KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 29, 2010

Stars yaivutia pumzi Amavubi

WACHEZAJI wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars wamepania kuifunga Rwanda katika mechi ya awali ya raundi ya pili ya michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani, itakayochezwa Jumamosi.
Wakizungumza na Burudani kwenye kambi yao iliyopo hoteli ya Atrium, Sinza, Dar es Salaam, wachezaji hao walisema lazima waifunge Rwanda ili wajiweke kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za michuano hiyo.
Mmoja wa wachezaji hao, Kigi Makasi alisema wanaendelea vizuri na mazoezi yao chini ya Kocha Marcio Maximo huku kila mchezaji akiwa na ari kubwa ya kushinda mechi hiyo.
“Kwa kweli sote tuna ari kubwa sana ya kuishinda Rwanda kwa sababu tumepania kufuzu kucheza fainali za michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo,”alisema.
Kipa Shaaban Kado alisema, mbinu wanazofundishwa na Maximo ni za kiwango cha juu na zimewafanya wawe na matumaini makubwa ya kushinda mechi hiyo.
Mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema, Stars ina nafasi kubwa ya kuitoa Rwanda kwa vile imeshakutana nayo mara kadhaa katika mechi za kimataifa na kirafiki na kuishinda.
“Dawa pekee ni kuishinda Rwanda kwa mabao mengi hapa nyumbani ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele,”alisema.
Stars ilifuzu kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kuibugiza Somalia mabao 6-0 katika mechi iliyochezwa mwezi uliopita kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment