'
Monday, January 2, 2017
SIMBA YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI
TIMU kongwe ya soka ya Simba, juzi ilianza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa Taifa Jang'ombe bao 2-1 katika mechi ya kundi A iliyochezwa usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Katika mechi hiyo iliyokuwa kali na ya kusisimua, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0. Mabao hayo yalifungwa na Muzamil Yassin na Juma Luizio.
Iliwachukua Simba dakika 27 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Muzamil baada ya kuuwahi mpira uliogonga mwamba na kurudi uwanjani, kufuatia shuti la Method Mwanjali.
Luizio aliiongezea Simba bao la pili dakika chache baadaye kwa shuti kali baada ya kuwatoka mabeki wa Taifa Jang'ombe.
Taifa ilipata bao la kujifariji dakika ya 76 baada ya beki Novaty Lufunga wa Simba kujifunga, alipokuwa katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Hassan Bakari.
Katika mchezo wa awali, URA ya Uganda iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ.
Kwa matokeo hayo, Simba inalingana kwa pointi na URA na Taifa, ambayo katika mechi ya ufunguzi iliichapa Jang'ombe Boys bao 1-0.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment