KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 15, 2017

MO DEWJI NA HANS POPPE WAJIWEKA PEMBENI SIMBA



Mwanachama na kijana tajiri barani Afrika kwa sasa, Mohammed Dewji, anayetaka kununua hisa Simba, amesikitishwa na uongozi wa klabu hiyo kwa kuingia mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa bila kumshirikisha.

Habari ambazo hazijathibitishwa na upande wowote, zinasema Mo Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, ameuandikia barua uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais wake, Evans Aveva, kutaka alipwe fedha zake, sh bilioni 1.4, alizokuwa anaikopesha Simba kwa kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi, sh milioni 80 kila mwezi.
Imedaiwa Mo Dewji alikuwa anatoa fedha hizo kwa makubaliano zitalipwa wakati mpango wake wa kununua hisa za klabu utakapokamilika. Mo alikubaliana na uongozi wa Simba kununua asilimia 51 ya hisa kwa Sh. Bilioni 20 mara baada ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba utakapokamilika.
Lakini zoezi hilo linaelekea kuingia doa baada ya Mo Dewji kuandika katika ukurasa wake wa Twitter akilalamikia uongozi wa klabu kuingia mkataba na SportPesa bila kumshirikisha. 

Mwenyekiti wa kamati ya Usajili Zacharia Hans Poppe, mmoja wa wanachama na viongozi maarufu wa Klabu ya Simba, ameamua kuachia ngazi kwenye kamati ya utendaji.
Uamuzi wake wa kuondoka kamati ya utendaji, moja kwa moja unamuondoa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa kamati ya usajili.
Hans Poppe amesema kuwa, ameondoka baada ya jopo lililoongozwa na Rais wa Simba, Evans Aveva kuingia mkataba na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportsPesa ambao wamesaini mkataba wa Sh bilioni 4.9 kwa miaka mitano.
Akizungumza katika mahojiano maalum , Hans Poppe amesisitiza, ameamua kukaa pembeni na huyu ndiye amekuwa injini ya usajili katika kikosi cha Simba akipambana na mahasimu wao wakubwa nchini Yanga
“Nitabaki kama mwanachama wa kawaida wa Simba. Nitaendelea na shughuli zangu nyingine,” alisema na alipoulizwa sababu za kujiuzulu alisema:

 “Mambo yamekwenda kwa uficho, mkataba umekuwa ukifichwa. Kamati ya utendaji imetaarifiwa siku moja kabla ya kusainiwa. Ilikuwa Alhamisi, Ijumaa wamesaini, nini kinafichwa.
“Mimi nakaa pembeni, nimeshaandika na barua. Sitaki kuwa sehemu ya watu wasio waungwana. Angalia hata Mo Dewji hakuwa akijua, lakini huyu mtu mwaka mzima ndiye katukopesha mishahara.
“Dewji alisema, mkitaka kusaini mkataba kama mmepata mdhamini mniambie. Maana na yeye tulimpa jukumu la kutafuta mdhamini, hata mimi nilipewa jukumu hilo, lakini leo unasikia wenzako wameingia mkataba na mdhamini mpya.
“Kabla tumekuwa tukishirikiana kwa kila jambo, kwenye shida na raha. Vipi leo, nini kimefanya tusiwe pamoja?
“Kawaida walitakiwa waje na mkataba, tuujadili na kuangalia vipengele. Kama kuna sehemu zikarekebishwe au kuongezwa vifanyiwe kazi, mwisho wakija tuseme hapa sawa, basi usainiwe. Nani atakataa mdhamini kama unaona ana faida na klabu?” alihoji Hans Poppe.
Ijumaa SportPesa Tanzania ilitangza rasmi udhamini wake wa miaka mitano kwa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, wenye thamani ya Sh. Bilioni 4.96.
Mkurugezi wa Utawala wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema kwamba wameingia mkataba huko kwa dhumuni la kuendeleza soka nchini na kuisaidia klabu ya Simba kufikia malengo yake.
Akifafanua, Tarimba ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa mahasimu wa Simba, Yanga alisema kwamba, katika mkataba wao kwa mwaka wa kwanza wadhamini hao watatoa Sh. Milioni 888 na miaka itakayofuata wataongeza asilimia 5 na miaka miwili ya mwisho watatoa Sh. Bilioni 1 na kwamba fedha hizo zitatolewa kwa awamu nne kwa mwaka.
Tarimba alisema kwamba Simba watapaswa kuyathibitisha matumizi ya fedha hizo kwamba yalifanyika kwa maendeleo ya soka.
Alisema licha ya mkataba huo, pia kutakuwa na motisha klabu hiyo ikishinda mataji, mfano kwa ubingwa wa Ligi Kuu watapewa zawadi ya Sh. Milioni 100.
“Pia ikishinda michuano kama (Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati) Kombe la Kagame pia watapewa zawadi na wakifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika watapata zawadi ya Milioni. 250,”alisema Tarimba.

No comments:

Post a Comment