KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, February 2, 2015

TFF YATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA KATIBU IRFA



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA), John Ambwene Mwakalobo uliotokea jana (Februari 1 mwaka huu) mkoani Iringa baada ya kuanguka akiwa nyumbani kwake.

Msiba huo ni pigo kwa wadau wa mpira wa mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Mwakalobo alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi. Mwaka 2011 alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa IRFA, kabla ya 2012 kushinda nafasi ya Katibu Msaidizi.

Alizaliwa Februari 4, 1954 na kupata elimu ya sekondari katika shule ya Azania, Dar es Salaam na baadaye mafunzo ya ualimu kwenye Chuo cha Ualimu Mpwapwa mkoani Dodoma. Alianzia kazi ya ualimu Newala mkoani Mtwara kabla ya kuhamia mkoani Iringa mwaka 1981. Alistaafu mwaka 2013.

TFF inatoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa msiba huo.

Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho (Februari 3 mwaka huu) kwao Kyela mkoani Mbeya. Ameacha mke, watoto wanne na mjukuu mmoja. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.

MECHI ZA MWISHO FDL SASA FEB 8 NA 10

 Mechi za raundi mbili za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote mawili zimerudishwa nyuma kutokana na maombi ya klabu hizo kupungaza gharama za kuendelea kuziweka kambini timu zao.

Hivyo, Februari 8 mwaka huu kundi A litacheza mechi zake za raundi ya 21 wakati zile za raundi 22 ambayo ndiyo ya mwisho zitafanyika Februari 13 mwaka huu. Mechi za Februari 8 ni KMC vs African Lyon, Kurugenzi vs African Sports, Majimaji vs JKT Mlale, Kimondo vs Friends Rangers, Ashanti United vs Villa Squad, Polisi Dar vs Lipuli.

Februari 13 mwaka huu ni African Lyon vs Polisi Dar, Kurugenzi vs Lipuli, Kimondo vs Majimaji, JKT Mlale vs Ashanti United, Friends Rangers vs African Sports, na Villa Squad vs KMC.

Kwa upande wa kundi B wataanza mechi za raundi 22 Februari 10 mwaka huu ili kupisha mechi za viporo za Polisi Mara zinazomalizika Februari 5 mwaka huu. Hivyo, Februari 10 mwaka huu itakuwa ni Burkina Faso vs JKT Kanembwa, Mwadui vs Polisi Tabora, Polisi Dodoma vs Green Warriors, Rhino Rangers vs JKT Oljoro, Panone vs Polisi Mara, Geita Gold vs Toto Africans.

Raundi ya 22 itachezwa Februari 15 mwaka huu kwa mechi kati ya JKT Kanembwa vs Green Warriors, Mwadui vs Burkina Faso, Polisi Tabora vs JKT Oljoro, Polisi Dodoma vs Panone, Toto Africans vs Rhino Rangers, na Geita Gold vs Polisi Mara.  

KIPA BORA WANAWAKE AZAWADIWA 500,000/-

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara akimkabidhi kombe nahodha wa timu ya Temeke baada ya kuibuka washindi wa mashindano ya Proin Women Taifa Cup, ambayo yalichezwa katika Dimba la Azam huku Proin Promotions na Azam wakidhamini mashindano hayo.


Nahodha wa Timu ya Pwani akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni mbili ambazo ni zawadi ya mshindi wa pili katika Mashindano ya Proin Women Taifa Cup na kumalizika kwa Temeke kuwa mabingwa kwa kuifunga Pwani goli 1- 0.
Nahodha wa Timu ya Ilala ambao ni washindi wa tatu akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni moja ambayo mshindi wa tatu katika mashindano hayo ni Ilala
 Na Mwandishi Wetu
Kipa bora wa michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake, Belina Julius wa Temeke amezawadiwa sh. 500,000 na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.

Dk Mukangara alitoa zawadi hiyo baada ya mechi ya fainali ya michuano iliyomalizika jana kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam. Dk Mukangara alikuwa mgeni rasmi kwenye fainali hiyo.

Temeke ndiyo walioibuka mabingwa wa michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini baada ya kuilaza Pwani bao 1-0 katika fainali iliyoonyeshwa moja kwa moja (live) na televisheni ya Azam.

Ilala ilifanikiwa kutwaa baada ya kuichapa Kigoma mabao 3-0. Bingwa amepata sh. milioni tatu, makamu bingwa sh. milioni mbili wakati mshindi wa tatu ameondoka na sh. milioni moja katika michuano hiyo iliyodhaminiwa na kampuni ya Proin.

TFF MBIONI KUOATA MDHAMINI LIGI YA FDL


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liko mbioni kupata mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Tunatarajia mdhamini huyo atakuwa tayari kwa ajili ya msimu wa 2015/2016.

Ligi Daraja la Kwanza inashirikisha timu 24 zinazocheza katika makundi mawili ya timu 12 kila moja kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.

Timu zinazocheza FDL msimu huu ni African Lyon (Dar es Salaam), African Sports (Tanga), Ashanti United (Dar es Salaam), Burkina Faso (Morogoro), Friends Rangers (Dar es Salaam), Geita Gold (Geita), Green Warriors (Dar es Salaam), JKT Kanembwa (Kigoma), JKT Mlale (Ruvuma) na JKT Oljoro (Arusha).

Nyingine ni Kimondo (Mbeya), Kinondoni Municipal Council (Dar es Salaam), Kurugenzi (Iringa), Lipuli (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mwadui (Shinyanga), Panone FC (Kilimanjaro), Polisi Dar es Salaam, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora, Rhino Rangers (Tabora), Toto Africans (Mwanza), na Villa Squad (Dar es Salaam).

Sunday, February 1, 2015

YANGA YALAZIMISHWA KUTOKA SULUHU NA NDANDA UNITED, KISIGA ABWAGA MANYANGA SIMBA


YANGA jana ilipunguzwa kasi katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Ndanda United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, timu zote mbili zilipata nafasi kadhaa nzuri za kufunga mabao, lakini kikwazo kikubwa kilikuwa washambuliaji wake kutokuwa makini.

Wakati huo huo, kiungo Shaaban Kisiga ‘Malone’ amejitoa katika klabu ya Simba SC kutokana na sababu ambazo bado hazijajulikana.

Kisiga alibeba vitu vyake baada ya mechi dhidi ya Mbeya City, Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na kuwaambia wenzake anaondoka na anazima simu zake zote ili akipigiwa asipatikane.

Katika mchezo huo, ambao Simba SC ililala 2-1, Kisiga alitokea benchi kipindi cha pili kama ilivyo ada yake kipindi hiki chini ya kocha Mserbia, Goran Kopunovic.

Siku zote Kisiga amekuwa akitokea benchi na kwenda kubadilisha mchezo, lakini Jumatano wiki hii hakuweza kuisaidia timu kuepuka kipigo cha timu ya Manispaa ya Mbeya.

Mchezaji mwingine mkongwe, Nassor Masoud ‘Chollo’ amepewa ruhusa maalum ya kwenda kutatua mataizo ya kifamilia.

Chollo ambaye siku hiyo alikosa penalti dakika ya mwisho ambayo kama angefunga Simba SC, ilipata sare, mke wake anaumwa na wana mtoto mdogo ambaye anahitaji uangalizi wa kina, wakati nyumbani hawana msaidizi.

SIMBA YAPIGWA FAINI SH. MILIONI TATU


Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga klabu ya Simba faini ya sh. milioni tatu kutokana na timu yake kuvaa jezi ambazo hazikuwa na nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu, kampuni ya Vodacom wakati wa mechi yao dhidi ya Kagera Sugar.

Mechi hiyo namba 50 ya Ligi Kuu ya Vodacom ilichezwa Desemba 26 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 13(7) ya Ligi Kuu inayotaka klabu kuheshimu masharti ya udhamini wa Ligi Kuu kwenye mechi zake.

Nayo Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa kanuni ya 28(4) kwa kusababisha mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati yake na Toto Africans iliyochezwa Januari 14 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuvurugika.

Kutokana na mchezo huo kuvurugika, Toto Africans imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu. Uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia kanuni ya 28(1) inayotawala ligi hiyo.

FRIENDS RANGERS YAPOTEZA MECHI KWA KUGOMA



Mechi namba 120 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kundi A kati ya Majimaji na Friends Rangers iliyochezwa jana (Januari 29 mwaka huu) Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilivunjika dakika ya 38 baada ya Friends Rangers kugoma kuendelea na mchezo.

Kwa kitendo hicho, Friends Rangers imepoteza mchezo huo. Hatua nyingine za kikanuni zitafuata baada ya kamati inayohusika kukutana.

Wakati huo huo, mechi ya FDL kundi A iliyochezwa leo (Januari 30 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kati ya African Lyon na Ashanti United imemalizika kwa sare ya bao 1-1.

FIFA KUCHUNGUZA TUHUMA ZA UPANGAJI MATOKEO


Ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) upo nchini kuchunguza tuhuma za upangaji matokeo.

Waamuzi waliosimamishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu  Tanzania (TFF) pamoja na watu wengine watahojiwa na ujumbe huo. Matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa na FIFA baada ya shughuli hiyo kukamilika.

Tunaendelea kuwahimiza wanafamilia wa mpira wa miguu wazidi kuzingatia kanuni za maadili za TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA katika utendaji wao. FIFA itahakikisha kuwa haki inatendeka katika uchunguzi ambao inaufanya.

TFF YAHADHARISHA MGOGORO WA ZFA KORTINI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)l imepokea kwa masikitiko taarifa za kuwepo tena kortini kwa kesi dhidi ya uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), jambo ambalo linaweza kuathiri ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, na Kombe la Shirikisho. 

Mwishoni mwa mwaka jana, TFF ilihadharisha juu ya masuala ya mpira wa miguu kupelekwa mahakamani, kwani kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za uendeshaji mpira wa miguu ambazo zinakataza masuala ya mchezo huo kupelekwa katika mahakama za kawaida.

Kutokana na hali hiyo, TFF iliiandikia barua ZFA kutaka mgogoro huo uondolewe kortini na yenyewe kuridhia kuwa tayari kupeleka ujumbe Zanzibar ili ukutane na pande zinazohusika.

Pia TFF ilisema timu za Tanzania Bara zisingeruhusiwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 iwapo kesi hiyo ingeendelea kuwepo kortini na kutaka iondolewe bila masharti yoyote.

ZFA iliithibitishia TFF kuwa kesi hiyo imeondolewa kortini bila masharti, hivyo timu za Tanzania Bara kuruhusiwa kushiriki katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Ni muhimu suala hilo likashughulikiwa haraka ili kutohatarisha ushiriki wa timu za KMKM na Polisi kwenye michuano hiyo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

WAANGALIZI WA SIRI KUSIMAMIA MECHI ZA MWISHO FDL




 Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litatuma waangalizi wa siri kwenye mechi za raundi ya 21 na 22 ambazo ni za mwisho kwa makundi yote ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakazoanza kuchezwa  Februari 10 mwaka huu.

Mwangalizi huyo (match assessor) atatumwa na Katibu Mkuu ambapo baada ya mechi atatuma ripoti kwake kwa hatua zaidi.

Mechi za raundi ya 21 kundi A zitachezwa Februari 10 mwaka huu kati ya KMC na African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani), Kurugenzi FC na African Sports (Uwanja wa Mufindi), Majimaji na JKT Mlale (Uwanja wa Majimaji), Kimondo FC na Friends Rangers (CCM Vwawa, Mbozi), Ashanti United na Villa Squad (Uwanja wa Karume) na Polisi Dar na Lipuli FC (Uwanja wa Azam Complex).

Raundi ya 22 itachezwa Februari 16 mwaka huu kwa kuzikutanisha African Lyon na Polisi Dar (Uwanja wa Karume), Kurugenzi na Lipuli FC (Uwanja wa Mufindi), Kimondo FC na Majimaji (CCM Vwawa, Mbozi), JKT Mlale na Ashanti United (Uwanja wa Majimaji), Friends Rangers na African Sports (Uwanja wa Taifa), na Villa Squad na KMC (Uwanja wa Azam Complex).

Kundi B raundi ya 21 ni Februari 17 mwaka huu kati ya Burkina Faso na JKT Kanembwa (Uwanja wa Jamhuri), Mwadui na Polisi Tabora (Uwanja wa Mwadui), Polisi Dodoma na Green Warriors (Uwanja wa Jamhuri), Rhino Rangers na JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Panone na Polisi Mara (Uwanja wa Ushirika), Geita Gold na Toto Africans FC (Geita).

Februari 22 mwaka huu ni JKT Kanembwa na Green Warriors (Lake Tanganyika), Mwadui na Burkina Faso (Mwadui), Polisi Tabora na JKT Oljoro (Ali Hassan Mwinyi), Polisi Dodoma na Panone (Uwanja wa Jamhuri), Toto Africans na Rhino Rangers (CCM Kirumba) na Geita Gold na Polisi Mara (Geita).

Mechi za viporo za Polisi Mara zitachezwa Februri Mosi dhidi ya JKT Kanembwa, na Februari 5 mwaka huu dhidi ya Polisi Tabora. Mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.

Wednesday, January 28, 2015

SIMBA YAPIGWA MWELEKA NA MBEYA CITY



TIMU ya soka ya Simba jana ilikwaa kisiki katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbeya City.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 23 lililofungwa na mshambuliaji chipukizi Ibrahim Ajibu. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Mbeya City ilisawazisha bao hilo dakika ya 76 kupitiakwa Paul Nonga baada ya kufanyika kwa shambulizi kali kwenye lango la Simba.

Bao la pili na la ushindi la Mbeya City lilifungwa kwa njia ya penalti na Yussuf Abdalla baada ya kipa Manyika Peter wa Simba kudaka mguu wa Raphael Alfa ndani ya mita 18 badala ya mpira.


Tuesday, January 27, 2015

NSSF, REAL MADRID KUZALISHA VIPAJI VYA SOKA TANZANIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau  akifafanua jambo kwa wageni waliohudhuria hafla fupi ya kusaini mkataba  kati ya shirika hilo na timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid wa kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Dk. Dau alisema katika uendeshaji wa kituo hicho, Real Madrid itakua na dhamana ya kushughulikia masuala yote ya ufundi, kuwatambua wachezaji, chakula, wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba wajibu wa shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau (aliyekaa kushoto) na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez (aliyekaa kulia) kwa pamoja wakisaini mkataba wa kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Wakishuhudia ni wawakilishi kutoka pande hizo mbili. Kituo hicho kitakua na uwezo wa kupokea wanafunzi 108 kwa wakati mmoja.
  
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dkt. Ramadhani Dau (kushoto) na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez (kulia) wakibadilishana mikataba ya kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Wakishuhudia ni wawakilishi kutoka pande hizo mbili. Kituo hicho kitakua na uwezo wa kupokea wanafunzi 108 kwa wakati mmoja.

Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid, Bw. Ruben De la Red Gutierrez akifafanua jambo kwa wageni waliohudhuria hafla fupi ya kusaini mkataba  kati ya timu yake  na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa kuanzishwa kwa kituo cha michezo (sports academy) katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kitahusisha wanafunzi 108 watakaogawanywa kwenye timu za chini ya umri wa miaka 13, 15, 17, 19, kikosi cha pili na timu ya wakubwa.


Na Mwandishi wetu

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeingia mkataba na klabu maarufu duniani ya Real Madrid ya Hispania wa kujenga kituo cha michezo kwa ajili ya kuzalisha vipaji.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo wa miaka 18, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau alisema ujenzi huo utagharimu Sh bilioni 16 na unatarajiwa kuanza kujengwa Mei mwaka huu na kwamba utakamilika baada ya miezi 18.

Dk Dau alisema kituo hicho ambacho kitajengwa kwenye kijiji cha michezo cha shirika hilo (NSSF Sports City), kitakuwa eneo la Mwasoga, Kigamboni, Dar es Salaam.

“Tuna eneo la zaidi ya ekari 400 ambapo tutajenga viwanja, shule ya michezo, nyumba za kuishi na maduka. Lengo letu tuzalishe na kuuza wachezaji. Tunakusudia kuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 13, 18, 20, timu B na timu ya wakubwa,” alisema Dk Dau.

Alisema utekelezaji wa kituo hicho utaanza hivi karibuni kwa kutumia majengo ya kukodi wakati wakisubiri ujenzi kukamilika.

“Hivi hapa baada ya kusaini mkataba, utekelezaji utaanza kwa kutumia majengo ya kukodi ambayo tunadhani yatakuwa maeneo ya Temeke na tutakuwa tukitumia viwanja vya Karume na Uhuru,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF alisema katika kuendesha kituo hicho, kila kitu kitafanywa na Real Madrid kuanzia masuala yote ya ufundi, kuwatambua wachezaji, chakula, wataalamu wa saikolojia na wataalamu wa viungo na kwamba wajibu wa shirika lake utakuwa kwenye kujenga tu.

“Sisi tunachukulia huu mradi ni uwekezaji na hatufanyi hisani, itazingatia misingi ya biashara na faida kubwa ni kwamba NSSF itaongeza kipato, lakini pia kituo kitatumika kuitangaza Tanzania kwa sababu yatakayofanyika yataoneshwa kwenye televisheni ya Real Madrid,” alifafanua Dk Dau.

“Lakini pia wakati umefika sasa kwa Tanzania kushiriki Kombe la Dunia Qatar 2022, kama unaandaa vizuri vijana wa miaka 13 sasa mpaka mwaka 2020 wanaweza kuwakilisha vizuri kwenye mechi za kufuzu na mwaka 2022 wakashiriki Kombe la Dunia, wakikosa la Qatar, basi hata hizo zinazokuja, hiyo pia ni moja ya madhumuni ya kituo hicho.”

Akizungumzia namna walivyofikia uamuzi wa kujenga kituo, Dk Dau alisema wazo hilo lilipatikana Agosti mwaka jana na kisha likapelekwa kwenye Mkutano wa Wanachama uliofanyika Arusha ambako waliazimia NSSF iwekeze rasmi kwenye michezo kabla ya kuwasilishwa kwenye bodi na utekelezaji kuanza kufanyika.

“Tulitembelea sehemu nyingi kuona wenzetu wanafanyaje. Binafsi nilitembelea nchi kadhaa za Ulaya, nilienda kituo cha Manchester United, Sunderland, Real Madrid kwa hapa Afrika nilikwenda Asec Mimosas (Ivory Coast) na TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC) kuona wanafanyaje, ziara ikazaa matunda kwani tulikubaliana na Madrid na ndio wamekuja kusaini mkataba leo (jana),” alifafanua Dk Dau.

Naye Mkuu wa Vituo vya Michezo wa Real Madrid, Rayco Garcia aliishukuru NSSF wa kuwa na mpango huo na kuahidi kufanya kazi ili kuipatia Tanzania mafanikio.

“Tukifanikiwa kuwatoa vijana hao, Tanzania itaweza kushiriki kwenye michuano mikubwa kama alivyosema Dk Dau, inabidi tufanye kazi ili vijana wafanikiwe, wafike mbali,” alisema Garcia.

Mbali na Garcia ambaye pia ni kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18 ya Madrid, wengine walioambatana kwenye msafara huo ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu hiyo, Ruben de la Red, Kocha Mkuu wa timu za vijana, Francisco Martin Ramos na Juan Jose San Roman Milla. Mwaka jana, wachezaji wa zamani wa Real Madrid walifanya ziara nchini

Monday, January 26, 2015

SIMBA, AZAM HAKUNA MBABE, OKWI APOTEZA FAHAMU UWANJANI


TIMU za soka za Simba na Azam jana zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Emmanuel Okwi kabla ya Azam kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Kipre Tchetche.

Katika mechi hiyo, timu zote mbili zilicheza kwa kasi huku kila moja ikipania kutoka uwanjani na ushindi.

Wakati huo huo, mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba jana alipoteza fahamu uwanjani baadaya kupigwa kiwiko na mchezaji mmoja wa Azam.

Kutokana na tukio hilo, Okwi alilazimika kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambako alilazwa na kuruhusiwa baada ya saa kadhaa.

Akizungumzia tukio hilo, daktari wa Simba, Salim Gembe, alisema mshambuliaji huyo amenusurika kufa.

"Okwi aligongwa kiwiko nyuma ya kichwa kwenye mishipa ya fahamu, kwa hiyo akapoteza
fahamu uwanjani. Ilikuwa mbaya sana, angeweza kupoteza maisha, lakini hali ile tuliidhibiti
wakati tunampa huduma ya kwanza uwanjani,”alisema.

“Baada ya hapo, tukaingia naye ndani kwenye zahanati ndogo ya uwanja, kuendelea kumpa tiba
hadi fahamu zikamrejea, lakini hali yake haikuwa nzuri sana, ikabidi tumkimbize Muhimbili,
ambako baada ya tiba ya takriban saa mbili, sasa yuko vizuri,”amesema Gembe.

Sunday, January 25, 2015

MRWANDA AIBEBA YANGA, YAICHAPA POLISI MORO BAO 1-0

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

YANGA jana ilirejesha imani kwa mashabiki wake baada ya kuichapa Polisi Moro bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mshambuliaji Danny Mrwanda ndiye aliyeifungia Yanga bao hilo la pekee dakika ya 42, akimalizia mpira uliopanguliwa na kipa Tony Kavishe, kufuatia shuti la Simon Msuva.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imechupa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hioyo, ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi 10. Azam inaendelea kuongoza ikiwa na pointi 20.

Katika mechi hiyo, Yanga ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini tatizo kubwa lilikuwa umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake.

Yanga SC ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, lakini ugonjwa wa kukosa mabao ya wazi ulijirudia kabla ya Mrwanda kuupatia tiba mwishoni mwa kipindi hicho.

Polisi ilizinduka katika kipindi cha pili na kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Yanga, ikiongozwa na Saidi Bahanuzi, lakini haikuwa na bahati ya kupata bao.

Saturday, January 24, 2015

6 ZAFUZU KUCHEZA ROBO FAINALI KOMBE LA TAIFA WANAWAKE


Timu za mikoa sita tayari imepata tiketi za kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake itakayoanza Januari 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati nyingine mbili zinajulikana leo (Januari 23 mwaka huu).

Mikoa ambayo timu zake tayari zina tiketi za robo fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin ni Ilala, Kigoma, Mwanza, Pwani, Tanga na Temeke.

Matokeo ya mechi za leo kati ya Iringa na Ruvuma, na ile kati ya Mbeya na Katavi ndiyo yatakayoamua ni timu zipi mbili kati ya hizo zinakwenda Dar es Salaam kucheza robo fainali.

Timu zote zilizofuzu hatua ya robo fainali zinatakiwa kuripoti Dar es Salaam keshokutwa (Januari 25 mwaka huu). Fainali ya michuano hiyo itachezwa Februari Mosi mwaka huu.

Wednesday, January 21, 2015

KLABU KUJIGHARAMIA HOTELI MICHUANO YA CAF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanyia marekebisho kanuni zake za michuano ya ngazi ya klabu kwa upande wa malazi ambapo sasa timu zitachagua na kujilipia zenyewe hoteli zinapokuwa kwenye mechi za ugenini.

Kabla ya marekebisho ya kanuni hiyo, timu ngeni ilikuwa ikilipiwa hoteli na timu mwenyeji kwa msafara usiozidi watu 25. CAF ilikuwa imepitisha hoteli maalumu katika kila nchi ambapo mwenyeji alitakiwa kuziweka timu ngeni.

Kwa marekebisho hayo, Chama cha Mpira wa Miguu cha nchi mwenyeji kitakuwa na wajibu wa kuitafutia hoteli timu ngeni iwapo tu kitaombwa kufanya hivyo, lakini jukumu la kulipia malazi litakuwa la timu yenyewe.

Mwaka huu Tanzania inawakilishwa na timu mbili za Azam na Yanga katika michuano ya CAF. Azam inacheza Ligi ya Mabingwa (CL) ambapo itaanzia nyumbani Februari 15 mwaka huu kwa kuikaribisha El Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Nayo Yanga itacheza michuano ya Kombe la Shirikisho (CC), na imepangiwa kucheza mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya BDF IX ya Botswana. Mechi hiyo itafanyika Februari 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tuesday, January 20, 2015

WACHEZAJI, VIONGOZI 12 KUHUKUMIWA NA KAMATI YA NIDHAMU YA TFF


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewapeleka wanamichezo 12 wakiwemo viongozi, makocha na wachezaji kwenye Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na matukio mbalimbali kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake.

Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe Idd Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, na Nassib Lugusha wa Polisi Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia waamuzi na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani katika mechi zao za FDL.

Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Polisi Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya waamuzi kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Naye Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Rhino Rangers, Albert Mbunji anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga maamuzi na kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Pia Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Oljoro JKT, Eliud Justine Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili; alimpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi akiba (fouth official) Mussa Magogo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kocha wa Polisi Tabora, Kim Christopher analalamikiwa kwa kumtolea mlugha chafu mwamuzi wa mechi kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Msimamizi wa Kituo cha Musoma, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona naye anapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa ushirikiano kwa maofisa wa mechi na kuchochea maofisa hao (waamuzi) kupigwa.

Kwa upande wake, Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye kamati ya Nidhamu kwa matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za Kombe la Taifa la Wanawake.

Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao mwamuzi wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga iliyochezwa mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje mchezo.

Naye Gunda analalamikiwa kwa kushindwa kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

SDL KUANZA MZUNGUKO WA PILI JANUARI 31
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Pili (SDL) sasa utaanza Januari 31 mwaka huu, badala ya Januari 24 mwaka huu kama ilivyopangwa awali ili kutoa fursa kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia usajili wa dirisha dogo.

Timu zinazocheza ligi hiyo katika makundi manne tofauti ni; Milambo FC, Mji Mkuu FC (CDA), Mvuvumwa FC, Singida United, na Ujenzi Rukwa (Kundi A), Arusha FC, Bulyanhulu FC, JKT Rwamkoma FC, Mbao FC, na Pamba SC (Kundi B).

Nyingine ni Abajalo FC, Cosmopolitan, Kariakoo Lindi, Kiluvya United, Mshikamano FC, na Transit Camp (Kundi C), wakati Kundi D ni Magereza Iringa, Mji Njombe, Mkamba Rangers, Town Small Boys, Volcano FC, na Wenda FC.

WACHEZAJI WAWILI WA LIGI KUU NA FDL WATOZWA FAINI


Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewapiga faini na kuwafungia mechi wachezaji wawili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa kufanya vitendo kinyume na kanuni zinazotawala ligi hizo.

Mshambuliaji Haruna Chanongo wa Stand United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga teke mwamuzi wa mechi dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Januari 3 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu.

Kipa Amani Simba wa Oljoro JKT amepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kukataa kupeana mkono na viongozi wakati wa kusalimia kabla ya kuanza mechi kati ya timu yake na Toto Africans iliyofanyika jijini Mwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14 ya FDL.

Timu ya Polisi Mara imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi ya FDL dhidi ya Mwadui ya Shinyanga iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Pia Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake kwenye mechi namba 40 dhidi ya Geita Gold, adhabu ambazo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 41.

Sunday, January 18, 2015

MTIBWA SUGAR YAPUNGUZWA KASI NA JKT RUVU



MTIBWA Sugar imepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na JKT
Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, Dar es Salaam jana.

Matokeo hayo yanairejesha Mtibwa kileleni baada ya kufikisha pointi 17, baada ya mechi tisa,
sawa na mabingwa watetezi, Azam FC, lakini timu ya Manungu inapandishwa kwa wastani wa
mabao.

JKT Ruvu imefikisha pointi 17 pia baada ya mechi 11, lakini inabaki nafasi ya tatu mbele ya vigogo
Yanga pointi 15 na Simba 12.

JKT ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya saba, mfungaji Samuel Kamuntu ambaye
aliuwahi mpira uliotemwa na kipa Said Mohammed Kasarama.

Mtibwa walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 36, mfungaji Ame Ally aliyemalizia kwa
kichwa kona iliyochongwa na Shijja Kichuya.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo jana, Coastal Union imelazimishwa sare ya bila kufungana
na Polisi Moro Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

SIMBA, AZAM ZASHINDA LIGI KUU, YANGA YABANWA

SIMBA jana ilizoa pointi zote tatu kutoka kwa Ndanda FC baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwande Sijaona mjini Mtwara.

Ushindi huo ni wa pili kwa Simba tangu ligi hiyo ilipoanza na umepokelewa kwa faraja kubwa na mashabiki wa timu hiyo baada ya kuishuhudia timu yao ikipata sare saba mfululizo na kupoteza mechi moja.

Mabao ya Simba yalifungwa na Dan Ssenkuruma dakika ya 26 aliyemalizia kwa shuti la mguu wa kushoto krosi kutoka kwa Ramadhani Singano 'Messi'.

Bao la pili lilifungwa na Elias Maguri dakika ya 68 baada ya kumalizia pasi kutoka kwa Ssenkuruma.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo,Azam walijikita kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuichapa Stand United bao 1-0 mjini Shinyanga.

Bao pekee na la ushindi la Azam lilifungwa na kiungo Frank Dumayo, ambaye ilikuwa mechi yake ya kwanza ya ligi kwa timu hiyo baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Nayo timu kongwe ya Yanga ilishindwa kutamba mbele ya Ruvu Shooting baada ya kulazimishwa kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

SIMBA, YANGA KURUDIANA MACHI 8


Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) imeingizwa mechi za viporo zilizotokana na timu za Azam,

Mtibwa Sugar na Simba kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 iliyomalizika wiki hii
kisiwani Zanzibar.

Vilevile mechi za viporo zimeingizwa kwa kuzingatia ushiriki wa timu za Azam kwenye Ligi ya
Mabingwa Afrika (CL) na Yanga kwenye Kombe la Shirikisho (CC) pamoja na mechi za kirafiki za
Taifa Stars.

Yanga itacheza na BDF ya Botswana kwenye mchezo utakaofanyika Februari 14 mwaka huu
Uwanja wa Taifa wakati Azam itaikabili El Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex,
Februari 15 mwaka huu.

Mechi za viporo itakuwa kama ifuatavyo; Januari 20- Kagera Sugar na Azam (Mwanza),
Januari 28- Simba na Mbeya City (Dar es Salaam), Februari 4- Coastal Union na Yanga
(Tanga), Februari 11- Azam na Mtibwa Sugar (Dar es Salaam) na Februari 11- Mgambo Shooting
na Simba (Tanga).

Februari 11- Yanga na Ndanda (Dar es Salaam), Februari 21- Mbeya City na Yanga (Mbeya),
Februari 25- Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons (Morogoro), Februari 28- Simba na Mtibwa
Sugar (Dar es Salaam), Machi 4- Ruvu Shooting na Azam (Pwani), na Machi 4- JKT Ruvu na
Yanga (Dar es Salaam).

Machi 4- Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro (Morogoro), Machi 8- Simba na Yanga (Dar es
Salaam), Machi 11 Azam na Mbeya City (Dar es Salaam), Machi 11- Yanga na Kagera Sugar (Dar
es Salaam), Machi 18- Azam na Ndanda (Dar es Salaam), Machi 18- Yanga na Stand United (Dar
es Salaam), Aprili 8- Simba na Tanzania Prisons (Dar es Salaam).