KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 8, 2010

Papic kutangaza kikosi chake leo



KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, Kostadin Papic leo anatarajia kukutana na viongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kuzungumzia usajili wa wachezaji wa kigeni na wa ndani.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema jana kuwa, kikao hicho kinatarajiwa kufanyika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Mwalusako alisema katika kikao hicho, Papic anatarajiwa kuwasilisha majina ya wachezaji watano wa kigeni watakaosajiliwa na Yanga msimu ujao na wengine 25 wa hapa nchini.
Kwa mujibu wa Mwalusako, kikao hicho ndicho kitakachohitimisha orodha ya usajili wa wachezaji wa Yanga kabla ya kuwasilishwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kikao hicho kinafanyika siku mbili baada ya Papic kurejea nchini juzi kutoka Serbia, alikokwenda kwa mapumziko mara baada ya ligi kuu ya msimu uliopita kumalizika.
Miongoni mwa wachezaji wa kigeni wanaotarajiwa kusajiliwa na Yanga msimu ujao ni beki wa kati, Isack Boakye, kiungo Ernest Boakye, mshambuliaji Keneth Asamoah kutoka Ghana na kipa Ivan Knezevic kutoka Serbia.
Pia kumezuka mvutano baina ya viongozi kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji wa kigeni, walioichezea timu hiyo msimu uliopita, ambapo baadhi wanataka waachwe wote wakati wengine wanataka wabaki wawili.
Kwa mujibu wa kanuni mpya za usajili za TFF, klabu zote za ligi kuu zinatakiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni. Mchezaji wa tano wa kigeni wa Yanga ni kipa Yaw Berko kutoka Ghana.
Mchezaji pekee wa kigeni mwenye mkataba na Yanga hadi sasa ni beki John Njoroge kutoka Kenya. Mkataba wa kipa Berko umeshamalizika, lakini uongozi umeamua kumuongezea mkataba mwingine.
Wachezaji wa kigeni waliotemwa na klabu hiyo ni Robert Jama Mba,Steven Bengo, Boniface Ambani, Moses Odhiambo, Obren Curkovic, Honore Kabongo, Wisdom Ndlovu na George Owino.
Michuano ya ligi kuu msimu ujao imepangwa kuanza Agosti 21 mwaka huu. Mazoezi ya Yanga kwa ajili ya ligi hiyo yamepangwa kuanza Julai 15.

No comments:

Post a Comment