni 60 kwa msimu, anapaswa kuuheshimu mpira katika maisha yake kwa sababu ndiyo ajira yake,”aliongeza.
Amewataka viongozi wa klabu kuzithamini timu za vijana kwa vile ndizo chimbuko la wanasoka. Alisema timu hizo zinapaswa kupewa huduma zote muhimu kama ilivyo kwa timu za wakubwa ikiwa ni pamoja na kuzipatia usafiri wa uhakika.
Manara alianza kucheza soka katika timu za mitaani za Sambwisi, Young Boys, Cosmo, TPC ya Arusha, Feisal na baadaye Yanga na Pan African. Alistaafu rasmi kucheza soka mwaka 1983 akiwa Yanga, ambayo katika miaka miwili ya mwisho, aliifundisha akiwa kocha mchezaji.

No comments:

Post a Comment