KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 1, 2010

POULSEN: Kuzifunga Algeria na Morocco ni kazi ngumu

Asema anahitaji muda zaidi kujua uwezo wa wachezaji wake

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Jan Pulsen amesema itakuwa vigumu kwa timu yake kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2012.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wiki hii, Poulsen (64) alisema hafikirii iwapo timu yake itakuwa na uwezo wa kuzishinda Algeria na Morocco katika michuano hiyo.
Kocha huyo kutoka Denmark alikuwa akizungumzia maandalizi yake katika michuano hiyo, inayotarajiwa kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali vya Afrika mwishoni mwa wiki hii.
Taifa Stars inatarajiwa kutupa karata yake ya kwanza kesho kwa kumenyana na Algeria mjini Algiers. Timu zingine zilizopangwa kundi moja na Taifa Stars ni Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
“Soka si kama kiwanda, ambako utakwenda na kuwasha mashine kisha unaanza kazi,”alisema kocha huyo, ambaye chini yake, Taifa Stars imecheza mechi moja na kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Kenya.
“Unafanyakazi na watu na inachukua muda, inachukua miezi, inawezekana hata mwaka mmoja na nusu,”aliongeza.
Poulsen alisema anaamini itakuwa vigumu kwa Taifa Stars kufuzu kucheza fainali hizo, zitakazoandaliwa kwa pamoja na Gabon na Equatorial Guinea mwaka huo.
“Unadhani tunaweza kuzifunga timu kama Morocco? Unaelewa wazi kwamba hiyo itakuwa kazi ngumu na unaelewa kabla hujauliza swali,”alisema kocha huyo.
Kwa mara ya mwisho, Taifa Stars ilifuzu kucheza fainali hizo mwaka 1980 zilipofanyika nchini Nigeria. Tangu wakati huo, timu hiyo imekuwa ikishiriki katika michuano hiyo na kutolewa hatua za awali.
Poulsen aliteuliwa kuwa kocha mpya wa Taifa Stars mapema mwaka huu, akichukua nafasi ya kocha wa zamani, Marcio Maximo.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilikataa kumuongezea mkataba Maximo baada ya kushindwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu kucheza fainali za mwaka 2008 na 2010.
Hata hivyo, Poulsen alisisitiza kuwa, bado anahitaji muda zaidi kuwaelewa vyema wachezaji wake.
Alisema timu aliyonayo sasa, ameiteua kwa msaada mkubwa wa makocha wazalendo, hivyo anahitaji muda zaidi kutambua uwezo wao.

No comments:

Post a Comment