KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 29, 2013

SIMBA YACHANUA, AZAM YAUA



Na Shaban Mdoe, Arusha

SIMBA jana ilivuna pointi tatu za kwanza katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Oljoro bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Ushindi huo ulileta ahueni kubwa kwa mashabiki wa Simba, kufuatia kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa mjini Tabora.

Kwa upande wa JKT Oljoro, kipigo hicho kilikuwa cha pili baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Coastal Union kwenye uwanja huo wiki iliyopita.

Katika mechi hiyo, Simba iliwachezesha kwa mara ya kwanza beki Gilbert Kaze na mshambuliaji Hamisi Tambwe kutoka Burundi, ambao walishindwa kucheza mechi ya awali kutokana na kukosa hati za uhamisho wa kimataifa na vibali vya kufanyakazi nchini.

Kaze alicheza vizuri kwa kushirikiana na Joseph Owino kwenye nafasi ya ulinzi wa kati, lakini Tambwe alishindwa kuonyesha cheche zake kutokana na kukosa nafasi mbili nzuri za kufunga mabao.

Bao pekee na la ushindi la Simba lilifungwa na mshambuliaji Haruna Chanongo dakika ya 34 kwa shuti la umbali wa mita 25 lililotinga moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa Shaibu Issa wa JKT Oljoro akiwa hana la kufanya.

Kabla ya kufunga bao hilo, Chanongo aliunasa mpira kutoka katikati ya uwanja na kusogea nao karibu na lango la JKT Oljoro. Kipa Shaibu hakuhangaika kuufuata mpira akidhani ungetoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.

JKT Olojoro ilipata adhabu ya penalti dakika ya 50 baada ya Issa Kandulu kuchezewa rafu na beki Joseph Owino ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, shuti la Babu Ally lilipanguliwa na kipa Abel Dhaira wa Simba.

Babu alipata nafasi nyingine nzuri ya kuifungia bao JKT Oljoro dakika ya 58 alipopewa pasi ndani ya eneo la hatari la Simba na kubaki ana kwa ana na kipa Dhaira, lakini shuti lake lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa huyo.

Simba: Abel Dhaira, Nasoro Masoud 'Cholo', Idrisa Rashid, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Abdulrahim Humud, Betram Mombeki, Hamisi Tambwe, Haruna Chanongo.

JKT Oljoro: Shaibu Issa, Yusuf Machogote, Napho Zuberi, Nurdin Mohamed, Shaibu Nayopa,Babu Ally, Swalehe Iddi, Hamisi Swalehe, Amri Omary, Sabri Ally, Esau Sani.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbeya City na Ruvu Shooting zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao  dakika ya saba lililofungwa na Paul Nongwa baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Ruvu Shooting.Shaban Suzan aliisawazishia Ruvu Shooting dakika ya 25 baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Mbeya City.

Bao la pili na la ushindi la Mbeya City lilifungwa na mkongwe Steven Mazanda dakika ya 90 kwa kiki kali ya chini iliyotinga moja kwa moja na kuamsha shangwe kwa wenyeji.

Azam FC ilitoka uwanjani kifua mbele dhidi ya Rhino Rangers baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

No comments:

Post a Comment