Hatimaye klabu ya Azam FC ya Tanzania imemuuza mshambuliaji wake Mrisho Khalfan Ngassa kwenda klabu ya Simba SC.
Azam, ambao walimsaini Ngassa kwa ada iliyovunja rekodi ya uhamisho kwa wachezaji wanaocheza Bongo, Million 55, wamemuuza Ngassa kwa ada ya millioni 25 iliyolipwa cash na mabingwa wa Tanzania, Simba.
Akizungumza na mtandao huu,Meneja wa Azam, Patrick Kahemele amesema kamati ya ufundi ya klabu pamoja na uongozi walikubalina kumuweka sokoni Mrisho Ngassa mara tu baada ya kumalizika kwa michuano ya Kagame Cup ambayo iliisha kwa Azam kushika nafasi ya pili nyuma ya Yanga.
"Klabu iliamua kumweka sokoni Ngassa mara tu baada ya michuano ya Kagame kumalizika, kwa kuwa mwenyewe alionesha nia ya kujiunga na klabu yake ya zamani Yanga, sisi tuliwapa kipaumbele Yanga, lakini pia Simba nayo ilionesha nia ya kumtaka. Tukafungua bid na kutangaza tunahitaji $50,000. Yanga baada ya kuwajulisha juu ya hili wakatuma ofa ya millioni 20, Simba nao wakatuma millioni 25. Ofa zote zilikuwa chini ya kiasi tulichohitaji lakini baada ya majadiliano ya viongozi wote wa Azam tukaona bora tumuuze tu, kwa bei ya millioni 25.
"Kwa kuwa Simba walikuwa wameshafikia viwango na sisi lengo letu lilikuwa ni kumuuza Yanga, asubuhi ya leo tukawatumia email Yanga tukiwaambia waboreshe ofa yao na tukawaambia bid ya Ngassa itafungwa saa saba mchana, lakini hadi muda huo unafika Yanga hawakuwa wametujibu chochote, kitendo ambacho tulikitafsiri hawana nia ya dhati ya kumsaini mchezaji huyo, kwa upande mwingine Simba walikuwa tayari wamefikia dau tulilolitaka hivyo tukafunga bid na kumuuza mchezaji huyo kwa Simba," alimaliza Patrick.
Tunaendelea kumtafuta Mrisho Ngassa na pale tutakapompata tutawaletea taarifa rasmi kuhusu alivyopokea taarifa za kuuzwa Simba.
By Aidan Charlie
No comments:
Post a Comment